Wastara aliyefunikwa uso akilia kwa uchungu
Na Kambi
Mbwana, Dar es Salaam
MUUNGANO
wa wasanii wa filamu Tanzania, unaojulikana kama Bongo Movie, umeuteka msiba wa
msanii Juma Kilowoko, maarufu kama Sajuki kwa kuiomba familia ya marehemu ili
wauzike mwili wa msanii mwenzao Ijumaa saa tano asubuhi, katika makaburi ya
Kisutu.
Alieoa nyumba moja na Sajuki, Haroub Mbeleki, kushoto, akizungumza machache na wadau wa sanaa waliofika msibani.
Ombi hilo
lilikubaliwa na baba mzazi wa marehemu, Juma Kitilu na kuagiza watu walioweka
msiba mwingine nyumbani kwao Songea, kuvunja na kupanga safari ya kuja jijini
Dar es Salaam kwa mazishi.
Katika
kikao kilichoitishwa na Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania TAFF, Simon
Mwakifwamba, kilitangaza taratibu za msiba huo ambapo pia Kamati sita ziliundwa
kwa ajili ya kuweka sawa.
Msanii mkongwe wa filamu Natasha, akiingia msibani.
Akizungumza
na Handeni Kwetu msibani hapo, Mwakifwamba alisema kamati hizo ni Kamati ya
Mazishi, Kamati ya Fedha, Kamati ya Itifaki, Kamati ya Chakula, Kamati ya
Habari, Kamati ya Usafiri na Kamati Kuu inayobeba na kusimamia kamati zote
zilizoundwa katika msiba huo.
Baba wa marehemu, Mzee Juma Kitilu, kulia akizungumza nyumbani kwa mtoto wake, marehemu Sajuki leo.
Alisema
kuwa wameshukuru baba wa marehemu kukubaliana na wazo lao la kumzika mwenzao
Dar es Salaam kutokana na umuhimu wake na hamu ya kutaka kuzikwa na mamia ya
mashabiki wake.
Marehemu Sajuki enzi za uhai wake
“Hili ni
pigo la wasanii na mashabiki wao kwa ujumla, hivyo tunachoshukuru kuwa familia
imetuelewa na wote kuwa kitu kimoja, hasa kwa kuhakikisha kuwa waliokuwa Songea
nao wanaingia hapa kuanzia au kesho,” alisema.
Wasanii wa vichekesho Tanzania, Mtanga kushoto na Kiwewe wakiingia msibani Tabata Bima leo.
Baba yake
Sajuki, mzee Kitilu alisema kuwa ameona hana sababu za kuwakatalia wasanii kwa
ombi la kushiriki kwa karibu msiba wa mwenzao, jambo lililomfanya akubali
haraka kwa ajili ya umuhimu wao.
Mtangazaji wa Clouds Tv, Zamaradi Mketema, akizungumza na wadau wa filamu katika msiba wa Sajuki nyumbani kwake Tabata Bima leo.
“Sina
sababu ya kuweka ngumu kwa wasanii wanaotaka kumzika mwenzao, hivyo wale wote
waliokuwa Songea, nimewaambia wafunge safari kwa ajili ya kuja Dar es Salaam
kumzika Sajuki Ijumaa,” alisema.
Awali,
Handeni Kwetu ilimshuhudia mke wa marehemu, Wastara akilia kwa kuomboleza msiba
wa mume wake, akisema kuwa alishatangaza kifo chake kwa wiki ya mwisho ya mwaka
2012.
“Uliniambia
nikuagie kwa wote uliowakosea katika kipindi cha maisha yako, kumbe ulishajua
unataka kuniacha peke yangu? Nitaweza mimi jamani maisha ya peke yangu Sajuki
wangu,” alisikika Wastara akilia na kushikwa na kwi kwi ya uchungu.
Kutokana
na imani ya Kiislamu, kupatikana picha ya Wastara ni kazi kubwa, maana mara
baada ya kufikwa na msiba huo, taratibu za kidini zilianza kuchukua mahali
kwake na kuhakikisha haonani na wanaume nje ya familia yake.
Sajuki
alikufa saa moja asubuhi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, ikiwa ni baada ya
kukaa hapo kwa siku kadhaa akitibiwa. Kabla ya kifo chake, Sajuki alikuwa na
maradhi ya tumbo, huku akianguka siku chache zilizopita jijini Arusha,
alipokwenda kufanya shoo.
Kuanzia
saa mbili za asubuhi, mamia ya watu na wasanii yalikuwa yakizidi kuingia
nyumbani kwa marehemu, Tabata Bima kwa ajili ya kushiriki msiba wa Sajuki,
uliohuzunisha watu wengi.
No comments:
Post a Comment