Na Mwandishi Wetu, Kibaha
MKUU wa Wilaya Kibaha, mkoani Pwani, Mheshimiwa Asumpter
Mshama, amewapongeza washindi wa Bahati Nasibu ya Biko ‘Ijue Nguvu ya Buku’ na
kuwataka kuweka umakini na malengo katika fedha zao wanazokabidhiwa ili
wanufaike kiuchumi.
Meneja Masoko wa Bahati Nasibu ya Biko, Goodhope Heaven kushoto akimuelekeza jambo Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mheshimiwa Asumpter Mshama katikati wakati wa kumkabidhi mshindi wa Sh Milioni 20 wa droo ya 19 ya Biko, Elisiana Laizer kulia mwenye gauni jekundu ndani ya benki ya NMB, Tawi la Mlandizi, wilayani Kibaha, mkoani Pwani.
DC Asumpter ameyasema hayo jana katika tawi la NMB, Mlandizi,
Wilayani Kibaha, mkoani Pwani katika makabidhiano ya Sh Milioni 20
zilizokabidhiwa kwa Mshindi wa droo ya 19, Elisiana Simon Laizer, mjasiriamali
wa kutengeneza sabuni, mwenye maskani yake Mlandizi, aliyeibuka kidedea katika
droo ya 19 ya bahati nasibu hiyo ya aina yake inayochezwa kwa njia ya ujumbe
mfupi wa maandishi kwa simu za mikononi za Tigo, Vodacom na Airtel.
Akizungumzia bahati nasibu hiyo ya Biko, DC Mshama alisema
michezo ya kubahatisha ina nafasi kubwa ya kukuza uchumi wao na uchumi wa Taifa
kwa kuhakikisha kwamba wanafanya shughuli zenye kuleta maendeleo badala ya
kuzitumia kwa mambo yasiyokuwa na msingi.






















