Abdallah Kigoda, Mbunge wa Handeni
Watanzania
tuchague viongozi watakaotusaidia, si wachuma fedha
Na Kambi Mbwana, Dar
es Salaam
KATIKA mfululizo wa makala zangu kwenye Gazeti la Mtanzania
Jumatano, ‘Mgodi Unaotembea’ pamoja na Mtanzania Jumapili, wakati mwingine nakutana
na maswali ambayo, ukiyafikiria vizuri, jibu lake linaweza kukuliza.
Ndio, kama wewe unaona uozo
wa jambo linalokumiza limeanzia kwa mtu mmoja aliyekuwapo madarakani kwa muda
huo, ukweli ni kwamba umeanza zamani. Ingawa si kwa maeneo yote, lakini kwa
kiasi kikubwa matatizo haya yanawaumiza Watanzania wengi.
Jumapili ya Novemba 11 niliandika makala iliyokwenda kwa
jina la Njaa, shida ya maji vitawatoa roho Handeni. Makala hiyo ilielezea kwa
kirefu matatizo yanayowakabiri watu wa Handeni na vitongoji vyake.
Maoni mengi niliyapata. Lakini, huyu alinisikitisha sana. Na huu ndio ujumbe
wake ambao nikaamua kuuandikia tena makala kuweka sawa mambo niliyojadili
angalau watu wafahamu na kutafutia ufumbuzi.
“Ndugu, Mbwana, Makala yako katika gazeti la Mtanzania
Jumapili, Novemba 11 kuhusu tabu ya njaa na shida ya maji Handeni ni ya kusikitisha
sana. Mimi
nilikaa Handeni mwaka 1982 na 83 wakati wa mbunge Mussa Masomo hali ilikuwa
hivyo hivyo.
“Hawa Wabunge wanafanya kazi gani? Naomba unijulishe iwapo
Mussa Masomo bado yupo hai. Mimi Method Mhagachi, DSM,” ulimaliza ujumbe uliotumwa
na mfuatiliaji mzuri wa gazeti la Mtanzania.
Ujumbe huu uliniumiza kichwa. Hasa baada ya kugundua kuwa
kero ninayoiona mimi kubwa kwangu, haijawahi kutoka kwa wakazi na wananchi wa
Handeni. Kwa bahati mbaya, si Handeni tu, bali katika maeneo mengi ya Tanzania.
Ingawa juhudi nyingine zimekuwa zikichukuliwa na serikali
Kuu, chini ya Rais wake, Jakaya Mrisho Kikwete, lakini wakati mwingine
anaangushwa na anaowaamini. Ndio, maana kila wilaya ina fungu lake inapata
katika kila bajeti.
Pia kuna mfuko wa jimbo. Mbali na mfuko wa jimbo, bado kuna
rasilimali fedha na rasilimali watu ambao kwa pamoja wanaweza kushirikiana
kuleta maendeleo ya watu wao.
Katika kuliangalia hilo, jibu
lake ni kwamba majimbo hayo yenye matatizo
lukuki yansababishwa na wabunge wao wasiokuwa na jipya kwa wananchi wao.
Tuliseme hili ingawa litakuwa chungu kwa wasiopenda ukweli.
Wale wanaosema kuwa eti tunaishi mjini habari za mikoani
tunazipata wapi? Wakaongeza kuwa harakati zinazofanywa ni kuwachafua watu
wachache. Sio kweli. Nimekuwa nikitembelea katika maeneo mengi kujionea hali ya
mambo inavyoendelea.
Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, nimetembelea
katika mikoa ya Kilimanjaro, Mwanza, Tabora, Singida, Morogoro na Tanga ambapo
ndio nyumbani ninapotembelea pia vijiji na Kata zote, kama
vile Misima, Kwamatuku, Komkonga, Mkata na kwingineko. Na kama
tusipotumia haki ya kukosoana na kuelimishana nchi yetu haiwezi kusonga mbele.
Kati ya wabunge wengi wanaoshinda katika majimbo yao, hakika wanatumia njia
za panya kuwapatia nafasi hizo nyeti. Wabunge hawa ni wale ambao wameshakaa
katika majimbo yao
kwa miaka mingi, huku wakikosa mwelekeo.
Majimbo yao
yamekuwa na changamoto nyingi. Wananchi wanaendelea kutaabika, huku wabunge wao
wakionekana kwenye luninga katika warsha, semina, ama vikao vya Bunge vinavyowalipa
vizuri.
Wabunge ambao kwa miaka mingi tangu alipochaguliwa katika
nafasi hiyo, hajaweza kutembelea hata mara moja kwa wananchi waliomuweka
madarakani. Haya yote yanasababishwa na umasikini wa kipato na fikra sahihi.
Wananchi wengi hawana uelewa katika mambo ya uraia. Hawajui
hata haki zao za msingi za kuwapata viongozi wao.
Umasikini wa fikra pevu ni wa kubaini kuwa kususia kupiga
kura au kuchukua mia mbili kama rushwa ya
kumuweka mtu madarakani ni hatari katika maisha yake kwa kipindi cha miaka
mitano.
Kwa bahati mbaya, masikini yoyote akipewa mia 200 hakika
atakubeba mgongoni hadi kufa kwako. Atakusifia kadri anavyoweza. Atakuombea kwa
Mungu dhambi zako ziondolewe kwasababu tu amepewa mia 200 ya kununua dagaa.
Hizi ndio changamoto za masikini. Hizi ndio dosari za watu
hasa wa mikoani ambao kwa hakika ndio kwenye maisha magumu kupita kiasi. Kwa
kusema hayo, nadhani kuna haja sasa ya kila mwananchi kujitambua.
Kwanza wajuwe kura ni haki yao ya msingi. Pili wasijaribu kudanganywa
kwa shilingi mia 200 wanazopewa na wenye nazo. Badala yake wahoji au watake
mambo ya kimaendeleo katika maeneo ambayo kwa hakika ni kazi ya viongozi wao.
Ifahamike kwamba, kiongozi kufanikisha maisha bora kwa watu
wake ni jukumu lake. Hakuwekwa madarakani ili atembelee magari ya kifahari na
familia yake bali pia awatumikie mabosi wake, ambao ni wananchi wake.
Lakini kama mtu ameingia madarakani na hana analofanya huyo
hafai kama ukoma. Hakuna kuangaliana usoni.
Hakuna kuogopana katika kusema mambo ya maana yenye umuhimu na Taifa letu lenye
kila rasilimali.
Wananchi wasikubali kupumbazwa na visenti vya kununulia
sukari, badala yake wawabane zaidi viongozi wao ili waboreshe maisha yao kwa ujumla.
Waboreshe katika mambo mbalimbali, yakiwamo kilimo bora,
miuundo mbinu, huduma za afya, nishati ya umeme ambayo kwa hakika ni yanaweza
kupunguza makali ya maisha.
Badala ya kupokea visenti vya kula, wananchi watake kutoka
kwa viongozi pembejeo za kilimo na mengineyo yenye kuinua uchumi wao.
Wakati wa uhai wa bibi yangu (Luwaya) katika kijiji chetu
cha Komsala, Handeni, mkoani Tanga, nakumbuka hata kuwe na njaa vipi lakini
chai kwake ni lazima. Ingawa wapo waliohangaika kutafuta chakula, lakini yeye alikuwa
tofauti.
Kumbe alikuwa anaikamua miwa na na kuipika sukari kwa njia
ya kienyeji. Hii iliweza kumuondolea bajeti ya sukari kutoka kwa watoto wake.
Kazi yake kubwa ilikuwa ni kulima kidogo mazao aliyomudu, ikiwamo miwa, mahindi
na mpunga.
Lakini vipi leo. Je, wananchi wanahamasishwa kulima? Kama wapo wanaopenda kulima. Je, changamoto za wadudu,
kukosa uwezo wa kununulia pembejeo wanamudu vipi? Serikali yao ya kijiji, Kata, wilaya na Taifa
inawajali?
Je, mabadiliko ya tabia nchi, kunakosababisha mvua
kutonyesha kwa wakati, wananchi wanaelimishwa juu ya hilo? Nasema hivi maana katika maeneo mengi,
wakulima wamekuwa wakilima kila wakati na kuambulia patupu.
Wanalima wakitegemea mvua itanyesha mwezi ujao. Lakini
hainyeshi na ikinyesha si kubwa, hivyo kuozesha mbegu zao walizopata kwa shida.
Mara kwa mara wanapishana na mvua. Kama hivyo
ndivyo, wataalamu wetu wa kilimo ndio wakati wa kufanya kazi zao.
Kama hivyo haitoshi,
wakulima waelimishwe pia kupanda mazao yanayostahimili ukame kwa baadhi ya
maeneo. Waelimishwe juu ya kuhifadhi vyakula ama kutoiuza ardhi kwa matapeli
wanaokwenda kuwalangua kwa njaa zao.
Haya ni mambo ya watalawa. Kama
mtu muda mwingi yupo mijini na kusubiri Uchaguzi Mkuu hakika ni majuto makubwa
kwa wananchi wake.
Huu ndio ukweli. Vijijini kuna changamoto nyingi sana. Ingawa tunajua kuwa
kilimo ndio uti wa mgongo, lakini watu wanaoishi huko hawajaliwi wala
kukumbukwa. Viongozi wengi, wakiwamo wabunge wao ni wachumia matumbo yao.
Wanachosubiri Uchaguzi Mkuu na kununua mashati ambayo ndani
yake huweka mia 200 ambazo mwananchi huona nyingi na kuwapigia kura
zinazowaumiza kwa miaka mitano kila mwaka, ingawa baadaye hudanganya kwamba
wanakubalika.
Nani anakubalika kwa wananchi wake? Na aseme leo kuwa
anakubalika kwakuwapatia maisha bora wananchi wake. Na aseme alichofanya leo
kwa muda aliokaa katika jimbo lake. Kisha watu tupime ukweli na uongo wake.
Hakuna kitu. Bure kabisa. Kama
wapo, sio wengi. Baadhi yao
hulindwa na visenti vyao. Ndio maanza Mgodi Unaotembea unasema, masikini ukimpa
mia 200 atakubeba mgongoni.
Atakuona wewe ni Mungu mtu. Hata kama uwe tapeli, mwizi. Kutokana
na hilo, kuna
haja ya kuangalia mustakabali wa maisha yetu.
Tukumbushane juu ya kuwachagua wenye dhamira ya kweli ya
kuwaongoza Watanzania wenzao na sio wale wenye malengo ya kuvuna utajiri ili
wanufaike na familia zao, wakati sisi watoto wetu wanasomea kayumba, huku
wakitembea uchi kwa kukosa nguo za kuvaa.
Tukutane wiki ijayo.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment