https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Thursday, January 03, 2013

Mtanga asema Mungu anawapa kadi nyekundu

Dada huyu akishuka kwenye gari huku analia
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MSANII wa Vichekesho hapa nchini, Hamis Changale, maarufu kama Mtanga, ameshangazwa na kadi nyekundu zinazoendelea kwa wasanii na kusababisha vifo vyao, hali inayoogopesha.
Wadau na wasanii wakijadili jambo kwenye msiba wa Sajuki

Mtanga aliyasema hayo mapema leo, akisema kadi hizo nyekundu zinatolewa kwa wasanii nyota, akiwamo Steven Kanumba, Sharomillionea, Mropelo, John Maganga na sasa ameondoka Juma Kilowoko, maarufu kama Sajuki.

Thea akijadili jambo msibani kwa Sajuki
Mtanga alisema vifo hivyo ni kama kadi nyekundu kwa wasanii Tanzania, jambo linalomnyima raha kwa kusikia au kuona nyota wanaendelea kupukutika kila siku kwa sababu za kushangaza.

 Hali inavyoendelea msiba wa Sajuki Tabata Bima

“Alipokufa Kanumba, watu wengi tuliogopa kutokana na kifo chake, lakini bado ikaja tena kwa wasanii zaidi ya watano, akiwamo Sharomillionea aliyekufa mwishoni mwa mwaka jana na kuzikwa kwao Lusanga.
Msanii wa vichekesho, Mtanga

“Na leo tena mwenzetu Sajuki anafungua pazia la vifom kwa wasanii wa Tanzxasnia kwa mwaka huu kuonyesha kuwa bado Mungu anaendelea kutoa kadi nyekundu kwa wasanii kila siku ya Mungu,” alisema Mtanga.
Sajuki enzi za uhai, wakati ni mgonjwa akiwa na mke wake, Wastara

Kwa mujibu wa Mtanga, kadi nyekundu katika mchezo wa soka ni tukio linalotokea kati ya mchezaji uwanjani na mwamuzi kwa ajili ya kumtoa nje ya uwanja mchezaji aliyefanya kitendo ambacho si cha kiungwana.

Taarifa za kifo cha Sajuki kimeendelea kuwagusa Watanzania na viongozi wa Serikali, baada ya Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba kuwa miongoni mwa waombolezaji waliofika msibani Tabata Bima kwa ajili ya kuungana katika msiba wa Sajuki.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, aliwata Watanzania kutumia fursa ya kifo kwa ajili ya kumuombea marehemu pamoja na kuwataka wasanii wawe kitu kimoja.

Wednesday, January 02, 2013

'Sajuki alisema hawezi kuishi tena duniani'



Wastara akiwa amefunikwa uso huku akilia kwa uchungu

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NI dhahiri kuwa wakati mwingine baadhi ya watu hutabiri vifo vyao, kiasi hata ha kuwazuia ndugu zao waache kufuja fedha katika kuuguza kutokana na maradhi yao.
 Rais wa TAFF, Simon Mwakifambwa, akitangaza kamati za kuratibu msiba wa Sajuki, nyumbani kwake Tabata Bima leo.

Hii hutokea sana katikaa jamii. Baadhi yao hufikia kusema “Nasikitika siwezi tena kuishi katika Dunia hii. Mwisho wa maisha yangu"

Nimelazimika kuandika maneno haya, maana kauli ya mwisho ya msanii wa filamu, Juma Kilowoko, maarufu kama Sajuki ilikuwa ni kumtaka mke wake amuombee msamaha kwa watu wote aliowahi kuwakosea katika kipindi cha maisha yake.

Maneno haya yalikuwa mahungu kwa mwanadada Wastara Juma, mke wa marehemu Sajuki. Naomba uwaambie ndugu zangu kuwa uhai wangu tena ni mdogo sana.

Siwezi kuishi, maana sioni dalili nzuri za kuniponya” maneno haya yalitoka katika kinywa ha Wastara ambaye kwa kipindi hicho, alikuwa akilia na kusaga meno kuonyesha huzuni yake.

Jamani mimi nitaweza kuishi peke yangu? Sajuki wangu kwanini umenitendea hivyo? Yani kweli unasema nikuagie kwa watu kama hutapona kumbe kweli umeshajua unaniacha peke yangu,” Wastara aliendelea kulalama, huku akizidi kufunikwa uso wake.

Inauma sana. Sajuki amekufa katika kipindi ambacho watu wengi walifahamu uhai wake utaendelea kuwapo. Kama Sajuki alistahili kufa, basi ingekuwa mwaka jana alipokuwa kwenye hali mbaya kiasi cha kulazimika kuchangiwa na wasamalia wema kwa ajili ya kwenda India.

Kwa mujibu wa taarifa, Sajuki alipokwenda India, maradhi yaliyompeleka ya Tumbo yaliongezeka mengine ya Kansa ya ngozi. Shughuli ilikuwa kubwa sana. Mbaya zaidi, Sajuki hakuwa na uwezo wa kustahimili ugonjwa wake.

Hata hivyo, katika kipindi cha mwisho wa mwaka 2012, Sajuki alikuwa kwenye afya kiasi Fulani. Muda wote alikuwa akisikika akimshukuru Mungu wake kwa kumpa uhai.

Katika kumshukuru Mungu, Sajuki pia alikuwa haishi kumshukuru Mungu kwa kumpa mke mwema, mwenye upendo wa kweli. Mwanamke ambaye licha ya kukutana na vikwazo vingi, lakini aliendelea kufunga khanga yake akitetea upendo wake kwa Sajuki.

Kwanini? Pamoja na yote hayo, lakini leo tunaongelea kifo chake. Na saa tano za asubuhi, keshokutwa Ijumaa, mwili wake utazikwa katika makaburi ya Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Msiba wake ni mzito sana. Wasanii wote pamoja na wadau wanalia. Serikali nayo kwa kupitia Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo inalia kutokana na msiba wa Sajuki.

Amekufa na katika kipindi ambacho watu wanashangaa kwanini bundi wa vifo vya wasanii wa maigizo na filamu anaendelea kukaa kwenye paa za nyumba za wasanii hao Tanzania?

Sajuki amekufa katika kipindi cha siku 37 kabla ya arobaini ya msanii Hussein Mkiety, maarufu kama Sharomillionea, inayotarajiwa kusomwa Januari nne, kijijini kwao Lusanga.

Mamia ya watu walikuwa wakimiminika katika viwanja vilivyokuwapo nyumba ya marehemu Sajuki, maeneo ya Tabata Bima. Ukifika hapo nyuso zao zinasema.
Wengi wanalia na kuomboleza kifo hicho. Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), kwa kupitia Rais wake, Simon Mwakifambwa na wadau wengine wamekuwa wakipita huku na kule kwa ajili ya kuweka sawa taratibu za msiba huo wa Sajuki.
Taarifa ya Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara amewatumia salamu za rambirambi, ndugu, jamaa na wasanii wote nchini kufuatia kifo cha Sajuki ilimuumiza na kutaka Watanzania kumuombea dua njema.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo kifo chake ni pengo kubwa kwa Serikali, wadau wa tasnia ya filamu na michezo ya kuigiza nchini kwa ujumla. “Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Sajuki na sina maneno ya kuelezea masikitiko na huzuni nilinayo, kwani kifo chake ni pigo katika tasnia ya filamu za michezo ya kuigiza,” alisema Dkt. Mukangara.

Dkt. Mukungara amewataka ndugu, jamii na wasanii wote kuwa wavumilivu na watumilivu wakati wote wa msiba na kumuombea marehemu makao mema kwa Mwenyezi Mungu. Sajuki ni mzaliwa wa mkoa wa Ruvuma na sanaa yake alianza kujihusisha nayo alipojiunga na kikundi cha Kaole Sanaa Group, ambapo baadaye alicheza filamu Revenge  ya Kampuni ya RJ.

Mwaka 2008 aliamua kuanza kutengeneza kazi zake mwenyewe ambapo filamu yake ya kwanza iitwayo Two Brothers  kwa kushirikiana na Shija  Deogratious ilitoka. Sajuki baadaye aliamua kuanzisha kampuni yake iitwayo WAJEY Production Company ambapo alitengeneza filamu nyingi zikiwemo Mboni Yangu, Round, Briefcase , Kijacho, Kozopata, Mchanga na Keni, 077( Zero Seven Seven).nk 


Sajuki alifanikiwa kucheza michezo ya kuigiza na filamu na wasanii wengi wenye majina hapa nchini. Sajuki amebobea katika Uigizaji, Utayarishaji na Uongozaji wa filamu. Sajuki alianza kuugua mwaka 2010 na hali ilizidi kudhoofu mwaka 2011, ambapo alikwenda kutibiwa nchini India kutokana na michango kutoka kwa wadau tasnia ya filamu. 

Alirudi na kuonekana kapata nafuu kidogo jambo ambalo lilileta matumaini na furaha kwa watanzania; aliporejea tu aliweza kutoa filamu iitwayo Kivuli  huku filamu nyingine ikiwa katika hatua ya utengenezaji.

Ambapo pia filamu ya kumchangia iliandaliwa na kuitwa Sayla na kushirikisha wasanii na viongozi wa serikali, akiwamo Zitto Kabwe, ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, January Makamba na wengineo.

Bongo Movie wauteka msiba wa Sajuki

Wastara aliyeshikwa kichwa akilia kwa uchungu kutokana na msiba wa mumewe Sajuki



Wastara aliyefunikwa uso akilia kwa uchungu

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MUUNGANO wa wasanii wa filamu Tanzania, unaojulikana kama Bongo Movie, umeuteka msiba wa msanii Juma Kilowoko, maarufu kama Sajuki kwa kuiomba familia ya marehemu ili wauzike mwili wa msanii mwenzao Ijumaa saa tano asubuhi, katika makaburi ya Kisutu.

Alieoa nyumba moja na Sajuki, Haroub Mbeleki, kushoto, akizungumza machache na wadau wa sanaa waliofika msibani.

Ombi hilo lilikubaliwa na baba mzazi wa marehemu, Juma Kitilu na kuagiza watu walioweka msiba mwingine nyumbani kwao Songea, kuvunja na kupanga safari ya kuja jijini Dar es Salaam kwa mazishi.

Katika kikao kilichoitishwa na Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania TAFF, Simon Mwakifwamba, kilitangaza taratibu za msiba huo ambapo pia Kamati sita ziliundwa kwa ajili ya kuweka sawa.
Msanii mkongwe wa filamu Natasha, akiingia msibani.

Akizungumza na Handeni Kwetu msibani hapo, Mwakifwamba alisema kamati hizo ni Kamati ya Mazishi, Kamati ya Fedha, Kamati ya Itifaki, Kamati ya Chakula, Kamati ya Habari, Kamati ya Usafiri na Kamati Kuu inayobeba na kusimamia kamati zote zilizoundwa katika msiba huo.
Baba wa marehemu, Mzee Juma Kitilu, kulia akizungumza nyumbani kwa mtoto wake, marehemu Sajuki leo.

Alisema kuwa wameshukuru baba wa marehemu kukubaliana na wazo lao la kumzika mwenzao Dar es Salaam kutokana na umuhimu wake na hamu ya kutaka kuzikwa na mamia ya mashabiki wake.
Marehemu Sajuki enzi za uhai wake

“Hili ni pigo la wasanii na mashabiki wao kwa ujumla, hivyo tunachoshukuru kuwa familia imetuelewa na wote kuwa kitu kimoja, hasa kwa kuhakikisha kuwa waliokuwa Songea nao wanaingia hapa kuanzia au kesho,” alisema.

Wasanii wa vichekesho Tanzania, Mtanga kushoto na Kiwewe wakiingia msibani Tabata Bima leo.

Baba yake Sajuki, mzee Kitilu alisema kuwa ameona hana sababu za kuwakatalia wasanii kwa ombi la kushiriki kwa karibu msiba wa mwenzao, jambo lililomfanya akubali haraka kwa ajili ya umuhimu wao.
Mtangazaji wa Clouds Tv, Zamaradi Mketema, akizungumza na wadau wa filamu katika msiba wa Sajuki nyumbani kwake Tabata Bima leo.

“Sina sababu ya kuweka ngumu kwa wasanii wanaotaka kumzika mwenzao, hivyo wale wote waliokuwa Songea, nimewaambia wafunge safari kwa ajili ya kuja Dar es Salaam kumzika Sajuki Ijumaa,” alisema.

Awali, Handeni Kwetu ilimshuhudia mke wa marehemu, Wastara akilia kwa kuomboleza msiba wa mume wake, akisema kuwa alishatangaza kifo chake kwa wiki ya mwisho ya mwaka 2012.

“Uliniambia nikuagie kwa wote uliowakosea katika kipindi cha maisha yako, kumbe ulishajua unataka kuniacha peke yangu? Nitaweza mimi jamani maisha ya peke yangu Sajuki wangu,” alisikika Wastara akilia na kushikwa na kwi kwi ya uchungu.

Kutokana na imani ya Kiislamu, kupatikana picha ya Wastara ni kazi kubwa, maana mara baada ya kufikwa na msiba huo, taratibu za kidini zilianza kuchukua mahali kwake na kuhakikisha haonani na wanaume nje ya familia yake.

Sajuki alikufa saa moja asubuhi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, ikiwa ni baada ya kukaa hapo kwa siku kadhaa akitibiwa. Kabla ya kifo chake, Sajuki alikuwa na maradhi ya tumbo, huku akianguka siku chache zilizopita jijini Arusha, alipokwenda kufanya shoo.

Kuanzia saa mbili za asubuhi, mamia ya watu na wasanii yalikuwa yakizidi kuingia nyumbani kwa marehemu, Tabata Bima kwa ajili ya kushiriki msiba wa Sajuki, uliohuzunisha watu wengi.




DC Kilindi anusuru machafuko ya wakulima na wafugaji


Mkuu wa Wilaya Kilindi, Selemani Liwowa

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MKUU wa Wilaya ya Kilindi, mkoani Tanga, Selemani Liwowa, amenusuru kutokea kwa machafuko ya wakulima na wafugaji katika wilaya yake, baada ya wakulima wa kijiji cha Mswaki kuwateka ng’ombe waliokuwa kwenye mashamba yao na kuwapeleka kijijini kama ishara ya kuonyesha uharibifu unaofanywa na wafugaji katika vijiji vyao.

Hatua hiyo ilisababisha kutoelewana na kumfanya Mkuu wa wilaya kwenda katika kijiji hicho wiki iliyopita kwa ajili ya kuangalia tatizo na kuepusha mgogoro huo unaosumbua katika vijiji vya wilaya Kilindi na Tanzania kwa ujumla.

Akizungumza na Handeni Kwetu, kwa njia ya simu, DC Liwowa alisema kwa uchunguzi wao umegundua kuwa baadhi ya wenyeviti wa vijiji vyao wanaruhusu kuingia kwa wafugaji bila kufuata utaraatibu jambo lililoleta balaa katika kijiji cha Mswaki na Turiani, wilayani kwake.

Alisema wakulima hao waliamua kuwachukua ng’ombe hao naa kuwapeleka kijijini kwa ajili ya kushitaki kwa serikali ya kijiji, lakini baadaye wafugaji hao walibadilisha na kusema kuwa mifugo yao imetekwa kwa ajili ya kuiba.

“Hili ni tatizo lililotokea wiki iliyopita na wala sio jipya kama inavyodaiwa, hasa baada ya wafugaji wanaoachia ng’ombe zao kulalama kwa kusema kuwa mifugo yao imetekwa na wakulima, hivyo kuleta kutoelewana miongoni mwao.

“Mimi na ujumbe wangu tulipata fursa ya kwenda katika maeneo yale kuweka mambo sawa, hivyo tuligundua kuwa baadhi ya wenyeviti wanaruhusu wafugaji kuendelea kuingia katika sehemu zao bila kuangalia athari zinazoweza kujitokeza,” alisema.

Migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji imeendelea kuwa tatizo katika wilaya mbalimbali hapa nchini, jambo linalotakiwa liangaliwe upya na Watanzania wote, wakiwamo viongozi wa vijiji, Kata, Tarafa na wilaya kwa ujumla.


Sajuki afariki Dunia Hospitali ya Muhimbili



Marehemu Sajuki
 
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MSANII wa filamu hapa nchini, Juma Kilowoko, maarufu kwa jina la Sajuki, amefariki Dunia leo saa moja asubuhi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Sajuki amekufa huku akiwa na kumbukumbu za kuanguka mwishoni mwa mwezi Desemba mkoani Arusha, alipokwenda kufanya shoo, akiizungumzia kama kujichanganya kwa ajili ya kutafuta fedha za kumpeleka tena India kupata matibabu.

Mke wa marehemu Sajuki, (Wastara)

Akizungumza mapema leo, Katibu wa Baraza la Filamu Tanzania (TAFF), Wilson Makubi, alisema kwamba maandalizi ya msiba huo yatatangazwa baada ya wahusika na wadau kujipanga.

Alisema habari za kifo chake zimeanza kusambaa tangu saa moja asubuhi, hivyo wadau na mashabiki wake watapewa utaratibu juu ya msiba wa msanii huyo mwenye mafanikio katiika tasnia ya filamu Tanzania.

“Sajuiki ni msanii mahiri na amekufa katika siku ya pili ya mwaka huu mwezi Januari, hivyo hakika ni pengo kwa wasanii wote pamoja na mashabiki kwa ujumla, ukizingatia kuwa tulikuwa na mapenzi naye.

“Watu walishajichanga kwa ajili ya kumpeleka India msanii huyo jambo ambalo lilifanikiwa kwa dhati, hata hivyo jitihada hizo Mungu ameona amchukuwe kiumbe wake kwa ajili ya maisha ya milele,” alisema.

Kifo cha Sajuki kwa wasanii kimefungua dimba kwa mwaka 2013, huku ukiwa na kumbukumbu za kuondokewa na wasanii watano katika kipindi cha mwaka 2012, akiwamo Steven Kanumba, Sharomillionea na wengineo.


Tuesday, January 01, 2013

Coco beach yafurika sherehe za mwaka mpya



Licha ya ufukwe kuwa sehemu ya starehe kwa watu wengi, lakini baadhi ya wazazi wameshindwa kuwa makini kiasi cha kuwaachia watoto kuogelea bila kuangalia usalama wao. Pichani mtoto huyu aliyembeba mwenzake akionekana akikimbia wimbi la maji katika ufukwe wa Bahari ya Hindi, Coco Beach, baada ya kuangushwa kiasi cha kujiweka hatarini na aliyembeba. Picha na Kambi Mbwana.
Watanzania wanaoishi jijini Dar es Salaam, wakijimwaga katika ufukwe wa bahari ya Hindi, Coco Beach, leo wakisherehekea Sikukuu ya Mwaka Mpya. Ufukwe huo ulijaa watu wengi waliokwenda kutembelea katika eneo hilo wao na familia zao. Hata hivyo, watoto walikuwa wengi wakiingia baharini bila kuwa na waangalizi jambo linaloweza kuwa hatari kwao. Picha na Kambi Mbwana.

Lowassa asifia sera ya vikoba Tanzania




Waziri Mkuu wa zamani na mbunge wa Jimbo la Monduli, Edward Lowassa, akitoa hotuba kwa wananchi wa kijiji cha Mswakini, Wilayani Monduli, wakati wa uzinduzi wa Vikoba kijijini hapo.
Wakati Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ambaye pia ni mbunge wa Monduli mambo yalionekana hivi, akiwa anaingia sambamba na mke wake, Regina Lowassa, katika uzinduzi wa Vikoba katika kijiji cha Mswaki mapema leo.
Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Monduli, aliyejulikana kwa jina laa Judith, akikabidhi hati kwa Edward Lowassa, ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa Vikoba katika kijiji cha Mswakini


Na Mwandishi Wetu, Monduli
WAZIRI Mkuu wa zamani, ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, amesema kuwa ushirika wa Vikoba ni sawa na mshipa wa damu kwa sera ya maisha bora kwa kila Mtanzania.

Lowassa ameyasema hayo leo katika uzinduzi wa Vikoba vya Mswakini, wilayani Monduli, ikiwa ni ishara ya kutambua njia ya kumkomboa Mtanzania.

Akizungumza na wanakikundi hicho, Lowassa alisema kwamba hiyo ni sera aliyoingia nayo madarakani Rais Jakaya Kikwete.

Alisema kuna haja ya kuwa na vikoba nchi nzima kwa ajili ya kuongeza kasi ya maisha bora kwa kila Mtanzania, ukizingatia ni mfumo mzuri kiutendaji wa biashara kwa wote waliokuwa kwenye vikundi hivyo.

Matokeo ya sensa yamshangaza Rais Kikwete

Rais Jakaya Mrisho Kikwete

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WATANZANIA wamefikia idadi ya 44,929,002 mwaka 2012 kutoka watu 34,443,603 katika sensa ya watu na makazi iliyotangazwa jana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.

Idadi hiyo ni kubwa na kumuogopesha Rais Kikwete na kutangaza watu watumie uzazi wa mpango, ikiwa ni kutokana na kugundulika kuwa jumla ya idadi ya watu wote nchini sasa, ni milioni 44,929,002, ikiwa ni ongezeko la watu milioni 10 tangu ilipofanyika Sensa ya mwaka 2002.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, upande wa Tanzania Bara kuna Watanzania milioni 43,625,434, wakati Zanzibar  kuna watu milioni 1,303,568.

Akizungumza baada ya kufanya uzinduzi huo, Rais Kikwete jana aliwataka Watanzania wahakikishe kwamba wote wanafuata uzazi wa mpango, akisema kuwa ongezeko hilo ni kubwa na serikali itashindwa kuwahudumia kama inavyotakiwa.

“Sensa ya mwaka 2002 ilionyesha kuwa Watanzania tupo milioni 34, lakini hii ya mwaka huu tumefikia milioni 44 na kuonyesha kuwa ni ongezeko kubwa sana.

“Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Watanzania tutafikia watu milioni 51, ikiwa ni kwasababu ya watu kuzaliana na ndio maana kuna haja ya kupanga uzazi,” alisema Kikwete.

Wakati Taifa linapata Uhuru, inakadiriwa kuwa mwaka 1967, Watanzania Bara walikuwa milioni 12.3 wakati Tanzania Visiwani walikuwa 300,000 ambapo sasa wapo milioni 1,303,568.

 

Poulsen ataja 22 wa kuivaa Morocco



Kocha wa Stars, Kim Poulsen
 
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WACHEZAJI 22 wameteuliwa na kocha Mkuu wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Kim Poulsen kwa ajili ya kuingia kambini Januari 6 mwaka huu jijini Dar es Salaam kwa kujiandaa na mechi za kirafiki dhidi ya Morocco itakayochezwa Machi mwaka huu.

Kwa mujibu wa Kocha Kim, wachezaji hao wanatakiwa kuripoti kambini katika hoteli ya Tansoma saa 11.30 jioni tayari kwa mazoezi yatakayoanza Januari 7 mwaka huu.

Wachezaji walioitwa ni makipa Juma Kaseja kutoka Simba ambaye pia ndiye nahodha wa Stars, Aishi Manula na Mwadini Ally wote kutoka Azam. Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Amir Maftah (Simba), Erasto Nyoni (Azam), Issa Rashid (Mtibwa Sugar), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga) na Shomari Kapombe (Simba).

Viungo ni Salum Abubakar (Azam), Athuman Idd (Yanga), Amri Kiemba (Simba), Khamis Mcha (Azam), Frank Domayo (Yanga), Mwinyi Kazimoto (Simba) na Shabani Nditi (Mtibwa Sugar).

Washambuliaji ni John Bocco (Azam), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Mrisho Ngasa (Simba), Simon Msuva (Yanga), na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Mbali ya Kim, benchi la ufundi la Taifa Stars linaundwa na Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi), Juma Pondamali (Kocha wa makipa), Leopold Tasso (Meneja), Dk. Mwanandi Mwankemwa (Daktari wa timu), Frank Mhonda (Mtaalamu wa tibamaungo) na Alfred Chimela (Mtunza vifaa).

Mjasiriamali anayelia na masharti ya mikopo



Mama Kipande akiandaa kuku
 
Na Kambi Mbwana, Aliyekuwa Korogwe 
KADRI siku zinavyozidi kusonga mbele, akina mama wengi wanaendelea kuchangamkia kazi mbalimbali zinazoweza kuinua maisha yao na familia zao kwa ujumla.

Wakati wengine wanashiriki kazi zinazotumia akili na nguvu, wapo wengine wanaomenyeka kwenye ujasiriamali kwa kumiliki migahawa, cafe na hoteli katika sehemu mbalimbali za Tanzania, ukiwa ni mpango wa kuboresha maisha yao. 

Kutokana na hilo, familia nyingi zimekuwa zikiishi vyema hasa kwa wale ambao wazazi wao wamekuwa wakishiriki kufanya kazi kwa namna moja ama nyingine. 
Mama Kipande kushoto akiandaa kuku mgahawani kwake

Sio katika majiji tu yenye mchanganyiko wa watu wengi, bali hata kwenye miji inayoendelea, ukiwamo wilaya ya Korogwe watu hufanya bidii mno katika kazi zao kwa ajili ya kuinua uchumi wao na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza na Handeni Kwetu, Mama Kipande anasema akiwa kwenye mgahawa wake huo uliopo Manudu, wilayani Korogwe, mkoani Tanga kuwa biashara yake hiyo inampa ahueni nyingi za kimaisha kutokana na watu wengi kuchagua kupata chakula kwake.
Kwa jinsi watu walivyokuwa wakipata chakula huku wakizungumzia hili na lile, lilinifanya niulize kuwa wingi wao ni wa kila siku au la.
Kwa jinsi mji wa Korogwe unavyozidi kupanuka, hata suala la biashara kwa wajasiriamali linazidi kufanya vyema, huku bidhaa kama vile unga, mchele, mafuta ya kula, maharage na bidhaa nyingine zikiuzwa kupita kiasi.
Mama Kipande anasema biashara yake hiyo ni ya zamani na kila mmoja anamjua kutokana na kuifanya kwa muda mrefu.
Anasema watu mbalimbali wamekuwa wakienda kwenye mgahawa wake kupata chain a chakula cha mchana, huku yeye akihakikisha kuwa huduma nzuri na chakula safi kinapatikana katika mgahawa wake huo.
“Hii ni biashara niliyodumu nayo kwa miaka zaidi ya 20 sasa, huku nikishukuru kwakuwa watu wananiunga mkono na nafanya biashara nzuri na kuimudu familia yangu.
“Vyakula vya kila aina vinapatikana katika mgahawa wangu, huku nikipokea watu kutoka kada mbalimbali, ukizingatia kwamba chakula changu ni kizuri na kinapendwa na watu wengi,” alisema Mama Kipande.
Kwa siku anauza kuku wasiopungua 10 katika mgahawa wake, wakati mchele anapika kilo nane hadi 10 kulingana na biashara kwa siku inavyochanganya na watu wanavyokwenda kupata chakula.
Mjasiriamali huyo anasema kwamba mgahawa wake unatumia unga wa sembe kilo 25 kwa siku tatu, huku unga wa ngano kiloba cha kilo 25 ukitumika kwa siku mbili tu, huku mafuta ya kula dumu moja la lita 18 likitumika kwa siku moja.
Kutokana na biashara hiyo kwenda vizuri, wakati mwingine hukutana na vikwazo vya hapa na pale, vikiwapo vya kuondoshwa katika nyumba anazofanyia biashara yake kwasababu zisizoeleweka.
Hata hivyo, wateja wake wengi wamekuwa wakimuelewa na kumfuata popote anapokuwa, jambo linalompa mwangaza kuwa biashara yake imeshajijenga yenyewe na watu wanapenda huduma yake kila siku ya Mungu.
Awali biashara yake alikuwa akiifanya Old Korogwe, lakini aliamua kuondoka baada ya kuona mwingiliano wa watu wengi ulikuwa ukihamia katika mji wa Manundu, hivyo kufuata mazingira.
Baaada ya kufika Manundu, wapo waliokuwa wakitoka Old Korogwe kwenda kupata chakula Manundu, hivyo kuona kuwa biashara anayofanya ni muhimu na anapaswa kuwa makini kwenye utendaji wake wa kazi.
Licha ya kufanya biashara hiyo kwa muda mrefu na kuelewa mazingira yote ya biashara, lakini mjasiriamali huyo anasema kwamba hafahamu lolote juu ya mambo ya kukopa, akiogopa kufilisiwa mali zake kutoka kwa wakopeshaji hao.
Anasema woga huo ameupata kwa kuwa na udhoefu wa watu wengine kusumbuliwa na kulazimika kukimbia maeneo yao kwasababu ya kukwepa madeni yao, hivyo jambo hilo linamfanya aone hana sababu ya kujenga tabia ya kukopa bila mpango.
“Huwa naogopa sana kukopa kwakujua naweza kuiacha familia yangu kwenye tabu, huku mama yao nikikimbia kwasababu ya kukwepa madeni, ukizingatia kwamba najua kuwa aina hiyo ya maisha ni ngumu na lazima nikubali hali yangu.
 “Sitaki kukopa bila sababu za msingi, maana mpaka sasa naweza kufanya biashara mwenyewe bila tatizo lolote, hivyo ili nikope napaswa kufanya biashara kubwa zaidi na lakini sio nifanye ili mradi kuna hela zipo zinahitaji wakopaji,” alisema Mama Kipande.
Aidha Mama Kipande anasema kwamba kingine kinachomfanya ashindwe kukopa ni kutokana na masharti magumu yanayowekwa kwa ajili ya kuwakopesha watu, hasa ardhi, nyumba na vitu vingine vya thamani.
Suala hili linasababisha akina mama wengi washindwe kuitumia vyema fursa ya mikopo maana hawana vitu vya thamani, jambo linalowafanya walowee kwenye dimbwi la ufukara, ingawa njia za kuwakomboa zipo.
Anasema serikali kwa kushirikiana na taasisi na benki za biashara zinatakiwa kuweka sera nzuri ya kuwakopesha watu kwa vikundi bila kuwapa masharti magumu ili kuwainua akina mama ambao mara nyingi ndio walinzi wa familia.
“Akina mama wakiendelea familia kwa pamoja imeendelea, maana mama hawezi kumuacha mtoto wake anatembea bila nguo wakati ana senti yake ndani, lakini baba hilo anaweza kuliona na akalifumbia macho.
“Katika hili ipo haja sasa ya kuangalia upya mwendo wetu kwa ajili ya kujenga uchumi imara kwa watu wote, wakiwamo akina mama,” alisema.
Mama Kipande pia anaitaka serikali kuangalia kwa kina upandaji wa gharama za maisha kwa kuhakikisha kuwa bei za vyakula hazipandi bila sababu ya msingi ili wao wasiwakandamize zaidi wateja wao.
Kuhusu usafi na mgambo wa jiji; mama Kipande anasema kwamba katika mgahawa wake suala la usafi ni jambo la muhimu, hasa kwa kuhakikisha kuwa wateja wake wananawa kwa sabuni na maji ya moto kabla na baada ya kula.
Hali hii inawafanya watu wengi kuingia katika mgahawa wake kwa kuona kuwa wanazingatia chakula kizuri na usafi katika eneo lote.
Kuhusu mgambo wa jiji, mama Kipande anasema usumbufu upo endapo biashara inafanywa bila kufuata sheria au wale wasioangalia suala zima la usafi wa mazingira na kwenye maeneo yao ya kazi.
Kwa sababu hiyo, kuna kila sababu ya serikali kutoa elimu zaidi kwa wajasiriliamali ili kuwafanya wamudu na kuitaka fursa ya ukopaji ili wapanuwe biashara zao kwa kupitia wataalamu wa fedha na biashara katika kila wilaya.

Mtanzania Leslie Liunda aula CUF







Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemteua ofisa wake Leslie Liunda wa Tanzania, kwenda Ethiopia kukagua viwanja na hoteli ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa utaratibu wa utoaji leseni kwa klabu zitakazoziwezesha kushiriki michuano inayoandaliwa na Shirikisho hilo.

Akizungumza leo na Handeni Kwetu, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Boniface Wambura, alisema ofisa huyo atawasili nchini Ethiopia kesho (Januari 2 mwaka huu).

Kazi hiyo anatarajiwa kukamilisha Januari 6 mwaka huu na baadaye kupeleka ripoti yake CAF.

Utekelezaji wa kazi yake hiyo nchini Ethiopia utahusisha wadau mbalimbali ikiwemo Shirikisho la Mpira wa Miguu la Ethiopia (EFF), Wizara ya Michezo ya nchi hiyo, viongozi wa klabu na mameneja wa viwanja husika.


LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...