Na Mwandishi
Wetu, Tanga
TAASISI ya
Kifedha ya Bayport Financial Services, imekabidhi kompyuta nane katika wilaya
za Handeni, Korogwe, Muheza na Pangani zote za mkoani Tanga, ikiwa ni
mwendelezo wa msaada wa kompyuta 205 zenye thamani ya Sh Milioni 500 kwa ajili
ya ofisi za serikali nchini Tanzania, huku mpango huo ukiasisiwa mwishoni mwa
mwaka jana.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, William Mwakufwe aliyeshika sehemu ya kompyuta akiwa na Mratibu wa Masoko wa Bayport Financial Services, Mercy Mgongolwa wa pili kutoka kulia pamoja na Meneja wa Bayport Handeni, Candy Masunzu. Kushoto ni Afisa Utumishi wa Wilaya ya Handeni, Noel Abel katika tukio la kupewa msaada wa kompyuta mbili kutoka Bayport wiki iliyopita wilayani Handeni, mkoani Tanga.
Utaratibu wa
makabidhiano ya kompyuta hizo ulianza Handeni Jumatatu ya Juni 5, huku wilaya
ya Korogwe wakipokea Juni 6, Muheza Juni 7 kabla yakumalizia Pangani Juni 8,
ambapo kila wilaya ilipokea kompyuta mbili kwa ajili ya kupunguza changamoto ya
vifaa vya kiutendaji katika ofisi za umma.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Korogwe, George Nyalonga mwenye koti jeusi naye akipokea kompyuta mbili kutoka Bayport wiki iliyopita.
Akizungumza
mjini Tanga katika makabidhiano hayo, Mratibu wa Masoko na Mawasiliano wa
Bayport Financial Services, Mercy Mgongolwa, alisema ni furaha yao kuona mpango
wao wa kutoa kompyuta kwa ofisi za umma unaendelea vizuri kwa Mkoa wa Tanga
kufikiwa na msaada huo.
Mratibu wa Masoko wa Bayport Financial Services, Mercy Mgongolwa wa tatu kutoka kushoto waliosimama akimkabidhi sehemu ya kompyuta mbili Afisa Utumishi wa Wilaya ya Muheza, Godhope Ringo, akiwa na baadhi ya watumishi wa wilaya ya Muheza katika tukio hilo lililofanyika wiki iliyopita wilayani humo.
Alisema
taasisi yao itaendelea kuwa karibu na serikali kwa kushiriki kutatua changamoto
zilizokuwa ndani ya uwezo wao pamoja na kushirikiana na Watanzania wote kwa
kupitia sekta ya mikopo ili kuhakikisha kwamba nchi yao inasonga mbele
kimaendeleo.
“Tupo katika
serikali ya Hapa Kazi Tu kama alivyoasisi Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dr John Pombe Magufuli, hivyo kwa kuliona hilo taasisi ikaona ipo
haja ya kusambaza kompyuta kwa ofisi za serikali ambazo hata hivyo utaratibu wa
kutoa msaada huu ulipangwa na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, chini ya Waziri wake, Mh Angelllah Kairuki
mwaka jana,” Alisema Mercy.
Naye
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Korogwe, George Nyalonga, aliwapongeza
Bayport kwa kuamua kujitoa katika jamii sambamba na serikali yao hususan baada
ya kusambaza kompyuta huku wilaya yake ikipangwa kupokea kompyuta mbili.
“Hakika
nawashukuru sana Bayport kwa kutusaidia kompyuta mbili kwenye Halmashauri yetu,
nikiamini kuwa zitatusaidia kwa kiasi kikubwa mno na kufanikisha utendaji kazi
bora kwa watumishi wa umma na kuwezesha ndoto za kuwaletea maendeleo wana
Korogwe,” Alisema Nyalonga.
Wilaya ya
Muheza kompyuta hizo zilipokewa na Afisa Utumishi wake Godhope Ringo, ambapo
hakusita kuonyesha furaha ya vitendea kazi hivyo akisema kukua kwa sayansi na
teknolojia ni sehemu ya kuhitajika kwa kiasi kikubwa matumizi bora ya kompyuta
kwenye ofisi zote za umma.
“Kwa niaba
ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Muheza, hakika tumepokea kwa
shauku kubwa mashine hizi mbili na tunawaomba muendelee kushirikiana na sisi
kwa namna moja ama nyingine hususan za kuhakikisha kwamba wilaya yetu na
Tanzania kwa ujumla inasonga mbele,” Alisema Ringo, mbele ya wakuu wa Idara wa
Halmashauri hiyo.
Kwa
kusambaza kompyuta hizo nane katika wilaya nne za Mkoa wa Tanga, Bayport
inaendelea kutimiza ndoto zake kuhakikisha kwamba wanashirikiana na serikali
kuwapatia maendeleo Watanzania kwa sekta mbalimbali, ikiwamo ya mikopo ya fedha
inayotoa kwa miaka 10 tangu kuanzishwa kwake nchini Tanzania mwaka 2006 na
kuwawezesha watumishi wa umma kwa kiasi kikubwa ambao ndio wakopaji wake wakuu.
No comments:
Post a Comment