Baadhi ya nguo za maharusi zinavyoonekana katika duka la urembo na mitindo lililozinduliwa rasmi jana, huku mgeni rasmi akiwa ni mwimbaji wa muziki wa taarabu nchini Tanzania, Bi Khadija Kopa.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MWIMBAJI wa muziki wa taarab nchini Tanzania, Bi Khadija Kopa, amewataka wanawake kuendelea kujikwamua kiuchumi wao wenyewe bila kusubiri kuwezeshwa na wanaume.
Khadija aliyasema hayo jana katika ufunguzi wa duka kubwa la kisasa la urembo na nguo za wanawake linalojihusisha pia na kupamba maharusi, kukodisha na kuuza nguo za maharusi, linalojulikana kama Taiba Beauty, linalomilikiwa na mjasiriamali Twaiba Ahmed Ally.
Mwimbaji mkongwe wa muziki wa taarabu nchini, Bi Khadija Kopa, akizungumza na waandishi hawapo pichani katika uzinduzi wa duka la nguo za wanawake na za harusi linalomilikiwa na mwanamama Twaiba Ahmed Ally.
Alisema kwamba wapo wanawake wanaoamini kuwa hawawezi kuendelea hadi wawezeshwe, jambo linalohitaji kupingwa vikali ili wanawake waweze kupiga hatua kiuchumi na kujikomboa wao wenyewe.
Mmiliki wa duka la nguo za maharusi lililopo mtaa wa Livingstone na Mkunguni, Bi Twaiba Ahmed Ally, katikati akikata keki ya uzinduzi wa duka hilo jana. Kulia ni mwimbaji wa taarabu nchini, Khadija Kopa akilishwa keki kama mgeni rasmi. Kushoto ni mtangazaji wa kipindi cha Ng'ari Ng'ari kutoka Clouds Tv, Sakina Lyoka.Twaiba akimlisha keki Khadija Kopa katika tukio la uzinduzi huo jana.
Bi Twaiba akimlisha keki Sakina Lyoka jana.
Bi Sakika Lyoka akimlisha keki mmiliki wa duka hilo, bi Twaiba Ahmed. Kushoto ni Khadija Kopa.
“Naomba wanawake tuache dhana kuwa hatuwezi kuendelea hadi tuwezeshwe na wanaume, ukizingatia kuwa Dunia imebadilika na wapo wenzetu wanaofanya kazi nzuri kiasi cha kutufanya tuige nyendo zao ili tusonge mbele, akiwamo Bi Twaiba Ahmed,” Alisema Kopa.
Akizungumzia hilo, Bi Twaiba alisema ni jukumu lao kuhakikisha kwamba wanawake wanasonga mbele kiuchumi, akisisitiza namna ya ujihusishaji na masuala yote ya ujasiriamali na kazi nyingine.
“Nashukuru kwa sapoti kubwa ninayoipata, akiwamo Bi Khadija Kopa, hivyo nitaendelea kufanya juhudi ili nizidi kupiga hatua kubwa kibiashara kwa kusimamia changamoto zote zinazonikabili. “Katika duka langu nafanya shughuli zote zinazomhusu mwanamke, wakiwamo wale wanaofunga ndoa kwa kuwapamba, kuwakodisha vifaa vya harusi bila kusahau wale wanaotaka kununua kwa fedha taslimu, ofisi yangu ikipatikana katika mtaa wa Mkunguni na Livingstone, Kariakoo, jijini Dar es Salaam,” Alisema.
Mbali na kuuza vifaa vya maharusi na nguo za kawaida za wanawake, pia Twaiba anajihusisha na ufundishaji wa upambaji kwa wanawake, shughuli inayomfanya aheshimiwe na wengi wanaojihusisha na sekta hiyo ya mitindo na urembo.
No comments:
Post a Comment