Na Kambi Mbwana, Dar
es Salaam
MWIMBAJI wa muziki wa kizazi kipya, Ahmad Ally ‘Madee’,
amesema ni ujinga kama ataamua kulikimbia kundi aliloasisi mwenyewe la Tip Top
‘Connection’ la Manzese, jijini Dar es Salaam kama wanavyozusha baadhi ya wadau wa muziki huo nchini.
Habari za Madee kulihama kundi hilo
zilienea wiki kadhaa zilizopita na kugusa watu wengi, jambo ambalo hata hivyo
limedaiwa kupikwa na watu wasiokuwa na nia njema na kundi hilo linalotesa katika muziki huo nchini.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam,
Madee alisema kwamba kama ataamua kukimbia kundi hilo, ni wazi atakuwa amefanya kitu cha
kushangaza, maana yeye ni miongoni mwa
waasisi wake hivyo hawezi kuchukua uamuzi huo.
Alisema kama kutakuwa na tofauti miongoni mwa wasanii,
atakachofanya ni kuwekana sawa lakini sio uamuzi wa kuhama na kufanya muziki
nje ya kundi hilo
kwa madai kuwa haliwezi kumjenga zaidi ya kumbomoa kisanaa.
“Nimekuwa mwasisi wa kundi la Tip Top Connection hivyo kamwe
siwezi kuhama kama wanavyosema baadhi ya watu
ambao hawaangilii wapi tunapotoka na tunapokwenda katika sanaa ya muziki wa
kizazi kipya.
“Siwezi kuhama Top Top na kama
kutakuwa na tofauti nitakuwa mwepesi kukaa na kulizungumzia na sio uamuzi huo
ambao daima najua utafanywa kwa ajili ya kuliangamiza kundi hili lenye umri mrefu
kwa sasa,” alisema Madee.
Tip Top licha ya kuwa na wasanii mahiri katika kona ya
muziki huo nchini, lakini limekuwa likikabiriwa na changamoto za wasanii wake
kulihama kwa sababu mbalimbali, yakiwamo maslahi kama
yanavyodaiwa na wahanga wenyewe.
No comments:
Post a Comment