Nyosh Al Sadaat
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WAZEE wa Ngwasuma, FM Academia, kesho Jumamosi wanafanya shoo ya aina
yake katika Ukumbi wa Kijiji Cha Makumbusho, uliopo Kijitonyama, jijini Dar es Salaam,
huku wakipania kuwapa burudani za aina yake mashabiki wao.
Onyesho hilo
linafanyika huku bendi hiyo ikitamba na nyimbo mbalimbali, ukiwamo ule wa
Otilia, wimbo unaopendwa vilivyo na mashabiki wao katika kumbi wanazokuwapo
wakali hao wa dansi nchini.
Akizugumza jana jijini Dar es Salaam,
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Kelvin Mkinga, alisema kwamba mashabiki wao
waende kwa wingi kujionea manjonjo yao
katika tasnia hiyo nchini.
Alisema wanamuziki wao wamekuwa wakifanya shoo za aina yake,
wakiwa na lengo la kuonyesha makali yao, hivyo
mashabiki wao waendelee kupokea burudani safi
kutoka kwa vijana wao.
“FM Academia ni bendi kongwe na imara sana katika tasnia ya muziki wa dansi hapa
nchini, hivyo naamini mashabiki wetu wataendelea kutuunga mkono kwa ajili ya
kuwapatia burudani zaidi.
“Naamini sisi ni wakali na hatuna mpinzani, hivyo jukumu
letu ni kufanya kazi nzuri zaidi kwa kutunga nyimbo na kuandaa shoo za aina
yake, ukizingatia tuna watu mahiri kuanzia waimbaji hadi wanenguaji,” alisema
Mkinga.
FM Academia ipo chini ya Rais wa Vijana, Nyosh Al Sadaat,
sambamba na wakali wengine, akiwamo Patchou Mwamba, ambaye pia ni mkali katika
tasnia ya filamu hapa nchini, akishiriki katika filamu mbalimbali.
No comments:
Post a Comment