Mbwana Samatta kulia na Thomas Ulimwengu
Na Kambi Mbwana, Dar
es Salaam
NI dhahiri wachezaji wawili wa Kitanzania, Mbwana Samatta na
mwenzake Thomas Ulimwengu wanaonyesha namna gani Watanzania wanahitaji kuwekeza
zaidi kwenye soka la vijana, maana ndio matunda ya soka letu.
Wachezaji hao wawili wanachezea katika timu ya TP Mazembe ya
nchini Kongo (DRC), huku nafasi zao zikiwa muhimu ndani ya timu hiyo. Ingawa
katikati ya mwaka huu Ulimwengu alionekana kupwaya kidogo, lakini sasa
amezinduka.
Labda ni kwa kuona mwenzake, Samatta anavyozidi kunga’ra
ndani ya timu hiyo, jambo lililomfanya aone bado ana deni kwa Watanzania
wenzake kwa kuona wanafika mbali zaidi na kucheza soka la kulipwa katika nchi
nyingine.
Kabla ya kupata nafasi hiyo, Samatta alionyesha makali yake
katika timu ya Mbagala Malket, kabla ya kununuliwa na Mohamed Dewji ‘Mo’ na
kubadilishwa jina la African Lyon. Hata hivyo Samatta hakudumu kwenye timu
hiyo.
Aliuzwa katika timu ya Simba
SC na kufanya njia ya kumpeleka Kongo
anapocheza hadi sasa na kuonyesha umahiri wake uwanjani.
Uwezo wake uwanjani na kucheza kwa akili, kumemfanya awe
lulu katika timu zote alizochezea, huku juhudi zake zikichangia kuipandisha
daraja Mbagala Malket na baadaye kuja kuitwa African Lyon inayocheza ligi ya Tanzania
Bara.
Wakati yeye akipita katika njia hiyo, mwenzake Ulimwengu
ametokea katika timu ya vijana, Serengeti Boys. Wote ni wakali wawili
wanaofanya kazi kwa pamoja TP Mazembe. Wanaishi kama wafalme ndani ya timu
hiyo.
Hakika vichwa hivyo viwili ni dira ya soka la Tanzania.
Hakuna Mtanzania asiyependa kuona matunda ya vijana hao. Umuhimu wao katika
timu hiyo ya nchini Kongo, ni nafasi ya kila mdau wa michezo kuona ana deni kwa
vipaji vya Tanzania.
Kila mdau na kiongozi wa soka la Watanzania ajaribu kuvuta
picha ya kuwakomboa vijana ili kuwaingiza zaidi katika soka, ukizingatia kuwa
ndio ajira kubwa hapa duniani.
Leo hii Samatta anaishi kama
mfalme katika timu ya TP Mazembe. Umuhimu wake unatokana na jitihada zake na
mguu wake uwanjani. Kujituma kwake na kuweka malengo kumechangia mafanikio yake
hayo.
Lakini, tunawezaje kuibua wachezaji wengine na kuwa kama akina Samatta na mwenzake Ulimwengu, ukizingatia
kwamba vipo vingi na vimefunikwa na mfumo wetu na kuwafanya vijana waone kazi
nzuri ni kukata mkaa vijijini?
Ingawa wapo wachezaji wengine wanaocheza soka la kulipwa,
akiwamo Henry Joseph Shindika anayecheza katika timu ya Kongsvinjer ya nchini Norway, lakini
hawa wenzake wanawika zaidi pale Kongo.
Uwezekano wa wachezaji hao wawili kusonga mbele zaidi upo.
Wakati wowote wanaweza kuondoka Kongo, maana mchango wao ni mkubwa kiasi cha
kuifikisha nusu fainali timu yao
katika michuano ya Mabingwa Afrika.
Huu ni wakati wa kuthamini na kuangalia harakati zetu za
soka. Hadi sasa, Tanzania
haina jitihada za kuwekeza kwenye soka la vijana. Ndio maana hata wale
wanaopata nafasi za kuonyesha uwezo wao, mara kadhaa ni juhudi zao binafsi.
Hata ligi yetu haina mvuto. Haina ushindani zaidi ya wadau
hao kuangalia mechi mbili za Simba na Yanga, wakiangalia idadi kubwa ya
mashabiki watakaoingia uwanjani hivyo kuingiza fedha nyingi kwa wakati mmoja.
