MKOA wa Morogoro, ukiwa chini ya Mkuu wake wa Mkoa, Joel
Bendera, jana ulizizima kutokana na kuwapo kwa mazishi ya msanii nguli wa Hip
Hop, Albert Mangweha (Ngwair), aliyozikwa katika makaburi ya Kihonda Kanisani,
mkoani hapa.
Afande Sele akizungumza jambo.
Sugu akizungumza na wasanii alipofika kuaga mwili wa Ngwair, Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Tukio la kuzikwa lilitanguliwa na shughuli ya uagaji
iliyofanyika pia katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, baada ya kuona
mkanyagano wa watu wengi nyumbani, usiku wa Jumatano, ambapo taarifa za
kuwasili kwa mwili
Kamati ya Mazishi, ikiwa chini ya wajumbe wake, akiwamo Adam
Juma, ilikubaliana haraka kuwa wapenzi wa muziki nchini wapate fursa ya kuaga
katika Uwanja wa Jamhuri na sio nyumbani kwao kutokana na ufinyu wa eneo hilo.
Huyu jamaa alilia sana katika kaburi la Ngwair, akiomboleza mengi, kama vile Ngwair wewe ulisababisha mimi nifeli shule ya Sekondari Mazengo, leo unaniacha peke yangu.
Mwanadada Wema Sepetu, akitafakari jambo katika kuagwa kwa msanii Ngwair.
Mji wa Morogoro ulianza kuzizima tangu asubuhi, baada ya
kushuhudia vikundi vya watu wengi vikielekea uwanja wa Jamhuri, sambamba na
magari mengi, pikipiki maarufu kama Bodaboda pamoja na baiskeli zilizoenda au
kurudi.
Wasanii na viongozi mbalimbali, akiwamo Mbunge wa Mbeya
Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu kama Sugu nao walikuwapo katika tukio la kuaga
mwili wa marehemu Ngwair na baadaye kwenye mazishi yake ambayo yalizua mkanyagano
wa aina yake.
Idadi kubwa ya watu ambao haiwezi kujulikana mara moja
ilijitokeza katika shughuli za kumuaga marehemu, ambapo pia walikimbilia
makaburini kwa ajili ya kushuhudia mwili wake ukiingia kaburini.
Awali, Mkuu wa Mkoa Morogoro, Bendera, alifika nyumbani kwa
mama wa marehemu saa nne za asubuhi, ambapo alipata fursa ya kuwapa pole wafiwa
na ndugu wa marehemu waliokuwapo katika eneo hilo wakijadili hili na kufanya
lile msibani hapo.
Akizungumza na wana familia ambapo pia baadaye alizungumza
tena uwanja wa Jamhuri, Bendera alisema kuwa Tanzania imepoteza msanii nyota na
mwenye bahati ya kupendwa na watu wengi.
Hii ni hatari kubwa, maana Ngwair ameonyesha ni kiasi gani
alikuwa nyota katika tasnia ya muziki wa Hip Hop na umahiri wake, sambamba na kuishi
na watu vizuri.
Hii leo ni Historia katika Mkoa wa Morogoro, hususan kwa
kushuhudia watu wengi wakiwa na huzuni katika kumuaga msanii wao mpendwa kwa
namna moja ama nyingine, hivyo serikali itaendelea kufanyia kazi changamoto
zinazowakabiri vijana hawa,” alisema Bendera.
Naye Mbunge wa Mbeya Mjini kwa Tiketi ya Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Joseph Mbilinyi marufu kama ‘Sugu’, alisema
wasanii wamechoka kuishi kimasikini wakati watu wengi wanaheshimu kazi zao.
“Inaumiza kuona tunazikwa kwa mtindo huu wakati maisha yetu
ni magumu mno, hivyo hatuwezi kuona hali hii inaendelea kuota mizizi, hivyo
wasanii tuendelee kuwa makini katika hili.
“Matatizo yaliyompata Ngwair katika maisha yake ni sehemu ya
changamoto zilizopo katika tasnia hii ya muziki wa kizazi kipya, ingawa tukifa
mazishi yetu yanakuwa ya heshima mno,” alisema.
Pamoja na kukusanya
watu wengi, lakini watu wengi walionekana kwenda uwanjani kuwaona wasanii
wengine, hivyo kusababisha mkanyagano kila anapoingia au kutoka msanii nyota.
Wale wasanii ambao wamekuwa na majina makubwa, akiwamo Wema
Sepetu, alilazimika kujificha kila wakati, maana kila akionekana sura, watu
walipiga mayowe.
Hata hivyo, matatizo yalianza kujitokeza katika shughuli ya
kuaga mwili wa marehemu, maana jeshi la Polisi, lilionekana dhahiri kushindwa
kasi na mvutano wa mashabiki waliokuwa wanavamia eneo moja kwa ajili ya kutaka
kwenda kumuaga marehemu.
Wakati shughuli ya kuaga marehemu ikiendele, ghafla, rafiki
wa Ngwair, waliyopata matatizo wote Afrika Kusini, Mgaza Pembe, maarufu kama M
to The P, aliletwa uwanjani hapo kwa ajili ya kumuaga marehemu Ngwair.
Baada ya kuona muda unazidi kwenda na watu hawaishi,
shughuli ya kumuaga Ngwair ilikatishwa kwa ajili ya kuanza msafara wa kuelekea
makaburini, Kihonda Kanisani.
Barabara zote zilizopita msafara wa mwili wa Ngwair, ulikuwa
umejaa watu wakiwa na nia ya kumungalia nyota wao akielekea kwenye nyumba yake
ya milele baada ya kufariki Afrika Kusini, Jumanne ya wiki iliyopita.
Kufika makaburini, umati mkubwa wa watu ulikuwapo, hivyo
ndugu wa marehemu kukosa muda wa kutia mchanga katika kaburi la Ngwair, hasa
pale watu waliposhindwa kusogea.
Kaka wa marehemu, Kenneth Mangweha, aliwashukuru Watanzania
kwa moyo wao wa upendo kiasi cha kushirikiana na wao kuhakikisha kuwa mwili wa
Ngwair unazikwa Tanzania.
“Nashukuru sana, natumia muda huu kuwatakia upendo zaidi na
zaidi Watanzania wenzetu, sambamba na kumtakia mapumziko mema huko mbinguni
Ngwair,” alisema Kenneth.
Kwa hakika, hatari kubwa iliweza kujitokeza katika makaburi
ya Kihonda Kanisani, maana barabara yote, ilijaa watu, baada ya eneo lote la
makaburi kuzagaa watu, wakishuhudiwa na Bendera.
Mangwair ametajwa kama miongoni mwa wasanii waliotikisa nchi
kutokana na vifo vyao kujaza watu wengi, hasa mkoani Morogoro alipozikwa, baada
ya kuagwa Jumatano kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam, akizikwa mishale ya saa
tisa za mchana.
Kama ilivyokuwa jijini Dar es Salaam, wasanii mbalimbali wa
maigizo na filamu, waliweza kuja mjini Morogoro kwa ajili ya kumshuhudia msanii
mwenzao akizikwa.
No comments:
Post a Comment