https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Saturday, October 26, 2013

Tamasha la Utamaduni Handeni na mipango kabambe ya kimaendeleo




Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
ILI kujenga jamii bora na yenye kujua tamaduni zao, kunahitajika kuandaliwa matamasha muhimu yenye dhamira ya kweli katika kona mbalimbali za nchi yetu. Huo ni mpango mzuri na wenye tija.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu, pichani.
Katika suala hilo, wale wadau wanaotarajia au waliowahi kuandaa matamasha ya aina hiyo ni dhahiri wanatakiwa waungwe mkono badala ya kukatishwa tamaa.


Kwa sasa, tamasha ambalo linatajwa katika vinywa vya watu wengi ni lile la Handeni, linalotarajiwa kufanyika Desemba 14, wilayani Handeni mkoani Tanga.


Tamasha hilo la utamaduni na michezo linatambulika kwa jina la ‘Handeni Kwetu,’ jina lililotokana na mtandao ‘blog’ ya Handeni Kwetu.
Mratibu wa Tamasha la Handeni, Kambi Mbwana, pichani.
Vyovyote litakavyotajwa na wadau wa matamasha duniani kote, ili mradi linatimiza na kutoa majibu halisi ya namna ya kutangaza na kukuza utamaduni wa Tanzania, si vibaya na njia ya kulitangaza mbele ya jamii.


Katika mazungumzo yaliyofanyika mapema wiki hii, mwishoni mwa wiki iliyopita, Mratibu Mkuu wa tamasha hilo, Kambi Mbwana, anasema kuwa lengo la kuandaa tamasha hilo ni kushirikiana na serikali na wananchi wote kujua mbinu imara za kuutangaza utamaduni wetu.
Mbunge wa Handeni na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt Abdallah Kigoda, pichani.
Anasema kwa maeneo kama Handeni na kwingineko, kumekuwa na changamoto kubwa za wananchi kuacha utamaduni wao na kufuata wa wenzao jambo linalotakiwa lipingwe vikali.

“Nilikaa chini na kutafakari namna gani ya kuwaunganisha watu wote katika tukio moja na kuwa sehemu ya wao kuangalia ngoma zetu, nyimbo zetu na mbinu za kijamii kwa ujumla wake.

“Naamini katika umri wa taifa letu la Tanzania, kuna mengi yametokea na yaliwahi kutokea hasa wakati wa ukoloni, hivyo naamini siku hiyo tutajua ni kiasi gani watu wa asili ya Handeni walikuwa na mchango kwenye jamii yao,” alisema Mbwana.

Mbwana ambaye ni mwandishi wa habari na mmiliki wa ‘blog’ ya Handeni Kwetu (www.handenikwetu.blogspot), anasema kwamba kwa kukutana watu wote ni sehemu ya kuangalia namna ya kulitumikia taifa letu la Tanzania na kubuni mbinu za kujikomboa kiuchumi.

Mdau huyo wa mambo ya utamaduni, michezo na sanaa kwa ujumla wake ukiwamo muziki, anasema kwamba Handeni ni miongoni mwa wilaya zenye changamoto kubwa hivyo kuna haja ya wadau wote kukutana kwa pamoja na kuangalia namna ya kuzitatua, hasa kwa kupitia tamasha hilo.

“Huu si wakati wa kuangalia Mkuu wa Wilaya (DC) Muhingo Rweyemamu anafanya nini au Mbunge Abdallah Kigoda na viongozi wote wa serikali, ila jambo la muhimu ni kushirikiana nao kuleta maendeleo.

“Mtu wa kwanza katika maendeleo ni mwananchi mwenyewe, hivyo naomba kuwakaribisha Watanzania na hata wale wasiokuwa Watanzania kukutana pamoja na sisi kwenye tamasha hili,” alisisitiza Mbwana.

Aidha, Mbwana anatumia muda huo kuwaomba wadau wote, wakiwamo viongozi wa serikali, mashirika na kampuni kujitokeza kudhamini tamasha hilo litakalokuwa la aina yake.

Tamasha la Utamaduni la Handeni Kwetu linafanyika kwa mara ya kwanza, likipangwa kuanza saa tatu asubuhi hadi saa 12 jioni, ambapo vikundi mbalimbali vya sanaa vitashiriki.

Ili kuleta hali ya kimkoa, Mbwana anasema juhudi zinafanyika kupata vikundi katika baadhi ya wilaya za Mkoa wa Tanga ili kuimba nao, kucheza nao na kushiriki nao katika jambo la kimaendeleo.

Mdau huyo wa habari anasema kwamba hadi sasa wadau kadhaa wamejitokeza kudhamini tamasha hilo linalotikisa katika maeneo ya Handeni na Tanzania kwa ujumla.

Anawataja wadau hao kuwa ni pamoja na Yusuphed Mhandeni, ambaye ni Mchumi wa CCM Kata ya Makumbusho kwa kupitia Kampuni yake ya Yusuphed Trans, yenye magari yanayotoka Dar es Salaam kwenda Mkata, wilayani Handeni, Grace Products, Screen Masters na mtandao wao wa Saluti5.com, Dullah Tiles & Construction Ltd, Katomu Solar Specialist, Country Business Directory (CBD) na Michuzi Media Group.

Wengine ni duka la mavazi la Chichi Local Ware, Smart Mind & Arters chini ya Anesa Company Ltd, ikidhamini kwa kupitia kitabu chao cha ‘Ni Wakati Wako wa Kung’aa’, Lukaza Blog, Kajunason Blog, Jiachie Blog na Taifa Letu.com.

Mbwana anasema kwamba kwa kupitia tamasha hili, wadau wote watapata fursa ya kutangaza biashara zao, ukizingatia kuwa tamasha hili linatarajia kukutanisha watu wengi zaidi sehemu moja.

“Tunaomba udhamini kwa watu wote ili tushirikiane katika kufanikisha tamasha hili la kihistoria, huku tukiamini kuwa wenzetu wa Kilindi, Korogwe tutakuwa nao pamoja.

“Maandalizi yanaendelea kuhakikisha kuwa tunafanya kitu cha tofauti katika tamasha hilo, nikiamini kuwa mguso huu utaendelea kushika kasi na habari hizi njema kuenea nchini kote,” alisema.

Mbwana anasema kwamba wazo la kufanyika kwa tamasha hilo limepewa baraka na viongozi wote, akiwamo DC Rweyemamu na Mbunge, Abdalah Kigoda, ambaye pia ni Waziri wa Viwanda na Biashara.

Anasema kuwa kwa kufanyika kwa tamasha hili ni muendelezo wa mipango mingi mizuri ya kimaendeleo itakayoandaliwa kwa kushirikiana na Watanzania wote, hususan wananchi wa Handeni.

Mwisho kabisa Mbwana alitumia muda huo kuwakumbusha wafanyabiashara mbalimbali wilayani Handeni na Tanga kwa ujumla, kuingia moja kwa moja katika tamasha hili la aina yake.

Friday, October 25, 2013

Mkuu wa kituo cha Polisi wilaya Kilindi mkoani Tanga, Lusekelo Edward akiwa wodini baada ya kupigwa risasi

Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, Lusekelo Edward, akiwa amelazwa katika Hospitali ya Mkoa Tanga (Bombo), baada ya kupigwa risasi tatu mkononi na ubavuni na watu wasiojulikana katika kijiji cha Lulago wilayani humo juzi. Anayemhudumia ni muuguzi wa zamu wa Hospitali hiyo, Janneth Mkamba. Picha na Salim Mohammed wa Gazeti la Mwananchi.

Mapacha Watatu kusherehekea miaka minne


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
BENDI ya Mapacha Watatu, inatarajia kufanya sherehe ya kutimiza miaka minne tangu kuanzishwa kwake Ijumaa ya Novemba 15 katika Ukumbi wa Letasi lounge, zamani Business Park, jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Mapacha Watatu, Jose Mara pichani.
Onyesho hilo la kihistoria limepangwa kufanyika kwa ajili ya kuwashukuru wadau na mashabiki wao kutokana na kuwaunga mkono kwa miaka kadhaa sasa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Meneja wa bendi hiyo, Khamis Dacota, alisema kuwa mipango ya kuhakikisha kuwa bendi yao inafanya sherehe ya miaka minne inaendelea.

Alisema lengo lao ni kuwashukuru mashabiki wao kwa kuimba vibao motomoto vyenye kukonga nyoyo za wapenzi wao, hivyo ni jukumu la wadau hao kuingia kwa wingi kwenye shoo hiyo.

“Tumefanya mpango wa kufanya sherehe hii ya kutimiza miaka minne katika ukumbi wa Letesi, huku tukiamini ndio eneo murua kwa ajili ya kuwashukuru mashabiki wetu.

“Litakuwa ni onyesho la aina yake, ukizingatia kuwa Mapacha Watatu ni bendi imara yenye kila sababu ya kufanya vizuri katika tasnia ya muziki wa dansi hapa nchini,” alisema.

Mapacha Watatu ipo chini ya Khalid Chokoraa na Jose Mara, huku muasisi mwingine wa bendi hiyo Kalala Junior akiamua kurudi katika bendi yake ya zamani The African Stars, Twanga Pepeta.

Rais Kikwete alipokagua jengo la Bunge mjini Dodoma jana

 Rais Kikwete akikaribishwa kutembelea Jengo la Bunge mjini Dodoma na Naibu Spika Mhe. Job Ndugai leo Oktoba 24, 2013
Rais Kikwete akiangalia sehemu ya viti ndani ya Ukumbi wa Bunge mjini Dodoma leo Oktoba 24, 2013
 Rais Kikwete akitembelea Ukumbi wa Bunge mjini Dodoma leo Oktoba 24, 2013
Rais Kikwete akizungumza na Naibu Spika Mhe Job Ndugai na Katibu wa Bunge Dkt Thomas Kashilila baada ya kutembeleaUkumbi wa Bunge mjini Dodoma leo Oktoba 24, 2013
Rais Kikwete akisindikizwa na Naibu Spika Mhe Job Ndugai na Katibu wa Bunge Dkt Thomas Kashilila baada ya kutembelea Ukumbi wa Bunge mjini Dodoma jana Oktoba 24, 2013. PICHA NA IKULU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jana, Alhamisi, Oktoba 24, 2013 ametembelea na kukagua Jengo la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma kujionea maandalizi ya jinsi Wabunge wa Bunge Maalum la Katiba watakavyokaa katika Ukumbi wa Bunge hilo. Bunge hilo Maalum la Katiba litakuwa na Wabunge 600 tofauti ya Bunge la sasa lenye Wabunge 354 ambao ni pamoja na Wabunge 239 wa kuchaguliwa kutoka majimboni, Wabunge Wanawake Viti Maalumu 102, Wabunge wa kuteuliwa toka Baraza la Wawakilishi Zanzibar 5, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wabunge 7 (kati ya 10) wa kuteuliwa na Rais.

Thursday, October 24, 2013

Mgombea Urais TFF, Athuman Nyamlani afungua kampeni zake kwa kutaja vipaumbele tisa vya kukuza soka la Tanzania



Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MSUGUANO wa mbio za Urais katika Shirikisho la Soka nchini (TFF), umeendelea leo baada ya mgombea wa nafasi hiyo kubwa katika ngazi ya mpira wa miguu Tanzania, Athman Nyamlani kutaja vipaumbele tisa vya maendeleo ya soka, iwapo atapata ridhaa ya wapiga kura kuliongoza Shirikisho hilo.
Mgombea nafasi ya Urais wa TFF, Athuman Nyamlani, akifanya mahojiano na waandishi katika moja ya matukio ya kimichezo Tanzania.
Maneno ya Nyamlani yamekuja baada ya kujitosa katika kinyang’anyiro hicho cha Uchaguzi Mkuu wa TFF, akipambana na Jamal Malinzi.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), ikiwa sehemu ya uzinduzi wa kampeni zake za uchaguzi utakaofanyika Jumapili, Nyamlani alisema akipewa nafasi hiyo, atainua kiwango cha soka kwa kutekeleza msingi imara wa soka la Tanzania.

Nyamlani ambaye kitaaluma pia ni hakimu wa Mahakama ya Wilaya Kinondoni, alisema katika kipindi cha miaka minne ataimarisha usimamizi na Manejimenti ya soka katika ngazi zote kwa kupitia nafasi hiyo ya urais sanjari na kushirikiana na viongozi wa klabu na vyama vya soka vya wilaya na mikoa kwa ujumla wake.

Alisema ataimarisha usimamiaji na menejimenti ya soka katika ngazi zote kwa kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa viongozi na kusimamia sheria na taratibu za uendeshaji wa soka la Tanzania na suala la viongozi  kujiendeleza kielimu litapewa kipaumbele na litakuwa ni agenda endelevu.
Nyamlani alisema suala lingine ambalo litakuwa katika utekeleza wake ni rushwa katika soka nchini.

“Naomba nikiri kuwa kumekuwa na malalamiko na vitendo vya rushwa ambavyo vinawahusisha viongozi wa soka. Hivyo basi kwa kushirikiana na serikali na viongozi wa soka katika ngazi zote nitahakikisha naendeleza mapambano dhidi ya rushwa,” alisema Nyamlani.

Watanzania wanavyojifua mashindano ya Tusker Project Fame

Washiriki Tusker Project Fame msimu wa 6 kutoka Tanzania Angella Karashani(Angel)na Elisha Maghiya(Hisia)wakisikiliza musiki kwa makini wakisubiri kupata maelezo kutoka kwa viongozi wa jumba la Tusker Project Fame wakati wa mazoezi ya kujinoa na shoo ya Jumapili.
 Mmoja wa washiriki kutoka Tanzania Hisia (katikati mwenye tisheti nyeusi)akiwa pamoja na washiriki wenzake wa kiume wakifurahia mtoko baada ya kuwashinda washiriki wa kike.

Waziri Mkuu Pinda afungua Mkutano wa biashara kati ya Tanzania na China mjini Guangzhou China leo


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akifungua mkutano wa Biashara kati ya Tanzani na China kwenye Hoteli ya Dong Fang mjini Guangzhou akiwa katika ziara ya kikazi nchini China Oktoba 24,2013.
Baadhi ya washirki wa mkutano wa Biashara kati ya Tanzania na China wakimsikiliza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakati alipofungua mkutano huo kwenye Hoteli ya Dong Fang mjini Guangzhou akiwa katika ziara ya kikazi nchini China Oktoba 24,2013.
Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji nchini, Juliet Kairuki akizungumza katika mkutano wa Biashara kati ya Tanzani na China kwenye Hoteli ya Dong Fang mjini Guangzhou. Mkutano huo ulifunguliwa na Waziri Mkuu,Mizengo Pinda akiwa katika ziara ya kikazi nchini China Oktoba 24,2013.

Mdau alichambua shidano la Bongo Star Search, ahoji uhalali wake na faida kwa washiriki



Na Jonathan Tito, Dar es Salaam
KWA wadau wa muziki wa Bongo Fleva, watakuwa wameusikia vizuri wimbo mpya wa Elibariki Emanuel ‘Ney wa Mitego’ na kuutafakari kwa kina.
Madame Rita, Mkurugenzi wa Benchmark Production ambao ndio waratibu wa shindano la Bongo Star Search Tanzania.

Katika mashairi ya wimbo huo uitwao ‘Salamu Zao’, msanii huyo amezungumza mengi akitaka salamu zake zifikishwe kwa watu mbalimbali.


Ney alimtaka Diamond afikishe ujumbe wake kwa Zitto Kabwe, amwambie aachane na Bongo Fleva, aendelee na siasa, maana Kigoma Stars amewatelekeza.

Salamu nyingine ni kwa Madam Rita Paulsen, zikihusu ‘kufulia’ kwa washindi wa shindano la Bongo Star Search (BSS).

Pia Ney alizungumza na Ridhiwani akimtaka amueleze baba yake, Rais Jakaya Kikwete kwamba masela hawamuelewi na Wamakonde wa Mtwara hawataki tena korosho, bali gesi na anaweza kuwaua kwa mkong’oto.

Mwandishi wa makala haya, Jonathan Tito. Ni mtazamo wake binafsi, si msimamo wa Mtandao huu wa Handeni Kwetu Blog.
Ney alikwenda mbali na kumtafuta rafiki wa Edward Lowasa ili amfikishie salamu kuwa anamtaka agombee urais 2015, akiahidi kumpigia kampeni.

Chakushangaza anataka salamu nyingine zifikishwe hadi kwa marehemu Steven Kanumba na Albert Mangwear, kwamba atakayetangulia kufa akawambie wasanii hao kuwa wakati wa misiba yao kuna watu waliiba fedha za rambirambi.

Naamini salamu zote zitakuwa zimefikishwa kwa wahusika, hata zile za Kanumba na Ngwear, huenda ikawa Mack 2B aliyefariki mwezi uliopita, akawa ameshazifikisha.

Jukumu la kumfikishia salamu Mkurugenzi Benchmark Production, Madam Ritha, mwandaaji na mratibu wa shindano la BSS, alipewa mshindi wa mwaka jana wa shindano hilo, Walter Chilambo.

Timu ya Taifa ya wanawake Msumbiji kuwasili Oktoba 25, Uchaguzi Bodi ya Ligi kufanyika kesho

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Timu ya Taifa ya wanawake kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 inawasili nchini kesho (Ijumaa, Oktoba 25 mwaka huu) saa 8.30 mchana tayari kwa mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza ya Kombe la Dunia dhidi ya Tanzania itakayofanyika Jumamosi (Oktoba 26 mwaka huu).

Msemaji wa TFF, Boniface Wambura.
Msemaji wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Boniface Wambura, alisema kuwa Msumbiji itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa ndege ya LAM ikiwa na msafara wa watu 25 wakiwemo wachezaji, benchi la ufundi na viongozi. Timu hiyo itafikia kwenye hoteli ya Sapphire iliyopo maeneo ya Gerezani, Dar es Salaam.


Mara baada ya kuwasili JNIA, kocha na nahodha wa timu hiyo watazungumza na waandishi wa habari juu ya mechi hiyo itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.


Kwa upande wa U20 chini ya Kocha Rogasian Kaijage imejiandaa vizuri kwa ajili ya mechi hiyo, na kesho saa 10 jioni itafanya mazoezi yake ya mwisho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Viingilio kwa mechi hiyo ni sh. 1,000 kwa viti vya rangi ya kijani, bluu na rangi ya chungwa. Viingilio vingine ni sh. 2,000 kwa VIP C, sh. 5,000 kwa VIP B wakati VIP A itakuwa sh. 10,000.

Mgambo auawa na askari polisi apigwa risasi katika vurugu wilayani Kilindi mkoani Tanga

KIJIJI cha Lulago, wilayani Kilindi mkoani Tanga, kimeingia katika hofu kubwa baada ya mgambo Mbwana Salim kuuawa kutokana na kutoelewana katika moja ya majukumu yake kikazi, huku askari polisi naye akipigwa risasi ya tumbo.
Kamanda wa Polisi mkoani Tanga, Costantine Masawe, pichani. Picha na Maktaba Yetu.
Baada ya kuuliwa kwa mgambo huyo na watu wasiofahamika, askari polisi waliingia na mmoja wapo kujikuta akipigwa risasi ya tumbo katika kadhia hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa za awali katika kijiji hicho, sakata hilo lilianzia kwenye vurugu za wafanyabiashara ambao inasemekana waligoma kulipa ushuru.

Kamanda wa Polisi Mkoa Tanga, Costantine Masawe, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo wilayani Kilindi mkoani Tanga.

“Taarifa hizo zimetufikia kutokana na askari wetu kupigwa risasi wakati anajaribu kutimiza majukumu yake na taarifa zaidi tutaendelea kuzitoa juu ya tukio hilo,” alisema.

Kamanda Masawe alisema baada ya kutokea vurugu hizo na mgambo kuuliwa, askari waliingia na kufukuzana na watu wanaosadikiwa kuwa walishiriki kwenye tukio hilo, ambapo mwisho wake ulifikia kwa askari kupigwa risasi ya tumbo na sasa yupo hospitali akipatiwa matibabu.

Benki ya NMB yatoa msaada Hospitali ya wilaya Ileje

Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Janet Mbene akishukuru uongozi wa benki ya NMB kwa msaada wa mashuka na vitanda vya akina mama katika hospitali ya Itumba wilaya ya Ileje .Msaada huo wenye thamani ya shilingi milioni Tano umetolewa na benki ya NMB kupitia tawi la Ileje mwishoni mwa wiki katika viwanja vya hospitali ya Itumba.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Ileje, Nd. Mohamed Mwala akimshukuru Meneja wa Kitengo cha Huduma za Serikali wa NMB , Bw. Elieza Msuya baada ya kupokea msaada wa vitanda na mashuka ya hospitali ya wilaya ya vilivyotolewa na benki ya NMB. Anayeshuhudia makabidhiano hayo ni Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Janet Mbene 
Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Janet Mbene akimshukuru Meneja wa Kitengo cha Huduma za Serikali wa NMB , Bw. Elieza Msuya baada ya kupokea msaada wa vitanda na mashuka ya hospitali ya Itumba wilaya ya Ileje vilivyotolewa na benki ya NMB. 

Mwanamuziki Yvonne Chaka Chaka afanyiwa dinner ya nguvu jijini Washington DC

Balozi wa kudumu wa African Union Mhe. Amina Salum Ali akiwashukuru wageni waalikwa wakiwiwemo Waheshimiwa Mabalozi kutoka nchi mbalimbali kutoka bara la Afrika wanaowakilisha nchi zao nchini Marekani kwa kufika kwao kwenye chakula cha jioni Fairmont Hotel iliyopo Washington, DC walichomuandalia mwanamuziki maarufu kutoka Afrika ya Kusini, Yvonne Chaka Chaka kwa heshima ya kuwa Balozi wa kampeni ya kutokomeza ugonjwa wa malaria Barani Afrika. Balozi Amina Salum Ali aliwashukuru Benki ya Dunia kwa juhudi za makusudi wanazofanya kuhakikisha Bara la Afrika linatokomeza kabisa gonjwa hili hatari la Malaria, pia Balozi Amina Salum Ali alimshukuru Bwn. Tim Ziemer kutoka USAID kwa jitihada zao za kupigana kuutokomeza ugonjwa wa malaria Duniani hususani Bara la Afrika.
Kushoto ni Mwanamuziki wa Afrika ya Kusini Yvonne Chaka Chaka akifuatilia hotuba ya Balozi wa African Union Mhe. Amina Salum Ali, kulia ni Kaimu Balozi wa Afrika ya Kusini nchini Marekani Mhe. Johnny Moloto.
Kutoka kushoto ni Mhe. Balozi wa Swaziland Rev. Dr. A. M. Ntshangase, Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe. Liberata Mulamula na Balozi wa Botswana nchi Marekani Mhe. Dr.Tebelelo Mazile Seretse.
Dr. Anne Maryse B. Pierre-Louis ambaye ni mkuu wa utawala na mtaalam wa maswala ya afya kutoka Benki ya Dunia akielezea jitihada za Benki ya Dunia inazofanya kupigana kuutokomeza ugonjwa wa Malaria Barani Afrika. Pia alimshukuru mwanamuziki kutoka Afrika ya Kusini, Yvonne Chaka Chaka kwa kazi nzuri anayofanya ya kuwa Balozi wa kampeni ya kutokomeza ugonjwa wa Malaria Barani Afrika.

Tuesday, October 22, 2013

Vyuo 10 hapa nchini Tanzania vyafungwa na serikali

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Phillip Mulugo, pichani.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imekunjua makucha yake kwa kutangaza kuvifuta vyuo 10 ambavyo havikusajiliwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) .

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Philip Mulugo, alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaama mbele ya Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii na kuongeza kuwa kufutwa kwa vyuo hivyo ni kutokana na kutokufuata utaratibu wa kusajiliwa.

Alivitaja vyuo hivyo ni Media and Research Center, Vision Hotel and Tourism College, East Africa College of Hospitality and Tourism, The Africa Institute of Business Management na Aspiration Training Center, vyote vya Dar es Salaam.

Vingine ni Dar es Salaam School of Hair Design, Media and Values Training Institute na Information Technology Training Center vya Dar es Salaam. Pia alikitaja Chuo cha Morogoro School of Medical Sciences cha Morogoro.

Katika hatua nyingine, Mulugo alikiri kuwa kuna upungufu katika kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kupitia bodi ya mikopo.

Alisema kuna changamoto nyingi zinazoikabili bodi hiyo zikiwamo urejeshwaji wa mikopo kwa wanafunzi waliomaliza chuo, mfumo wa utoaji wa mikopo, ufinyu wa bajeti na makosa yanayotokana na wanafunzi kukosea kujaza fomu za mikopo

Malaika wajinadi kwa mpya mbili



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
BENDI ya Malaika inayoongozwa na Rais wake Christian Bellah, jana ilijitambulisha rasmi kwa wanahabari sambamba na kuachia vibao vyao viwili vyenye ubora wa hali ya juu.
Rais wa bendi ya Malaika, Christian Bellah pichani.
Nyimbo hizo ni Mtu wa watu na Nakuhitaji, huku zikionekana kukubaliwa na wengi wakiwamo waandishi waliopata nafasi ya kusikiliza kwa mara ya kwanza.

Akizungumza katika utambulisho huo, Bellah moja ya wanamuziki wenye uwezo wa juu wa kuimba, alisema kuwa mipango yao ni kuwa bendi tishio katika tasnia ya muziki wa dansi hapa nchini.

Alisema kuwa bendi yao imesheheni waimbaji wazuri na wenye kiu ya mafanikio, hivyo anaamini kuwa wote watafanya kazi kwa ushirikiano na kukwea kileleni.

“Hii ni bendi yenye mipango na tunaamini kwa pamoja mashabiki hawatajutia hata kidogo kutuunga mkono maana tupo imara kupita kiasi.

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...