Mc Donald Mwakamele wa pili kutoka kulia waliosimama mstari wa mbele
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KUKUA kwa maendeleo ya Teknolojia, kunawafanya binadamu
wengi kuendelea kuumiza kichwa kwa ajili ya kuufaidisha ulimwengu kwa namna
moja ama nyingine.
Watu wengi, wakiwamo wana taaluma wa aina mbalimbali,
wamekuwa wakikaa na kusumbua vichwa kwa ajili ya kubuni au kuendeleza yale
yanayoweza kuikomboa Dunia katika vitu vya aina aina.
Licha ya Dunia kupiga hatua katika maendeleo ya sayansi na
teknolojia, lakini kwa Watanzania, imekuwa vigumu kuona ndugu zao wamefanikiwa
kugundua vitu ambavyo baadaye vitakuwa tegemeo la Dunia.
Ndipo hapo kila kitu utakuta kimebuniwa na watu wa nchi
zilizoendelea, huku sisi tukiwa hodari wa kutumia teknolojia hizo kwa gharama
kubwa.
Mc Donald Mwakamele akiwa juu ya nguzo
Wakati naendelea kuwaza hayo, nashangazwa na hatua ya
Mtanzania mwenzetu, Donald Mwakamele, anayejenga chuo cha Mc Donald Live Line
Training Centre, katika mji wa Dakawa, wilaya ya Mvomelo, mkoani Morogoro.
Ni chuo cha kisasa kitakachojishughulisha na masuala ya
kutengeneza bila kuzima umeme, hasa ikizingatia kwa sasa Taifa linakabiriwa na
matatizo mengi yanayosababisha muda mwingi kuwa gizani.
HANDENI KWETU ilitembelea eneo la chuo,
ambapo pia siku hiyo, wakati ambao wageni kutoka kutoka nchi mbalimbali duniani
walikwenda kujifunza namna chuo hicho kitakavyofanya kazi zake.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete
Mmiliki na Mkurugenzi Mkuu wa chuo hicho, Mc Donald
Mwakamele, anasema anaingia kwenye teknolojia hiyo, huku akiwa na mwarobaini wa
umeme wa uhakika miaka michache ijayo.
Teknolojia hiyo ya umeme, inaingia huku ikiwa ngeni katika
nchi nyingi duniani, zikiwamo za Barani Afrika, ambazo zinaendelea kutengeneza
umeme usiokuwa wa uhakika, pamoja na kuzima bila sababu za msingi.
“Kwa mfano, hapa naweza kuchomoa kikombe chochote katika
mitambo iliyopo hapa na jamii inayopata umeme kutokana na njia hii, kamwe
haiwezi kuathiriwa na ukarabati huu ambao hapo kabla ulikuwa mpaka wazime
umeme.
“Hii Dunia ya leo inahitaji ubunifu wa hali ya juu, ndio
maana nikaona ipo haja ya sisi watu tulioingia katika mambo haya ya mitambo ya
umeme, kuwa makini mno na kubuni mbinu mbadala za kusaidia tatizo la umeme,”
alisema Mwakamele.
Mwakamele aliyewahi kuwa mfanyakazi wa Shirika la Umeme
Tanzania Tanesco, anasema wazo hilo la chuo cha
umeme, limetokana na kuendeleza mawazo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Jakaya Mrisho Kikwete.
Miaka ya 1988, Jakaya Kikwete, alikuwa na mawazo ya Tanzania
kuwa na chuo cha namna hiyo, kitakachokuwa kinafundisha masuala ya umeme, hasa
teknolojia ya kutengeneza bila kuzima umeme.
Chuo cha namna hiyo kinahitaji mtaji mkubwa, ndio maana kwa
upande kimechukua muda mrefu kuweka mipango na mikakati ya kufanikisha suala
hilo, huku akiamini kufanikiwa kwa teknolojia hiyo, ni msaada mkubwa kwa vizazi
vya leo na kesho vinavyokabiriwa na matatizo ya umeme.
Kwa kuanzia, chuo hicho kitafundisha wakurugenzi, maprofesa na
wengineo, kwa ajili ya kuwapa makali zaidi, ili waende kutoa elimu hiyo katika
sehemu zao za kazi.
