https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Friday, October 19, 2012

MAMBO FULANI MUHIMU


Mpe moyo, usimkatishe tamaa

              Wawili wapendanao.

MAMBO FULANI MUHIMU 
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NI dhahiri kila mtu ana mapungufu yake katika suala zima la uhusiano wa kimapenzi.

Sio wote ni wajuzi wa mambo. Sio wote wanaelewa wapi kwa kuwashika wenzao, hadi wajisikie raha katika suala la mapenzi.

                                                     Kambi Mbwana, Mwandishi wa Safu hii
Kila mtu na utundu wake. Wapo ambao ni wazito kabisa, wakikosa mbinu nzuri zinazoweza kustawisha mapenzi yao kwa wale waliowapenda.

Ndio, maana watu hao husubiri hulka na utundu wa wenzao tu, wakitaka waendeshwe kwa kila hatua. Waambiwe simama, inuka, lala au fanya hivi!

Bila kuendeshwa, kamwe hawawezi kung’amua wenyewe na kubuni yale yanayoweza kuwapa raha wenzao. Hayo ndio ya kujadili leo.

Naamini nitaweza kutoa darasa japo kwa kiasi kidogo, huku nitarajia kujibu maswali yako, hasa kama sitaingia moja kwa moja, kutokana na sababu za kimaadili, maana gazeti linasomwa na watu wengi, wakubwa na watoto.

Nimeamua kusema haya, huku nikijua fika, ingawa baadhi yao ni wazito, lakini wachache wao hupenda kujifunza na kuwagurahisha wapenzi wao.

Ni kutokana na hilo, kuna kila sababu ya kuwapa moyo, pale tutakapogundua kwamba kwa siku hiyo, wapenzi wetu wamejituma, kukazana na kufanya yale yaliyotupa raha na amani katika uhusiano wetu.

Tusiwanyanyase na kuwaona bado ni mizigo. Tuone kama walioamua kuwa na sisi kwa raha na tabu, ndio maana wanaamua kujitoa kwa moyo.

Kuna watu ambao hujikuta wakitoa matamshi makali kwa wapenzi wao. “Huna lolote, bado mgeni kwenye ulimwengu wa mapenzi na mengineyo.

Kuna mtu aliwahi kulalamika juu ya jambo hili. Dada huyo alisema, “sijawahi kusifiwa hata siku moja na kila siku naambiwa sifai”.

Kwa sababu hiyo, dada huyo alijikuta akihoji labda hayupo moyoni kwa mwanaume huyo, ambaye kwa hakika yeye amempenda na kuamua kujitoa kwake.

Sawa, lakini hapa udhaifu upo kwa mwanaume. Nasema hivyo, maana hajui harakati na jinsi gain wasichana wanatakiwa kupikwa kadri unavyotaka wawe.

Haya utayafanya siku chache baada ya kuingia naye kwenye makubaliano ya kuanzisha mapenzi, hivyo hakuna haja ya kuwaona si lolote si chochote.

Kama wewe ni hodari wa mapenzi, pia una wajibu wa kuelewa, si wote ni wajuzi, huku pia ukiwa mwepesi wa kumsifia mwenzako katika siku zote za uhusiano wenu, hasa kama amefanya kitu cha tofauti.

Kama leo unaona kabisa mpenzi wako amefanya jambo geni, kwanini usimsifie ili aongeze bidii? Haina haja ya kumuona mgeni kila wakati.

Kama mabadiliko yapo, ni wakati wako wa kuona kumbe uliyekuwa naye, angalau anaumiza kichwa, kuwaza namna ya kukutosheleza.

Anafanya hivyo maana hataki akukose. Hataki kuona unakuwa na uhusiano mpya kila wakati, ukizingatia kwamba wapo wanaoanzisha uhusiano mpya kwa kisingizio kuwa wapenzi wao, wake au waume zao hawawatoshelezi katika mambo fulani muhimu.

Huo ndio ukweli wa mambo, Tunapaswa kuwa makini kwa ajili ya kulinda, kudumisha na kustawisha uhusiano wetu, maana hapo ndipo utamu wa mapenzi unapoanzia na kushika kasi siku zote.

Tukutane wiki ijayo.

0712 053949
0753 806087

Thursday, October 18, 2012

Super D kumpika Ibrahim Mawe



                              Ibrahimu Mawe

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
BONDIA Ibrahimu Mawe, maarufu kama 'King Class Mawe', anatarajia kuingia kambini mwishoni mwa wiki hii kujiandaa na kujiandaa na pambano lake na Said Mundi, anayetokea Tanga, kwa Wagosi wa Kaya, litakalopigwa Desemba 9, katika Ukumbi wa PTA, Sabasaba, jijini Dar es Salaam na kusubiriwa kwa hamu na mashabiki wa ngumi.

Maandalizi ya Class Mawe, yanakuja siku chache baada ya kushinda katika patashika yake na Jonas Segu wa Dar es salaam, aliyempiga na kuwafurahisha mashabiki wake katika mchezo huo wa masumbwi hapa nchini.

Akizungumza mapema leo mchana jijini Dar es Salaam, kocha wa mchezo wa masumbwi, Rajabu Mhamila, maarufu kama ‘Super D’, amesema bondia huyo atakuwa katika mikono yake kwa ajili ya kujiandaa na pambano hilo.

Alisema bondia wake ataanza mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na pambano hilo muhimu, akiwa na lengo la kufanya vizuri zaidi katika mchezo wa masumbwi na kurithi mikoba ya wapiganaji wengine waliotamba hapa nchini.

“Naomba wadau wampe sapoti kijana huyu katika pambano lake lijalo, ukizingatia kwamba nia ni kuhakikisha kuwa anapiga hatua zaidi katika mchezo wa masumbwi hapa nchini na kufikia malengo ya wakali wengine.

“Naamini kila kitu kitakuwa sawa, ndio maana Class ataingia kambini mapema kwa ajili ya kumnoa vizuri ili awe nyota na kutikisa katika ulingo wa masumbwi na kuupandisha chati kama wadau tunavyopania,” alisema.

Ibrahim Class ni miongoni mwa mabondia wanaochipukia kwa kasi hapa nchini, huku akiwa na mipango imara ya kuwachapa wapinzani wake katika mapambano mbalimbali yanayoandaliwa kwa ajili ya kuonyesha cheche zake.

                                         Kambi Mbwana
Wakati mwingine kuuza sura sio mbaya. Kambi Mbwana, akifotolewa na Mpiga picha mwanadada, Rahel Pallangyo leo, Oktoba 18, mwaka 2012...

Wednesday, October 17, 2012

Kagera nayo yaivuta Simba mkia



                                          Amri Kiemba akijituma uwanjani leo
                                          
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MABINGWA watetezi, Simba SC, leo wameendelea kuvutwa mkia baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na timu ya Kagera Sugar, mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Mabao ya Simba yalipatikana dakika ya 8 likifungwa na Felix Sunzu na 53 liliofungwa na Mrisho Ngassa, wakati mabao ya Kagera Sugar yalifungwa na Temi Felix dakika ya 63 kwa shuti kali na Salum Kanoni aliyeifungia timu yake kwa njia ya penati, dakika ya 66.

Licha ya kutoka sare hiyo, Simba bado wanaendelea kuongoza ligi hiyo yenye ushindani wa aina yake na kila timu ikipania kushinda katika mechi zake.

Mpira ulianza kwa kasi ya ajabu, huku Kagera wakionekana kupagawa zaidi, ingawa nafasi kadhaa ilizopata ilishindwa kuzitumia.

Mwamuzi wa mchezo huo alikuwa ni Reonald Swai kutoka jijini Arusha aliyechezesha pambano hilo lililokuwa na upinzani wa aina yake.

Wachezaji walioanza katika mechi hiyo dhidi ya Simba ni pamoja na Andrew Ntalla, Salum Kanoni, Martin Muganyizi, Amandus Nesta, Benjamin Affe, Maleges Mwanga, Daud Jumanne, George Kavilla, Shija Mkina, Enyinna Darlington na Wilfred Ammeh.

Wakati Simba walioanza ni Juma Kaseja, Said Chollo, Amir Maftah, Juma Nyoso, Paschal Ochieng, Mwinyi Kazimoto, Mrisho Ngassa, Amri Kiemba, Felix Sunzu, Haruna Moshi 'Boban' na Emmanuel Okwi.


Tenisi ni mchezo matajiri?





                                          Mchezaji wa tenisi, Mohamed Dewji
Mchezo wa tenisi ni mzuri mno lakini wengi wanaoingia humo ni wale ambao wazazi wao wana chochote kitu. Sababu inayosababisha hilo ni namna ya mchezo wenyewe pamoja na vifaa vyake kuuzwa bei ghari mno.

Mtu ambaye hata kula yao nyumbani ni tabu, hawezi kutumia kiasi kikubwa cha pesa kununulia vifaa hivyo vya mchezo wa tenisi. Pichani ni mcheza tenisi, Mohamed Dewji, kama alivyokutwa na mpiga picha mahiri wa michezo, Rahel Pallangyo, leo katika Viwanja vya Gymkhana, jijini Dar es Salaam.

Ipo sababu ya wadau kuliangalia suala hilo ili kuufanya mchezo huo ni wa watu wote badala ya wale wenye nazo, zikiwamo sura nyeupe kwa Tanzania. Wakati nasema hayo, soka ndio mchezo pekee kwa Tanzania ambao unavutia kuchezwa na kila mtu. 

Kwa maoni na ushauri
kambimbwana@yahoo.com
0712 053949
0753 806087

Wachezaji sita wafariki ajalini Kagera


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za vifo vya wachezaji watano wa timu ya Rusumo FC ya mkoani Kagera vilivyotokea jana jioni (Oktoba 16 mwaka huu).
 
                                         Angetile Osiah, Katibu Mkuu wa TFF                                          
 Rusumo FC ilikuwa ikitoka kwenye mechi ya michuano ya Polisi Jamii Wilaya ya Ngara ambapo ikiwa njiani kurudi Rusumo kutoka mjini Ngara ilipata ajali ya gari na wachezaji watano kufariki papo hapo.

Wachezaji wengine ambao ni majeruhi wamelazwa Hospitali ya Wilaya ya Ngara ya Murugwanza huku wawili hali zao zikiwa mbaya.

Msiba huo ni pigo kwa familia za marehemu, klabu ya Rusumo FC, Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Ngara (NDFA), Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Kagera (KRFA) na familia ya mpira wa miguu kwa ujumla nchini kutokana na mchango wa wachezaji hao katika ustawi wa mchezo huu kupitia klabu yao.

TFF inatoa pole kwa familia za marehemu, Rusumo FC, NDFA na KRFA na kuwataka kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Kutokana na msiba huo, mechi zote za Ligi Kuu ya Vodacom zinazochezwa leo (Oktoba 17 mwaka huu) kutakuwa na dakika moja ya maombolezo ili kutoa heshima kwa marehemu hao. Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi.


Chegge, Temba kupamba shindano la Mfalme wa Mic Dar Live


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
Shindano kabambe la kumsaka Mfalme wa Mic (The Mic King), litapambwa na wakali wa Bongo Fleva, Said Juma ‘Chegge’ na Amani James Temba ‘Mheshimiwa Temba’.

                                                       Said Juma, Chege
Kila kitu kuhusu shindano hilo ambalo mshindi wake atajinyakulia zawadi ya gari la kifahari ni Jumapili hii kwenye Ukumbi wa Dar Live, Mbagala Zakhem, Dar es Salaam.

Mratibu wa Shindano la The Mic King, Luqman Maloto amesema kuwa sambamba na Chegge pamoja na Temba, bi. Mkubwa anayetamba kwa sasa kwenye ulingo wa Bongo Fleva, Bi. Cheka, naye atakuwepo.

“Siku hiyo, kutakuwa na shoo maalum kwa wakali wapya kutoka timu ya Mkubwa na Wanawe kutambulishwa chini ya Meneja Said Fella ‘Mkubwa’,” alisema Luqman na kuongeza:

“Vilevile Bendi ya Extra Bongo ikiongozwa na Ally Choki, Banza Stone, Khadija Mnoga ‘Kibotel’ na Rogert Hegga ‘Katapila’, itakuwepo kufanikisha siku hiyo nzuri.”

Luqman aliongeza kuwa Jumapili iliyopita, walisakwa vijana 12 kutoka Temeke, wiki hii ni zamu ya Wilaya ya Ilala, nayo kushindana na kupata 12 Bora yao.

“Niwasihi tu mashabiki wajitokeze kwa wingi kwani msisimko tuliouona mwanzoni ulikuwa si wa kitoto. Ikumbukwe kwamba mshindi atajiondokea na gari la kifahari,” alisema Luqman.

Usiku wa kizazi cha dansi ndani ya Extra Bongo

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
BENDI ya muziki wa dansi ya Extra Bongo, kesho Ijumaa, wanatarajia kufanya shoo ya nguvu katika Ukumbi wao wa nyumbani wa White House, Kimara Korogwe, jijini Dar es Salaam.

Burudani hizo zitaongozwa na Mkurugenzi wa bendi hiyo, Ally Choki, sambamba na wakali wengineo wanaofanya vyema katika tasnia ya muziki wa dansi hapa nchini.

                                           Ally Choki
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Choki alisema kwamba shoo yao hiyo itapambwa na wakali wao wote, akiwamo Rogert Hega 'Catapiler', Ramadhani Masanja ‘Banza Stone’ na Khadija Mnoga 'Kimobitel'.

Alisema kuwa usiku huo wa kizazi cha dansi utawahusisha wanamuziki hao walio na bendi hiyo katika maonyesho yatakayofanyika kweye kumbi Bongo Resort na Meeda Sinza.

Baadhi ya nyimbo zao ni 'Kila Chenye Mwanzo', 'Game 111', 'Nguzo Tano', 'Mtaji wa Maskini', 'Elimu ya Mjinga', 'Simba Ananguruma', 'Kumekucha', 'Mtu Pesa', 'Password',' Chuki Binafsi', 'Jirani', 'Umbeya hauna Posho', 'Fadhila kwa Wazazi' 'Mtenda Akitendewa', 'Mjini Mipango' na nyinginezo.

Aidha, onyesho hilo pia linatarajiwa kupambwa na kikundi cha burudani cha Baikoko na mwanamuziki wa muziki wa kizazi kipya Husein Machozi ambaye atakuwa anatambulisha wimbo wake mpya.

Mabondia kufanya mazoezi pamoja Jumamosi

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MABONDIA mbalimbali wa uzito wa juu hapa nchini, wanatarajia kukutanishwa Jumamosi na kufanya mazoezi ya pamoja, huku wakishuhudiwa na mmoja wa wafadhili wa Evender Hollfied, Andrew Jowel.

Kufanya mazoezi kwa pamoja ni sehemu ya kufanya mchakato wa kujitafutia mafanikio makubwa katika sekta ya masumbwi na kuinua kiwango cha mchezo huo hapa nchini.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, muandaaji wa tukio hilo, ambaye pia ni bondia mahiri hapa nchini, Japhet Kaseba, alisema lengo ni kutathimini namna ya kuendeleza mchezo wa masumbwi Tanzania.

                                          Japhet Kaseba 
Alisema anaamini mabondia watakaofika siku hiyo katika kambi ya ngumi ya Kaseba, iliyopo Mwananyamala jijini Dar es Salaam watakuwa na mwamko zaidi wa kufikia malengo yao.

“Tayari mabondia mbalimbali wanajua kuwa tutakuwa na mgeni huyo aliyekuja kutembelea Tanzania, huku akiwa anajua mambo mengi yanayohusu mchezo wa masumbwi duniani.

“Kuanzia saa tisa alasiri, mabondia wote tutaanza mazoezi ya pamoja katika gym yangu, hivyo kila anayependa kushiriki afike maana lengo ni kuangalia namna ya kujitangaza na kuonyesha kwamba Tanzania wapo mabondia wenye vipaji na dhamira ya kweli ya kufika mbali,” alisema Kaseba.

Kaseba ni miongoni mwa mabondia wenye mafanikio makubwa katika mchezo wa masumbwi, huku akiogopwa na mabondia wakali wanaoshindwa kucheza naye kila anapojitokeza promota wa kumkutanisha nyota huyo ambaye pia aliwahi kuwa bingwa wa Dunia wa Kick Boxing.

Mwanaharakati haogopi jina la kigogo


MGODI UNAOTEMBEA

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WASWAHILI ni wajuzi sana wa maneno. Katika kipindi cha maisha yao, walijikita katika kubuni misemo ambayo mingi kati yao imekuwa na mashiko wakati wote. Hata kama ukiishiwa nguvu, lakini ukiumbuka mmoja wapo, nguvu za ziada huibuka.

                                          Mwasisi wa CCM, Mwalimu Julius Nyerere
Angalia msemo huu. Kwenye nia pana njia. Msemo huu unatufundisha kuwa chochote tunachohitaji kufanya, lazima tuweke nia maana itazalisha njia ya kufanikisha dhamira hiyo kwa kila binadamu anayeandamwa na vikwazo.
                                          Ridhiwan Kikwete
Mwenda pole hajikwai. Msemo huu unatufundisha kufanya kazi zetu kwa utulivu bila kuacha papara, ndio maana hapo pia ukatungwa msemo mwingine wa haraka haraka haina baraka.

Sio lengo langu kuoredhesha misemo ya wahenga, maana ni mingi na haiwezi kujaa kwenye ukurasa wote huu wa Mgodi Unaotembea. Lengo langu ni kuwambusha Watanzania juu ya mabadiliko ya kisiasa na wale wanaojiita ni wanaharakati.

Wanaharakati ambao baadhi yao ni watunga uongo na uzandiki bila ukomo. Wanaharakati wa Tanzania, wengi wao wanapotunga hasidi zao, wanashindwa kuupangilia ili uonakane una ukweli japo kwa asilimia chache.

Kwa wiki kadhaa sasa kumekuwa na maoni mbalimbali ya juu ya uchaguzi wa ndani wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Uchaguzi huo umebadilisha hisia za wanaharakati na kuanza kuleta porojo mahali ambako si mahali sahihi.

Watu hao wanahoji uhalali wa watoto wa vigogo kuingia kwa wingi katika uchaguzi huo. Ati wameihodhi CCM na kuifanya ya kindugu. Hapo yanasemwa maneno mengi, akitajwa Rdhiwan Kikwete, kama mfano wa wanachama hao.

Wanaharakati hao waliandika meseji na kutuma kwa kila wanayehisi kuwa hajaelewa somo la mabadiliko yasiyojengwa kwa hoja na watu hao.

"HATARI: Angalia watoto wa vigogo waliopita UVCCM ngazi ya Taifa; Dickson Membe, Fredy Lowassa, Ridhiwani Kikwete, Ashura Hussein Mwinyi, Beny Samuel Sitta, Debora Mwandosya, Irene Pinda, Felister Ndugai, Chrisopher Ndejembi, Sharifa Bilali, Hawa Kigoda, Judith Mukama, na Jerome Msekwa.

“Nchi imekwisha, inatia hasira, wacha watoto wa masikini tupambane kupitia mlango mwingine, "CHADEMA" ili kutetea masikini wenzetu, wazazi na wadogo zetu. Vita hii inaanza sasa upatapo meseji hii tuma kwa wazalendo wenzako,” mwisho wa ujumbe huo na kumalizia kuwa aliyetuma meseji hiyo ati ni mwanaharakati.

Hizi ni meseji za kijinga mno. Na wenye akili timamu hawawezi kubabaishwa nazo, maana zimebuniwa kwa nia ya kujiridhisha kuwa utakaowaingia wanaweza kuwaelewa, hata kama sababu zao ni ndogo mno.

Kwanini nasema hivi? Kwangu mimi siwezi kubabaishwa na jina la mtoto wa kigogo katika sehemu husika, kama lengo langu ni kugombea mahali Fulani. Tena ndio kwanza naona raha juu ya kupambana na mtu huyo.

Mtoto wa kigogo hakatazwi kuwa mwana CCM kama walivyokuwa wapinzani na kushika nafasi mbalimbali za vyama vyao. Ila sitamuelewa mtoto wa kigogo nitakapobaini kuwa anakwenda kinyume au ni mwizi.

Yani, anatumia nafasi yake vibaya kwa ajili ya kujitajirisha mwenyewe. Sina ugomvi na Ridhiwan ati kwasababu ameamua kuchukua fomu za kuwania ujumbe wa CCM. Kila mmoja ana haki na wajibu sawa wa kuchagua na kuchaguliwa.

Naandika makala haya kama mwanzo wa kuwaelimisha hao wanaharakati na wasiokuwa wanaharakati juu ya kutetea wanachokiamini. Hakuna haja ya kubabaishwa na jina la mtoto wa kigogo hata kama tunajua ghiriba inaweza kufanywa wakati wowote.

Tangu uchaguzi huo wa CCM ulipoanza kutimua vumbi katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani, majina mapya nay a zamani yameingia. Tena, wapo ambao hawakutarajiwa lakini hatimae wameibuka na ushindi.

Unaotakiwa kujengwa ni ujasiri na kujituma hadi mwisho wake. Lolote kwenye uchaguzi linaweza kutokea na sio kulalama kuwa ni wengi watoto wa vigogo.

Mjini Nachingwea, kijana wa kidato cha sita, Fadhili Liwaka ameweza kumuangusha Waziri wa Sheria na Katiba wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mathias Chikawe katika uchaguzi wa CCM.

Hawa walikuwa wanawania nafasi moja ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Nachingwea mkoani Mtwara, huku matokeo hayo yakishangaza wengi. Chikawe mwenyewe hakujua kwamba angeweza kuangushwa na kijana huyo.

Kama Liwaka angekuwa mwoga kama wanavyowaaminisha hawa wanaharakati, sidhani kama angekuwa na ujasili wa kupambana na kigogo huyo wa Serikali ya Jakaya Mrisho Kikwete, ukizingatia kuwa ana nafasi kubwa.

Kwa bahati mbaya, mbinu inayoganywa na wapinzani ni kueneza sumu hata zile ambazo hazina kichwa wala miguu. Kukaa na kufikiria haya ni kuishiwa hoja. Wangapi wanarithi kazi za wazazi wao na bado halisemwi?

Mbona wapo wazazi madaktari na watoto wao nao wanaingia kwenye sekta hiyo? Wangapi ni walimu na watoto wao ni walimu? Au wanaharakati wanaona kwenye siasa tu? Hizi ni sababu zisizokuwa na mashiko hata kidogo.

Nitawaona wanaharakati wana akili timamu watakapowajengea uwezo wa kupambana na majina hayo na sio kuwaaminisha kushindwa. Mwanaharakati makini ni yule anayepanga kila mbinu kuweza kukabili vishindo hivyo.

Tena, haya majina yanayooogopwa ni ya kawaida kabisa. Mtu unaweza kujieleza vizuri na bado mtoto wa Kikwete, Mwinyi wakakosa nafasi hiyo. Hata kama wakipata leo, lakini uchaguzi utakaofuata watashindwa tu.

Kikwete ndio kipindi chake cha mwisho hiki. Huenda kama uwepo wake umewafanya watoto wake wapewe nafasi basi wakaikosa katika uchaguzi ujao. CCM sio mali ya mtu mmoja. CCM ni mali ya kila mmoja.

Ila kinachofanywa ni kupeana zamu katika nafasi hizo, maana wote hawawezi kuwa viongozi wa chama na serikali. Ili mmoja wao apewe nafasi, ni lazima awashawishi wajumbe ili wampigie kura.

Huo ndio ukweli. Kila mmoja wetu anapaswa kuwa makini katika nyendo zake na harakati zenye ushawishi na dhamira za kweli. Wapambanaji wasiamgalie nani ni mtoto wa kigogo au nani wa mkulima, maana wote wana haki sawa.

Wasiamgalie jina la mtoto wa Kigoda na wengine. Na kama huo ndio utaratibu wao, basi unapaswa kukoma kama lengo lao ni kukipa nguvu chama chao na sio kuendeshwa ovyo kisa watu Fulani wanataka mabadiliko ya kisiasa.

Sio kila tunaloambiwa na wanaharati tunataka kuliweka kichwani, maana hakika mengine hayana kichwa wala miguu. Mwanaharakati anataka kuwakomboa watu wake, lakini bado anawaaminisha kuwa hakuna linaloweza kufanikiwa kama vigogo wataachwa watoto wao.

Wanasahau kuwa wapo vigogo ambao nao wanahitaji nafasi hizo za chama nab ado wanakosa baada ya kuangushwa kwenye chaguzi hizo. Nakerwa sana na mwenendo huo. Mtu aliyenitumia meseji hiyo nilimlaumu kupita kiasi.

Akili yake huenda ina matege. Anafanya siasa nyepesi ama rahisi. Haina tija kwake na Taifa kwa ujumla. Kwa bahati mbaya, akiambiwa ukweli mtu wa aina hiyo, atawaka kwa hasira. Atajiona yeye ndio kila kitu, wakati sio mkweli.

Atajiita yeye ni mjuzi wa kila jambo akilingia vyeti vyake ambavyo huenda amevipata kwa ujanja ujanja kama wafanyavyo baadhi yao. Hapana. Huu sio mwendo sahihi na lazima Watanzania na wale wanaharakati wajifanyie mabadiliko.

Huwa simpendi mtu asiyejiamini. Mtu ninayempenda ni yule anayeona anaweza kupata kile anachotaka hata kama kuna vizingiti vya kila aina. Hayo ndio maisha mazuri. Katika hilo, nami najifunza kuacha woga katika kile ninachokitaka na kukiamini.

Mawazo haya yaenee kwa kila mmoja wetu. Tusiangalie vigogo waliopo kwenye Chama tawala CCM, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama Cha Wananchi (CUF) na wengineo maana siku zote kwenye ukweli uongo hujitenga.

Baada ya kusema hayo, naomba nikuage msomaji wangu wa Mgodi Unaotembea na tukutane tena wiki ijayo katika dhmira ya kweli ya kujenga nchi kwa kushirikiana sote bila kuangalia nani Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi au CCM.

Ndugu msomaji wangu mpendwa. Sasa unaweza kujadili na mimi mambo mbali ya kisiasa katika group la Handeni Kwetu, ambao ni uwanja mpana zaidi, baada ya huu Mgodi Unaotembea unaotoka kila Jumatano katika Gazeti lako la Mtanzania.

Ndudu msomaji wangu mpendwa. Sasa tunaweza kukutana katika uwanja mpana zaidi, kwenye group la face book linaloitwa Handeni Kwetu na kuchambua mambo mbalimbali ya kisiasa, kimichezo na kiutamaduni na naomba uwe pamoja nami.
 
0712 053949
0753 806087

Monday, October 15, 2012


BABA WA TAIFA

Nyerere asingekufa kwa maradhi, angeuliwa na CCM

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
LEO ni Oktoba 14. Tanzania nzima inaingia katika kumbukumbu ya kifo cha mwasisi wa Taifa hili, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyekufa Oktoba 14, mwaka 1999 nchini Uingereza alipokwenda kwa matibabu.

Kwa mujibu wa madaktari wake, Nyerere mtu muhimu kabisa katika Taifa hili, alikufa kwa maradhi ya kansa ya damu (leukemia), akiwa katika harakati nyingi za kuokolewa maisha yake, katika Hospitali ya St Thomas, London, Uingereza.

                                         Mwalimu Julius Nyerere
Kifo chake kilitetemesha wengi, wakiwamo wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na wale wasiokuwa na vyama vya siasa. Katika kuiangalia kumbukumbu yake, naweza kusema kifo chake kitaendelea kuwa pigo hasa kwa CCM.

Chama ambacho licha ya kukipenda na kukiheshimu kupita kiasi, kimegeuzwa na wachache wao, walioamua kuja kufanya biashara kwa mgongo wa kisiasa.

Nathubutu kusema kwamba, uhakika wa kuendelea kuishi kwa baba wa Taifa, ungekuwa mdogo mno kwa mwenendo wa CCM kuanzia miaka ya 2000 hadi muda huu.

Kama asingeshikwa na maradhi hayo, basi ni dhahiri msiba huo ungekuwamba, huku sababu kubwa ikiwa siasa chafu, rushwa ya uchaguzi, hasa ndani ya CCM, sambamba na siasa za makundi na kushughulikiana wao kwa wao.

Nyerere, asingeweza kudumu, maana watu anaowaamini wanageuka na kuvaa joho la ukatili, wakiwa ndani ya chama kilichounganisha watu wengi. Chama ambacho kwa namna moja ama nyingine, kimeundwa kwa jasho la walalahoi.

Watu ambao kwa miaka 35 sasa, maisha yao, uhuru wao ni mdogo mbele ya matajiri wachache wanaoingia kulangua kwenye siasa. Kwanini nasema hivyo. Nyerere kwa mtazamo wake, alisema bila CCM nchi hii itayumba.

Aliyasema haya kwa imani kubwa aliyokuwa nayo kwa Watanzania na  mbele ya chama chake hicho cha CCM, ambacho kwa sasa kipo chini ya Mwenyekiti wake, Jakaya Mrisho Kikwete.

Hali ya mambo inavyoendelea, uwezekano wa CCM kutawala milele ni mdogo mno. Kumekuwa na mabadiliko makubwa ya upepo wa kisiasa. Chuki za wazi wazi ndani ya uongozi wa chama hicho kikongwe zimetamalaki.

Uhai wake ungekuwa mdogo mno. Watu wanageuka na kufanya siasa zisizokuwa na tija kwa CCM na bado wanachekewa. Wenye maono yao wanatembea na kusema vibaya juu ya kauli za Nyerere, wakisema hazitakiwi kufuatwa.

Kinachofuata sasa ni kuona kejeli za wazi wazi kwa baba wa Taifa, maana waliobakia kwenye mfumo wa chama, hawana mawazo mazuri ya kukitetea chama mbele ya umati wa watu wanaona kwamba chama kimezeeka na kinatakiwa kufa.

Wale ambao wanatembea kwa matao wakisema kifo rasmi cha CCM ni mwaka 2015. Wanasema kaburi lake limeshaandaliwa. Hizi ni kejeli ambazo nachelea kusema kuwa zingemfurahisha Nyerere, hata kama leo angekuwa hai.

Hizo tu na nyingine nyingi zingempa presha na jaka moyo, hivyo uhai wake kuwa mdogo mno. Kama huo sio ukweli, basi upo mbali na uongo. Nikiwa kama Mtanzania, naheshimu kwa dhati mchango wa Baba wa Taifa.

Amefanya mengi mazuri, ikiwamo kuruhusu kwa kauli moja mfumo wa vyama vingi vya siasa, kama ishara nzuri ya kukua kwa Demokrasia ndani ya nchi hii ambayo kwa sasa inaendelea kutafunwa na mchwa aliowasema.

Mchwa hao wamekuwa wakijenga mtandao wao kwa njia za hatari mno. Wengine wanafika mbali kwa kuingia ubia na wafanyabiashara wakubwa kwa ajili ya kuitafuna nchi hii.

Watanzania masikini hawana haki tena. Kila kinachofanyika ni usanii mtupu. Bado tu hiyo suio dalili za kuangamiza roho za wapendwa wetu? Je, Nyerere angechekea haya yanayofanyika sasa, ikiwamo fedha kutumika nyingi hata kwenye chaguzi za ndani?

Wanataka nini? Mgombea kumwaga noti katika Uchaguzi wa Umoja wa Vijana CCM, (UVCCM) anatafuna nini? Fedha hizo anazitoa wapi na ili apate nini? Chama kimehamshwa kutoka kwa wakulima na wafanyakazi na kuingia kwenye mikono ya walanguzi, wafanyabiashara wakubwa wenye malengo yao kisiasa.

Ukifanya hesabu za wafanyabiashara wakubwa wanaoingia kwenye siasa utachoka. Ni wengi mno. Kila mtu humo ni mwanasiasa na mgongo wake ni CCM. Hao ndio wanaoharibu mfumo mzima wa CCM, ingawa wakiambiwa watabisha.

Tuambiane ukweli hata utatuuma. Tusidanganye kuwa tunamuenzi Nyerere wakati mambo yanaendeshwa kienyeji na wajanja wachache wananufaika. Huo ndio ukweli wa mambo.

Kila mmoja awe na nia ya kuwakomboa Watanzania wenzake kwa kutumia fursa mbalimbali zinazopatikana na rasilimali zilizopo. Kama madini yetu yanachimbwa na sisi kuambulia mashimo, bado tunamuenzi Nyerere?

Kama wazee wetu wasiokuwa na elimu waliwabaini wajanja, watumia nguvu zao vibaya, wakoloni na kuwatimua, vipi wasomi wa leo wanawaingiza kwa mgongo wa uwekezaji?

Elimu yao ipo wapi na inatumika vipi kuwakomboa watu wote. Hili lazima lisemwe hadharani kwa ajili ya kujenga haki ya kila mwananchi. Tanzania hii sio ya watu wachache wanaonufaika na familia zao, huku walalahoi wakiendelea kushinda njaa.

Kwa bahati mbaya, haya yanatokea wakati serikali ipo chini ya CCM, chama ambacho mwasisi wake, Nyerere alikitabiria kutawala milele kwa kusema bila hicho nchi itayumba. Kama hivyo ni kweli, ina maana Rais huyo wa Kwanza wa Tanzania, hajajua kuwa kuna siku hali itakuwa mbaya kwa chama chake.

Kwa wataalamu wa mambo ya siasa wanajua kuwa bila chama cha Mapinduzi chini ya Kikwete kukaa na kuangalia tatizo, uwezekano wa kushinda katika chaguzi tatu zijazo, yani mwaka 2015, mwaka 2020 na 2025 ni mdogo mno.

Na hilo likitokea, basi damu nyingi itamwagika kama inavyomwagika sasa, maana wenye nia ya kutawala wamekuwa wakipakaza sumu na kushitaki kwa nguvu ya umma (wananchi), wakisema CCM imeshindwa kuwakomboa Watanzania kwa kuwaacha kwenye madhira ya umasikini huku viongozi wao wakila raha na familia zao.

Nadhani kwa kupitia kumbukumbu ya kifo cha mwalimu Nyerere, Watanzania na viongozi wa Taifa hili, wakiwamo wana CCM wana kila sababu ya kujitazama upya kama kweli wanahitaji kumuenzi mwenyekiti wao wa zamani.

Wafanyie kazi ushauri wake, uongozi wake na sera zake zilizotukuka badala ya kusema kwenye vijiwe vya siasa, wakati chama chao kinayumba. Kuna mchambuzi mmoja, aliwahi kuandika katika makala yake, Nyerere akifufuka leo anakufa tena.

Najaribu kuyaelewa mawazo yake, maana akifufuka leo, atakuta CCM mpya yenye kila aina ya uozo, huku dalili za kubaki madarakani kwa miaka mingi ijayo ikikosekana, kama hali itaendelea kuwa kama ilivyokuwa sasa.

Wakati ni huu. Bado CCM imara, Taifa imara linawezekana kwa kuangalia makosa yao, mapungufu yao kwa ajili ya kusonga mbele na sio kurudi nyuma wala kubaki lilipo.

Mungu ibariki Tanzania.

0712 053949
0753 806087

Mwisho


Milovan kuelezea sare yao na Coastal leo


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KOCHA Mkuu wa timu ya Simba, Milovan Cirkovic, leo anatarajia kuanika chanzo cha sare yake na Coastal Union ya Tanga pamoja na muendelezo wa ligi hiyo, huku wakikipiga na Kagera Sugar, kesho katika Uwanja wa Taifa.

Kutoka sale na Coasta Union kumepokelewa kwa shingo upande na mashabiki wa timu hiyo, hasa wale waliokwenda kuishuhudia mechi hiyo ya aina yake na kuipatia Simba pointi moja, hivyo kufikisha pointi 17.


                                         Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga

Simba wanaingia uwanjani kucheza na Kagera Sugar huku wakiwa na machungu ya kusimamishwa na Wagosi wa Kaya, licha ya kujipanga kwa ajili ya mchezo huo uliohudhuliwa na mashabiki wengi wa jijini Tanga na maeneo mengine ya nchi.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema kocha huyo atazungumza yote yaliyosababisha asihndwe kupata pointi tatu kutoka kwa Wagosi wa Kaya, mechi iliyopigwa Jumamosi, katika Uwanja wa Mkwakwani.

Alisema kwamba anaamini kwa kujua mapungufu yake, ni sababu ya kuwaamisha mashabiki wake kuwa watashinda mbele ya Kagera Sugar wanaotoka mjini Bukoba na kuikuta Simba yenye machungu na mchezo huo.

“Simba tuna uchungu na mechi hiyo ya Kagera Sugar, ila sitaki kuzama sana kwenye mambo ya kiufundi maana yataongelewa na kocha wetu kwa ajili ya kuwatoa hofu mashabiki na wanachama wote hapa nchini.

“Naamini kuna mengi yametokea na yatatokea katika ligi hii yenye ushindani wa aina yake, lakini huenda limepatia ufumbuzi na kocha wetu, Milovan hivyo kuendeleza wimbi la ushindi na hatimae kunyakua ubingwa kwa mara ya pili mfululizo,” alisema Kamwaga.

Ligi ya Tanzania Bara imezidi kuwa na ushindani wa aina yake, huku kila timu ikipania kushinda katika mechi zake zote, jambo linalozifanya timu kongwe za Simba na Yanga zitumie nguvu kubwa ili kuzipa ushindi.

FM Academia kuvamia Hill Take Ijumaa


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
BENDI ya muziki wa dansi ya FM Academia, maarufu kama Wazee wa Ngwasuma, wanatarajia kufanya shoo ya nguvu katika Ukumbi wa Hill Take, uliopo Ukonga, jijini Dar es Salaam, Ijumaa ya Oktoba 19.

Kuvamia ukumbi huo ni sehemu ya kuwapatia burudani mashabiki wao wa Ukonga, wakiamini kuwa litaacha watu hoi kutokana na mipango yao waliyoiweka kwa ajili ya kufanya shoo ya nguvu na kuwaburudisha mashabiki wao.

Akizungumza jijini Dar es Salaam na Handeni Kwetu, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa bendi hiyo, Kelvin Mkinga, alisema kwamba mipango kwa ajili ya shoo hiyo imekamilika kwa ajili ya kuwapatia raha mashabiki wao wa Ukonga.

Alisema bendi yao imekuwa ikitamba na nyimbo mbalimbali zinazopendwa na watu wengi, hivyo anaamini mashabiki wao watapata raha za aina yake na kuendelea kuwaunga mkono katika tasnia ya muziki wa dansi hapa nchini.

“Ni bendi yenye mipango imara katika tasnia ya muziki wa dansi, hivyo naamini mashabiki wetu watakuja kwa wingi katika ukumbi huo kwa ajili ya kucheza na Wazee wa Ngwasuma wenye nyimbo zinazopendwa na wengi.

“Nyimbo kama ‘Heshima kwa Mwanamke’, ‘Otilia’ na nyinginezo ni kati ya zitakazoporomoshwa na waimbaji wetu, hivyo naaamini mashabiki watakuja kwa wingi kuburudika pamoja na kudhihirisha FM Academia ni zaidi yao,” alisema Mkinga.

FM Academia ipo chini ya Rais wa Vijana, Nyosh Al Sadaat, akiwa sambamba na wakali wengine akiwamo Patchou Mwamba, ambaye pia ni mkali katika tasnia ya filamu baada ya kushiriki katika filamu mbalimbali hapa nchini.

Tumeshindwa werevu, tujifunze na ujinga

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NI aibu kila siku kuendeleza kilio kile kile cha ubabaishaji wa soka la Tanzania, linaloongozwa na Shirikisho la Soka nchini (TFF). Wadau wa michezo wamekuwa wakilia sana juu ya uendeshaji mbovu wa soka, hasa uamuzi wa utata wa marefa, timu kutumia fedha nyingi, rushwa katika kusaka ushindi kwenye mechi zao.
 
Ratiba isiyokuwa na mashiko kwa baadhi ya timu, huku wasimamizi wa soka, wakiwa wepesi wa kuangalia zile mechi zenye faida, yani zinapokutanisha timu za Simba na Yanga.
 
Ni kama vile tumeshindwa werevu, hivyo walau sasa tujifunze na ujinga katika kudidimiza zaidi soka letu, maana sioni mipango inayoweza kuinua michezo, ukiwamo mpira wa miguu unaopendwa kwa kiasi kikubwa hapa nchini.
 
TFF inayoongozwa na Rais wake, Leodgar Tenga, akiwa na watendaji wake wengine, kama vile Angetile Osiah, Mkurugenzi wa Ufundi, Sunday Kayuni na wengineo, wamekuwa hohe hahe hadi kuchelewesha Kampuni ya kuendesha ligi.
 
Haya yanasababisha ligi na mpira wa miguu kwa ujumla kuwa wa kusua sua, maana yale yanayofanywa leo ndiyo yale yale yaliyolidumaza soka la Tanzania, huku likiachwa na nchi nyingine, kama vile Kenya, Uganda na kwingineko.
 
Leo hii timu ya Taifa ya Tanzania, inafanya kazi kubwa sana kuweza kuibuka na ushindi katika mechi zake zinapokutana na nchi za Uganda na Kenya. Lakini, timu hizo ni zile zilizokuwa zinafungwa mara kwa mara na Taifa Stars.
 
Ukiyasema haya, watashindwa kukuelewa, hivyo kuchelewesha kwa kiais kikubwa maendeleo ya michezo hapa nchini. Angalia, ligi kutoendeshwa na Kampuni kama invyotakiwa na wadau, kunaroa ladha halisi.
 
Watu wanajiendesha wanavyotaka wao. Timu inajiandaa na mechi yake, lakini inapelekewa barua ya haraka, ikitangaza kusogeza mbele au kurudisha nyuma mechi husika. Timu ya African Lyon, inazuiliwa kudhaminiwa na Kampuni ya Zantel, maana ligi ipo chini ya Kampuni ya Vodacom Tanzania.
 
Sawa, ila fedha zinazotolewa na vodacom zinatosha k,wa timu hizo? Kama zinatosha, je, hao Vodacom wanazitoa kwa wakati? Kumekuwa na ghiriba nyingi katika uendeshaji wa ligi ya Tanzania, hivyo kusababisha kutoelewana.
 
Kwa mfano, baadhi ya timu ikiwamo African Lyon zinalalamika kuwa hawajashirikishwa katika udhamini huo wa Vodacom. Wanfika mbali zaidi kwa kusema kuwa hawajapa nafasi ya kuangalia aina ya mkataba huo.
 
Pamoja na hayo, mkataba wa Vodacom na TFF juu ya ligi hiyo ulisumbua kwa wiki kadhaa, hadi kuchelewesha kutoka kwa ratiba na kuanza kwa ligi hiyo. Haya ni maajabu makubwa na matatizo ya ligi hiyo ya Tanzania Bara.
 
Ukiangalia kwa haraka, yote hayo ni majibu kuwa ligi haiwezi kuwa na tija kama kutakuwa na malalamiko ya kupitiliza. Timu zinalalamikia ukandamizaji huo ambao kwa kiasi kikubwa unachekewa na hao TFF.
 
Nalisema hili bila kuficha, maana ni ajabu ya mipango yenye matege. Tutawezaje kuwa na wachezaji bora wakati ligi yetu haieleweki? Sisi ni wa hapa hapa kwanini tunakuwa na mipango ya kucheza Kombe la Afrika au Dunia?
 
Hii ni aibu kubwa. Ndio maana hata ukiangalia mechi hizo, utagundua kwamba hakuna mikakati wala ufundi zaidi ya ushindi wa lazima. Kwa wale wenzetu wa Simba na Yanga ndio kabisa.
 
Kwanza wana mtaji mkubwa wa mashabiki na wanachama wenye  nazo hivyo kuweza kufanya lolote wanalohitaji. Haya lazima tuyaangalie upya. Tuwe na dhamira ya kweli na kuacha udanganyifu, ubabaishaji katika kuinua michezo.
 
Kunyume cha hapo hatutakuwa na jipya katika uendeshaji wa soka, ndio maana Taifa linaachwa nyuma na harakati za nchi nyingine za Afrika juu ya kuendeleza michezo.
 
Sikatai Taifa lina wachezaji imara na wenye vipaji vya hali ya juu, ingawa nao wanaangushwa na aina ya viongozi wa soka la Tanzania. Ubabaishaji ni mkubwa katika kila nyanja, ikiwamo uwanjani na usajili kwa ujumla.
 
Kumekuwa na janja janja nyingi, huku Simba na Yanga zikisikilizwa kupita kiasi, ingawa ukisema hili watakataa. Huwezi kubisha kuwa tuna vijana mahiri lakini hawawezi kusonga mbele kama hatutakuwa na mipango endelevu.
 
Wachezaji kama vile Mrisho Ngassa, Juma Kaseja, Nurdin Bakari, Juma Nyoso, Nadir Haroub Canavaro, Haruna Moshi Boban na wengineo wana vipaji vizuri na wanaweza kufanikisha maendeleo ya michezo hapa nchini.
 
Tatizo hawawezi kwenda mbele bila kuongozwa na hao wanaowaongoza ndio wameoza kabisa. Haya lazima yasemwe kama tuna lengo la kuboresha soka letu. Huo ndio ukweli wa mambo.
 
Vinginevyo tutakuwa tunacheza soka la nyumbani bila kuwa na maendeleo yoyote, inagwa Mataifa mengine yanazidi kuchanja mbuga. Viongozi wa soka kuanzia ngazi ya klabu, mikoa na Taifa kwa ujumla wajipange katika hilo.
 
Wasiopenda kasi ya mabadiliko wawekwe kando kwa ajili ya Tanzania. Nasema hivyo huku nikiamini kuwa mashabiki wanaopenda soka ni wengi mno. Ukitaka kuhakikisha hilo, hudhuria mechi za Simba, Yanga au timu ya Taifa.
 
Kama mipango itawekwa, basi soka la Tanzania litapanda kwa timu zetu zote, kama vile Coastal Union, Kagera Sugar, Azam FC, Mtibwa Sugar, African Lyon, Toto African na nyinginezo, hivyo kuingiza mashabiki wengi katika mechi zao.
 
Mashabiki wa soka hawatachagua tena mechi za kuingia. Wataingia kwa kila mechi, maana wanapokwenda huko wanapata kitu kizuri. Nasema hivyo kwasababu, leo hii mashabiki wanaingia kwa Simba na Yanga kwakuwa ndio timu zao wanazopenda.
 
Hawapendi soka lao, ila wanapenda timu hizo kongwe. Kama hivyo ndivyo, tunawezaje kuwabadilisha watu juu ya mtazamo wao? Hakika ni mikakati. Mipango imara pamoja na kuacha ubabaishaji katika aina ya viongozi wetu.
 
Sheria zifuatwe na dhamira ya kweli iendelee kuwekwa kwa ajili ya kuinua kiwango cha michezo kwa nchi yetu. Huo ndio ukweli wa mambo. Tusipofanya hivyo, tutajiweka kwenye mtihani na kulaumu wakati hatuna mikakati.
 
Hakuna mtu asiyejuwa mambo mazuri ya kufanya. Wote waliokuwapo kwenye nafasi za uongozi wa soka, hakika ni wenye akili zao timamu. Hivyo watumie vichwa vyao kubuni na kuendeleza mambo yenye tija kwa Taifa letu.
 
Nasema haya kwa kujua kuwa tumekuwa na mapungufu mengi katika uendeshaji wa soka letu, hivyo nadhani huu  ni wakati sasa wa kujifanyia marekebisho kama kweli ipo chembechembe za kuinua soka la Tanzania.
 
Kwa sasa, bila kuangalia ni Simba inayoongoza ligi, Azam FC, Yanga, Mtibwa Sugar, ila hakuna soka linalosuuza nyoyo za watazamaji zaidi ya wengi wao kutumia rushwa aidha ya fedha au ya mapenzi yao kwa timu hizo, hasa hizo kongwe.
 
Kama tumeshindwa werevu sio mbaya tukiendelea kujifunza na ujinga, ila wasipite watu vichochoroni wakijifanya wana uchungu na soka letu, maana wakati huu wapo kimya wakiendelea kutafuna kile wanachopata.
 
Wakati ni huu. Tujisahihishe ili kulifanya Taifa lisiwe kichwa cha mwendawazimu kama alivyowahi kusema, Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi.
 
0712 053949
0753 806087

Wema, Aunt Ezekiel wawaomba radhi Watanzania


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WASANII wawili wa filamu wenye majina makubwa hapa nchini, Wema Sepetu na mwenzake Aunt Ezekiel wamewaangukia Watanzania kwa kusema hawajajua kama watawakera watu haswa baaada ya picha zao kuzagaa katika mitandao ya kijamii na vyombo vingine vya habari.

Wema na Aunt walipokuwa katika ziara ya tamasha la Fiesta, walipigwa picha za utupu, walipokuwa jukwaani hivyo kuwakera watu wengi, ukizingatia kwamba wao ni kioo cha jamii na wanastahili kuishi kwa staha na sio kuanika nyeti zao.



Hivi ndio vivazi vya Wema Sepetu kushoto na Aunt Ezekiel kulia vilivyozua balaa hadi kuomba radhi leo kwa Watanzania, katika Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo. Katikati ni JB wakati wapo kwenye shoo ya Fiesta ya mjini Moshi.


                                          Wema Sepetu akiomba radhi kwa Watanzania

Wema na Aunt Ezekiel waliitumia siku ya jana katika Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo kuzungumza na waandishi wa habari, ili wafikishe vilio vyao, wakisindikizwa na Katibu wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAF), Willsona Makubi pamoja na msanii mwingine wa fgilamu, Tino Muya.

Akizungumzia sakata hilo, Wema alisema hawana uzoefu wa kupanda katika majukwa makubwa, hivyo baada ya kufanya hivyo, baadhi ya wapiga picha na wananchi wengine waliingia kwenye kazi hiyo na kusambaza picha zao.

“Sikujua kabisa kama picha zangu zingezagaa kwenye mitandao maana sina uzoefu huo kama waliokuwa nao wasanii wengine wa muziki wanaopanda jukwaani kila wakati, ila kwa sasa nimejua na naamini sitawakera tena Watanzania.

“Nipo chini ya miguu yao na mkawaeleze kwamba tabia yangu inawachosha pia hata ndugu zangu, maana nao ni waathirika kwakuwa wanazipata kwenye vyombo vya habari na jinsi ninavyoonyeshewa vidole,” alisema Wema.

Naye Aunt alisema tangu sasa amekuwa msanii mpya naa kioo cha jamii, maana atajilinda katika kila jambo analofanya ili aendelee kuheshimiwa na kutumainiwa kama msanii mwenye dhamana na kutangaza utamaduni wa Mtanzania.

Huku akiwa na masikitikio makubwa, Aunt alisema,“ Hata mimi na mwenzangu Wema tunapata tabu sana, hivyo tuliamua kukutana na viongozi wetu ili tutumie fursa hii kuzungumza na nyie tukijua fika mtafikisha vilio vyetu kwa Watanzania wote,” alisema mwanadada huyo ambaye jana alivaa vazi la heshima na kuahidi kuwa mtu mwenye maadili.

Akielezea sakata hilo, Makubi alisema wanaamini wasanii hao watafuata maadili ya Mtanzania katika kujiheshimu katika maisha yao yote, ndio maana baada ya tabia zao kuwa mbaya waliamua kujishusha na kutaka suluhu na jamii yao.

“Wasanii hawa wasamehewe na naamini watakuwa watu wenye maadili kuanzia hapa, hivyo ni jukumu letu kujua kuwa kadri siku zinavyokwenda wanazidi kupanuka kiakili na kujua wataacha tabia zao za kukera,” alisema.

Katika tamasha la Fiesta liliiofanyika katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara, wasanii hao waliambatana kwenye ziara hiyo na kupanda jukwaani kuwasalimia mashabiki wao, jambo ambalo hata hivyo liliwakera baadhi ya watu baada ya kupanda na vivazi vya utupu na kujiachia jukwaani hivyo kupigwa picha mbaya.

Sunday, October 14, 2012

‘Bebaneni mkichoka mtaacha’


 
 
SIWEZI KUVUMILIA
 
 
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
HUWEZI kumkataza mtu asitumie nafasi yake kufanya kile anachokipenda katika tasnia ya michezo, ukiwamo mpira wa miguu. Kila mtu anafanya kile anachokiona kwa manufaa yake na marafiki zake anaokula nao.
 
Katika hilo, hata kama watu wawe wakali vipi, lakini itatungwa sababu, uongo wa kila aina kusafisha au kusawazisha kinachopingwa na wadau wao. Kwangu mimi nasema, bebaneni mkikochoka mtaacha na kuendelea na maisha mengine.
 
Nayasema haya kwa uchungu mkubwa baada ya watu kulazimisha maji yapande mlima. Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Leodgar Tenga, juzi aliwaambia waandishi wa habari kuwa elimu kwwenye kuongoza soka sio lazima.
 
Tenga anayasema haya huku akijua wanachama wao wengi, wamelazimika kusimamisha chaguzi zao, au kusogeza mbele ili wabadilishe katiba zao kwa ajili ya kuingiza kipengele cha elimu ya kidato cha nne kuingizwa.
 
Wengi wamekutana na kadhia hii. Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Hassan Dalali, amekumbana nayo na kuachia nafasi yake ya uongozi wa Simba. Lakini leo hii kwakuwa kuna mtu anahitajiwa, ulazima huo unafutwa.
 
Tenga amelazimika kusema haya maana TFF inamuhitaji mgombea wa Chama cha Soka mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Amini Bakheresa. Bakheresa amekuwa akiwekewa pingamizi na wadau mbalimbali wa michezo.
 
Hata hivyo, wanaomuwekea pingamizi hushindwa baada ya watu wenye nafasi zao kuingilia kati kwa ajili ya kubebana. Ndio maana nasema, kwangu mimi siumizwi na suala hilo la kuwasaidia marafiki zenu, ila sioni haja ya kipengele cha elimu kuwa hoja.
 
Vinginevyo waheshimiwa watajizalilisha tu. Tenga na jopo lake la TFF linajipaka kinyesi, maana hawawezi kuwakataza wachache na kuwaruhusu wengine. Tangu mwanzo, sikuwahi kukubali mabadiliko ya katiba ili kuingizwa kipengele cha elimu.
 
Nilifanya hivyo kwakujua uongozi hausomewi kamwe. Uongozi ni kipaji na sio kila mtu anaweza kuwa viongozi. Nilifanya hivyo kwakuangalia viongozi wengi mahiri katika Taifa hili ambao hawak,uwa na elimu kubwa.
 
Hata kwenye soka, Dalali aliongoza kwa  mafanikio makubwa akiwa Simba. Aliweza kuipa ubingwa timu yake bila kufungwa hata mechi moja. Lakini kipengele cha elimu kikamuondoa, tena kwa kubarikiwa na TFF.
 
Leo hii vipi DRFA wembe huo usitumike? Kuna nini hapo kwenye ofisi za TFF na DRFA? Aibu hii itakwisha lini? Hakika siwezi kuvumilia. Aidha, iwekwe wazi kuanzia sasa kuwa yoyote anaweza kuwa kiongozi hata kama akiwa hana elimu ya kidato cha nne.
 
Kila mwenye uwezo huo wa kuongoza, apewe nafasi na sio kwa watu wachache. Nalisema hili hadharani, maana kuna siku kutatokea mkanganyiko wa kiuongozi na kuzua balaa. Hili linawekwa kwenye kumbukumbu na vizazi vijavyo watalifanyia kazi.
 
Hakika siwezi kuvumilia na nitaendelea kusubiri wenye mtazamo wao, harakati zao na wanaotaka kuweka kumbukumbu sawa kuwa wakali zaidi katika hilo.
 
Kwakuwa mimi sina nia yoyote ya kuwania nafasi hiyo kwa sasa, pia siwezi kulia wala kucheka ninapoona sheria hazifuatwi, maana najua fika hata niseme vipi, wakubwa hao wakiamua lao hakuna wa kuwazuia, ndio maana mbeleko yao kwa maswahiba zao zipo pale pale.
 
Tena kwa dharau tele. Eti wanasema kelele za chura hazimnyimi tembo kunywa maji na dua ya kuku haipati mwewe. Haya bwana nyie endeleeni kubebana hadi mtakapochoka wenyewe na kuanza kufuata sheria na taratibu mlizoweka wenyewe.
 
Tukutane wiki ijayo.
 
0712 053949
0753 806087

Thursday, October 11, 2012

Chaguzi za ndani zikibebe Chama Cha Mapinduzi








MGODI UNAOTEMBEA





Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KATIKA mikoa mbalimbali ya Tanzania, kumekuwa kukiendelea na chaguzi za ndani za Chama cha Mapinduzi CCM na kushuhudia majina kadhaa yakigonga vichwa vya watu wengi.

Chaguzi hizo zimeanza siku chache baada ya Mwenyekiti wake, Jakaya Mrisho Kikwete, kuwapasha wabaya wao kuwa chama hicho hakiwezi kufa, hasa kwa wanachama wao kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali za chama hicho.

                                          Jakaya Kikwete, Mwenyekiti wa CCM


Nafasi kama vile Mwenyekiti wa Mkoa, Wilaya, Katibu, Mweka Hazina katika ngazi mbalimbali, pamoja na Mjumbe wa NEC Taifa.

Hizi ni nafasi zilizoombwa kwa wingi mno na kuonyesha jinsi chama hicho kinavyoendelea kuungwa mkono na wanachama wengi, ingawa baadhi ya wapinzani wanaona chama hakina mashiko na kinajichimbia kaburi.

Ni matokeo mazuri mno. Kila mtu anayapenda kwa wale wenye mapenzi mema na chama chao kinachojiweka katika umahiri wa aina yake na kushindana na vyama vinavyoendelea kuzaliwa kila siku na kuungwa mkono na watu wake.

Kama idadi ya watu walioomba kuteuliwa kugombea nafasi hizo zimeongezeka, kwanini waseme chama kimekufa?

Hata hivyo wahenga walisema lisemwalo lipo. Na katika kuwasikiliza wadau hao, lazima ukweli usemwe na juhudi ziwekwe kama tahadhari ya kukijenga chama.  Je, chaguzi hizo za ndani zina manufaa na chama?

Je, wale walioenguliwa katika nafafsi hizo wamekubali matokeo au ndio wanaanza kujenga matawi yao kwa ajili ya kukihujumu chama chao? Vipi wale walioshindwa katika chaguzi hizo, je wamekuabali kuwa hayo ni matokeo ya kawaida?

Hili linapaswa kueleweka vizuri. Leo wenye chama chao wanaweza kufurahia kuwa chama bado kinapendwa, lakini wachache wao wakawa tofauti. Kwa mfano, Waziri Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye ameshindwa nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), kupitia Wilaya ya Hanang, Mkoa wa Manyara.

Sumaye ameshindwa mbele ya mwanasiasa mwenzake wa CCM, Dk. Mary Nagu, ambaye pia Mbunge wa Jimbo la Hanang na Waziri wa Nchi, Ofisi wa Rais, Uwekezaji na Uwezeshaji.

Uchaguzi huo ni kati ya ile inayochanganya vichwa vya watu wengi, ukizingatia kwamba chaguzi za ndani za CCM zimekuwa na matokeo magumu na joto la ushindani kwa kila mgombea na yule anayepiga kura.

Haijulikani kwanini chaguzi za chama hicho ni ngumu. Labda ni kwasababu wanaopiga kura ni wenye kufanana itikadi, ingawa kwenye malengo hutofautiana kwa kiasi kikubwa.

Kujuana au kurubuniwa kwa rushwa nako ni hatua ngumu kwa chama chao. Ingawa rushwa hukumewa na kila mtu, lakini sio sababu ya kuamini kuwa kichocheo hicho ndani ya chaguzi kimeachwa.

Kikwete alitahadharisha kuwa yoyote atakayebainika anatoa rushwa kwenye uchaguzi huo, hatachekewa, akiwa na maana ya wagombea wote kuacha kutumia rushwa.

Wakati Kikwete anasema hivi, wale wagombea na wapiga kura wao wanapaswa kuwa na uzalendo na chama chao. Wao wasipokuwa makini, uwepo wao hauwezi kuwa na manufaa zaidi ya kukibomoa chama chao.

Wafanye siasa zenye mashiko na mvuto kwa kila mmoja wetu. Wawe kioo cha jamii ndani ya chama au nje ya chama. Wasifanye siasa za kujionyesha mbele ya hadhira, huku malengo halisi, yakiwamo kutetea maslahi ya chama yakiwa adimu.

Kila mgombea au kiongozi wa chama lazima avae uhusika na kukitetea chama chake mbele ya wapiga porojo wengine, hasa waliokuwa upande wa upinzani.

Kama Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kinahaha kufanya mikutano yao mikoani kujenga chama chao, kwanini hawa wa CCM wakae hadi Uchaguzi Mkuu.

Chadema wanatamba na kauli mbiu zao, Dira ya Mabadiliko Movement for Change (M4C), wakati Chama cha Wananchi (CUF) wamekuja na kauli mbiu yao ya (Vision for Change) (V4C), tena wakianzia harakati zao hizo katika ngome ya Chadema, jijini Arusha.

Baada ya kuibuka hayo, Chadema na CUF walianza kurushiana makombora wakisema kuwa chama hicho kimedandia hoja na mwelekeo wao, ingawa CUF nao baadaye walijibu kwa kusema wao ndio waasisi wakubwa.

Kwa mujibu wa CUF, mwaka 2008 na kuiweka rasmi kwenye ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010, hivyo yoyote anayefikiri kuwa hoja yao imetoka Chadema wanajidanganya.

Sitaki kusema nani mkweli kati ya Chadema na CUF, ila hizo ni changamoto nzuri za siasa za Tanzania, zinazoongozwa na CCM iliyokaa madarakani kwa miaka mingi, tangu Taifa hili lilipopata Uhuru wake mwaka 1961.

CCM wala isisononeshwe na vuguvugu la mabadiliko kwa Chadema na CUF, au hata vyama vingine navyo vikifuata nyayo hizo kwa ajili ya kuwapatia elimu ya uraia Watanzania na kuleta ushindani katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2015.

Kikubwa kinachotakiwa kufanywa na hao wana CCM ni kukubali kujifunza kutokana na makosa, sambamba na lengo la kuendelea kukaa madarakani kwa kufanyia kazi kero za Watanzania.

Kwa siku za hivi karibuni, Serikali inayoongozwa na CCM, chini ya Kikwete, imekuwa ikifanyia kazi kero hizo, zikiwamo za usafiri, jambo linalowafanya watu waanze kuamini huenda mambo yakawa mazuri katika siku za usoni.

Haya yakiendelezwa na kubuniwa  miradi mingine ya maendeleo, watu wataichukia CCM kwa mambo mengine, likiwamo hilo la ukongwe wake.

Katika kulijua hilo, ni jukumu la kila kiongozi wa CCM, kijana au mzee, mwanamke au mwanaume kufanya kazi kwa ajili ya chama chake.

Najua mapungufu kwa baadhi ya waliochaguliwa au kupitishwa kuwania nafasi hizo haziwezi kukosekana, lakini kama wenyewe wanajua hilo wanaweza kuyafanyia kazi, ndio maana kamati ziliona wanafaa wagombee nafasi hizo.

Watu kama vile Amos Makalla, Juma Nkamia, Mwita Gachuma na wengineo ni kati ya wale waliofanikiwa kushinda katika nafasi walizoomba mwaka huu.

Makalla ambaye pia ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, ameshinda Mjumbe wa NEC Taifa, kupitia Wilaya ya Mvomero, wakati Nkamia, ameshinda kwa Wilaya ya Nchemba.

Ukiangalia kwa haraka, utagundua kuwa wanachama wengi na wenye majina makubwa wameshindwa katika chaguzi hizo, hivyo wasipokuwa na moyo wa subira, wataongeza idadi ya makundi hasimu ndani ya CCM.

Kila mmoja akisema aumizwe na kuanguka kwake, hali ya mambo ndani ya CCM itakuwa tete, hivyo kukipasua zaidi katika uchaguzi Mkuu ujao. Hakuna anayebisha kuwa waliochaguliwa leo, ndio watakaoibeba au kukiangusha chama mwaka 2015.

Wakifanya siasa zenye tija na malengo ya dhati, sidhani kama chama kitaanguka, hasa kama wakikubali matokeo na kuwabeba kila anayetajwa na chama, iwe kwenye nafasi ya Urais, Ubunge, Udiwani au Uenyekiti wa Serikali za Mitaa.

Najua yapo machungu makubwa ya kuachwa au kushindwa bila sababu za msingi, lakini ifikie wakati wanachama wote wawe kitu kimoja. Kwa mujibu wa Kikwete, sio kila mmoja wao anaweza kuwa kiongozi ndani ya CCM.

Walioachwa au watakaoshindwa katika chaguzi zinazoendelea ndani ya chama, wote wawe kitu kimoja na kuleta ushirikiano kwa ajili ya kukiweka chama chao katika mazingra mazuri ya ushindi na kuonyesha kuwa bado wanakubalika.

Haya yatatimia kama wote wakiwa kitu kimoja na kuacha zile siasa za kupakana matope, kutukanana au kurushiana makombora yasiyokuwa na msingi wowote. Kunyukana kwao, ni hasara kwa chama chao na kuvipa kiburi cha majigambo vyama vya upinzani vinavyotembea kwa matao kwa kuona uwezo wa kufanya lolote kwa Watanzania wanao.

Vyama ambavyo vimekuzwa na Serikali ya CCM, vinavyokula ruzuku za Watanzania, huku vikiwa na jeuri kubwa au uchu wa kushika dola, ingawa katika harakati zao hizo, wanaweka mbele maslahi yao na kuacha moyo wa uzalendo nyuma, hali inayoweza kuleta vurugu kubwa kama kila mmoja atakuwa na uchu wa kushika dola.

Huo ndio ukweli. Kila mmoja wetu aujuwe na kuufanyia kazi, wakiwamo washindi au washindwa katika chaguzi za ndani za CCM zinazoendelea kutimua vumbi katika mikoa mbalimbali ya Tanzania na kuleta vicheko na vilio kwa wenye nia ya kuwa viongozi wa chama hicho, kama mwanzo wa kuweka dira ya kushika nafasi kubwa zaidi iwe kwenye chama au serikali.

0712 053949
0753 806087

Mwisho


LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...