Asha Baraka, Mkurugenzi wa Twanga Pepeta
Na Kambi Mbwana, Dar
es Salaam
MKURUGENZI wa bendi ya The African Stars, Twanga Pepeta,
Asha Baraka, amesema bendi yake ina wanamuziki wengi kiasi kwamba wengine
wanashindwa kupanda jukwaani zaidi ya mara tatu katika kumbi nyingi wanazofanya
shoo.
Hiyo ni kauli ya kwanza kutolewa na mwanamama huyo ambaye
tangu kutangaza kuondoka kwa nguli wa muziki wa dansi nchini kwenye bendi hiyo,
Mwinjuma Muumini, Asha hajasikika akisema lolote juu ya kuhama kwa mkali huyo.
Akizungumza mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Asha alisema kwamba bendi yake
ina waimbaji wengi na hawawezi kuwa na upungufu wa aina yoyote katika safu zao,
licha ya kuhama tena kwa Muumini.
Alisema wapo waimbaji wanaopanda jukwaani mara moja kwa siku
katika shoo zao, hivyo ni wazi kuwa wengine wanachukulia nafasi hiyo kutafuta
mahali kwa kuonyesha makali yao
zaidi katika ramani ya muziki wa dansi nchini.
“Mpaka sasa wapo waimbaji zaidi ya watano ambao ni mahiri na
wana mashabiki wengi, akiwamo Kalala Junior, Dogo Rama, Salehe Kupaza, Badi
Bakule, Luiza Mbutu, Janeth Isinika, Amigo Ras na wengine wenye wapenzi lukuki.
“Naamini bila hata kuangalia nani hayupo kwetu, tunapaswa
kujivunia kuwa nao waliokuwapo kwasababu wanamuziki wanapokuwa wengi zaidi,
lazima wachache wao waimbe wimbo mmoja shoo nzima,” alisema.
Twanga Pepeta ni miongoni mwa bendi zinazofanya vyema katika
tasnia ya muziki wa dansi hapa nchini, ikiwa na nyimbo nzuri zinazopendwa na
wengi, ukiwamo wa ‘Shamba la Twanga’ unaozidi kuiweka juu bendi hiyo.
No comments:
Post a Comment