Baada ya hapo, elimu hiyo itaanza kutolewa kwa watu wa
kawaida, bila kuangalia elimu zao, maana suala la ufundi, linahitaji vichwa
zaidi pamoja na wale wenye uthubutu wa kufanya kazi.
Hata hivyo, katika kuangalia nani anaweza kuingia kwenye
chuo hicho, kutahitaji kwanza vipimo vya wanafunzi hao, ukizingatia kwamba lengo
lake haswa ni kuendeleza taaluma hiyo ya
umeme.
“Tangu niache kufanya kazi katika shirika la umeme la
Tanesco, mengi nimegundua ikiwamo watu kushindwa kujifunza zaidi, badala yake
wanafanya mzaha na kuendeleza majungu sehemu za kazi.
“Hayo yamesababisha Taifa lishindwe kuendelea, ndio maana
Tanesco ya leo inachojua wao ni kuzima umeme bila sababu za msingi, bila kujua
hasara kiasi gani inapatikana kwa kuzima umeme japo kwa nusu saa tu,” alisema.
Mwakamele anasema katika mwendelezo wa chuo hicho, taaluma
hiyo ya umeme itaendelezwa zaidi, ikiwamo kufua umeme wa kutokana na jua (solar
panel), akiamini kuwa huo pia utasababisha huduma hiyo kuwa ya rahisi zaidi.
Ili mteja apate umeme,
anahitaji kuwa na fedha nyingi, huku Shirika lenyewe likiendeshwa bila mipango,
jambo ambalo anaamini Mc Donald Training Centre litaondosha matatizo hayo.
Kufanikisha mikakati hiyo, kutalisaidia Taifa, maana bila
umeme wa uhakika, nchi haiwezi kupiga hatua katika masuala mbalimbali, yakiwamo
uchumi, unaohitaji kuwa na viwanda vinavyoendeshwa na umeme.
Hadi sasa, Chuo hicho kimetumia zaidi ya Sh Milioni 900,
huku taratibu za usajili zikitarajiwa kuanza hivi karibuni.
Mwakamele, anasema utaalamu wake na elimu yake imetokana na
kusomeshwa na serikali, ambayo leo anapanga namna ya kuinufaisha kwa teknolojia
hiyo.
Mbali na kuanzisha chuo hicho, Mwakamele anamiliki Kampuni
ya Mc Donald Live Line Technology Ltd. Injinia huyo anasema, ni budi wataalamu
wote wanaohusika na mambo ya umeme kuichukia tabia ya kuzima nishati hiyo
inayosababisha Taifa kupata hasara kubwa.
Kutokana na kadhia hiyo, kampuni mbalimbali pamoja na watu
wa majumbani wamekuwa wakipata hasara, hasa pale kifaa kinapoungua kutokana na
umeme kukatika, eti kwa sababu ya matengenezo ya Tanesco.
“Taifa linaweza kutoka huko, ndio maana leo nimepokea ugeni
kutoka nchi mbalimbali, wakija kwa nia ya kujifunza juu ya hili, ukizingatia
kwa sasa napenda kutoa elimu tu, huku uinjinia nikiachia watu wengine nje au
waliokuwa kwenye kampuni yangu ya Mc Donald Live Line Technology Ltd inayopiga
hatua kubwa zaidi kwa kushuhudia ugunduzi huu mpya.
“Katika hili, naomba jamii iendelee kuniunga mkono huku wale
wasionitakia mema wakikaa chonjo, maana nimeingia kwa kasi na siwezi kuogopa
hujuma na vitisho kutoka kwa wapinzani wangu, kwakuwa lengo si kuonyeshana
umwamba, bali ni kutangaza vipaji na uwezo wa kufanya kazi kwa ajili ya
Tanzania yetu,” alisema.
Kwa mujibu wa Mc Donald, ugeni wake kwenye chuo hicho
ulitembelea Septemba 13 ingawa njia ya kupeleka umeme kwenye eneo hilo zilizimwa kwa sababu ya matengenezo mafupi, kama walivyosema Tanesco, hivyo kuwafanya watu hao
wasionyeshwe teknolojia hiyo, zaidi ya kushuhudia mitambo ya aina mbalimbali
iliyofungwa katika chuo hicho.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment