Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAKATI marehemu Hassan Chabanga Dyamwale mbunge wa zamani wa Handeni, mkoani Tanga, akitarajiwa kusafirishwa leo kuelekea nyumbani kwao Handeni tayari kwa maziko, Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia ametuma
salamu za rambirambi kufuatia kifo cha aliyewahi kuwa Katibu Mtendaji wa
kilichokuwa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT), Chabanga Hassan
Dyamwale (76).
Mbali
wa wadhifa huo katika eneo la mpira wa miguu, pia Dyamwale atakumbukwa
zaidi akiwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii na kwa miaka ya hivi
karibu alikuwa Mjumbe wa Kamati huru ya uchaguzi TFF tangu 2004 mpaka
2012.
Hayati
Dyamwale aliyezaliwa Juni 01, 1941, aliondoka FAT mwaka 1978, lakini
pia aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Michezo nchini miaka ya mwanzo ya 1980
kabla ya kuhamishiwa Handeni mkoani Tanga kuwa Ofisa Utamaduni, lakini
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati huo, Mwalimu Julius
Nyerere akamrudisha Dar es Salaam.
“Nimeguswa
na kifo cha Mzee Chabanga Hassan Dyamwale. Inna Lillah wainaillah
Rajauun. Natuma salamu zangu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa,
majirani na marafiki wa hayati Mzee Dyamwale ambaye nimetaarifiwa kuwa
amefariki dunia Agosti 13, mwaka huu kwenye Hospitali ya Muhimbili,”
amesema Karia.
“Ni
msiba mkubwa kwa wanafamilia ya michezo hususani soka,” amesisitiza
Rais Karia na kuomba familia, ndugu, jamaa, marafiki kuwa watulivu
katika kipindi hiki kigumu baada ya kumpoteza mpendwa Dyamwale.
Rais
Karia amesema: “Namfahamu Mzee wetu huyu tangu miaka mingi akiwa
mteuliwa kutoka serikalini kushika wadhifa wa utendaji ndani ya FAT
wakati ule (Kwa sasa ni TFF), alifanya kazi kwa uhodari mkubwa na
uadilifu,” amesema Rais Karia.
Rais
Karia amesema kwamba mbali ya kuwa mtendaji ambaye alifanya mabadiliko
makubwa katika soka la Tanzania kutoka ligi ya kituo kimoja hadi ligi ya
mikondo miwili (nyumbani na ugenini). Taarifa zinasema kwamba alifanya
kazi hiyo akiwa kwenye hema.
Pia
Rais Karia alimfahamu Mzee Dyamwale alipokuwa Meneja wa Uwanja wa Taifa
(sasa Uwanja wa Uhuru) aliyekuwa mtaalamu wa masuala ya ujenzi wa
viwanja.
Rais
Karia amesema kwamba atambukuka zaidi hayati Dyamwale kwa uhodari wake
wa kazi na msimamo kwenye jambo aliloliamini lilileta mafanikio makubwa
katika soka la Tanzania.
Kumbukumbu nyingine zinaonesha kuwa Dyamwale ndiye aliyebuni mpango wa watoto kuingia bure uwanjani miaka ya 1980 maarufu yosso. Marehemu Dyamwale anatarajiwa kusafirishwa leo kuelekea wilayani Handeni, mkoani Tanga kwa ajili ya maziko yatakayofanyika huko nyumbani kwao Handeni.