Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MAMBO yamezidi kunoga katika bahati nasibu ya ‘SMS’ ya Biko, ‘Ijue
Nguvu ya Buku’, baada ya mkulima kutoka wilayani Handeni, mkoani Tanga, Yahaya
Ally Khamis, kuibuka kidedea kwa kuzoa Jumla ya Sh Milioni 20 kutoka kwenye
bahati nasibu hiyo inayozidi kushika kasi nchini Tanzania, ikiwa ni droo yake
ya 15 tangu kuanzishwa kwake.
Mwakilishi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha nchini Tanzania, Humud Abdulhussein kushoto, akiagana na Balozi wa Biko, Kajala Masanja mara baada ya kumaliza kuchezesha droo ya 15 leo jijini Dar es Salaam, ambapo mkulima wa wilayani Handeni, mkoani Tanga, Yahaya Ally Khamis aliibuka kidedea kwa kuzoa jumla ya Sh Milioni 20.
Bahati nasibu hiyo imechezeshwa leo jijini Dar es Salaam na
Balozi wa Biko, Kajala Masanja kwa kushirikiana na mwakilishi wa Bodi ya
Michezo ya Kubahatisha Tanzania, Humud Abdulhussein.
Akizungumza katika droo hiyo, Meneja Masoko wa Biko, Goodhope
Heaven, alisema kwamba bahati nasibu yao imezidi kupanua mbawa zake kwa kutua
wilayani Handeni, mkoani Tanga kwa mshindi wao Yahaya ambaye ana umri wa miaka
50 anayejishughulisha na kilimo.
Alisema ni faraja yao kuona mchezo wao umekuwa ukitoa
washindi katika sehemu mbalimbali za Tanzania, akiamini kuwa ni mwendelezo wa
kuhakikisha kwamba kila mtu anaibuka na mamilioni ya Biko.
Balozi wa Biko Kajala Masanja akichezesha droo ya 15 ya Bahati Nasibu ya
Biko ambayo donge nono la Sh Milioni 20 liliangukia kwa mkulima wa
wilayani Handeni, mkoani Tanga, Yahaya Ally Khamis baada ya kuchezeshwa
droo hiyo jana, jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mwakilishi wa Bodi ya
Michezo ya Kubahatisha Tanzania, Humud Abdulhussein.
Kucheza mara nyingi zaidi ndio nafasi ya ushindi, hivyo
tunawaomba Watanzania wacheze kwa wingi na mara nyingi zaidi kwa kupitia
mitandao ya simu za mikononi ya Tigo Pesa, M-Pesa na Airtel Money ambapo mbali
na donge nono la Sh Milioni 20 linalotolewa kwa washindi Jumatano na Jumapili,
pia tunatoa zawadi za papo kwa hapo kuanzia Sh 5,000, 10,000, 20,000, 50,000,
100,000, 500,000 na Sh Milioni 1,000,000 zinazolipwa kwenye simu za washindi
walizotumia kuchezea bahati nasibu yetu,” Alisema Heaven.
Akizungumza kwa simu saa chache baada ya kutangazwa mshindi,
Khamis, alimshukuru Mungu kwa kumletea zawadi nzuri ya Sh Milioni 20 kwa
kupitia mchezo wa Biko unaochezeshwa kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi kwa
mitandao ya simu ya Tigo, Vodacom na Airtel.
“Namshukuru Mungu kwa kunipa zawadi hii kutoka Biko,
nikiamini kuwa fedha hizi zitanipatia mafanikio makubwa kwa kupitia biashara
zangu za kilimo ninazoshughulika nazo,” Alisema Khamis. Naye mwakilishi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania,
Abdulhussein, aliupongeza mchezo wa Biko na kuongeza kuwa unachezeshwa kwa
kufuata sheria, kanuni na taratibu zote.
No comments:
Post a Comment