NI aibu kila siku kuendeleza kilio kile kile cha ubabaishaji
wa soka la Tanzania,
linaloongozwa na Shirikisho la Soka nchini (TFF). Wadau wa michezo wamekuwa
wakilia sana
juu ya uendeshaji mbovu wa soka, hasa uamuzi wa utata wa marefa, timu kutumia
fedha nyingi, rushwa katika kusaka ushindi kwenye mechi zao.
Ratiba isiyokuwa na mashiko kwa baadhi ya timu, huku
wasimamizi wa soka, wakiwa wepesi wa kuangalia zile mechi zenye faida, yani
zinapokutanisha timu za Simba na Yanga.
Ni kama vile tumeshindwa werevu, hivyo walau sasa tujifunze
na ujinga katika kudidimiza zaidi soka letu, maana sioni mipango inayoweza
kuinua michezo, ukiwamo mpira wa miguu unaopendwa kwa kiasi kikubwa hapa nchini.
TFF inayoongozwa na Rais wake, Leodgar Tenga, akiwa na
watendaji wake wengine, kama vile Angetile Osiah, Mkurugenzi wa Ufundi, Sunday
Kayuni na wengineo, wamekuwa hohe hahe hadi kuchelewesha Kampuni ya kuendesha
ligi.
Haya yanasababisha ligi na mpira wa miguu kwa ujumla kuwa wa
kusua sua, maana yale yanayofanywa leo ndiyo yale yale yaliyolidumaza soka la
Tanzania, huku likiachwa na nchi nyingine, kama vile Kenya, Uganda na
kwingineko.
Leo hii timu ya Taifa ya Tanzania,
inafanya kazi kubwa sana kuweza kuibuka na
ushindi katika mechi zake zinapokutana na nchi za Uganda
na Kenya.
Lakini, timu hizo ni zile zilizokuwa zinafungwa mara kwa mara na Taifa Stars.
Ukiyasema haya, watashindwa kukuelewa, hivyo kuchelewesha
kwa kiais kikubwa maendeleo ya michezo hapa nchini. Angalia, ligi kutoendeshwa
na Kampuni kama invyotakiwa na wadau, kunaroa
ladha halisi.
Watu wanajiendesha wanavyotaka wao. Timu inajiandaa na mechi
yake, lakini inapelekewa barua ya haraka, ikitangaza kusogeza mbele au
kurudisha nyuma mechi husika. Timu ya African Lyon, inazuiliwa kudhaminiwa na
Kampuni ya Zantel, maana ligi ipo chini ya Kampuni ya Vodacom Tanzania.
Sawa, ila fedha zinazotolewa na vodacom zinatosha k,wa timu
hizo? Kama zinatosha, je, hao Vodacom
wanazitoa kwa wakati? Kumekuwa na ghiriba nyingi katika uendeshaji wa ligi ya Tanzania, hivyo
kusababisha kutoelewana.
Kwa mfano, baadhi ya timu ikiwamo African Lyon zinalalamika
kuwa hawajashirikishwa katika udhamini huo wa Vodacom. Wanfika mbali zaidi kwa
kusema kuwa hawajapa nafasi ya kuangalia aina ya mkataba huo.
Pamoja na hayo, mkataba wa Vodacom na TFF juu ya ligi hiyo
ulisumbua kwa wiki kadhaa, hadi kuchelewesha kutoka kwa ratiba na kuanza kwa
ligi hiyo. Haya ni maajabu makubwa na matatizo ya ligi hiyo ya Tanzania Bara.
Ukiangalia kwa haraka, yote hayo ni majibu kuwa ligi haiwezi
kuwa na tija kama kutakuwa na malalamiko ya
kupitiliza. Timu zinalalamikia ukandamizaji huo ambao kwa kiasi kikubwa
unachekewa na hao TFF.
Nalisema hili bila kuficha, maana ni ajabu ya mipango yenye matege.
Tutawezaje kuwa na wachezaji bora wakati ligi yetu haieleweki? Sisi ni wa hapa
hapa kwanini tunakuwa na mipango ya kucheza Kombe la Afrika au Dunia?
Hii ni aibu kubwa. Ndio maana hata ukiangalia mechi hizo,
utagundua kwamba hakuna mikakati wala ufundi zaidi ya ushindi wa lazima. Kwa
wale wenzetu wa Simba na Yanga ndio kabisa.
Kwanza wana mtaji mkubwa wa
mashabiki na wanachama wenye nazo hivyo
kuweza kufanya lolote wanalohitaji. Haya lazima tuyaangalie upya. Tuwe na
dhamira ya kweli na kuacha udanganyifu, ubabaishaji katika kuinua michezo.
