Na Kambi Mbwana, Dar
es Salaam
MSIBA wa msanii nyota wa uchekeshaji hapa nchini, Hussein
Mkiety, maarufu kama 'Sharomilionea' umegusa hisia za wengi, huku King Majuto akikimbizwa
Hospitali baada ya kushikwa na presha, hivyo kutishia usalama wake.
Mtoto wa King Majuto, Hamza Majuto, aliimbia HANDENI KWETU
kuwa hali ya baba yake inaendelea vizuri kutokana na kuumizwa zaidi na msiba wa
Sharomlionea anayetamba katika ulingo wa filamu na muziki hapa nchini.
Nyota wa comedian nchini, Hussein Mkiety Sharomillionea alivyokuwa enzi za uhai wake.
Juu akiwa na nguli wa comedian nchini, King Majuto, aliyeumizwa sana na msiba huo.
Msanii huyo alikufa juzi saa mbili za usiku Maguzoni,
kilimita chache na kijijini kwao Lusanga, wilayani Muheza mkoani Tanga, baada
ya gari lake alilokuwa akisafiria lenye namba za
usajili T478 BVR Toyota Harrier kupinduka na kusababisha kifo chake.
Kamanda wa Polisi mkoani Tanga, Constantine Masawe, alikiri
kutokea kwa msiba huo na kusema kuwa mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali
ya Teule, Muheza, mkoani Tanga kwa taratibu za mazishi zinazopangwa na familia
yake.
“Marehemu alikufa majira ya saa
mbili za usiku kwenye barabara ya Segera alipokuwa anatoka Dar es Salaam kwenda
Muheza, hivyo mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Teule, huku gari lake likihifadhiwa
pia kwasababu haliwezi kutembea,” alisema Masawe.
Taarifa za kifo cha msanii huyo aliyeibukia hivi karibuni na
kufanya vema katika ulingo huo zilianza kuzagaa saa tatu za usiku, ikiwa ni
dakika chache baada ya kufariki katika ajali hiyo ya kusikitisha kwa nyota
huyo.
Katika mitandao yote ya kijamii kuanzia saa tatu za usiku
zilizagaa habari zake, huku kila mmoja kiwa na hisia tofauti zilizotokana na
madai ya kifo cha msanii huyo, ambaye baadaye jeshi la Polisi lilithibitisha
kwa kupitia Kamanda wake, Masawe.
Sharomilionea ameshacheza filamu nyingi za uchekeshaji na
kujipatia sifa kubwa, ikiwamo ile ya Sharo Millionea, Imekula Kwako, Jini
Mahaba, Porojo na nyinginezo zinazofanya vyema katika tasnia ya filamu nchini.
Katika filamu ya Jini Mahaba, Sharomillionea anayetamba pia
kwa msemo wake wa ‘Umebug Men’, anacheza kama
mtu maarufu anayekwenda kujitambulisha kwa wake zake (Kingwendu) na kushangazwa
na hali zao za maisha.
Sharomillionea anamshangaa mama yake mkwe anavyochambua
mboga za majani wakati yeye sio utaratibu katika maisha yake. “Huyu ndio mama
yako Men? Mbona anachambua majani,” aliuliza huku anakunja mdomo wake na
kujifuta uso.
Maneno hayo yanamuumiza mama yake mkwe na kuamua kumuita
mume wake (Kingwendu) na kuja kushangaa Sharobalo alivyokuwa katika mueneko wa
super Star na kujikuta akipagawa alipoanza kukejeliwa na mkwe wake.
Mbali na filamu hiyo ya Jini Mahaba, mkali huyo pia ametamba
katika filamu nyingi pamoja na nyimbo mbili alizorekodi, huku pia akililiwa na
wasanii wenzake kutokana na ushirikiano wake, mara baada ya kuibuka kisanii.
Wasanii wengi waliozungumzia kifo cha Sharomillionea
wakiongozwa na Steve Nyerere, walionyeshwa kuchanganyikiwa kwa msiba wa msanii
aliyeanza kutokea peupe na kutamba mno katika sanaa ya uchekeshaji.
Sharomillionea aliyetokea katika ubavu wa nguli wa
vichekesho nchini, King Majuto, anazikwa kesho Jumatano, kijijini kwao Lusanga, huku
wasanii wengi wakitarajia kuhudhuria msiba na mazishi ya nyota huyo aliyeipenda
pia nyumbani kwao Muheza.
No comments:
Post a Comment