Wale ndugu zangu wa African Lyon,
Kagera Sugar wanapokutana uwanjani, hata madaktari hakuna na wakiwapo gari la
wagonjwa (ambulance) hakuna. Juzi katika Uwanja wa Chamanzi, mchezaji wa
Coastal Union, Nsa Job, alipoumia gari la
wagonjwa halijakuwapo.
Haya ni mapungufu makubwa kwa wasimamizi wa mpira wa miguu,
nazungumzia Shirikisho la Soka nchini (TFF), linaloongozwa na Rais wake,
Leodgar Tenga.
Kama hivyo ndivyo, tunawezaje
kutafuta suluhu ya soka letu? Kama hatuna ligi
nzuri, vijana wengi zaidi wanapataje nafasi ya kucheza soka la kulipwa nje ya
nchi? Kama hatuna ligi ya vijana iliyokuwa
bora, vipaji vipya vya soka vinapataje nafasi?
Haya ni maswali ambayo majibu yake yapo katika meza ya Tenga
na watu wake. Haya ni maswali ambayo majibu yake yataendelea kuwa kitendawili
kigumu kwa watendaji wote wa TFF, maana juhudi zao ni kulipana mishahara na sio
kukuza kiwango cha michezo.
Wakati mwingine najivunia mafanikio ya akina Samatta na
Ulimwengu, lakini nikiona hakuna juhudi za kuwakuza wengine zaidi naishiwa
nguvu. Hata hawa wakichoka, nao watarudi nyumbani kwakuwa hakuna mipango.
Ni wakati sasa wa wadau na timu zetu kuangalia namna gani
wanawekeza katika soka la vijana ili wawe na nafasi ya kucheza muda mrefu. Kwa
mfano, makocha wengi wenye mipango duniani huwekeza zaidi kwenye soka la
vijana.
Pale Uingereza, kocha wa timu ya Arsenal anafikia wakati
kushindwa kueleweka kwa kuangalia zaidi vijana ambao wakati mwingine hawana
uzoefu. Lakini, kufumba kwake macho na masikio, wakati mwingine anaeleweka.
Lakini Tanzania
mambo ni tofauti. Tunaangalia zaidi wazee. Watu ambao maisha yao ya soka ni mafupi mno, kulingana na umri
wa wadogo zao. Timu kama Simba, Yanga na zote zinazoshiriki ligi ya Tanzania lazima
ione umuhimu wa kuwapa nafasi vijana.
Wafanye hivi kwakujua kuwa hayo ndio matunda ya kuvuna soka
lenye mvuto na kasi ya aina yake leo na hata kesho. Vijana nao waone wivu wa
kimaendeleo kwa wenzao wanaoishi kwa furaha na amani kubwa nchini Kongo.
Wachezaji kama vile Rashid Gumbo, Mrisho Ngassa, John Bocco,
Jerryson Tegete na wengineo waweke mkazo wanapokuwa uwanjani ili iwe nafasi ya
kuwapatia maisha mazuri katika mpira wa miguu ulimwenguni.
Wanapopata nafasi ya kupangwa uwanjani, wacheze kwa bidii na
kujiuza wenyewe, kama alivyofanya Samatta kwa
TP Mazembe. Mechi moja aliyocheza katika Mabingwa Afrika, ilichochea uongozi
kuona anafaa kuwamo kwenye timu yao.
Ukweli likatimia. TP Mazembe wakamsajili Samatta katika
kipindi ambacho alihitajika bado katika timu yake ya Simba. Kwanini wasije
akina Samatta wengine? Kwanini Ulimwengu mwingine asisajiliwe kwingine hata kama sio alipokuwa yeye?
Zipo timu nyingine zenye mvuto wa aina yake Afrika Mashariki
na Kati au Afrika Magharibi. Zipo timu kama Al Ahly, Zamalek na timu za Tunisia ambapo wachezaji wao wamekuwa
wakionekana sana
duniani.
Haya yaangaliwe. Haya yapewe mkazo kwa ajili ya soka la Tanzania.
Lazima watu wapambane kwa kutangaza soka la Tanzania, ili kukuza soka letu na
kuwafanya wanamichezo wetu wavune fedha nyingi kwa kupitia mpira wa miguu.
Kwa hili la Samatta, Ulimwengu ni somo kuwa mpira unalipa na
lolote linaewezekana endapo kila mmoja atafanya kazi kwa malengo.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment