https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Saturday, December 29, 2012

UTAJIRI WA GESI ASILIA: TUWASIKILIZE WATANZANIA WA MTWARA NA LINDI. TUSIWAPUUZE


Mwandishi wa makala haya, Zitto Kabwe

Na Zitto Kabwe, Dar es Salaam
Maandamano ya amani yaliyofanyika mjini Mtwara siku ya alhamis wiki hii yameibua hoja mbali mbali kutoka kwa viongozi, wananchi, vyombo vya habari na mjadala wa siku nzima kwenye mitandao ya kijamii hasa facebook, twitter na JamiiForums. 

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ameita waandamanaji wapuuzi na Waziri wa Nishati na Madini amewaita watu hatari na wahaini. CHADEMA tumetoa kauli kupitia kwa Waziri Kivuli wa Nishati na Madini kwamba udhaifu wa utendaji serikalini ndio chanzo cha maandamano haya.

Lakini kuna tatizo kubwa zaidi ambalo linaonekana siyo katika sekta hii tu bali pia katika sekta nyingine ambapo tunaona matokeo yake katika maisha ya watu wetu na naweza kusema ni dalili za kushindikana kwa sera za CCM. Sera hizi ndizo ambazo zimelifikisha taifa hili hadi hapa.

Kama hadi wananchi wa Mtwara ambako kwa muda mrefu imekuwa ni ngombe ya CCM wanaanza kuhoji matokeo ya sera za chama tawala basi ni dalili kuwa Watanzania wamefungua macho yao na wanaona.

Wanaona katika nishati, wanaona katika utawala bora, wanaona katia elimu (kuanzia ya msingi hadi ya juu kabisa!), wanaona katika afya, wanaona katika utendaji wa jeshi la polisi wanaona katika madini. Sera za CCM zimeshindwa. Zimeshindwa kuinua maisha yao na zinaonekana kuendelea kushindwa. Mtwara na Lindi wanataka nini?

Watu wa Mtwara wanataka gesi isiondoke Mtwara na badala yake viwanda na mitambo ijengwe Mtwara kisha kama ni umeme au mbolea isafirishwe kupelekwa sehemu nyingine ya nchi.

Watu wa Mtwara hawasemi kwamba Gesi yote na mazao yake vibaki Mtwara na Lindi. Wanasema umeme uzalishwe Mtwara usambazwe nchi nzima. Mbolea izalishwe Mtwara na kusambazwa nchi nzima.
Wanataka Bandari ya Mtwara iboreshwe na kuhudumia mikoa ya Kusini. Watu wa Mtwara hawasemi kwamba mapato yote ya Gesi yatumike Mtwara tu la hasha.

Sio dhambi hata kidogo kwa watu wa Mtwara kudai masuala haya. Watu wa Mtwara wamefanya maandamano kwa amani kabisa bila kuharibu mali na kutoa maoni yao.

Kwanini tuwasute na kuwasusubika kwa madai yao haya? Kwa nini tusiwasikilize? Kosa lao nini kudai viwanda ili wapate ajira?
Tumesahau kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara ni mikoa masikini kabisa nchini? 

Tumesahau kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara ilitumika kwa ukombozi wa kusini mwa Afrika kiasi cha kuwa katika hatari kabisa?

Tumesahau ‘sacrifice’ ya watu wa Mtwara na Lindi dhidi ya usalama wa nchi yetu? Tumesahau kuwa Korosho imekuwa zao kubwa la biashara na linaloingiza mapato mengi sana ya Fedha za kigeni?

Waziri Muhongo anasema Mtwara warudishe Fedha za Mkonge na Kahawa. Mbona hataji fedha za Korosho? Mwaka 2011 Korosho ilikuwa zao la pili kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni baada ya Tumbaku.

Lakini tujiulize, watu wa Mtwara na Lindi walifadi fedha za Mkonge? Walifaidi fedha za Kahawa? Wamefaidi fedha zao za Korosho? Tumesahau hata Reli iliyoachwa na Mkoloni ya Nachingwea – Mtwara iling’olewa na Serikali huru ya Tanzania?

Tujiulize zaidi, hivi watu wa Nzega wamefaidika vipi na Mgodi wa Resolute pale Lusu? Mgodi umefungwa ukiwa umezalisha na kuuaza dhahabu ya thamani ya dola za marekani 3.3 bilioni.

Hivi katika uhai wa mgodi huu Serikali Kuu imekusanya kodi kiasi gani? Halmashauri ya Wilaya ya Nzega imepata ushuru kiasi gani? Watu wa Mtwara wanayaona haya yaliyotokea Nzega na yanayotokea Tarime, Biharamulo, Kahama na Geita.

Watu wa Mtwara wana Haki kuandamana kuzuia haya yaliyotokea wenzao yasiwatokee wao kwenye Gesi asilia. Mtwara na Lindi wanakosea wapi?
Madai yao halali na mimi binafsi na chama changu tunayaunga mkono. Lakini kuna mahala lazima waelimishwe.

Watu wa Mtwara pia wanapaswa kuelewa kuwa juhudi zao zisiwatenganishe na Watanzania wengine kwani bado utajiri wa Taifa unafadisha kikundi cha Watanzania wachache sana.

Watu wa Mtwara wanahitaji kuungana na watu wa Mara, watu wa Mwanza, watu wa Shinyanga na watu wa Kagera kudai utajiri wa nchi utumike kwa maendeleo ya watu badala ya kunufaisha kundi dogo la watu.

Watu wa Mtwara wanapaswa kuunganisha nguvu na Watanzania wengine kuzuia uporaji wa rasilimali ya nchi dhidi ya kizazi kijacho. Watu wa Mtwara wasijitenge wakawa peke yao na Gesi yao. Nguvu ya mnyonge ni umoja. Serikali isiyosikia

Serikali ina hoja kuhusu kujenga Bomba la Gesi kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa gharama nafuu. Umeme unaotumiwa na asilimia 14 tu ya Watanzania.

Kwa kuwa hii asilimia 14 ndio wenye sauti basi watu wa Mtwara wataonekana hawana hoja kabisa. Lakini Serikali imejiuliza mara mbilimbili kuhusu mradi huu wa Bomba?

Tunaambiwa na Wataalamu kwamba kuna uwezekano mkubwa mwakani gesi asilia ya kiasi cha futi za ujazo trillioni 20 itakuwa imegunduliwa katika Kitalu namba 7 ( block 7) ambacho kipo mkoani Dar es Salaam katika Wilaya ya Temeke.

Iwapo gesi nyingi hivi itakuwa hapa Dar karibu kabisa na mitambo ya kuzalisha umeme, mradi huu wa Bomba unaojengwa kwa trillioni za shilingi utakuwa na maana tena? Huu mkopo utakuwa na tija?

Serikali imewaambia watu wa Mtwara gharama za kuleta bomba Dar dhidi ya gharama za kujenga mtambo wa kuzalisha umeme Mtwara na kuusafirisha umeme kwenda maeneo mengine ya Tanzania?

Serikali imeangalia faida ya kujenga gridi nyingine badala ya kuwa na gridi moja tu yenye kushikwa na bwawa la Mtera?

Leo bwawa la Mtera lisipozalisha hata megawati moja hata Dar es Salaam izalishe megawati alfu kumi umeme hautakuwapo maana uti wa mgongo wa gridi ni Mtera! Kwa nini tusiwe na gridi nyingine yenye uti wa mgongo Lindi au Mtwara?

Tuwasikilize watu wa Mtwara. Watanzania sio mabwege tena. Kuwaita watu wa Mtwara ni wahaini, wapuuzi au watu hatari haisaidii kujenga Taifa moja lenye watu huru. Serikali na wadau wote wa sekta ya Gesi likiwemo Bunge washirikiane na watu wa Mtwara kuhusu miradi ya gesi asilia.

Tuwe na Azimio la Mtwara, tamko la kuelekeza namna bora ya kutumia utajiri wetu wa Gesi bila kuathiri umoja wa Taifa letu.
Ujio wa Sera, Maono na Uongozi Mbadala

Sasa hivi wananchi wa Mtwara kama wananchi wa sehemu nyingine wanahitaji maono mbadala, uongozi mbadala, sera mbadala na mwelekeo mbadala wa kitaifa ambao utaangalia mahitaji yao, utazingatia raslimali zilizopo na utaunganisha utendaji wa sekta mbalimbali katika kutengeneza mfumo wa kiutawala na kiuchumi ambao utaliinua taifa zima.

Ni kwa sababu hiyo naamini chama changu ni jibu sahihi kwa matamanio na kiu ya wananchi wa Mtwara na sehemu nyingine nchini. Ikumbukwe kuwa katika Ilani yetu ya Uchaguzi ya 2010 tulielewa haja ya kuangalia mikoa hii ya Kusini kwa namna ya pekee na kuipa mwelekeo wa kipekee katika sera. 

Bado tuna makusudio hayo tunapoelekea 2015 na tukishika Dola wananchi wa Mtwara na sehemu nyingine zote zilizoachwa pembezoni mwa mafanikio wajue kuwa wamepata rafiki na mshirika wa karibu wa kushirikiana nao kuleta maendeleo.

Siyo katika suala la gesi tu bali katika nishati, maji, elimu, miundombinu, kilimo, ufugaji, uvuvi, utalii. Mtwara kama ilivyo mikoa mingine ina raslimali za kutosha kuweza kuwainua wananchi wake kimaisha, na zaidi ya yote kutoa mchango mkubwa wa kiuchumi. 

Hili ambalo ni kweli kwa Mtwara ni kweli kwa mikoa mingine kama Kigoma, Manyara, Katavi, Lindi n.k.

NB: ZITTO KABWE ni mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia Chadema.

Polisi-Mkutano wa Simba kesho marufuku



Kamanda wa Polisi Kinondoni, Charles Kenyela, akitangaza kuuzuia mkutano wa Simba uliopangwa kufanyika kesho, Travertine Hoteli, Magomeni.

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
JESHI la Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni kwa kupitia Kamanda wake Charles Kenyela, limepiga marufuku mkutano wa Simba uliopangwa kufanyika kesho, Travertine Hoteli, Magomeni, jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage

Mkutano huo uliitishwa na wanachama wapatao 698 kwa ajili ya kujadili mambo yanayoihusu timu yao, ikiwa chini ya Mwenyekiti wao, Ismail Aden Rage.

Akizungumza muda mfupi uliopita, Makao Makuu ya Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamanda Kenyela alisema mkutano huo wa Simba sio halali kwakuwa haujaandaliwa kwa kufuata taratibu za kisheria.

Alisema wamepokea barua kutoka Makao Makuu ya Simba, na kusainiwa na Katibu Mkuu wao, Evodius Mutalawa wakiomba polisi wauzuie mkutano huo kwakuwa una lengo la kuleta vurugu na kuichanganya klabu yao.

“Huu mkutano sio halali maana hata jeshi la polisi halijapokea barua rasmi zaidi ya nakala inayoelezea kufika kwetu.

“Jeshi la polisi haliwezi kufanya kazi kwa nakala, hivyo naomba wote wajuwe kuwa hatuwezi kuruhusu mkutano huo na tunaomba Travertine wapinge wanachama hao kukutana kwenye hoteli yao,” alisema Kenyela.

Kuzuiwa kwa mkutano huo huenda ikawa karata nzuri kwa viongozi wa Simba waliowahi kutamka kuwa walioitisha mkutano huo ni wahuni, hivyo hawawezi kufanikiwa kuitisha mkutano huo.

Kwa wiki kadhaa sasa, wanachama hao wa Simba waliwakuwa wakihaha kuitisha mkutano wao na kupanga ufanyike kesho asubuhi katika hoteli hiyo ya Travertine, Magomeni, kabla ya jeshi la polisi kutangaza kuipiga marufuku.

Arusha wapeta medani ya masumbwi



Meya wa Arusha, Gaudence Lyimo
Na Mwandishi Wetu, Arusha
JIJI la Arusha linazidi kubarikiwa baada ya kuteuliwa kuwa Makao Makuu ya Chama cha Ngumi za Kulipwa Cha Afrika ya Mashariki na Kati (ECAPBA), huku muombaji mkuu wa jambo hilo akiwa ni Mstahiki Meya wa Arusha, Gaudence Lyimo, akiwa na lengo la chama hicho kuwa karibu na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC).
o
Rais wa ECAPBA, Onesmo Ngowi
Akizungumzia suala hilo, Rais wa ECAPBA Onesmo Ngowi, alimhakikishia meya kuwa ECAPBA itahamishia makao yake makuu katika jiji la Arusha, ikitoka katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi.
Alisema kuwa Juhudi za Lyimo za kukuza michezo na kukuza utalii katika jiji la Arusha ni moja ya sababu zilizomfanya rais wa ECAPBA kuamua kuhamishia ofisi hizo katika jiji la Arusha.
“Uamuzi huo uliungwa mkono na mmoja wa wanachama wa  ECAPBA bw. Daudi Chikwanje ambaye ndiye Katibu Mkuu wa Chama Cha Ngumi za Kulipwa Cha Malawi.
“Nchi ya Malawi ni mwanachama wa ECAPBA pamoja na Kenya, Zambia, Ethiopia, Burundi, Sudan ya Kusini, DRC, Rwanda, Uganda na Sudan,” alisema.
ECAPBA inaratibu ubingwa unaojulikana kama ECAPBF ambao unawapa mabondia wa ukanda huu kuwa mabingwa imara wa ngumi Afrika.

Linah sasa atamani kurudi shule



Mwanadada Lina Sanga, aakionyesha pozi alipokuwa nchini Marekani kwenyee shughuli zake za muziki.

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MWIMBAJI wa muziki wa kizazi kipya maarufu kama Bongo Fleva, Linah Sanga, amesema shule ni jambo jema hivyo kuna haja ya wasanii kujikita zaidi humo.

Kauli ya Linah inakuja wakati wasanii wengi kuona hakuna haja ya kuendelea na masomo zaidi ya kujikita zaidi katika sanaa kwa kuangalia mafanikio yao.

Akizungumza na Handeni Kwetu mwishoni mwa wiki iliyopita, Linah alisema uzuri wa shule ni pale muziki utakapotupa mkono, hivyo kuweza kuajiriwa popote.

Alisema kinyume cha hapo, mtu ambaye aliwekeza zaidi kwenye muziki, endapo sanaa itamtupa mkono, maisha yake yanaweza kuwa magumu zaidi na kuchanganyikiwa.

“Shule ni nzuri zaidi, natamani hata leo kuendelea kusoma huku nafanya sanaa yangu nikiwa na malengo ya leo na kesho, hasa muziki utakapokuwa tofauti.

“Hivyo wasanii twendeni shule na sio kuangalia zaidi muziki, hasa wale vijana wanaoangalia mafanikio ya watu waliotangulia na kukimbia shule,” alisema Linah.

Linah ni miongoni mwa wasanii wa kike wenye mafanikio makubwa katika tasnia hiyo huku, huku nyimbo zilizomuweka juu zikiwa ni Atatamani, Lonely na nyinginezo, wakati huo yupo chini ya taasisi ya kulea na kukuza vipaji ya Tanzania House of Talents (THT).

Watanzania waaswa kupenda bidhaa za nyumbani



Mkurugenzi wa Grace Products, Elizabeth Kilili

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MJASIRIAMALI na Mkurugenzi wa Kampuni ya Grace Products Ltd, Elizabeth Kilili, amewataka Watanzania kupenda bidhaa za nyumbani ili kuziletea tija na hatimae zivuke mipaka.

Akizungumza na Handeni Kwetu jijini Dar ess Salaam leo asubuhi, Elizabeth alisema kwamba bila Watanzania wenyewe kupenda bidhaa za Kitanzania, haziwezi kufanikiwa.

Alisema biashara nyingi zinahitaji fedha, hivyo kama wapo walioamua kuwekeza humo na wateja wenyewe wakiangalia bidhaa za nje, wajasiriamali wa ndani hawawezi kuendelea.

"Tunaomba Watanzania wapende bidhaa zetu kama vile sabuni, mafuta, shampoo na nyingine zinazoandaliwa ndani yaa nchi na sio waangalie vitu kutoka nje ya nchi, ambavyo nyingine si nzuri.

"Tukifanya hivyo tutaweza kufanya vizuri katika soko la ndani na kuweka nguvu kuuza na nje ya nchi, ukizingatia kwamba fedha zinazoingia kwenye mzunguuko zinarudi kutokana na biashara kuungwa mkono,” alisema.

Mwanamama huyo ameingiza madukani bidhaa nne, ikiwamo sabuni ya kuogea ya Grace Manjano, mafuta ya kupaka, shampoo, sabuni ya kuoshea vyombo na chooni, ambazo zote hizo zina uwezo mkubwa wa kupambana na magonjwa ya ngozi na kukuacha mwili wa binadamu kuwa na afya nzuri na mvuto wa aina yake.


Friday, December 28, 2012

Klabu 14 zatishia kugomea Ligi Kuu


Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
SHIRIKISHO la Soka nchini (TFF), limesema kuwa klabu 14 zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom zimesusia kucheza hatua ya pili ya Ligi hiyo itakayoanza Januari 26 mwakani hadi zitakaporejeshewa fedha zao zilizochukuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoka kwenye moja ya akaunti za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage

Novemba 23 mwaka huu, TRA kwa uwezo ilionao kisheria iliielekeza benki ya NMB kuilipa fedha hizo (sh. 157,407,968) kutoka kwenye moja ya akaunti za TFF ikiwa ni Kodi ya Lipa Kama Unavyopata (PAYE) kutoka kwenye mishahara ya waliokuwa makocha wa timu za Taifa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotuma kwenye vyombo vya habari na Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wamburaa, ilisema kuwa uamuzi wao huo unatokana na kujua kuwa Serikali ndiyo inayolipa mishahara ya makocha wa nje moja kwa moja kwenye akaunti zao, huku ikiacha kukata PAYE kwa mishahara hiyo na kufikia kufikia malimbikizo ya sh. 157,407,968.

TFF bado inaendelea na mazungumzo na pande husika (Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa upande mmoja na TRA kwa upande mwingine) ili fedha hizo zirejeshwe kwani zilitolewa na mdhamini wa Ligi Kuu (kampuni ya Vodacom) kwa ajili ya maandalizi ya timu hizo tayari kwa mzunguko wa pili wa Ligi hiyo.

Katika hatua nyingine, TFF imesema kuwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) litamtuma nchini ofisa wake Abbas Sendyowa kukagua viwanja na hoteli ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa utaratibu wa klabu kupata leseni zitakazoziwezesha kushiriki michuano inayoandaliwa na CAF katika ukanda wao.

Ofisa huyo kutoka Uganda atawasili nchini Januari 7 mwakani ambapo anatarajiwa kukamilisha kazi hiyo Januari 14 mwakani na baadaye kupeleka ripoti yake CAF.

Aidha, Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imekubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA) kumuondoa Nazarius Kilungeja kugombea uenyekiti katika uchaguzi wa chama hicho.

Kutokana na uamuzi huo, Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeiagiza Kamati ya Uchaguzi ya RUREFA kuendelea na mchakato wa uchaguzi huo kama ilivyopangwa awali.


27 wa Yanga kukwea pipa kwenda Uturuki



Hamis Kiiza mmoja wa wachezaji wa Yanga, watakaokwenda Uturuki.
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NYOTA 27 wanaokipiga kwenye klabu ya Yanga, wanatarajia kuondoka kesho kwenda Uturuki kwa kuweka kambi ya wiki mbili.

Yanga itaondoka saa 10:30 alfajiri kwa ndege ya shirika la ndege la Uturuki na kufika Instambul Jumatatu saa 4:30 asubuhi kabla ya kwenda katika mji wa Antarya ambapo wataweka kambi yao.

Ofisa Habari wa klabu hiyo, Baraka Kizuguto, alisema maandalizi yote kwa ajili ya safari hiyo yamekamilika na timu hiyo itafikia katika Hotel ya Sueon Beach ambayo iko katika ufukwe wa bahari.

Kizuguto alisema ikiwa nchini humo iatacheza michezo mitatu ya kirafiki ya kimataifa na timu ambazo zitatangazwa mara baada ya timu hiyo kufika nchini Uturuki.

Aliwataja wachezaji hao kuwa ni Ali Mustapha 'Bartez' Said Mohamed na Yusuf Abdul, Geofrey Taita, Juma Abdul, Shadrack Nsajigwa, Oscar Joshua, Stephano Mwasika, Kevin Yondan na Nadir Haroub 'Canavaro'.

Wengine ni Twite Kabange, Haruna Niyonzima, Frank Domayo, Nizar Khalfan, Didier Kavumbagu, Said Bahanuzi, Hamis Kiiza, George Banda, Jerry Tegete, David Luhende, Rehani Kibindu na Simon Msuva.

Aliwataja viongozi wa benchi la ufundi kuwa ni Kocha Mkuu Ernest Brandts, kocha msaidizi Fred Minziro, kocha wa makipa Razack Siwa, daktari Sufian Juma, Ofisa Utawala Hafidh Salehe, Ofisa Habari Baraka Kizuguto na Mohamed Nyenye Mjumbe wa Kamati ya Utendaji.

Yanga imetumia zaidi ya sh. milioni 50 kwa ajili ya kugharamai kambi ya timu hiyo.

Simba wampigia magoti Kikwete



Ali Mselemu akionyesha msisitizo
 
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WANACHAMA wapatao 698 wa klabu ya Simba, wamemuandikia barua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, wakitaka awasaidie ili wafanye mkutano wao kwa haki, Desemba 30, katika Hoteli ya Travertine, kama walivyopanga.

Hatua hiyo imetokana na kutumia nafasi hiyo kumshtaki mwenyekiti wao, Ismail Aden Rage ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Mjini ili rais aone jinsi Rage anavyoichezea Katiba ya Simba.
Baadhi ya wanachama wa Simba, wakimsikiliza mzee wa zamani wa Simba, Ali Mselemu, mwenye kanzu na kofia kichwani, katika kujadili mkutano wao wa Desemba 30, Travertine Hoteli Magomeni.
                   
Akizungumza muda mchache uliopita na Handeni Kwetu, Travertine Hoteli, mmoja wa wanachama hao, Chuma Seleman, akiwa sambamba na wanachama wengine wa klabu hiyo, alisema wamefikisha barua yao Ikulu, ili kuonyesha mapenzi yao kwa Rais ambaye pia ni mwajiri wa Rage, katika nafasi yake ya Ubunge.

Alisema Rage ni Mbunge na pia ni Mwanachama wa Chama cha Mapinduzi CCM, hivyo kwa kukanyaga Katiba ya Simba, ina maana zote zilizosalia hawezi kuziheshimu.

Tumedhamiria kufanya mkutano wetu siku ile ile ya Desemba 30 kuanzia asubuhi hapa Travertine Hoteli, lakini pia tumwomba Rais ajuwe ubabaishaji huu wa Rage katika klabu yetu.

Mbali na Rais, pia tumewasilisha nakala sehemu mbalimbali, ikiwamo kwa Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo kwa ajili ya kuliweka sawa hili, ikiwamo kuachwa tufanye mkutano wetu kwa haki kama inavyosema Ibara ya 22 kifungu cha pili ya Katiba ya Simba inayosema siku 30 zikiombwa na wanachama wasiopungua 500 ambao kwa wao wamefikia 698 wana haki ya kuitisha mkutano wa dharura.

Hata hivyo, wanachama hao wamekuwa wakikutana na matatizo mengi, yakiwamo ya kuitwa wahuni huku wengine wakijitokeza wakisema kuwa mkutano huo haupo, jambo ambalo wahusika wanasema mkutano wao upo pale pale na wanachama wenye mapenzi na klabu yao waende kujadili mamabo ya kuisaidia klabu yao ya Simba.

Subiri kidogo nipo kwenye kikao na waandishi



Mwandishi wa habari wa Capital Radio ya jijini Dar es Salaam, Mastar Tindwa, akiandaa kifaa chake cha kazi mbele ya Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako kulia na Msemaji wa klabu hiyo, Baraka Kiziguto, kama walivyokutwa na kamera ya Handeni Kwetu Makao Makuu ya klabu hiyo muda mfupi uliopita.


Yanga walizungumzia safari yao ya Uturuki waliyopanga kuondoka alfajiri ya Desemba 30 na kukaa huko kwa wiki mbili. Picha na Kambi Mbwana.

ADC wavuna wanachama 2700 Handeni



Na Mwandishi Wetu, Tanga.
JUMLA ya wanachama wasiopungua 2700 wamefanikiwa kujiunga na Chama kipya cha Alliance Democratic Change (ADC) wilayani Handeni, mkoani Tanga.

Wanachama hao wamepatikana baada ya kufanya ziara ya kuzungumza na wananchi, kufungua matawi ya chama hicho na kusikiliza kero zao na jinsi ya kuzipatia ufumbuzi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Tanga, Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, Said Miraji, alisema ziara yao walifanya kwa kushtukiza na kugundua kuwa wilaya hiyo ina kero za maji, afya na elimu.

Alishangazwa kuona wananchi wa kata mbalimbali wilayani humo wakikabiliwa na tatizo la maji ingawa wana vyanzo vitano vya maji ambavyo ni Kitumbi, Bongi, Segera Michungwani, Msilwa na Chogo.

Alisema licha ya wananchi wengi kushindwa kutapa huduma ya maji katika maeneo yao lakini Mbunge wa Jimbo hilo, Abdallah Kigoda ambaye pia ni Waziri wa Viwanda na Biashara anafanya ziara ya kutembelea Jimbo hilo huduma ya maji inapatikana lakini anapomaliza ziara yaka huduma hiyo inatoweka.

“Hii hali ya upatikanaji wa maji kwa kipindi cha ziara ya Mh Mbunge wetu inatushangaza sana sasa tunajiuliza hao watu ambao wanaleta maji wanapomuaona mbunge wanatoa wapi," alihoji.
 
Aliongeza kuwa kuanza kwa elimu ya msingi kwa kigezo cha kupitia elimu ya awali sio agizo rasmi la kitaifa kwa sababu sio wazazi wote wenye uwezo wa kuwalipia karo watoto wao katika elimu hiyo ya awali .

Hata hivyo alisema katika suala la afya alieleza lipo tatizo la kutokupewa msamaha wa kupatiwa matibabu bure wazee,wazazi na watoto wadogo kama serikali ilivyoagiza kitu ambacho kinapeleka kuleta usumbufu kwa jamii husika kwa ujumla.

Alisema katika ziara yao fupi wilayani Handeni walifanikiwa kufungua matawi yapatayo 24 katika kata za Kabuku, Kwamkonga, Handeni Mjini, Mkata, Ndolwa na Misima.

Aidha alieleza kuwa wanatarajiwa kufanya ziara rasmi kwa uzinduzi wa matawi hayo mikutano ya hadhara katika wilaya za Mkinga, Handeni na Tanga mjini lengo ni kukiimrisha chama hicho ili kuweza kuchukua dola siku zijazo.

Tampro yapania kuzinusuru shule za Kata



Mussa Mzia, mwenyekiti wa TAMPRO, akifanya mahojiano na waandishi wa habari.
 
Na Rashid Mtagaluka, Dar es Salaam
JUMUIYA ya wanataaluma wa Kiislamu nchini TAMPRO
imesema kwa kushirikiana na taasisi nyingine, inaandaa mpango mkakati wa kuhakikisha inawasaidia vijana wanaosoma katika shule za sekondari za Kata ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao ya mwisho kama sehemu ya jitihada zao kwa jamii ya Watanzania.

Akisoma maazimio ya mkutano mkuu wa jumuiya hiyo uliomalizika juzi katika hotel ya Lamada jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Tampro Sadik Gogo alisema wamefikia uamuzi huo baada ya kuridhika na utafiti ilioufanya na kubaini kuna haja ya wao kama wanataaluma kutafuta njia ya kuwasaidia vijana hao kimasomo.

”Tampro kupitia kliniki yake ya Elimu, iliomba na kupata kibali Wizarani cha kufanya utafiti katika shule kadhaa za sekondari za kata hapa nchini na kugundua kuwa zina uwezo wa kufanya vizuri iwapo zitasaidiwa katika baadhi ya njanja” alisema Gogo.

Akifafanua baadhi ya nyanja hizo, Mkurugenzi huyo alisema ni pamoja na kuwapa mafunzo maalum walimu wa shule hizo na baadae kupeleka walimu wa kujitolea katika baadhi ya shule zitakazoonekana zina upungufu mkubwa.

Sambamba na mkakati huo ambao amedai unalenga kuisaidia serikali, Gogoi alisema Tampro kupitia mkutano huo imeazimia kuanzisha vituo vya Elimu maalum pamoja na huduma nyinginezo kwa watu wenye mahitaji maalum kama vile ya ulemavu.

Aidha Mkutano mkuu huo umeazimia kushirikiana na wadau wengine nchini kuwekeza katika sekta ya Afya kwa madai kuwa bila ya kuwa na watu wenye afya zilizoimarika ,ni ngumu Taifa kufikia maendeleo ya kisiasa na kiuchumi.

TAMPRO ni Jumuiya isiyo ya kiserikali iliyoanzishwa mwaka 1994 na kusajiliwa rasmi serikalini Agosti 22, 1997 ikiwa na malengo mengi na mojawapo ni kufanya tafiti, kutoa mafunzo na ushauri wa kitaalam katika maeneo mbalimbali ya maendeleo ya jamii.


Thursday, December 27, 2012

Mr Nice aliyewika na kutoweka Tanzania



Huyu ni Mr Nice, mkali aliyetokelezea sana kabla ya kutoweka katika 'game'
 
ALITOKELEZEA

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MWIMBAJI na mfalme wa muziki wa Takeu aliyousisi kwa Tanzania, Nice Lucas Mkenda maarufu kama Mr Nice ni miongoni mwa wasanii waliowahi kuvuma mno miaka ya nyuma. Kila mmoja alikuwa akipenda kumuona nyota huyo.

Nyimbo alizowahi kutoa msanii huyo ni pamoja na Mama, Kikulacho, Rafiki, Fagilia na nyinginezo ambazo hakika watu walizipenda na kuziheshimu.


Sio Tanzania tu, bali nchi nyingi za Afrika Mashariki na Kati, Nice alipendwa na kukubalika mno.

Nakumbuka, Nice ilibaki kidogo aonekane kama Rais, kwani nchini Msumbiji, visiwa vya Comoro, Uganda, Kenya, Rwanda jina lake lilivuma na wadau wengi walisema kumbi za kufanya shoo jamaa huyo zilikuwa chache, huku viwanja vya wazi ndio ilikuwa mahali pake.

Huyu Mr Nice alivuma balaa
 
Watoto mtaani walikuwa wakicheza au kunyoa kama Mr Nice, hasa ile style yake ya kunyoa unga unga na kupaka rangi nyeusi na kutelezesha mstari sehemu ya sikio na kuonekana nadhifu.

Kuvuka kwake kulizidi hasa alipokuwa akiingia kwenye ugomvi na kupigwa mara kwa mara na nyota mwenzake, Godfrey Tumaini, maarufu kama Dudu Baya, a.k.a Zeze Dudu.

Wengi walimlilia sana waliposikia anaonewa ovyo na Dudu Baya. Pamoja na sifa zote hizo, heshima yote hiyo, lakini hali ni mbaya. Jamaa huyo hasikiki tena jukwaani.

Imefikia wakati mwaka unakwisha bila kuonekana jukwaani. Katikati ya mwaka huu alionekana kwenye shoo ya Fiesta ya mjini Moshi, watu wakasema jamaa anataka kurudi tena?

Kwanini? Uwezo wake umeisha? Anaishi vipi? Wadau wa burudani tunakutana naye katika baadhi ya kumbi za starehe akipata moja moto moja baridi, hasa kwa wale wanaoendelea kumheshimu kumpa ofa.

Sasa basi, kama wewe ni swahiba wake, ndugu yake, Handeni Kwetu inataka kujua sanaa yake imeishaje? Mwambie kuwa tumemkumbuka sana. Mwambie aone nyota wapya wanavyovuna fedha kupita kiasi.

Hivi unajua kuwa kama leo hii Mr Nice angekuwa Diamond, Ommy Dimpozi sijui angeitwa nani. Majina yote yangekuwa yake, hasa yale Fremason kama wanavyozushiwa wengine.

Nakusalimia bwana Mr Nice kama kweli uwezo unao tukutane jukwaani kwa nyimbo nzuri na zitakazorudisha heshima yako, vinginevyo tutaendelea kusema kuliwahi kuwa na Mr Nice.

0712 053949
0753 806087

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...