Rais
wa TFF, Leodegar Tenga
|
MKUTANO Mkuu wa Uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) unatarajiwa kufanyika Septemba 29 mwaka huu baada ya ule wa
Dharura wa marekebisho ya Katiba ulipangwa kufanyika Julai 13 mwaka huu kumalizika.
Tarehe hizo zimepangwa na kikao cha dharura cha Kamati ya
Utendaji ya TFF kilichofanyika leo (Mei 9 mwaka huu) jijini Dar es Salaam chini
ya Rais wake Leodegar Tenga ambacho kulipokea rasmi maagizo ya
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na kupanga utekelezaji wake.
“Kamati ya Utendaji ya TFF imepokea rasmi barua ya FIFA na
kupanga utekelezaji wake. Tumepokea maagizo ya FIFA yanayotuelekeza cha
kufanya, si TFF wala mtu mwingine yeyote anayeweza kuongeza jambo lingine.
“Maagizo ni undeni Kamati ya Maadili, Kamati ya Rufani ya
Maadili, fanyeni marekebisho ya Katiba, anzeni tena uchaguzi, waliokuwepo na
wengine wapya waruhusiwe. Tumejitahidi kuhakikisha uchaguzi uwe kabla ya Oktoba
30 mwaka huu kama FIFA walivyotuagiza,” amesema Rais Tenga wakati akizungumza
na waandishi wa habari.
Amesema kazi kubwa itakuwa ni kutayarisha kanuni hizo, kwani
Kamati za Maadili lazima ziwe na kanuni zake na kuhakikisha kuwa hakuna
mgongano kati ya Kanuni za Nidhamu na Kanuni za Maadili.
Pia Rais Tenga amesema kuna kazi ya kuangalia jinsi
zitakavyoingia katika uchaguzi ambapo maana yake muda wa mchakato wa uchaguzi
utakuwa zaidi ya siku 40 za sasa, hivyo mabadiliko hayo yatagusa vilevile
Kanuni za Uchaguzi.
Kwa mujibu wa ratiba ya utekelezaji, rasmu ya mwanzo ya
Kanuni hizo inatakiwa iwe imetoka kufikia Mei 30 mwaka huu ambapo itapelekwa
FIFA kwa ajili ya kupata mawazo yao kabla ya kuendelea na hatua inayofuata.
Juni 15 mwaka huu Kamati ya Utendaji ya TFF itakutana
kupokea mapendekezo hayo ambapo baada ya kuyapitisha itayapeleka tena FIFA.
Taarifa (notice) ya Mkutano Mkuu wa Dharura ambayo kikatiba ni siku 30 itatolewa
Juni 12 au 13 mwaka huu.
Baada ya Mkutano
Mkuu wa Dharura wa marekebisho ya Katiba, Kamati ya Utendaji itakutana kati ya
Julai 14 na 15 mwaka huu kuunda Kamati ya Maadili na Kamati ya Rufani ya
Maadili ili kuruhusu mchakato wa uchaguzi uanze.
|
No comments:
Post a Comment