Mkurugenzi wa Twanga Pepeta, Asha Baraka
Na Kambi Mbwana, Dar
es Salaam
IKIWA ni mwezi mmoja sasa tangu alipojiondoa katika bendi ya
The African Stars, Twanga Pepeta, mwanamuziki na Rais wa bendi ya Victoria Sound,
Mwinjuma Muumini, ametunga kibao cha 'Shamba la bibi lina magugu', wimbo
unaotafsiriwa kama dongo kwa Mkurugenzi wa
Twanga Pepeta, Asha Baraka.
Wimbo huo aliuimba Muumini muda sio mrefu akiwa na
wanamuziki 19 wanaounda bendi yake hiyo, akiwamo Waziri Sonyo.
Mwinjuma Muumini (katikati), akitambulisha kikosi chake kipya kwa ajili ya mapambano ya muziki wa dansi, akiwa na bendi yake ya Victoria Sound. Mwenye cheni na mwili mkubwa ni Waziri Sonyo, mmoja wa wanamuziki wanaosubiriwa kwa hamu kwenye bendi hiyo kutokana na uwezo wake.
Akizungumza kwa furaha kubwa, Muumini alisema wimbo huo wa
Shamba la Bibi utakuwa moto wa kuotea mbali, huku akibaki anacheka baada ya
kuutakiwa kusema kuwa kweli wimbo huo amemtungia Asha Baraka.
Alisema harakati zake kwa sasa ni kuiweka juu bendi yake
hiyo, hivyo mashabiki wajiandae kupata
burudani kamili kutoka kwake, ingawa vionjo vya wimbo huo vinaonyesha kuwa
anamuimbia Asha Baraka, mmoja wa wadau makini wa muziki wa dansi nchini.
Mwinjuma Muumini, akiimba jukwaani.
“Huu wimbo nimeutunga kwa kufuata hisia na uwezo wangu,
ingawa najua watu watatafsiri kwa jinsi wanavyojuwa wao wenyewe, hivyo naomba
mashabiki wangu wawe makini juu ya hili, ukizingatia kwamba ni harakati za
kuniweka juu.
“Naamini watu watapata kitu kizuri kutoka kwangu, hivyo
Shamba la Bibi ni moto wa kuotea mbali na najua utawachoma wengi na kuwapa
mwanga mzuri, ikiwa ni harakati za kazi zangu katika maisha yangu ya muziki,”
alisema Muumini.
Muumini ameingia katika vita rasmi ya kuipaisha bendi yake,
akitangaza wanamuziki 19, akiwamo Sonyo, George Gama, Seleman Mumba, Jonas
Mlembeka, Moshi Hamis na wakali wengineo walioingia makubaliano ya kufanya kazi
na Victoria Sound.
No comments:
Post a Comment