Mrembo anavyoonekana baada ya kutengenezwa nywele zake na Salumu Mwombeki
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KILA kitu kinahitaji mipango kama
kweli dhamira ni kukiletea maendeleo na kutambulika pia kwa jamii mbalimbali.
Wakati hao yapo kwenye sekta zote zikiwamo za sanaa, hata
kwenye nyanja ya urembo huko nako ni kawaida.
Ili sekta hiyo iweze kupiga
hatua na kufanya kazi kwa mafanikio makubwa, ni wazi juhudi zinahitajika pamoja
na mipango kwa jamii husika.
Salumu Abdallah Mwombeki akiwa kazini kwake.
Katika mazungumzo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita,
Salum Abdallah Mwombeki, ambaye ni mtaalamu wa upambaji na mitindo kwa akina
mama, anamiliki saluni yake maeneo ya Tabata Chama.
Jina la kijana huyo limeenea kwa kiasi kikubwa katika mtaa
huo kutokana na umati wa watu kujaa katika saluni kwa ajili ya kujilemba,
ukizingatia kijana huyo kwa mikono yake, ana uwezo wa kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi.
“Nashukuru Mungu nimezidi kujipatia mafanikio makubwa
kutokana na kuweza kuwamudu vyema kuwalemba akina mama, kuanzia kubuni mavazi
ya kuvaa kwa wakati husika, hasa harusi na mengineyo.
“Pia wateja wangu wakija huwashauri mitindo ya kuwasuka
kulingana na aina ya vichwa vyao, nikiwa na lengo la kuwapendezesha na
kuwafanya waendelee kufanya kazi na mimi, ukizingatia kwamba kazi hii ni kipaji
changu,” alisema.
Salum anasema katika kazi hiyo, watu wengi bila kuangalia
hadhi na majina yao
wamekuwa wakimtafuta kwa ajili ya kufanya kazi nae, jambo ambalo linamfanya
aamini atafanikisha mipango ya kufanya kazi hiyo kwa mafanukio makubwa.
Kijana huyo anasema mipango yake ya baadaye ni kupanua
biashara zake hizo za saluni ya kike, huku akipanga kumiliki saluni
iliyotengenezwa maalum katika gari kubwa na kupaki mahali popote na kuwahudumia
wateja wake.
Anasema gari hilo
linaweza kuwekewa ratiba ya kuzunguukia maeneo mbalimbali, yakiwamo ya mikoani
na kuwapa nafasi watu mbalimbali kuipata huduma yake bila kuangalia wapo mahali
gani na wana kipato cha aina gani.
“Kwa mfano gari linaweza kusafiri hadi Mwanza, Arusha,
Tanga, Dodoma
na kupaki pembeni kwa ajili ya kuwapatia huduma hiyo watu ambao huenda walikuwa
wakikosa fursa hiyo kwasababu ya makazi yake kuwa Dar es Salaam,” alisema
Salum.
Kijana huyo anasema kwamba saluni yake hadi sasa inafikia
mtaji wa Shilingi Milioni 15, ikiwa na vitu vya kila aina vinavyohusu mambo ya
urembo wa akina mama.
Anasema mtu anapoingia hapo, hujikuta amebadilika kwa
kutengenezwa vizuri nywele zake kwa mitindo ya aina mbalimbali anayoitaka
mwenyewe.
Salumu aliyezaliwa miaka kadhaa iliyopita, anasema utundu wa
kupamba maharusi, usukaji wa nywele za aina mbalimbali ameupata kutoka kwa
Mungu, ingawa anaamini kuwa kipaji cha mama yake mzazi, Madina Nuru, pia
kimechangia.
Anasema mama yake alikuwa mjuzi wa usukaji wa vitu
mbalimbali, ikiwamo mikeka, jambo ambalo hata yeye limempa mwangaza huo, ambao
leo unamfanya aweze kuishi vizuri kwa kutumia kichwa na viungo vyake vya mwili,
hasa mikono.
Anasema katika ujuzi wake huo kwenye saluni yake, anashonea
nywele za bandia, usukaji wa rasta na mitindo mbalimbali inayotamba au kubuni
mingine kwa ajili ya kuwapendezesha zaidi wateja wake wanaofuata huduma yao.
Anasema awali, mwaka 2002 alikuwa akijishughulisha na
biashara za kuuza nywele za akina mama, lakini duka lake lilikufa lilipovunjwa
na wezi hivyo kumrudisha kutoka hatua kubwa ya kibiashara aliyokuwa nayo.
Jambo hilo
lilimfanya aanze kuendeleza kipaji chake cha usukaji kwa ajili pia ya kutafuta
maisha, ukizingatia kwamba tayari alishagundua uwezo wake.
Salumu anasema changamoto kubwa kwake ni kwa baadhi ya
wanaume wasiomuelewa katika kazi yake hiyo, huku wengineo wakiona hana jipya
zaidi ya kumendea wake za watu.
“Hapo nyuma niliwekewa mitego ya kila aina, maana wenye wake
zao wanajua tuna uhusiano wowote, wakati sio kweli, ila watu wao wanafuata
huduma ya urembo.
“Nashukuru maana leo wamenielewa na wengine wananipigia simu
kuwawekea oda wake zao, wakiamini kuwa wamegundua mikono yangu inawapendezesha
vizuri wake zao ambao naamini saluni yangu ndio chaguo lao,” alisema.
Mipango yake mingine ni kufungua kampuni ya mitindo
itakayohusika na mambo mbalimbali yanayohusu medani ya urembo na mitindo hapa
nchini.
Katika kutafuta mbinu za kufanya kazi kisasa na kwa
mafanikio makubwa, amekuwa mwepesi kutembelea matamasha mbalimbali, pamoja na
matukio ya mitindo katika kumbi za starehe na mahoteli.
Hata hivyo, huko haoni lolote, hasa anapogundua watu hao
wanafanya kazi kwa kubahatisha, kiasi cha wengineo kuwaharibu hata wateja wao,
wakiwamo maharusi wanaoingia katika matukio ya kukumbukwa duniani.
Kwa sasa saluni yake hajaipa jina zaidi ya wateja wake kuambiana
wenyewe, huku kituo cha Tabata Chama, kikiwa maarufu kiasi cha kuleta wateja
wapya kila baada ya saa chache.
“Saluni yangu sijaipa jina lakini inaleta wateja wapya,
maana wanajua kuwa ramani yao
ni kupanda magari yanayokwenda Tabata Kimanga na kushuka kituo cha Chama,
ambapo hapo hata mtoto mdogo ananijua na kuifahamu saluni yangu.
“Nashukuru kwa dhati, maana Mungu amenipa kukubalika na
kuheshimika kwa kazi yangu, ndio maana hata wasaidizi wangu nimewapa mwongozo
wa kumuheshimu mteja anayetoka mbali kwa ajili ya kupata huduma zetu,” alisema
Salumu.
Mtaalamu huyo anasema kikubwa anachojivunia ni uwezo wake
kujua mbinu gani za kusuka nywele za wateja wake na kutoka wakiwa na furaha,
huku gharama zake zikiwa ni nafuu na kuwavutia kila mtu, hivyo watu kutoka
mbali na kwenda kwenye saluni yake.
Anasema makubaliano yote ya ufanyaji kazi wake, hufanywa mtu
anapokwenda katika saluni yake kwa ajili ya kufanya naye kazi. Salumu anamaliza
kwa kuitaka jamii kujua kuwa kazi hiyo ni nzuri na isifikiriwe vyovyote
tofauti.
Anasema badala ya vijana kufanya kazi ambazo hazina maadili
kwa jamii yake, kuna haja ya kuungwa mkono kwa wale wanaoamua kutafuta riziki
kwa njia nzuri kama anavyofanya yeye, huku
akiwa na malengo makubwa duniani.
Anamaliza kwa kuwataka watu wanaojihusisha na kazi hiyo ya
saluni, kutengeneza nywele na mengineyo kuwa wepesi kujifunza na kufuata
ushauri wa waliowazidi kiufundi na kipaji cha ufanyaji kazi ili iwe njia yao ya mafanikio.
Makala haya yameandikwa na Kambi Mbwana.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment