Na Mwandishi Wetu, Mbulu
KWA miezi kadhaa sasa mvua
imeendelea kunyesha katika mikoa mbalimbali ya Tanzania, hali inayoonyesha
kukidhi kiu ya watu wengi waliokuwa wakiiomba inyeshe katika maeneo yao.
Hata hivyo, licha ya mvua hiyo
kunyesha, lakini baadhi ya maeneo imekuwa na matokeo mabaya kutokana na kuezua
nyumba, kuharibu miundo mbinu muhimu ikiwamo ya barabara.
Matokeo hayo yameibua changamoto
mpya hususan za kufikika kwa urahisi katika maeneo hayo yanayoendelea kukumbwa
na mvua kubwa. Mbali na mvua hiyo kunyesha, hata hivyo uwajibikaji unaendelea
kufanyika kwa sekta na watu mbalimbali kuendelea na maisha yao ya kila siku ili
wakuze uchumi.
Zoezi la kutoa msaada wa kompyuta lilivyokuwa linaendelea katika mikoa mbalimbali ya Tanzania.
Licha ya maeneo mengi
kukumbwa na mvua, lakini Taasisi ya Kifedha ya Bayport Financial Services
imeendelea na usambazaji wa kompyuta katika ofisi za serikali mikoani kama
ilivyozindua utaratibu huo mwishoni mwa mwaka jana.
Bayport ambayo ni Taasisi ya Kifedha
inayojihusisha na mikopo ya fedha, mwaka jana ilianzisha mpango wa kusambaza
kompyuta kwenye ofisi za serikali ambapo tukio la uzinduzi lilihudhuliwa na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Angellah Kairuki. Jumla ya kompyuta ambazo Bayport
iliamua kuzisambaza kwa serikali ni 205, ambapo tayari maeneo mbalimbali
wamefikiwa na kompyuta hizo kwa ajili ya kupunguza changamoto ya vifaa vya
ofisi.
Akizungumza katika usambazaji wa
kompyuta kwenye mikoa ya Singida, Manyara, Iringa, Songwe na Ruvuma, Mratibu wa
Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Mercy Mgongolwa, anasema
licha ya mvua kubwa kupiga, lakini wameendelea na zoezi lao la kuhakikisha
wanafikisha msaada wa kompyuta.
Anasema kufikisha kompyuta hizo ni
sehemu ya kushirikiana vizuri na ofisi za umma katika mikoa ya Tanzania ili
waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi, ukizingatia kuwa baadhi ya ofisi zimekuwa
na tatizo la kukosa huduma muhimu za kompyuta.
“Hatujaangalia mvua kubwa
inayonyesha katika nchi yetu kwa muda mrefu sasa, badala yake tuliendelea na zoezi
letu zuri la kufikisha kompyuta katika ofisi za umma kama tulivyopewa mpangilio
mzuri na Wizara ya Utumishi mwaka jana.
“Ukiacha maeneo tuliyosambaza
kompyuta kwa hatua ya awali, msimu huu wa mvua pekee tumefikisha vifaa hivi
katika maeneo ya Mbulu (Manyara), Kilolo (Iringa), Kondoa, Mbinga (Ruvuma),
Songwe na Busokelo mkoani Mbeya ambapo kila ofisi ya Umma iliyopangwa kupokea
msaada huo ilipokea kompyuta mbili,” Alisema Mercy.
Mratibu huyo wa Masoko wa Bayport
anasema kwamba ulimwengu umebadilika kutokana na mahitaji makubwa ya sayansi na
teknolojia, hivyo wazo la kutoa msaada wa kompyuta limekuja wakati muafaka,
akiamini kuwa litapunguza changamoto ya utendaji hafifu wa watumishi wa umma
waliokuwa wanakabiliwa na uhaba wa kompyuta.
Anayataja maeneo mengine ya nchi
ambayo yamepokea kompyuta zao ni pamoja na Arusha, Kilimanjaro, Morogoro,
Mbeya, Mwanza na Bukoba, huku wakijipanga kwa maeneo mengine yaliyopangwa
wafikishiwe msaada huo haraka ambapo ukiacha kompyuta 125 zilizobakia Utumishi,
nyingine 80 zinaendelea kusambazwa katika mikoa mbalimbali ya Tanzania.
“Ni matumaini yetu kuwa watumishi wa
umma watatoa huduma bora kwa wananchi wao kwa kupitia msaada wa kompyuta
tunaotoa kwa ofisi serikali kama tulivyoelekezwa na serikali tulivyopeleka wazo
la kutoa msaada wa kompyuta 205 zenye thamani ya Sh Milioni 500,” Alisema
Mercy.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Mbulu, mkoani Manyara, Deogratias Kashasha, anasema msaada wa kompyuta mbili
waliyopokea kutoka Bayport umekuja wakati muafaka, hivyo ni wajibu wao kufanya
kazi kwa bidii kwa kuzitumia vyema mashine hizo.
“Wenzetu wa Bayport wamefanya jambo
sahihi kwa sababu wametuletea msaada wa kompyuta ambazo kwa hakika zitatusaidia
kwa namna moja ama nyingine kutoa huduma bora kwa Watanzania kwa kupitia ofisi zetu.
“Dunia ya leo inahitaji matumizi
makubwa ya kompyuta kwa mambo mengi, hivyo wakati tunashukuru kwa msaada huu,
niwahakikishie kwamba zitarahisisha utendaji kazi kwa watumishi wetu kulingana
na matumizi tutakayojipangia,” Alisema Kaimu huyo Mkurugenzi wakati anapokea
kompyuta hizo hivi karibuni ofisini kwake.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Singida, Rashid M.Mandoa Anasema kwamba ni jambo la kutia moyo kuona taasisi ya
Bayport imeamua kujitoa vyema kusaidia wadau wao kuwasaidia vifaa vya
kiutendaji vya kompyuta ambazo ni muhimu.
Anasema hakuna asiyejua umuhimu wa
kompyuta kwa mambo mengi kama vile kuweka rekodi mbalimbali za kiofisi,
kuunganisha mawasiliano ya kiofisi au hata kuweka urahisi wa kumbukumbu katika
maeneo mengi hali inayoweza kurahisisha.
“Tumepokea msaada huu wa kompyuta
mbili kutoka kwa Bayport likiwa ni wazo zuri lililoanzishwa mwaka jana
tulipoona linazinduliwa pia na ofisi ya Utumishi wa Umma kwa minajiri ya
kuorodesha maeneo yatakayofikiwa, huku wilaya yetu ikiwa miongoni mwao.
“Hakika tunashukuru kwa msaada huu
na kwa kiasi kikubwa utatusaidia kuwahudumia wana Singida ambao kwa namna
moja ama nyingine wana uhitaji mkubwa wa huduma bora kutoka kwenye serikali yao
ya Hapa Kazi tu,” Alisema huku akishuhudiwa na Meneja wa Bayport mkoani Singida
Awali Chaula.
Halmashauri ya Kilolo mkoani Iringa,
Mkurugenzi wake Violet Issacka Hakuwa nyuma kuwapongeza Bayport akiwataka
waendelee kushirikiana naye katika kuwakomboa na kuwahudumia wananchi kwa
kupitia sekta mbalimbali za kimaendeleo.
“Ni bahati kubwa kufikiwa na msaada
huu kwa sababu tunaamini si kila Halmashauri ya Tanzania inaweza kupata msaada
wa kompyuta kutoka kwenye taasisi ya Bayport Financial Services.
“Tufanya kazi kwa bidii na tunaomba
Bayport muendelee kushirikiana na sisi kwa mambo mengine ya kimaendeleo,
tukiamini kuwa uwezo huo mnao kutokana na kuguswa kwenu kwa mambo mengi ya
kijamii mnayoendelea kuyafanya kila siku,” Alisema.
Bayport ni miongoni mwa taasisi
zinazojitolea kwenye jamii kwa mambo mengi, huku mwaka jana wakifanya sherehe
kubwa za kutimiza miaka 10 ya huduma zao za mikopo sanjari na kujitolea kwenye
jamii kwa mambo mengi.
No comments:
Post a Comment