Pages

Pages

Thursday, September 12, 2013

Muhdini Gurumo aandaliwa shoo mbili za nguvu ili kumuaga kwa mkwanja



Mwenyekiti wa Kamati ya Gurumo 53, Asha Baraka, akizungumza jambo mbele ya wadau na waandishi wa habari alipokuwa akitangaza rasmi shoo mbili za kumuaga mwanamuziki mkongwe Muhidini Gurumo kushoto kwake. Shoo ya kwanza itafanyika Oktoba 11 katika Ukumbi wa Diamond Jubilee (VIP), ikifuatiwa na ile ya TCC Sigara Chang'ombe, Novemba Mosi mwaka huu.



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MWANAMUZIKI mkongwe aliyestaafu kuimba akiwa na bendi ya Msondo Ngoma, Muhdini Gurumo, ameandaliwa shoo mbili za kumuaga, moja wapo ikipangwa kufanyika Oktoba 11, ikiwa ni VIP, huku ikifanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.

Nyingine itafanyika Novemba Mosi mwaka huu katika Ukumbi wa TCC Sigara Chang’ombe, jijini Dar es Salaam, zote zikiwa na lengo la kumuaga kwa heshima mwanamuziki huyo na kumpa nafasi ya kuyamudu maisha yake baada ya kuachana na muziki.




Mdau wa muziki wa dansi nchini, Deo Mutta  Mwanatanga, akizungumza jambo mbele ya wadau na waandishi wa habari katika mkutano huo na juu yake akiwa amepiga picha ya pamoja na Gurumo kulia pamoja na Chidumule kushoto kwake kama ukumbusho wake kwa kupata bahati ya kupiga picha na wajuzi wa muziki huo nchini.




Juma Mbizo, ambaye ni mratibu wa Kamati ya Gurumo 53 aliyeshika cd, akiwaonyesha waandishi wa habari leo mchana katika Mkutano wao kutangaza shoo mbili za kumuaga rasmi Muhdini Gurumo, aliyetangaza kuachana na muziki wa dansi hapa nchini. Kushoto kwa Mbizo ni Cosmas Chidunumule, mwanamuziki mkongwe aliyeachana na muziki wa Kidunia (ameokoka), akiafutiwa na Said Kibiriti, moja ya viongozi wa bendi ya Msondo Ngoma. Kulia kwa Mbizo ni Muhdini Gurumo na Asha Baraka, ambaye ndio mwenyekiti wa Kamati hiyo.



Wadau wakiendelea na mjadala wa kuitangaza siku ya tukio la kumuaga rasmi Muhdini Gurumo baada ya kustaafu muziki wa dansi akiwa na bendi ya Msondo Ngoma. Aliyebeba laptop kulia ni Katibu wa Kamati hiyo, Said Mdoe, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Screen Masters, akiafutiwa na Richard Sakala, Mjumbe, Asha Baraka mwenyekiti wao, Gurumo, Juma Mbizo mratibu, Cosmas Chidumule mjumbe na Said Kibiriti, Mjumbe wa Kamati inayojulikana kama Gurumo 53.



Baadhi ya wadau wa muziki wa dansi hapa nchini, Deo Mutta Mwanatanga, akiandika baadhi ya vitu vilivyokuwa vinazungumzwa katika kutangaza shoo mbili za kumuaga mwanamuziki Muhdini Gurumo, italayofanyika Oktoba 11 mwaka huu katika Ukumbi wa Diamond Jubilee na ile ya Novemba Mosi mwaka huu katika Ukumbi wa TCC Sigara Chang'ombe.
 

Akizungumza leo na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa shoo hiyo iliyopewa jina la (Gurumo 53), Asha Baraka, alisema kuwa ni heshima kuwa na mwanamuziki kama Gurumo, hivyo wadau wameamua kuandaa shoo hizo za kumtafutia fedha mkali huyo.

Alisema wazo hilo limefanyiwa kazi kwa pamoja, akiwa na wadau kadhaa, akiwamo Said Mdoe Katibu wa Kamati hiyo, Richard Sakala mjumbe, Cosmas Chidumule, Waziri Ally, Said Kibiriti na Juma Mbizo, ambaye ndio mratibu wa Kamati hiyo.

“Lengo si kumpa karatasi za kuthamini mchango wake katika tasnia ya muziki wa dansi Tanzania, ila kuhakikisha kuwa anapata mwangaza wa maisha yake baada ya kuachana na muziki.

“Huyu ni mwanamuziki mwenye uwezo wa juu wakati huo, hivyo kwa sasa lazima sisi wadau tuhakikishe anajiweka katika ramani nzuri, ikiwa ni kutambua ataishi vipi nje ya muziki,” alisema.

Naye Gurumo aliwaambia waandishi wa habari kuwa ameamua kuachana na muziki kwasababu umri na afya yake hairuhusu kufanya kazi hiyo, hivyo asitokee mtu wa kupotosha ukweli wake huo.

“Nasikia watu wanasema naachana na muziki Msondo nikiwa na lengo la kurudi tena Sikinde, jambo ambalo si kweli kwakuwa sioni nitamuimbia nani wakati nimechoka.

“Naomba kwa sasa kuwapa nafasi watu waliojitolea kunisaidia hasa kwa kuunda kamati hii ambayo nitapanda jukwaani kuimba mara ya mwisho, ukizingatia kuwa kazi yangu inahitaji kuagana na mashabiki wangu jukwaani na si mahali pengine,” alisema.

Katika hatua nyingine, mwanamuziki Cosmas Chidumule, alisema kuwa licha ya kuwa ameokoka, ila atapanda jukwaani kuimba na mzee Gurumo kama sehemu ya kutambua mchango wake.

“Nimeokoka lakini si sababu ya kunifanya nishindwe kumheshimu mwanamuziki ambaye nina uhakika mchango wake ulinifanya niwe juu katika muziki wa dansi Tanzania,” alisema. 



No comments:

Post a Comment