BABA WA TAIFA
Nyerere
asingekufa kwa maradhi, angeuliwa na CCM
Na Kambi Mbwana, Dar
es Salaam
LEO ni Oktoba 14. Tanzania nzima inaingia katika kumbukumbu
ya kifo cha mwasisi wa Taifa hili, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere, aliyekufa Oktoba 14, mwaka 1999 nchini Uingereza alipokwenda kwa
matibabu.
Kwa mujibu wa madaktari wake, Nyerere mtu muhimu kabisa
katika Taifa hili, alikufa kwa maradhi ya kansa ya damu (leukemia), akiwa
katika harakati nyingi za kuokolewa maisha yake, katika Hospitali ya St Thomas, London,
Uingereza.
Kifo chake kilitetemesha wengi, wakiwamo wanachama wa Chama
cha Mapinduzi (CCM) na wale wasiokuwa na vyama vya siasa. Katika kuiangalia
kumbukumbu yake, naweza kusema kifo chake kitaendelea kuwa pigo hasa kwa CCM.
Chama ambacho licha ya kukipenda na kukiheshimu kupita
kiasi, kimegeuzwa na wachache wao, walioamua kuja kufanya biashara kwa mgongo
wa kisiasa.
Nathubutu kusema kwamba, uhakika wa kuendelea kuishi kwa
baba wa Taifa, ungekuwa mdogo mno kwa mwenendo wa CCM kuanzia miaka ya 2000
hadi muda huu.
Kama asingeshikwa na
maradhi hayo, basi ni dhahiri msiba huo ungekuwamba, huku sababu kubwa ikiwa
siasa chafu, rushwa ya uchaguzi, hasa ndani ya CCM, sambamba na siasa za
makundi na kushughulikiana wao kwa wao.
Nyerere, asingeweza kudumu, maana watu anaowaamini wanageuka
na kuvaa joho la ukatili, wakiwa ndani ya chama kilichounganisha watu wengi.
Chama ambacho kwa namna moja ama nyingine, kimeundwa kwa jasho la walalahoi.
Watu ambao kwa miaka 35 sasa, maisha yao, uhuru wao ni mdogo mbele ya matajiri
wachache wanaoingia kulangua kwenye siasa. Kwanini nasema hivyo. Nyerere kwa
mtazamo wake, alisema bila CCM nchi hii itayumba.
Aliyasema haya kwa imani kubwa aliyokuwa nayo kwa Watanzania
na mbele ya chama chake hicho cha CCM,
ambacho kwa sasa kipo chini ya Mwenyekiti wake, Jakaya Mrisho Kikwete.
Hali ya mambo inavyoendelea, uwezekano wa CCM kutawala
milele ni mdogo mno. Kumekuwa na mabadiliko makubwa ya upepo wa kisiasa. Chuki
za wazi wazi ndani ya uongozi wa chama hicho kikongwe zimetamalaki.
Uhai wake ungekuwa mdogo mno. Watu wanageuka na kufanya
siasa zisizokuwa na tija kwa CCM na bado wanachekewa. Wenye maono yao wanatembea na kusema
vibaya juu ya kauli za Nyerere, wakisema hazitakiwi kufuatwa.
Kinachofuata sasa ni kuona kejeli za wazi wazi kwa baba wa
Taifa, maana waliobakia kwenye mfumo wa chama, hawana mawazo mazuri ya
kukitetea chama mbele ya umati wa watu wanaona kwamba chama kimezeeka na
kinatakiwa kufa.
Wale ambao wanatembea kwa matao wakisema kifo rasmi cha CCM
ni mwaka 2015. Wanasema kaburi lake
limeshaandaliwa. Hizi ni
kejeli ambazo nachelea kusema kuwa zingemfurahisha Nyerere, hata kama leo angekuwa hai.
Hizo tu na nyingine nyingi zingempa presha na jaka moyo,
hivyo uhai wake kuwa mdogo mno. Kama huo sio ukweli,
basi upo mbali na uongo. Nikiwa kama
Mtanzania, naheshimu kwa dhati mchango wa Baba wa Taifa.
Amefanya mengi mazuri, ikiwamo kuruhusu kwa kauli moja mfumo
wa vyama vingi vya siasa, kama ishara nzuri ya
kukua kwa Demokrasia ndani ya nchi hii ambayo kwa sasa inaendelea kutafunwa na
mchwa aliowasema.
Mchwa hao wamekuwa wakijenga mtandao wao kwa njia za hatari
mno. Wengine wanafika mbali kwa kuingia ubia na wafanyabiashara wakubwa kwa
ajili ya kuitafuna nchi hii.
Watanzania masikini hawana haki tena. Kila kinachofanyika ni
usanii mtupu. Bado tu hiyo suio dalili za kuangamiza roho za wapendwa wetu? Je,
Nyerere angechekea haya yanayofanyika sasa, ikiwamo fedha kutumika nyingi hata
kwenye chaguzi za ndani?
Wanataka nini? Mgombea kumwaga noti katika Uchaguzi wa Umoja
wa Vijana CCM, (UVCCM) anatafuna nini? Fedha hizo anazitoa wapi na ili apate
nini? Chama kimehamshwa kutoka kwa wakulima na wafanyakazi na kuingia kwenye
mikono ya walanguzi, wafanyabiashara wakubwa wenye malengo yao kisiasa.
Ukifanya hesabu za wafanyabiashara wakubwa wanaoingia kwenye
siasa utachoka. Ni wengi mno. Kila mtu humo ni mwanasiasa na mgongo wake ni
CCM. Hao ndio wanaoharibu mfumo mzima wa CCM, ingawa wakiambiwa watabisha.
Tuambiane ukweli hata utatuuma. Tusidanganye kuwa tunamuenzi
Nyerere wakati mambo yanaendeshwa kienyeji na wajanja wachache wananufaika. Huo
ndio ukweli wa mambo.
Kila mmoja awe na nia ya kuwakomboa Watanzania wenzake kwa
kutumia fursa mbalimbali zinazopatikana na rasilimali zilizopo. Kama madini yetu yanachimbwa na sisi kuambulia mashimo,
bado tunamuenzi Nyerere?
Kama wazee wetu wasiokuwa
na elimu waliwabaini wajanja, watumia nguvu zao vibaya, wakoloni na kuwatimua,
vipi wasomi wa leo wanawaingiza kwa mgongo wa uwekezaji?
Elimu yao
ipo wapi na inatumika vipi kuwakomboa watu wote. Hili lazima lisemwe hadharani
kwa ajili ya kujenga haki ya kila mwananchi. Tanzania hii sio ya watu wachache
wanaonufaika na familia zao, huku walalahoi wakiendelea kushinda njaa.
Kwa bahati mbaya, haya yanatokea wakati serikali ipo chini
ya CCM, chama ambacho mwasisi wake, Nyerere alikitabiria kutawala milele kwa
kusema bila hicho nchi itayumba. Kama hivyo ni kweli, ina maana Rais huyo wa
Kwanza wa Tanzania,
hajajua kuwa kuna siku hali itakuwa mbaya kwa chama chake.
Kwa wataalamu wa mambo ya siasa wanajua kuwa bila chama cha
Mapinduzi chini ya Kikwete kukaa na kuangalia tatizo, uwezekano wa kushinda
katika chaguzi tatu zijazo, yani mwaka 2015, mwaka 2020 na 2025 ni mdogo mno.
Na hilo likitokea, basi damu
nyingi itamwagika kama inavyomwagika sasa,
maana wenye nia ya kutawala wamekuwa wakipakaza sumu na kushitaki kwa nguvu ya
umma (wananchi), wakisema CCM imeshindwa kuwakomboa Watanzania kwa kuwaacha
kwenye madhira ya umasikini huku viongozi wao wakila raha na familia zao.
Nadhani kwa kupitia kumbukumbu ya kifo cha mwalimu Nyerere,
Watanzania na viongozi wa Taifa hili, wakiwamo wana CCM wana kila sababu ya
kujitazama upya kama kweli wanahitaji kumuenzi
mwenyekiti wao wa zamani.
Wafanyie kazi ushauri wake, uongozi wake na sera zake zilizotukuka
badala ya kusema kwenye vijiwe vya siasa, wakati chama chao kinayumba. Kuna
mchambuzi mmoja, aliwahi kuandika katika makala yake, Nyerere akifufuka leo
anakufa tena.
Najaribu kuyaelewa mawazo yake, maana akifufuka leo, atakuta
CCM mpya yenye kila aina ya uozo, huku dalili za kubaki madarakani kwa miaka
mingi ijayo ikikosekana, kama hali itaendelea kuwa kama
ilivyokuwa sasa.
Wakati ni huu. Bado CCM imara, Taifa imara linawezekana kwa
kuangalia makosa yao, mapungufu yao kwa ajili ya kusonga
mbele na sio kurudi nyuma wala kubaki lilipo.
Mungu ibariki Tanzania.
0712 053949
0753 806087
Mwisho
No comments:
Post a Comment