Haruna Moshi 'Boban'
Na Kambi Mbwana, Dar
es Salaam
ETI Simba walitangulia na baiskeli ya miti? Yani licha ya
kufika mbali, lakini wenye baiskeli nzuri wamewapita kama
wamesimama. Kwa bahati mbaya, baada ya kuwapita, wameacha lawama na mabishano
kutoka kwa wadau na mashabiki wa timu hiyo.
Simba ipo chini ya mwenyekiti wake, Ismail Adeni Rage,
ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Mjini mwenye maneno mengi. Siku zote nimekuwa
nikisema, ukitaka kumuadhibu Rage, jichunge usimuangalie usoni.
Anatia huruma mtu huyu. Akiongeza na utundu wake wa
kuzungumza, hata jambo la hatari, uongo kwake utakuwa wa kweli na kuona
anaonewa. Kwanini nasema hivi? Simba iliweza kuchukua uamuzi wa hatari wa
kujenga makundi ndani ya timu yao, licha ya
kujipambanua kuwa ina ndoto za kuipaisha juu zaidi timu yao.
Wapo wachezaji wanaonekana ni zaidi kuliko wenzao. Hao hata kama wakisema nini, uongozi na benchi la ufundi
litawasikiliza na kuwapigia makofi.
Kwa mfano, hivi karibuni timu ya Simba ilimuadhibu beki
wake, Juma Nyosso kwa kumshusha kutoka kwenye kikosi cha kwanza hadi kutakiwa
afanyie mazoezi na timu B.
Mbali na Nyosso, Simba pia ilimfungia mshambuliaji wao
tegemeo, Haruna Moshi Boban kwa utovu wa nidhamu. Baada ya kuwafungia wachezaji
hawa, Simba ilizidi kupoteza thamani yake kutoka kileleni hadi leo ipo nafasi
ya tatu.
Mbaya zaidi, aliyekuwa nafasi za chini, Yanga, leo ipo
kileleni na kuwaacha Simba wakiendelea kuparuana bila kujua kuwa walikata tawi
walilokalia. Sina lengo la kuchekea makosa ya wachezaji hao waliopewa adhabu,
lakini tuangalie pia na hali halisi.
Kabla ya kuwaadhibu wachezaji hao, Simba haikufungwa mechi
hata moja zaidi ya kutoka sare katika michezo yao kadhaa. Yanga yenye kasi na moyo wa
kujisahihisha, inaongoza ligi hiyo kwa kujikusanyia pointi 29.
Anayefuata ni Azam FC yenye pointi 24, huku Simba wao wakiwa
na pointi 23, ikiwa ni tofauti ya pointi 6 kwa anayeongoza ligi hiyo. Ni
hatari. Simba inahitaji marekebisho pamoja na ushirikiano kwa wachezaji wote.
Simba haihitaji roho moja ya Juma Kaseja ili itetee ubingwa
wake. Wala haihitaji nguvu za Emmanuel Okwi ili ifanye vyema. Bali
inahitaji nguvu za wachezaji wote bila kuangalia haiba na nguvu za mmoja mmoja.
Simba pia inahitaji utii wa uongozi mzuri wenye kila dhamira
ya kuwapatia mafanikio ya kitaifa na Kimataifa. Simba haitaji kuwa na wingi za
fedha kwa ajili ya kuwahonga waamuzi zaidi ya kuwaweka kitimu kuwaaminisha kuwa
wana deni na timu yao.
Nilijaribu kufuatilia sakata la Nyosso na Boban na kugundua
udhaifu mkubwa kutoka kwa benchi la ufundi pamoja na uongozi mzima. Simba
haikuwa kitu kimoja zaidi ya jitihada za mchezaji mmoja mmoja, ambaye hata
hivyo baadaye waligawanyika tena.
Pamoja na mapungufu yao,
lakini wachezaji hawa ni roho ya Simba. Utasema nini kuhusu pumzi na uwezo wa
Boban? Vipi kuhusu Nyosso ambaye jitihada zake uwanjani ni mbeleko ya kuibeba
timu hiyo katika mechi mbalimbali.
Hivi Boban na Nyosso ndio watovu wa nidhamu peke yao Simba? Haya ni
maswali ambayo majibu yake yatazidi kuipasua Simba na kuifanya ishuke zaidi ya
hapa. Mwenyekiti wake, Rage na viongozi wenzake waliangalie hili.
Kukata tawi ulilokalia ni ujinga. Kila mtu afanye kazi kwa
kuangalia namna ya kuleta maendeleo na sio ubabaishaji usiokuwa na faida kwa
Taifa. Timu inayojaribu kuweka mwanya wa kuingiza porojo na malalamiko haiwezi
kuwa na maendeleo.
Angalia, hata TP Mazembe inayotesa katika rekodi Afrika
Mashariki na Kati, haiwezi kuendeleza mazuri yake kama
uongozi utajiendesha kwa mizengwe. Kila mmoja lazima ajuwe mpira ni pesa na
unalipa kupita kiasi.
Soka ndio mchezo unaoweza kutengeneza mabilioni ya shilingi
katika dakika 90 au 120 za mchezo husika, hasa mechi zenye mguso na ushindani.
Hapa kwetu, tunaangalia jinsi fedha nyingi zinavyoingia kwa kuzikutanisha timu
za Simba na Yanga.
Utasema nini kuhusu mechi ya robo fainali ya Ligi ya
Mabingwa ya Afrika, endapo timu moja wapo ya Tanzania itaingia na kukutana na TP
Mazembe, Al Ahly au nyinginezo za Afrika zenye wapenzi wengi nchini mwao?
Ni dhahiri fedha zitaingia nyingi. Lakini, watu hawaingii
kwenda kuangalia mipira ya minazi isiyokuwa na metokeo mazuri kwao. Wanaingia
wakijua wataburudisha nafasi zao kwa kuangalia ufundi na uchezaji soka wa
kuvutia.
Lakini leo hii Simba inayojiandaa kwa michuano ya awali ya
Ligi ya Mabingwa, haitakuwa na jipya maana imemaliza mzunguuko wa kwanza wa
ligi na matokeo mabaya yanayoanza kuzalisha sumu ya malumbano wao kwa wao.
Matokeo hayo yamesabisha pia Makamu Mwenyekiti wake, Geofrey
Kaburu kuambiwa ajiuuzulu bila sababu za kueleweka. Kwa mujibu wa vyanzo vya
ndani, Kaburu amekubali kuachia ngazi, ila anasubiri kikao cha Kamati ya
Utendaji, kitakachoitishwa hivi karibuni.
Haya ni maajabu. Ukiangalia kwa kina, utagundua kuwa timu
hiyo haina mipango na kawaida yao
ni kukata tawi inalokalia. Kwanini Kaburu na sio Rage? Kwanini wajiuzulu
viongozi na sio benchi la ufundi linalojua mbinu za ushindi au kufungwa?
Kama wamekubali uongozi,
basi matatizo yameanzia hatua hiyo, hasa kwa ubabaishaji wa kiongozi kuingilia
mambo ya ufundi ya wachezaji wao. Ni rahisi kiongozi kutaka Fulani apangwe kwa
sababu anazojua mwenyewe.
Kama hivi ndivyo, basi
akiambiwa ajiuzulu hapo hakuna tatizo. Lazima ajiuzulu kwasababu ya ubabaishaji
wake. Haya lazima tuyajadili leo.
Ndio ukweli wa mambo. Simba iliyoanza vyema na kushika
usukani wa ligi inaweza kuachia ubingwa huo kutokana na mipango yao mibovu na kuingilia
hata mambo ya kiufundi.
Hili ukilisema, uongozi utakuwa mbogo na kulazimisha msemaji
wao, Ezekiel Kamwaga aitishe mkutano na wana habari kukanusha uchambuzi wa
mwandishi. Hayo ni matatizo makubwa na huenda yakaitafuna Simba.
Nimewahi kusema mara kadhaa kuwa timu zetu zinajiendesha kwa
ajili ya soka la nyumbani tu, maana Kimataifa, hawana mipango.
Kimataifa mtu anaweza kubashiri kuwa Simba, Yanga ikivuka
hatua ya pili atafanya kitu cha kushangaza umati na kweli, mzunguko wa kwanza
wakaangukia pua na kushindwa kuendelea.
Ni kwasababu ya ubabaishaji wao. Wamewekeza kwenye soka la
mdomoni, kwenye kurasa za mbele au za nyuma za magazeti wakipambwa na kubebwa,
hata kama wataalamu wanajua hakuna soka
linalochezwa.
Waswahili wana msemo wao, siku zote mbuzi hula kwenye urefu
wa kamba yake. Simba yenye migogoro isiyokwisha, kusema itaingia fainali ya
Ligi ya Mabingwa Afrika ni kujipa presha ya bure tu.
Zaidi ya hapo ni kutabiri kuwa haina cha maana itakachovuna
zaidi ya kuganga njaa, kuingiza mashabiki wengi katika mechi moja na kutolewa
nje katika kila michuano itakayoingia, iwe ni Mabingwa au Kombe la Shirikisho
Afrika.
Hali hii itaendelea kudumaza soka letu na kuwafuja
wanamichezo wetu. Wachache watakaovuma nje ni kwa bidii zao wenyewe. Wachezaji
kama vile Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na wengineo wapo nje kwa bidii zao
wenyewe.
Ni nani atajigamba kwamba amechangia kuwapeleka hao nje nchi
kucheza soka la kulipwa katika timu ya TP Mazembe ya nchini Kongo?
Na aseme leo. Jibu hakuna. Tena wapo ambao wanapoona
wachezaji wao wanatakiwa nje kujaribiwa huwawekea mtimanyongo au kuwafungia
kwasababu wanazojua wenyewe.
Ni ajabu na kweli. Haya lazima yasemwe na kupingwa na kila
mmoja wetu. Ndio maana nasema, kinachoendelea ndani ya timu ya Simba, ni
kuonyesha picha ya kushangaza, hasa pale uongozi ulipojaribu kukata tawi
ililokalia.
Naomba kuwasilisha hoja.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment