https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Friday, November 23, 2012

Kinyang’anyiro cha Chalenji kuanza kesho Uganda


Mrisho Ngassa akimiliki mpira uwanjani.
                     

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MASHINDANO ya Kombe la Chalenji 2012 yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi leo nchini Uganda na kumalizika Desemba 8, katika mji wa Kampala, nchini Uganda, huku timu 12 zikionyeshana kazi katika michuano hiyo.

Timu hizo ni pamoja na Burundi, Ethiopia, Eritrea, Kenya, Malawi, Rwanda, Somalia, Sudan ya Kusini, Tanzania, Sudan, Zanzibar na Uganda, ambao ndio mabingwa watetezi wa mashindano hayo ya Kombe la Chalenji mwaka huu.

Mashindano hayo kwa mwaka huu yalikuwa yafanyike nchini Kenya, lakini wadhamini wake, Kampuni ya East African Breweries Ltd (EABL) waliomba michuano hiyo ifanyike nchini Uganda na kuridhiwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Michuano hiyo inaanza huku wawakilishi wa Tanzania, timu ya Taifa, Kilimanjaro Stars na ndugu zao Zanzibar Heroes wakiwa tayari kwa vita katika mashindano hayo yenye ushindani wa hali ya juu kwa washiriki wote.

Kwa mujibu wa CECAFA, viwanja vitakavyotumika katika mashindano ya mwaka huu ni Namboole na Nakivubo vyote vya Kampala Uganda, huku Namboole ukiweza kuchukua mashabiki zaidi ya 45,000 utakaotumika kwa ajili ya mechi za ufunguzi, mechi zote za kundi A na mechi za hatua ya robo fainali, nusu fainali na fainali.

Wakati Namboole ukichukua mashabiki 45,000, Uwanja wa Nakivubo nao una uwezo wa kuchukua mashabiki 15,000, ingawa waandaji wameupanga uwanja huo utumike katika mechi chache katika mashindano hayo.

Wawakilishi wa Tanzania, timu ya Kilimanjaro Stars, imepangwa kuanza kutimua vumbi na Sudan kesho Jumapili, ikiwa ni siku moja baada ya kuanza katika mji huo wa Kampala, nchini Uganda, ardhi ya mabingwa watetezi.

Benchi la ufundi la Tanzania linaloongozwa na kocha wake, Kim Poulsen na Sylvester Marsh, wametangaza vita katika mashindano hayo kwa ajili ya kuiwezesha kutwaa ubingwa huo na kuleta imani kwa Watanzania.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...