Washindi
chaguzi za CCM, wapime viatu vyao
Na Kambi Mbwana, Dar
es Salaam
CHAGUZI za ndani za Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimekuwa
zikiendelea huku kukiwa na malalamiko mengi ya rafu kutoka kwa baadhi ya
wagombea. Wapo wanaolalamika juu ya kufanyiwa mchezo mchafu, ukiwamo kumwaga
fedha kwenye uchaguzi wao.
Malalamiko hayo yamekuwa yakisemwa baada ya uchaguzi au
kabla, jambo ambalo hata hivyo ni kawaida katika chaguzi zenye upinzani na
ushindani wa wagombea.
Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Mrisho Kikwete
Kwa mfano, juzi katika uchaguzi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), wapo watu waliolalamika kuwa
kuna kundi likikuwa likitoa rushwa chooni, ikiwa ni muendelezo wa vituko
vilivyotokea kwa wingi kwenye uchaguzi huo uliofanyika mjini Dodoma.
Kituko kingine cha aina yake ni purukushani iliyoibuka baada
ya mwanachama wa CCM, ambaye pia Mbunge wa Afrika Mashariki, Shy Rose Bhanji,
alipomuuliza mgombea wa nafasi ya mwenyekiti wa UWT, Sophia Simba namna ya
kuitumikia nafasi yake ipasavyo na kwa manufaa makubwa ndani ya chama chake hicho.
Siphia Simba, mwenyekiti UWT
Majibu ya Simba inaonyesha hayakumfurahisha Shy hasa
aliposema kuwa bado ni mchanga kisiasa na hajui watu wanavyofanya. Ni majibu
mepesi katika uchaguzi mzito unaotingisha nchi nzima, hasa jumuiya hiyo, ambayo
kila mtu anaifuatilia.
Ikumbukwe kuwa, ndani ya CCM yenyewe, uchaguzi wa jumuiya
hiyo ulikuwa na nguvu kiasi cha kutingisha makundi mawili ambayo yalikuwa kati
ya Simba na Anne Kilango.
Shy Rose Bhanji, mbunge wa Afrika Mashariki
Kila mtu alikuwa akiamini kuwa ana ari na sababu ya kuongoza
kiti hicho, ambacho ni dhahiri kina manufaa makubwa na chama chao.
UWT endapo inatumika vizuri, inaweza kutangaza sera za chama
pamoja na kuwavuta akina mama wengi zaidi kwenye chama chao pamoja na
kuwabakiza waliopo kwa kunadi vitu vya kimaendeleo ama kuwaunganisha wanawake
Tanzania Bara na Visiwani.
Ni kwa kulijua hilo, naamini
sasa kuna haja ya washindi wa chaguzi za ndani za chama hicho, kujipima kama viatu walivyovaa vinawatosha. Nimekuwa nikilisemea
hili katika makala zangu mara kwa mara kwa ajili ya kuijenga CCM imara.
Nimekuwa pia nikiikosoa mwenendo wowote mbaya ndani ya CCM,
ikiwamo rushwa, ingawa wachache wao wanashindwa kunielewa na kuanza kunitumia
meseji zisizokuwa na kichwa wala miguu kwa sababu wanazojua wenyewe.
Ukiacha nafasi za mwenyekiti wa Mkoa, wilaya, mweka hazina
au Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, chaguzi za jumuiya za CCM ni
nyeti na zimeanza zamani mno.
Umoja wa Wanawake Tanzania
pamoja na Umoja wa Vijana CCM (UVCCM), ulianzishwa zamani, huku Bibi Titi
Mohamed akiwa mwenyekiti wa kwanza wa umoja wa wanawake Tanzania.
Kwa mujibu wa historia na harakati za CCM, tangu wakati huo
inaitwa TANU, jumuiya hizo ziliundwa kwa ajili ya kukiweka chama hicho katika
hali nzuri, sambamba na kuwavuta wengine, mfumo ambao hadi leo umeendelea.
Kwa bahati mbaya, nyakati za leo, mambo yamekuwa
yakibadilika kutokana na wanaopewa nafasi hizo, baadhi yao kutokuwa na jipya. Ni watu ambao viatu
wanavyolilia kupewa na chama, haviwatoshi.
Kwa wale wanaojua adha ya kuvaa vatu visivyokutosha, iwe
kidogo au kikubwa, watakubaliana na mimi kuwa ni mbaya mno. Ndio maana nasema,
walau sasa wale ambao wameshapata bafasi hizo za chama, wajiangalie tena.
Wajipime wenyewe kama kweli
wanaweza kuwa na mchango na CCM katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Wameingia madarakani katika kipindi kigumu mno. Kipindi ambacho fikra za watu
wengi zinaamini enzi za CCM zimekwisha.
Kipindi ambacho wakati wao wanawania nafasi hizo, wengine
wanapita chini chini kujaribu kutafuta namna ya kupenyeza watu ambao baadaye
iwe turufu kwao. Hizi ni dalili mbaya kwa CCM, hasa kama
watu hao wamefanikiwa.
Ni wakati sasa wa Viongozi wa CCM Taifa, akiwamo mwenyekiti
wake, Jakaya Mrisho Kikwete na wenzake kukaa na kuwapima kwa vitendo washindi
wao. Hili sio baya likifanywa na CCM, maana lengo ni kuwaweka sawa.
Kama walitoa sera zao mbele
ya wajumbe na wapiga kura wao katika uchaguzi huo wa ndani, basi waseme pia
namna ya kukisaidia chama ili kiende sambamba na presha ya vyama vya upinzani
vyenye hamu ya kuongoza dola.
Ni dhahiri CCM ipo kwenye kipindi cha hatari. Kama juhudi zisipochukuliwa, dalili za kuanguka katika
uchaguzi mkuu ujao ni kubwa. Hili lisemwe hata kama
watu wachache halitawafurahisha.
Wale waliozea kusifiwa au kudanganywa kuwa mambo yapo
vizuri, wakati hali ni mbaya na jamii imekuwa ikiweka chuki za wazi wazi kwa
viongozi wa ndani wa chama na wanachama wao kwa ujumla.
Kwa mfano, kampeni za kuwania nafasi za udiwani katika
baadhi ya maeneo zimekuwa zikiendelea kwa vyama kuwania viti hivyo. Ingawa
wakati wa kura bado, lakini matokeo katika chaguzi hizo pia ziwe kipimo cha
CCM.
Wanachama na viongozi wa CCM wasikubali kuweka viongozi
ambao kwa miaka mitano hawatakuwa na mchango wowote. Wasiwe viongozi wa kukaa
ofisini tu, au wafanya kazi kwa simu, wakizungumza kwa wao.
Viongozi wa chama, kuanzia ngazi ya shina hadi Taifa wapende
kuzungumza na wananchi ambao hao ndio walengwa wakuu. Wazungumze na wapiga
kura, ambao hao ndio watakaokuwa na kazi moja ya kuibakisha CCM madarakani au
kuimwaga.
Kama hivyo ndivyo, basi
tuanze kwanza kuangalia uhalali wa nafasi za chama na kuangalia pia viatu vya
washindi ili wajipime pia utendaji wao katika kipindi cha uongozi wao.
Najua wapo watakaohoji sababu hiyo ukizingatia kwamba
asilimia kubwa ya viongozi wameshapatikana, ila huko kushinda, ndio iwe sababu
ya wao wenyewe kuangalia namna ya kuongoza kwa manufaa na CCM.
CCM wilaya, mkoa na Taifa hili lazima walijuwe ili chama
kibaki salama katika Uchaguzi Mkuu ujao, utakaofanyika mwaka 2015. Uchaguzi
ambao huenda ukawa mchungu sana
kwa CCM, maana watu wengi, wakiwamo vijana ambao ndio wapiga kura, wamekuwa na
hasira na chama hiki kikongwe na kutamani kukiweka kando.
Wapinzani wamekuwa wakifanya jitihada mbalimbali, zikiwamo
za mikutano katika maeneo tofauti, jambo ambalo CCM nao lazima walijuwe.
Wasikae kucheka, kuwaona wapinzani ni majuha, wakati elimu
ya uraia inasambazwa kwa kasi ya ajabu na watu wanaanza kujua wajibu na haki
zao za kuongozwa na vyama tofauti na CCM.
Nasema hili bila kuangalia wale rafiki zangu wanaonisema au
kunitukana. Wale ambao nia yao
haswa watu tubaki kimya, tuchekee matatizo ya CCM, ili iwe nafasi ya kuanguka
katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Nalisema hili pia bila kuangalia wanachama wangapi wa CCM na
viongozi wake watanikosoa, wakisema makala yangu yameegemea kukichafua. Huo
ndio ukweli. Daima hauwezi kuwafurahisha kila mmoja duniani.
Sitarajii kukaa kwa bashasha na kusubiria kuwafurahisha kila
mmoja, maana katika Dunia hilo
jambo sio rahisi. CCM wajiangalie katika kipindi ambacho chama kimewaona
wanafaa hivyo nafasi zao lazima ziwe na tija kwa chama.
Yale makundi hasimu za wagombea yavunjwe na wanachama wote
wawe kitu kimoja, bila kuangalia aliyeshinda au aliyeshindwa. Bila hivyo,
makundi hayo pia yatazidi kuwa mwiba mchungu kwa chama hicho, ndio maana
ninahoji uhalali wa viatu vya watu hao.
Huo ndio ukweli, ikiwa ni mwelekeo wa mwisho mwisho katika
chaguzi za Chama cha Mapinduzi zenye joto kali katika wilaya na mikoa
mbalimbali, huku kila mtu akiona ana kila sababu ya kuwa kiongozi wa chama,
ingawa lengo lake haswa linashindwa kujulikana, hasa eneo lake linapotawaliwa
zaidi na upinzani siku baada ya siku.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment