Na Kambi Mbwana, Dara es Salaam
TIMU ya Mtibwa Sugar ya Morogoro leo asubuhi (Desemba
14 mwaka huu) imeibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Toto Africans ya Mwanza
katika mechi ya michuano ya Kombe la Uhai inayoshirikisha timu za vijana wenye
umri chini ya miaka 20 (U20) za klabu za Ligi Kuu ya Vodacom.
Juma Luzio alifunga mabao yote matatu (hat trick)
katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es
Salaam. Alifunga mabao hayo dakika za 44,81 na 88.
Hata hivyo, Toto Africans ndiyo walioanza kufunga
katika mechi hiyo ya kundi A. Bao hilo
katika michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa kupitia
maji Uhai lilifungwa dakjika ya 22 na Pastol Makula.
Nayo Simba imenguruma baada ya kuitandika Mgambo
Shooting ya Tanga katika mechi nyingine ya michuano hiyo iliyochezwa leo
asubuhi kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi. Wafungaji kwa washindi walikuwa
Ramadhan Mdoe dakika ya 19, Mohamed Salum dakika ya 77 na Ramadhan Singano
dakika ya 89.
Michuano
hiyo inaendelea leo mchana na jioni. Mechi ya Ruvu Shooting na Kagera Sugar
iliyokuwa ichezwe mchana Uwanja wa Azam, Chamazi sasa itafanyika saa 10 kamili
jioni katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.
Mechi
nyingine za leo ni Coastal Union vs JKT Ruvu
(mchana- Karume), African Lyon vs Azam (jioni- Chamazi). Vilevile mechi kati ya
JKT Oljoro na Yanga inachezwa leo Uwanja wa Chamazi.
Kesho
(Desemba 15 mwaka huu) ni mapumziko, na michuano hiyo itaendelea Jumapili
kwenye viwanja vyote viwili- Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume na Uwanja wa Azam-
Chamazi.
No comments:
Post a Comment