Mwenyekiti wa Kamati ya Gurumo 53, Asha Baraka, akizungumza
jambo mbele ya wadau na waandishi wa habari alipokuwa akitangaza rasmi shoo
mbili za kumuaga mwanamuziki mkongwe Muhidini Gurumo kushoto kwake. Shoo ya
kwanza itafanyika Oktoba 11 katika Ukumbi wa Diamond Jubilee (VIP), ikifuatiwa
na ile ya TCC Sigara Chang'ombe, Novemba Mosi mwaka huu.
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MWANAMUZIKI mkongwe aliyestaafu kuimba akiwa na bendi ya Msondo Ngoma, Muhdini Gurumo, ameandaliwa shoo mbili
za kumuaga, moja wapo ikipangwa kufanyika Oktoba 11, ikiwa ni VIP, huku
ikifanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.
Nyingine itafanyika Novemba Mosi mwaka huu
katika Ukumbi wa TCC Sigara Chang’ombe, jijini Dar es Salaam, zote zikiwa na
lengo la kumuaga kwa heshima mwanamuziki huyo na kumpa nafasi ya kuyamudu maisha
yake baada ya kuachana na muziki.
Mdau wa muziki wa dansi nchini, Deo Mutta Mwanatanga,
akizungumza jambo mbele ya wadau na waandishi wa habari katika mkutano huo na
juu yake akiwa amepiga picha ya pamoja na Gurumo kulia pamoja na Chidumule
kushoto kwake kama ukumbusho wake kwa kupata bahati ya kupiga picha na wajuzi
wa muziki huo nchini.
Juma Mbizo, ambaye ni mratibu wa Kamati ya Gurumo 53
aliyeshika cd, akiwaonyesha waandishi wa habari leo mchana katika Mkutano wao
kutangaza shoo mbili za kumuaga rasmi Muhdini Gurumo, aliyetangaza kuachana na
muziki wa dansi hapa nchini. Kushoto kwa Mbizo ni Cosmas Chidunumule,
mwanamuziki mkongwe aliyeachana na muziki wa Kidunia (ameokoka), akiafutiwa na
Said Kibiriti, moja ya viongozi wa bendi ya Msondo Ngoma. Kulia kwa Mbizo ni
Muhdini Gurumo na Asha Baraka, ambaye ndio mwenyekiti wa Kamati hiyo.
Wadau wakiendelea na mjadala wa kuitangaza siku ya tukio la
kumuaga rasmi Muhdini Gurumo baada ya kustaafu muziki wa dansi akiwa na bendi
ya Msondo Ngoma. Aliyebeba laptop kulia ni Katibu wa Kamati hiyo, Said Mdoe,
ambaye pia ni Mkurugenzi wa Screen Masters, akiafutiwa na Richard Sakala,
Mjumbe, Asha Baraka mwenyekiti wao, Gurumo, Juma Mbizo mratibu, Cosmas
Chidumule mjumbe na Said Kibiriti, Mjumbe wa Kamati inayojulikana kama Gurumo 53.
Baadhi ya wadau wa muziki wa dansi hapa nchini, Deo Mutta
Mwanatanga, akiandika baadhi ya vitu vilivyokuwa vinazungumzwa katika kutangaza
shoo mbili za kumuaga mwanamuziki Muhdini Gurumo, italayofanyika Oktoba 11
mwaka huu katika Ukumbi wa Diamond Jubilee na ile ya Novemba Mosi mwaka huu
katika Ukumbi wa TCC Sigara Chang'ombe.
Akizungumza leo na waandishi wa habari,
Mwenyekiti wa shoo hiyo iliyopewa jina la (Gurumo 53), Asha Baraka, alisema
kuwa ni heshima kuwa na mwanamuziki kama Gurumo, hivyo wadau wameamua kuandaa
shoo hizo za kumtafutia fedha mkali huyo.
Alisema wazo hilo limefanyiwa kazi kwa
pamoja, akiwa na wadau kadhaa, akiwamo Said Mdoe Katibu wa Kamati hiyo, Richard
Sakala mjumbe, Cosmas Chidumule, Waziri Ally, Said Kibiriti na Juma Mbizo,
ambaye ndio mratibu wa Kamati hiyo.
“Lengo si kumpa karatasi za kuthamini
mchango wake katika tasnia ya muziki wa dansi Tanzania, ila kuhakikisha kuwa
anapata mwangaza wa maisha yake baada ya kuachana na muziki.
“Huyu ni mwanamuziki mwenye uwezo wa juu
wakati huo, hivyo kwa sasa lazima sisi wadau tuhakikishe anajiweka katika
ramani nzuri, ikiwa ni kutambua ataishi vipi nje ya muziki,” alisema.
Naye Gurumo aliwaambia waandishi wa habari
kuwa ameamua kuachana na muziki kwasababu umri na afya yake hairuhusu kufanya
kazi hiyo, hivyo asitokee mtu wa kupotosha ukweli wake huo.
“Nasikia watu wanasema naachana na muziki
Msondo nikiwa na lengo la kurudi tena Sikinde, jambo ambalo si kweli kwakuwa
sioni nitamuimbia nani wakati nimechoka.
“Naomba kwa sasa kuwapa nafasi watu
waliojitolea kunisaidia hasa kwa kuunda kamati hii ambayo nitapanda jukwaani
kuimba mara ya mwisho, ukizingatia kuwa kazi yangu inahitaji kuagana na
mashabiki wangu jukwaani na si mahali pengine,” alisema.
Katika hatua nyingine, mwanamuziki Cosmas
Chidumule, alisema kuwa licha ya kuwa ameokoka, ila atapanda jukwaani kuimba na
mzee Gurumo kama sehemu ya kutambua mchango wake.
“Nimeokoka lakini si sababu ya kunifanya
nishindwe kumheshimu mwanamuziki ambaye nina uhakika mchango wake ulinifanya
niwe juu katika muziki wa dansi Tanzania,” alisema.
No comments:
Post a Comment