Kunyume cha hapo hatutakuwa na jipya katika uendeshaji wa
soka, ndio maana Taifa linaachwa nyuma na harakati za nchi nyingine za Afrika
juu ya kuendeleza michezo.
Sikatai Taifa lina wachezaji imara na wenye vipaji vya hali
ya juu, ingawa nao wanaangushwa na aina ya viongozi wa soka la Tanzania.
Ubabaishaji ni mkubwa katika kila nyanja, ikiwamo uwanjani na usajili kwa
ujumla.
Kumekuwa na janja janja nyingi, huku Simba na Yanga
zikisikilizwa kupita kiasi, ingawa ukisema hili watakataa. Huwezi kubisha kuwa
tuna vijana mahiri lakini hawawezi kusonga mbele kama
hatutakuwa na mipango endelevu.
Wachezaji kama vile Mrisho Ngassa, Juma Kaseja, Nurdin
Bakari, Juma Nyoso, Nadir Haroub Canavaro, Haruna Moshi Boban na wengineo wana
vipaji vizuri na wanaweza kufanikisha maendeleo ya michezo hapa nchini.
Tatizo hawawezi kwenda mbele bila kuongozwa na hao
wanaowaongoza ndio wameoza kabisa. Haya lazima yasemwe kama
tuna lengo la kuboresha soka letu. Huo ndio ukweli wa mambo.
Vinginevyo tutakuwa tunacheza soka la nyumbani bila kuwa na
maendeleo yoyote, inagwa Mataifa mengine yanazidi kuchanja mbuga. Viongozi wa
soka kuanzia ngazi ya klabu, mikoa na Taifa kwa ujumla wajipange katika hilo.
Wasiopenda kasi ya mabadiliko wawekwe kando kwa ajili ya Tanzania.
Nasema hivyo huku nikiamini kuwa mashabiki wanaopenda soka ni wengi mno.
Ukitaka kuhakikisha hilo,
hudhuria mechi za Simba, Yanga au timu ya Taifa.
Kama mipango itawekwa, basi soka la Tanzania litapanda kwa
timu zetu zote, kama vile Coastal Union, Kagera Sugar, Azam FC, Mtibwa Sugar,
African Lyon, Toto African na nyinginezo, hivyo kuingiza mashabiki wengi katika
mechi zao.
Mashabiki wa soka hawatachagua tena mechi za kuingia.
Wataingia kwa kila mechi, maana wanapokwenda huko wanapata kitu kizuri. Nasema
hivyo kwasababu, leo hii mashabiki wanaingia kwa Simba na Yanga kwakuwa ndio
timu zao wanazopenda.
Hawapendi soka lao, ila wanapenda timu hizo kongwe. Kama hivyo ndivyo, tunawezaje kuwabadilisha watu juu ya
mtazamo wao? Hakika ni mikakati. Mipango imara pamoja na kuacha ubabaishaji
katika aina ya viongozi wetu.
Sheria zifuatwe na dhamira ya kweli iendelee kuwekwa kwa
ajili ya kuinua kiwango cha michezo kwa nchi yetu. Huo ndio ukweli wa mambo.
Tusipofanya hivyo, tutajiweka kwenye mtihani na kulaumu wakati hatuna mikakati.
Hakuna mtu asiyejuwa mambo mazuri ya kufanya. Wote
waliokuwapo kwenye nafasi za uongozi wa soka, hakika ni wenye akili zao timamu.
Hivyo watumie vichwa vyao kubuni na kuendeleza mambo yenye tija kwa Taifa letu.
Nasema haya kwa kujua kuwa tumekuwa na mapungufu mengi
katika uendeshaji wa soka letu, hivyo nadhani huu ni wakati sasa wa kujifanyia marekebisho kama
kweli ipo chembechembe za kuinua soka la Tanzania.
Kwa sasa, bila kuangalia ni Simba inayoongoza ligi, Azam FC,
Yanga, Mtibwa Sugar, ila hakuna soka linalosuuza nyoyo za watazamaji zaidi ya
wengi wao kutumia rushwa aidha ya fedha au ya mapenzi yao kwa timu hizo, hasa hizo kongwe.
Kama tumeshindwa werevu sio
mbaya tukiendelea kujifunza na ujinga, ila wasipite watu vichochoroni
wakijifanya wana uchungu na soka letu, maana wakati huu wapo kimya wakiendelea
kutafuna kile wanachopata.
Wakati ni huu. Tujisahihishe ili kulifanya Taifa lisiwe
kichwa cha mwendawazimu kama alivyowahi
kusema, Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment