Na Kambi Mbwana, Muheza
MKUU wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu, jana aliwakera watu
wengi waliovamia hospitali ya Teule kwa ajili ya kuangalia jinsi msanii Hussein
Mkiety, maarufu kama Sharomillionea
anavyoandaliwa kwa ajili ya kuzikwa kijijini kwao Lusanga, wilani Muheza,
mkoani Tanga.
Kabla ya hapo, baba mkubwa wa Marehemu, aliweka utaratibu wa
baadhi ya ndugu na jamaa kushiriki kwa karibu kuandaa mazishi ya msanii huyo
aliyefanya vyema katika sanaa hapa nchini.
“Haiwezekani jamani watu wote mliokuwapo hapa kuingia katika
chumba cha kuhifadhia maiti badala yake wote tuhamie nyumbani kwao kwa ajili ya
kuzika na sio kuminyana hapa.
“Naamini uamuzi huu ni mbaya na unakera kwa kiasi kikubwa,
lakini lazima mjuwe kuwa naongea hapa kama mtu wa serikali na itakuwa vyema
kama mashabiki na wakazi wote wa Tanga tutaelewana katika hilo,” alisema Subira
huku akiangaliwa vibaya na wananchi.
Kauli ya Mkuu huyo wa Wilaya ya Muheza, ilifuatiwa na amri
ya jeshi la Polisi kuwazuia watu kuendelea kuingia katika upande wa chumba cha
kuhifadhia maiti.
Idadi kubwa ya mashabiki na wasanii walikuwa wengi katika
wilaya ya Muheza kuangalia namna gani kijana wao mpendwa anaingizwa katika
nyumba ya milele baada ya kufariki kwa ajali ya gari karibu na kijiji chao cha
Lusanga.
No comments:
Post a Comment