Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za vifo vya wachezaji watano wa
timu ya Rusumo FC ya mkoani Kagera vilivyotokea jana jioni (Oktoba 16 mwaka
huu).
Angetile Osiah, Katibu Mkuu wa TFF
Rusumo FC ilikuwa ikitoka
kwenye mechi ya michuano ya Polisi Jamii Wilaya ya Ngara ambapo ikiwa njiani
kurudi Rusumo kutoka mjini Ngara ilipata ajali ya gari na wachezaji watano
kufariki papo hapo.
Wachezaji wengine ambao ni
majeruhi wamelazwa Hospitali ya Wilaya ya Ngara ya Murugwanza huku wawili hali
zao zikiwa mbaya.
Msiba huo ni pigo kwa
familia za marehemu, klabu ya Rusumo FC, Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya
Ngara (NDFA), Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Kagera (KRFA) na familia ya
mpira wa miguu kwa ujumla nchini kutokana na mchango wa wachezaji hao katika
ustawi wa mchezo huu kupitia klabu yao.
TFF inatoa pole kwa familia
za marehemu, Rusumo FC, NDFA na KRFA na kuwataka kuwa na uvumilivu katika
kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Kutokana na msiba huo, mechi zote za Ligi
Kuu ya Vodacom zinazochezwa leo (Oktoba 17 mwaka huu) kutakuwa na dakika moja
ya maombolezo ili kutoa heshima kwa marehemu hao. Mungu aziweke roho za
marehemu mahali pema peponi.
No comments:
Post a Comment