MGODI UNAOTEMBEA
Na Kambi Mbwana, Dar
es Salaam
WASWAHILI ni wajuzi sana
wa maneno. Katika kipindi cha maisha yao,
walijikita katika kubuni misemo ambayo mingi kati yao imekuwa na mashiko wakati wote. Hata kama
ukiishiwa nguvu, lakini ukiumbuka mmoja wapo, nguvu za ziada huibuka.
Mwasisi wa CCM, Mwalimu Julius Nyerere
Angalia msemo huu. Kwenye nia pana njia. Msemo huu
unatufundisha kuwa chochote tunachohitaji kufanya, lazima tuweke nia maana
itazalisha njia ya kufanikisha dhamira hiyo kwa kila binadamu anayeandamwa na
vikwazo.
Ridhiwan Kikwete
Mwenda pole hajikwai. Msemo huu unatufundisha kufanya kazi
zetu kwa utulivu bila kuacha papara, ndio maana hapo pia ukatungwa msemo
mwingine wa haraka haraka haina baraka.
Sio lengo langu kuoredhesha misemo ya wahenga, maana ni mingi
na haiwezi kujaa kwenye ukurasa wote huu wa Mgodi Unaotembea. Lengo langu ni
kuwambusha Watanzania juu ya mabadiliko ya kisiasa na wale wanaojiita ni
wanaharakati.
Wanaharakati ambao baadhi yao ni watunga uongo na uzandiki bila ukomo.
Wanaharakati wa Tanzania,
wengi wao wanapotunga hasidi zao, wanashindwa kuupangilia ili uonakane una
ukweli japo kwa asilimia chache.
Kwa wiki kadhaa sasa kumekuwa na maoni mbalimbali ya juu ya
uchaguzi wa ndani wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Uchaguzi huo umebadilisha hisia
za wanaharakati na kuanza kuleta porojo mahali ambako si mahali sahihi.
Watu hao wanahoji uhalali wa watoto wa vigogo kuingia kwa
wingi katika uchaguzi huo. Ati wameihodhi CCM na kuifanya ya kindugu. Hapo
yanasemwa maneno mengi, akitajwa Rdhiwan Kikwete, kama
mfano wa wanachama hao.
Wanaharakati hao waliandika meseji
na kutuma kwa kila wanayehisi kuwa hajaelewa somo la mabadiliko yasiyojengwa
kwa hoja na watu hao.
"HATARI: Angalia watoto wa
vigogo waliopita UVCCM ngazi ya Taifa; Dickson Membe, Fredy Lowassa, Ridhiwani
Kikwete, Ashura Hussein Mwinyi, Beny Samuel Sitta, Debora Mwandosya, Irene
Pinda, Felister Ndugai, Chrisopher Ndejembi, Sharifa Bilali, Hawa
Kigoda, Judith Mukama, na Jerome Msekwa.
“Nchi imekwisha, inatia hasira, wacha watoto wa masikini
tupambane kupitia mlango mwingine, "CHADEMA" ili kutetea masikini
wenzetu, wazazi na wadogo zetu. Vita hii inaanza sasa upatapo meseji hii tuma
kwa wazalendo wenzako,” mwisho wa ujumbe huo na kumalizia kuwa aliyetuma meseji
hiyo ati ni mwanaharakati.
Hizi ni meseji za kijinga mno. Na wenye akili timamu
hawawezi kubabaishwa nazo, maana zimebuniwa kwa nia ya kujiridhisha kuwa
utakaowaingia wanaweza kuwaelewa, hata kama
sababu zao ni ndogo mno.
Kwanini nasema hivi? Kwangu mimi siwezi kubabaishwa na jina la
mtoto wa kigogo katika sehemu husika, kama
lengo langu ni kugombea mahali Fulani. Tena ndio kwanza naona raha juu ya
kupambana na mtu huyo.
Mtoto wa kigogo hakatazwi kuwa mwana CCM kama
walivyokuwa wapinzani na kushika nafasi mbalimbali za vyama vyao. Ila
sitamuelewa mtoto wa kigogo nitakapobaini kuwa anakwenda kinyume au ni mwizi.
Yani, anatumia nafasi yake vibaya kwa ajili ya kujitajirisha
mwenyewe. Sina ugomvi na Ridhiwan ati kwasababu ameamua kuchukua fomu za
kuwania ujumbe wa CCM. Kila mmoja ana haki na wajibu sawa wa kuchagua na
kuchaguliwa.
Naandika makala haya kama
mwanzo wa kuwaelimisha hao wanaharakati na wasiokuwa wanaharakati juu ya
kutetea wanachokiamini. Hakuna haja ya kubabaishwa na jina la mtoto wa kigogo
hata kama tunajua ghiriba inaweza kufanywa
wakati wowote.
Tangu uchaguzi huo wa CCM ulipoanza kutimua vumbi katika
mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani, majina mapya nay a zamani
yameingia. Tena, wapo ambao hawakutarajiwa lakini hatimae wameibuka na ushindi.
Unaotakiwa kujengwa ni ujasiri na kujituma hadi mwisho wake.
Lolote kwenye uchaguzi linaweza kutokea na sio kulalama kuwa ni wengi watoto wa
vigogo.
Mjini Nachingwea, kijana wa kidato cha sita, Fadhili Liwaka
ameweza kumuangusha Waziri wa Sheria na Katiba wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mathias Chikawe katika uchaguzi wa CCM.
Hawa walikuwa wanawania nafasi moja ya Ujumbe wa Halmashauri
Kuu ya CCM, Nachingwea mkoani Mtwara, huku matokeo hayo yakishangaza wengi.
Chikawe mwenyewe hakujua kwamba angeweza kuangushwa na kijana huyo.
Kama Liwaka angekuwa mwoga kama wanavyowaaminisha hawa
wanaharakati, sidhani kama angekuwa na ujasili
wa kupambana na kigogo huyo wa Serikali ya Jakaya Mrisho Kikwete, ukizingatia
kuwa ana nafasi kubwa.
Kwa bahati mbaya, mbinu inayoganywa na wapinzani ni kueneza
sumu hata zile ambazo hazina kichwa wala miguu. Kukaa na kufikiria haya ni
kuishiwa hoja. Wangapi wanarithi kazi za wazazi wao na bado halisemwi?
Mbona wapo wazazi madaktari na watoto wao nao wanaingia
kwenye sekta hiyo? Wangapi ni walimu na watoto wao ni walimu? Au wanaharakati
wanaona kwenye siasa tu? Hizi ni sababu zisizokuwa na mashiko hata kidogo.
Nitawaona wanaharakati wana akili timamu watakapowajengea
uwezo wa kupambana na majina hayo na sio kuwaaminisha kushindwa. Mwanaharakati
makini ni yule anayepanga kila mbinu kuweza kukabili vishindo hivyo.
Tena, haya majina yanayooogopwa ni ya kawaida kabisa. Mtu
unaweza kujieleza vizuri na bado mtoto wa Kikwete, Mwinyi wakakosa nafasi hiyo.
Hata kama wakipata leo, lakini uchaguzi utakaofuata watashindwa tu.
Kikwete ndio kipindi chake cha mwisho hiki. Huenda kama
uwepo wake umewafanya watoto wake wapewe nafasi basi wakaikosa katika uchaguzi
ujao. CCM sio mali
ya mtu mmoja. CCM ni mali
ya kila mmoja.
Ila kinachofanywa ni kupeana zamu katika nafasi hizo, maana
wote hawawezi kuwa viongozi wa chama na serikali. Ili
mmoja wao apewe nafasi, ni lazima awashawishi wajumbe ili wampigie kura.
Huo ndio ukweli. Kila mmoja wetu anapaswa kuwa makini katika
nyendo zake na harakati zenye ushawishi na dhamira za kweli. Wapambanaji
wasiamgalie nani ni mtoto wa kigogo au nani wa mkulima, maana wote wana haki
sawa.
Wasiamgalie jina la mtoto wa Kigoda na wengine. Na kama huo
ndio utaratibu wao, basi unapaswa kukoma kama lengo
lao ni kukipa nguvu chama chao na sio kuendeshwa ovyo kisa watu Fulani wanataka
mabadiliko ya kisiasa.
Sio kila tunaloambiwa na wanaharati tunataka kuliweka
kichwani, maana hakika mengine hayana kichwa wala miguu. Mwanaharakati anataka
kuwakomboa watu wake, lakini bado anawaaminisha kuwa hakuna linaloweza
kufanikiwa kama vigogo wataachwa watoto wao.
Wanasahau kuwa wapo vigogo ambao nao wanahitaji nafasi hizo
za chama nab ado wanakosa baada ya kuangushwa kwenye chaguzi hizo. Nakerwa sana na mwenendo huo. Mtu
aliyenitumia meseji hiyo nilimlaumu kupita kiasi.
Akili yake huenda ina matege. Anafanya siasa nyepesi ama
rahisi. Haina tija kwake na Taifa kwa ujumla. Kwa bahati mbaya, akiambiwa
ukweli mtu wa aina hiyo, atawaka kwa hasira. Atajiona yeye ndio kila kitu,
wakati sio mkweli.
Atajiita yeye ni mjuzi wa kila jambo akilingia vyeti vyake
ambavyo huenda amevipata kwa ujanja ujanja kama wafanyavyo baadhi yao. Hapana. Huu sio
mwendo sahihi na lazima Watanzania na wale wanaharakati wajifanyie mabadiliko.
Huwa simpendi mtu asiyejiamini. Mtu ninayempenda ni yule
anayeona anaweza kupata kile anachotaka hata kama
kuna vizingiti vya kila aina. Hayo ndio maisha mazuri. Katika hilo, nami najifunza kuacha woga katika kile
ninachokitaka na kukiamini.
Mawazo haya yaenee kwa kila mmoja wetu. Tusiangalie vigogo
waliopo kwenye Chama tawala CCM, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Chama Cha Wananchi (CUF) na wengineo maana siku zote kwenye ukweli uongo
hujitenga.
Baada ya kusema hayo, naomba nikuage msomaji wangu wa Mgodi
Unaotembea na tukutane tena wiki ijayo katika dhmira ya kweli ya kujenga nchi
kwa kushirikiana sote bila kuangalia nani Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi au CCM.
Ndugu msomaji wangu mpendwa. Sasa unaweza kujadili na mimi
mambo mbali ya kisiasa katika group la Handeni Kwetu, ambao ni uwanja mpana
zaidi, baada ya huu Mgodi Unaotembea unaotoka kila Jumatano katika Gazeti lako
la Mtanzania.
Ndudu msomaji wangu mpendwa. Sasa tunaweza kukutana katika uwanja mpana zaidi, kwenye group la face book linaloitwa Handeni Kwetu na kuchambua mambo mbalimbali ya kisiasa, kimichezo na kiutamaduni na naomba uwe pamoja nami.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment