Rais wa FM Academia, Nyosh El Sadaat
Na Kambi Mbwana, Dar
es Salaam
BENDI ya muziki wa dansi ya FM Academia, maarufu kama Wazee
wa Ngwasuma, inatarajia kufanya onyesho la nguvu katika uzinduzi wa pub ya ‘Babylon’, iliyopo Kilosa,
mkoani Morogor kwa ajili kiwanja hicho kipya cha burudani.
Ngwasuma wanafanya shoo hiyo wakiwa na lengo moja la
kuonyesha makali katika ramani ya muziki wa dansi hapa nchini, huku wakiwa na
wakali mbalimbali wanaofanya makubwa katika mustakabali wa bendi hiyo.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa ukumbi huo,
Daudi Mfaume, alisema kwamba maandalizi ya kuwaleta wakali hao katika mji wao
huo yamekamilika, huku wakiamini kuwa mashabiki wao watapata makubwa.
Alisema kuwa Ngwasuma wamekuwa na mashabiki wengi katika mji
wa Morogoro, hivyo kwakuwaleta Kilosa, mashabiki wao watapata kitu adimu na
kuweka historia kamili katika tasnia ya muziki wa dansi hapa nchini.
“Tumepanga kuwaleta wakali wa muziki wa dansi hapa nchini,
Wazee wa Ngwasuma kwa ajili ya kuwapatia burudani mashabiki wao watakaoingia
katika uzinduzi huo wa Babylon wakiwa kama wadau na mashabiki wa muziki nchini.
“Naamini kila kitu kitakwenda sawa, hivyo wadau na mashabiki
wa muziki wa dansi wa mkoani Morogoro, wajiandae kwa ajili ya burudani hiyo
itakayofanyika katika ukumbi mpya wa burudani katika mji wetu wa Kilosa,”
alisema Mfaume.
Wazee wa Ngwasuma ipo chini ya Rais wa Vijana, Nyosh El Sadaata,
akiwa sambamba na waimbaji wengine nguli, akiwamo Patchou Mwamba, ambaye pia
anatamba katika tasnia ya filamu, baada ya kucheza filamu mbalimbali
zinazokubalika nchini.
No comments:
Post a Comment