Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Generali, George Waitara, kulia akizungumzia ziara ya Mlima Kimanjaro. Anayefuata kushoto kwake ni Joseph Kitani, Mratibu Mkuu wa safari hiyo kutoka Kampuni ya KJ Traders ya jijini Dar es Salaam.
Na Kambi Mbwana, Dar
es Salaam
WATANZANIA wengi wamejipa ujinga wa kuamini kuwa jukumu la
kutembelea hifadhi mbalimbali lipo kwa wageni na sio wazalendo wenyewe.
Hao wanagoma kabisa kuweka taratibu za kutembelea hifadhi za
Taifa kwa ajili ya kuangalia vivutio vya utalii, hivyo kueneza sumu hiyo kwa
vizazi vyao.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki
Mtoto ambae hajawahi kupewa ratiba ya kufanya matembezi
katika vivutio walau mara tatu kwa mwaka, kamwe hawezi kubadilisha taratibu
hizo hata pale anapokuwa kwenye familia yake, anapotoka katika mikono ya
wazazi.
Hilo
ni tatizo kubwa. Linakuwa siku hadi siku. Hakuna mwenye mapenzi mema na moyo wa
kujifunza vitu vinavyohusu historia ya maisha yao. Ni wageni kila wakati, kiasi cha
kushindwa kujua mahala gani kuna vitu vya kustaajibisha.
Kwa mfano, unaweza kushangaa kusikia wapo watu wanaoishi
karibu na Mlima Kilimanjaro, lakini hawajawahi hata siku moja kupanga namna ya
kuupanda mlima huo mrefu Barani Afrika, badala yake wanasuburi wazungu waende
kutalii.
Kwa bahati mbaya, wazawa wanagoma kuzunguukia hifadhi hizo
kwa visingizio visivyokuwa na mashiko, maana katika kufanikisha suala hilo la kukuza utalii wa
ndani, utaratibu mzuri umewekwa na gharama nafuu kwa kila Mtanzania.
Nadhani ni hapo unapokaa na kupongeza mawazo ya kutangaza
sekta zetu za utalii, kubuni mbinu mpya za kuwafikishia ujumbe Watanzania juu
ya kuweka utaratibu wa kutembelea katika hifadhi zao, ukiwamo Mlima
Kilimanjaro.
Mlima ambao unasisimua kuutazama katika picha na kuleta hamu
kubwa ya kuupanda, ukizingatia kwamba una historia kubwa ya maisha ya Tanzania
na watu wake.
Nasema haya baada ya kuona juhudi za Kampuni ya KJ Traders
kuandaa matembezi ya mlima Kilimanjaro, Desemba sita mwaka huu kwa ajili ya
kutangaza sekta ya utalii wa ndani, huku wakishirikiana na Bodi ya Utalii
Tanzania (TTB).
Matembezi hayo yamepangwa kuzinduliwa na Mkuu wa Majeshi
Mstaafu, Generali George Waitara, yakiwa na lengo na kutangaza mlima huo na
kuamsha hisia mpya kwa Watanzania kwa ajili ya kupenda vitu vyao.
Mratibu Mkuu wa matembezi hayo ni Joseph Kitina, akileta
matumaini na funzo kwa kila Mtanzania kuona kuwa ana deni la kupanga ratiba ya
kutembelea sehemu mbalimbali za nchi katika hali ya kuangalia vivutio vyetu vya
utalii.
Endapo tutakuwa tunaelewa thamani ya vitu vyetu, hata wale
wanaokuja wataweka mkazo zaidi hivyo kuvutia makundi ya watalii watakaoingia nchini.
Kama Watanzania wenyewe watashindwa kuweka mbinu za
kutangaza vivutio vyao, hakuna anayeweza kubadilisha mtazamo wao. Ndio maana kila
juhudi zinazofanywa kwa ajili ya kutangaza utalii wa ndani zinakwama.
Jukumu la kutembelea vivutio vyetu visiachwe kwa wageni tu,
hivyo kuna haja ya kushirikiana kwa pamoja na wadau wa sekta ya utalii,
wakiwamo KJ Traders.
Huo ndio ukweli. Yoyote yule anayekwenda nje ya eneo lake na
kukaa walau kwa saa 24, basi huyo ni mtalii. Haijalishi anakwenda huko kufanya
kitu gani. Iwe ni kutembelea hifadhi za Taifa, kuhudhuria mikutano au kufanya
biashara zake.
Tofauti ya mtalii wa ndani ni kuwa huyu analipia gharama
ndogo kwa pesa za ndani, wakati mtalii kutoka nje ya nchi, hawa hulipia kwa
pesa za kigeni. Mtu anapokuwa kwenye shughuli hizo za kitalii, kunakuwa na
faida kubwa kwake na kwa Taifa husika.
Kazi kama vile upigaji wa picha, utafiti wa vitu mbali mbali,
ukiwamo miti na wanyama, au kuangalia mbuga za wanyama, ni kati ya mambo ambayo
mtu anapoyafanya eneo husika, basi amekuwa katika msingi ule wa utalii.
Wakati hayo yakiweza kufanywa na kila mdau wakiwamo hao KJ
Traders kwa kushirikiana na TTB na Wizara husika ya Maliasili na Utalii, Tanzania
imejaliwa kuwa na vivutio vingi vya Utalii katika kila mkoa na kuleta faida
kubwa.
Ukiacha huo Mlima wa Kilimanjaro ambao baadhi yao huthubutu kusema upo katika nchi jirani ya Kenya, lakini Tanzania
pia imejaliwa kuwa na maeneo mengi ambayo kila mmoja kwa nafasi yake yanaweza
kuiletea tija nchi yao.
Hifadhi kama vile Ngorongoro, Mikumi, Hifadhi ya Ziwa
Manyara, Ziwa Ruaha, Selous na mengineyo mengi ni kati ya sehemu ambazo
zikitangazwa kwa kiasi kikubwa na Watanzania wenyewe, nchi inaweza kuingiza
fedha nyingi za kigeni.
Lakini sisi wenyewe tukidharau thamani zetu zilizozaga
katika mikoa mbalimbali, hakika hatuwezi kusonga mbele kwa lolote. Huo ndio
ukweli. Katika kuusema, natumaini pia wale wenye mtazamo tofauti juu ya sekta
ya utalii watabadilika.
Watazinduka na kuona kuwa kila mmoja lazima awe balozi wa
kutangaza utalii wa ndani. Kila mmoja anapaswa kuona kuwa juhudi zake na uwepo
wake unafanikisha kwa dhati kuwashawishi wageni kutembelea, endapo yeye naye
ana uelewa huo.
Kampuni ya KJ inakuja na mtazamo huo wa kutembelea mlima
Kilimanjaro katika kipindi ambacho, sekta ya utalii ni moja wapo ya faida kwa
nchi zote duniani. Kwa kujitangaza, sekta hiyo itapiga hatua na kukuza uchumi
wa Taifa.
Kila mmoja anapaswa kufunga mkanda. Awe mlinzi na balozi wa
kweli. Ahoji baada ya kufahamu namna gani nchi inaweza kujitegemea kwa kupitia
sekta ya utalii, sambamba na kulinda hifadhi zetu ili ziwe za kuvutia.
Maeneo ya hifadhi yenye mgogoro mkubwa na wananchi, basi
kero hizo zitatuliwe kwa haraka ili kuwafanya nao wapende rasilimali hizo.
Kuna baadhi ya wananchi wamekuwa mbogo wanapoona baadhi ya
vivutio vilivyopo katika maeneo yao
vinachangia kuhangaika kwao ama kufanyiwa vitendo visivyokuwa vya kiungwana.
Kila mmoja ajuwe wajibu wake. Naamini kwa kuanzisha
utaratibu huo wa kutembelea hifadhi ya Mlima Kilimanjaro Desemba sita na
kufikia kilele chake Desemba tisa, kutachochea ari mpya kwa kila mtu na kupiga
hatua ya juu zaidi.
Utalii ni fedha. Kila mtu anayekuwa karibu na eneo husika
anaweza kuingiza chochote kitu kutokana na mzunguuko wa pesa, ukiacha zile
fedha zinazoingia kwa serikali, hivyo kuufanya uchumi wan chi usonge mbele
zaidi.
Haya yanakuja wakati ambao watu wanaamini kuwa kuna kila
sababu ya kuweka mkazo katika vivutio vyetu vya utalii, sambamba na kuibua ari
kwa watu kwa ajili ya kujipa tabia ya kutembelea kila wanapopata muda kwenye
hifadhi za Taifa.
Tukutane wiki ijayo.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment