Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbroad Slaa
Na Kambi Mbwana, Dar
es Salaam
JUHUDI za kukiangusha Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimeishiwa
nguvu badala yake tunashuhudia wapinzani, wakianza kuvutana wenyewe. Wapinzani
wameanza kuvutana, kutukanana au kurushiana makombora ya kila aina.
Jambo hilo
ni baya. Sidhani kama wataweza kweli kutimiza azma yao. Zaidi wataipa ushindi wa kishindo CCM
katika chaguzi zake zote zinazokuja mbele yake.
Nasema hivyo maana wafuasi wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) wamekuwa wakiwadharau wenzao wa Chama cha Wananchi (CUF),
wakisema wameishiwa.
Sawa, huenda ni kweli CUF wameishiwa, lakini hizo kejeli, zingefaa kutolewa na wafuasi wa CCM, wasiopenda kuona chama chao kinatoka madarakani.
Kinyume chake, kejeli na masimango zinatoka kwa Chadema,
chama kinachojiita kuwa ni namba mbili baada ya CCM.
Wakati haya yanaendelea, ni vigumu sana kuamini kweli CCM inatong’oka. CCM
kung’oka ni ngumu. Haitang’oka kamwe. Kwanini nasema hivyo? Wapinzani
wamemuacha adui yao
na wameanza kupigana wenyewe.
Kwa bahati mbaya, muunganiko wa vyama vya upinzani umekuwa
mgumu mno kufanikiwa. Hii ni kuonyesha kuwa wote wana malengo ya kuongoza.
Inaonyesha dhahiri nao wana kiu ya kujinufaisha wao na sio Watanzania wao.
Haya pia yaangaliwe. Kwa mfano, kila kinachofanywa na CUF
leo, lazima kisemwe na kusimangwa na
wapinzani wenzao. Ni ajabu. Hawa
wanapigana na CCM au CUF? Ama nao wameona CUF ni adui yao namba moja?
Kama ni kweli CUF ni adui
ya Chadema, basi wanapaswa wapigane kwanza wao kwa wao, kabla ya kuigeukia CCM
ambayo ipo madarakani. Haya yasemwe bila kuficha, hata kama
yatapokelewa kwa shingo upande na wenye vyama vyao.
Sote tunajua siasa za Tanzania. Lakini, ukiangalia
utagundua kwamba msigano zaidi unahamia CUF na Chadema, hivyo nguvu zao kwa
chama tawala ni ndogo mno.
Jambo hilo
linaipa ushindi zaidi CCM, ingawa wakati mwingine porojo, propaganda hutungwa
kwa umahiri wa aina yake kuaminisha wanachotaka wao.
Kwa mujibu wa Naibu Katibu wa CUF Tanzania Bara, Julius
Mtatiro, baadhi ya watu wa Chadema walikuwa wakipita katika maeneo mbalimbali
ya Bagamoyo wakisema kuwa mgombea wao amejitoa, hivyo wahamie Chadema.
Sawa hizi huenda ni mbinu za kampeni, lakini zinaashiria
kuwa kama ni kweli, basi wapinzani kwa
wapinzani wameamua kukomoana na kuiacha CCM iendelee kutesa kileleni.
Na mfumo huo umeifanya CCM iibuke kidedea katika kata nyingi
zilizofanya Uchaguzu Mdogo na kuwaacha wapinzani wakigawana viti sita tu.
Huu ni ushindi wa kishindo. Watu walitarajia labda CCM
ingeanguka zaidi katika uchaguzi huo, lakini Watanzania haswa wale wapenzi wa
CCM wakishuhudia mafanikio makubwa katika Uchaguzi huo mdogo.
Chadema wamekuwa wakipita huku na kule kusema kuwa CUF
wanaiga kila wanalofanya, ikiwamo harakati zao walizozipa jina la Movement for
Change (M4C), vugu vugu la mabadiliko katika harakati zao za operesheni Sangara
huku wapinzani wao nao wakizindua zao zilizokwenda kwa jina la Vision for
Change (Dira ya Mabadiliko).
Mvutano ulikuwa mkubwa mno. Hadi viongozi wa CUF walipotolea
ufafanuzi suala hilo,
wakisema harakati zao walizindua rasmia mwaka 2010 huku Chadema wao wakizindua
kwa mara ya kwanza mwaka 2012.
Sitaki kusema nani yupo sahihi katika vita hiyo, maana
nashangazwa na nguvu kubwa ya kudharauliana juu ya vyama hivyo vya upinzani.
CUF na Chadema hawatakiwi kufanyiana umafia, badala yake
wasaidiane kila linalowezekana kama kweli
lengo lao ni kuingia Ikulu na kuwaongoza Watanzania.
Ukisema hili watashangaa. Watasema hawana imani na CUF maana
kuna dalili kubwa kuwa ndugu zao hao wameingia kwenye ndoa na CCM. Wanaogopa
nao kuingia kwenye ndoa hiyo.
Ikiwa huo ni ukweli, ina maana sasa njia yao kuu ni kukikashfu kwa kila walivyoweza
ili kukichafua zaidi kwa Watanzania? Silaha kubwa ya Chadema ni kuona mikutano yao mingi inahudhuliwa na wananchi wengi, hata kama sio wapiga kura.
Wanashindwa kujua kuwa wengi wanaoingia katika viwanja vya
mikutano yao,
sio wapiga kura na inapofikia wakati huo hukaa pembeni. Ni hujuma kubwa.
Watanzania wengi wakiwamo vijana hawajui thamani ya kura zao.
Ni wepesi mno kuandamana lakini mifukoni mwao, majumbani
mwao hawana vitambulisho vya kupigia kura. Utashangaa, mihemko yao, kurusha matusi au
kufanya kila wanachoambiwa, wanapata wapi ujasili huo?
Mimi nilidhani CUF, Chadema na vyama vingine vya upinzani
vingekaa pamoja kumjadili mpinzani wao, CCM na sio kuanza kuparuana wenyewe,
kutumia nguvu kubwa kuhujumiana maana, ukizingatia kuwa dola ipo chini ya chama
tawala.
Wafuasi wa vyama hivyo hawatakiwi kusemana, kutukanana au
kuambiana lolote lisolojenga siasa za upinzani badala ya kubomoa zaidi. Kama
wote nia yao ni
kukiangusha chama tawala, kwanini sasa wanaona wao kwa wao ni maadui?
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba na
viongozi wenzake, akiwamo Katibu Mkuu wake, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Zanzibar,
Maalimu Seif Sharif Hamad aone mpinzani wao ni CCM na sio CUF.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake waone kuwa
adui yao si CUF
bali ni CCM, hivyo kufanya mikakati ya pamoja kukiondoa madarakani.
Kulisema hili kunahitaji ujasili, maana baadhi yao lengo lao ni kuongoza tu, hata kama sera na mikakati yao ina matege.
Najua yapo mapungufu mengi ndani ya CUF, lakini pia ni kama ilivyokuwa kwa wenzao Chadema, wanaofanya mambo
ambayo wakati mwingine yanashangaza. Hayo nayo ni mapungufu, ndio maana wanaona
vyama vyote ni adui yao.
Wao wakifanyiana umafia, CUF kuwasimanga Chadema, CCM
wanakuwa na kazi ndogo, ndio maana hata ushindi wao unaendelea kuwapo Tanzania.
Hata mwaka 2015, CCM itashinda kwa kishindo, ukizingatia
kuwa imewaachia wenyewe wapinzani watoane roho na wao kumalizia kidogo tu ili
wakubaliwe na Watanzania.
Ni rahisi CCM kuwaambia wapinzani ni waroho wa madaraka,
hawawezi kuwaongoza pamoja na vita ya udini na ukabila inayowezwa kuenezwa
zaidi kwa vyama hivyo vya upinzani na watu kuielewa na kuwaweka pembeni.
Huo ndio ukweli. Kwanza
wanahesabu viongozi waliokuwapo Chadema na asili zao. Pili wanarudi kwa wale
wanaosemwa na wenzao. Yani chanzo cha Chadema kuwadharau CUF na mengineyo
mengi, hivyo jibu kuwa hawa ni wadini na wakabila.
Kama hayo yakienezwa na kusomwa na Watanzania, kila mwenye
ndoto za amani, kuipenda Tanzania
yake, kuona utawala wa haki na sheria, hakika hawezi kuikacha CCM zaidi ya
kukichagua tena na tena katika chaguzi zake.
Vyama vya upinzani, vikiwamo CUF na Chadema waone kuwa
malumbano yao,
kufanyiana umafia ni karata turufu kwa kwa CCM na hawawezi kuindosha
madarakani.
Vinginevyo, kazi wanayo.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment