Pages

Pages

Friday, November 30, 2012

Wezi wa Sharomillionea wanaswa Muheza

Na Kambi Mbwana
VITU viliyoibwa vya marehemu Hussein Mkiety, maarufu kama 'Sharomillionea', vimesalimishwa na watu wanaosadikiwa kuwa ni wezi, waliompora mara baada ya kupata ajali na kupotea uhai wake, katika kijiji cha Songa Kibaoni, wilayani Muheza, mkoani Tanga, mapema wiki hii.

Ajali hiyo ilitokea Jumatatu saa mbili na nusu usiku na kusababisha kifo cha msanii huyo mahiri wa uchekeshaji hapa nchini.
Msanii huyo alitokuwa akitokea jijini Dar es Salaam na kuelekea Lusanga wilayani Muheza kwa ajili wa kuwasalimia wazazi wake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Constatine Massawe, alithibitisha kupatikana vitu hivyo ambapo alisema upatikanaji wake ulitokana na msako mkali uliofanya na uongozi wa serikali wilayani Muheza wakishirikiana na Jeshi la Polisi.

Massawe alisema baada ya kutokea kwa tukio hilo Jeshi la Polisi Mkoani Tanga liliweka mtego na kutangaza kuinunua simu ya mkononi ya msanii huyo aina ya blackberry na ndipo moja kati ya wezi ambao walihusika kwenye tukio hilo walipojitokeza na kuipeleka kwa ajili ya kuiuza na wakati walipofika eneo ambalo walikubaliana walikabidhi simu kwa ajili ya kuikagua na baade wezi hao kushtukia mtego huo na kukimbia huku wakiiacha simu hiyo.

Aidha kamanda Massawe alivitaja vitu ambavyo vimesalimishwa kwa jeshi hilo ni simu ya mkononi aina ya Black Berry, Betrii ya gari, tairi ya akiba, radio ya gari, begi ambalo lilikuwa na nguo za marehemu, saa ya mkononi na nguo ambazo alikuwa amevuliwa sharomilionea na vibaka wa eneo hilo mara baada ya kutokea ajali hiyo.

Kamanda Massawe alisema mpaka hivi sasa hakuna mtu yoyote anashikiliwa na jeshi la polisi kufuatia kutokea kwa uporaji huo huku Jeshi hilo likiendelea na uchunguzi ili kuwabaini waporaji hao na kuweza kufikishwa katika vyombo vya sheria ili kuweza kujibu tuhumu zinazowakabili na kutoa wito kwa wananchi kuacha kufanya vitendo vya uporaji pindi ajali zinapotokea katika maeneo yao.

"Tupo kwenye uchunguzi mkali ili kuhakikisha tuwatia mbaroni wale wote ambao waliohusika na kitendo cha kinyama alichofanyiwa msanii huyo alisema "Kamanda Massawe.

Thursday, November 29, 2012

Mkuu wa wilaya Muheza awakera wengi



Na Kambi Mbwana, Muheza
MKUU wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu, jana aliwakera watu wengi waliovamia hospitali ya Teule kwa ajili ya kuangalia jinsi msanii Hussein Mkiety, maarufu kama Sharomillionea anavyoandaliwa kwa ajili ya kuzikwa kijijini kwao Lusanga, wilani Muheza, mkoani Tanga.

Kabla ya hapo, baba mkubwa wa Marehemu, aliweka utaratibu wa baadhi ya ndugu na jamaa kushiriki kwa karibu kuandaa mazishi ya msanii huyo aliyefanya vyema katika sanaa hapa nchini.


“Haiwezekani jamani watu wote mliokuwapo hapa kuingia katika chumba cha kuhifadhia maiti badala yake wote tuhamie nyumbani kwao kwa ajili ya kuzika na sio kuminyana hapa.

“Naamini uamuzi huu ni mbaya na unakera kwa kiasi kikubwa, lakini lazima mjuwe kuwa naongea hapa kama mtu wa serikali na itakuwa vyema kama mashabiki na wakazi wote wa Tanga tutaelewana katika hilo,” alisema Subira huku akiangaliwa vibaya na wananchi.

Kauli ya Mkuu huyo wa Wilaya ya Muheza, ilifuatiwa na amri ya jeshi la Polisi kuwazuia watu kuendelea kuingia katika upande wa chumba cha kuhifadhia maiti.

Idadi kubwa ya mashabiki na wasanii walikuwa wengi katika wilaya ya Muheza kuangalia namna gani kijana wao mpendwa anaingizwa katika nyumba ya milele baada ya kufariki kwa ajali ya gari karibu na kijiji chao cha Lusanga.

Tunda Man anywea mazishi ya Sharomillionea



 
Picha mbalimbali za mazishi ya msanii Sharomillionea, Muheza Tanga





Na Kambi Mbwana, Muheza
MWIMBAJI wa muziki wa Bongo Fleva, Tunda Man, katika muda wote wa msiba wa Hussein Mkiety, maaruru kama Sharomillionea, alikuwa amenywea, wakati wote akiwa kimya, hivyo kuonyesha alikuwa kwenye mawazo makubwa.

Kuanzia katika Hospitali ya Teule Muheza ulipokuwapo mwili wa msanii Sharomillionea, Tunda Man anayetokea katika kundi la Tip Top Connection hakuweza kusema lolote, zaidi ya kupepesa macho yake kwa majonzi.

Baada ya kumaliza taratibu za mazishi ya Sharomillionea, msanii huyo aliyekuwa kwenye uswahiba na marehemu, alisema kuwa hakujisikia vizuri kwa kushuhudia msanii mwenzake amelazwa chumba cha maiti na baadaye kaburini.

“Ni mbaya sana kuangalia kuona mtu uliyechat naye muda uliopita, au ulikuwa naye wakati Fulani anaingizwa kaburini na kubadilishwa jina lake kirahisi namna hii.

“Nimeumia sana kwa msiba wa Sharomillionea, lakini sisi binadamu ni watu wa kupita hapa duniani zaidi ya kuombeana kwa Mungu maana huwezi jua nani anafuata nyayo baada ya leo kutoka hapa nyumbani kwa Sharomillionea,” alisema Tunda Man.

Tunda Man anatokea katika kundi la Tip Top Connection lenye mjumuiko wa wasanii mahiri, akiwamo kiongozi wao Ahmad Ally ‘Madee’, anayejiita pia Rais wa Manzese.




Tuesday, November 27, 2012

Kifo cha Sharomillionea chatikisa nchi




Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MSIBA wa msanii nyota wa uchekeshaji hapa nchini, Hussein Mkiety, maarufu kama 'Sharomilionea' umegusa hisia za wengi, huku King Majuto akikimbizwa Hospitali baada ya kushikwa na presha, hivyo kutishia usalama wake.

Mtoto wa King Majuto, Hamza Majuto, aliimbia HANDENI KWETU kuwa hali ya baba yake inaendelea vizuri kutokana na kuumizwa zaidi na msiba wa Sharomlionea anayetamba katika ulingo wa filamu na muziki hapa nchini.

Nyota wa comedian nchini, Hussein Mkiety Sharomillionea alivyokuwa enzi za uhai wake.
Juu akiwa na nguli wa comedian nchini, King Majuto, aliyeumizwa sana na msiba huo.
Msanii huyo alikufa juzi saa mbili za usiku Maguzoni, kilimita chache na kijijini kwao Lusanga, wilayani Muheza mkoani Tanga, baada ya gari lake alilokuwa akisafiria lenye namba za usajili T478 BVR Toyota Harrier kupinduka na kusababisha kifo chake.

Kamanda wa Polisi mkoani Tanga, Constantine Masawe, alikiri kutokea kwa msiba huo na kusema kuwa mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Teule, Muheza, mkoani Tanga kwa taratibu za mazishi zinazopangwa na familia yake.

“Marehemu alikufa majira ya saa mbili za usiku kwenye barabara ya Segera alipokuwa anatoka Dar es Salaam kwenda Muheza, hivyo mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Teule, huku gari lake likihifadhiwa pia kwasababu haliwezi kutembea,” alisema Masawe.

Taarifa za kifo cha msanii huyo aliyeibukia hivi karibuni na kufanya vema katika ulingo huo zilianza kuzagaa saa tatu za usiku, ikiwa ni dakika chache baada ya kufariki katika ajali hiyo ya kusikitisha kwa nyota huyo.

Katika mitandao yote ya kijamii kuanzia saa tatu za usiku zilizagaa habari zake, huku kila mmoja kiwa na hisia tofauti zilizotokana na madai ya kifo cha msanii huyo, ambaye baadaye jeshi la Polisi lilithibitisha kwa kupitia Kamanda wake, Masawe.

Sharomilionea ameshacheza filamu nyingi za uchekeshaji na kujipatia sifa kubwa, ikiwamo ile ya Sharo Millionea, Imekula Kwako, Jini Mahaba, Porojo na nyinginezo zinazofanya vyema katika tasnia ya filamu nchini.

Katika filamu ya Jini Mahaba, Sharomillionea anayetamba pia kwa msemo wake wa ‘Umebug Men’, anacheza kama mtu maarufu anayekwenda kujitambulisha kwa wake zake (Kingwendu) na kushangazwa na hali zao za maisha.

Sharomillionea anamshangaa mama yake mkwe anavyochambua mboga za majani wakati yeye sio utaratibu katika maisha yake. “Huyu ndio mama yako Men? Mbona anachambua majani,” aliuliza huku anakunja mdomo wake na kujifuta uso.

Maneno hayo yanamuumiza mama yake mkwe na kuamua kumuita mume wake (Kingwendu) na kuja kushangaa Sharobalo alivyokuwa katika mueneko wa super Star na kujikuta akipagawa alipoanza kukejeliwa na mkwe wake.

Mbali na filamu hiyo ya Jini Mahaba, mkali huyo pia ametamba katika filamu nyingi pamoja na nyimbo mbili alizorekodi, huku pia akililiwa na wasanii wenzake kutokana na ushirikiano wake, mara baada ya kuibuka kisanii.

Wasanii wengi waliozungumzia kifo cha Sharomillionea wakiongozwa na Steve Nyerere, walionyeshwa kuchanganyikiwa kwa msiba wa msanii aliyeanza kutokea peupe na kutamba mno katika sanaa ya uchekeshaji.

Sharomillionea aliyetokea katika ubavu wa nguli wa vichekesho nchini, King Majuto, anazikwa kesho Jumatano, kijijini kwao Lusanga, huku wasanii wengi wakitarajia kuhudhuria msiba na mazishi ya nyota huyo aliyeipenda pia nyumbani kwao Muheza.

Monday, November 26, 2012

Uwezo zaidi




Nelson Kessy wa Kigogo Mburahati, akijaribu bahati yake kwa kucheza mpira
(ball Control) wakati wa Mchujo wa Guinness Football Challenge (GFC) kwenye
viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.(Picha na
Mpigapicha wetu).

Wazee wa Ngwasuma kuvamia Morogoro Ijumaa



 Rais wa FM Academia, Nyosh El Sadaat
 
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
BENDI ya muziki wa dansi ya FM Academia, maarufu kama Wazee wa Ngwasuma, inatarajia kufanya onyesho la nguvu katika uzinduzi wa pub ya ‘Babylon’, iliyopo Kilosa, mkoani Morogor kwa ajili kiwanja hicho kipya cha burudani.

Ngwasuma wanafanya shoo hiyo wakiwa na lengo moja la kuonyesha makali katika ramani ya muziki wa dansi hapa nchini, huku wakiwa na wakali mbalimbali wanaofanya makubwa katika mustakabali wa bendi hiyo.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa ukumbi huo, Daudi Mfaume, alisema kwamba maandalizi ya kuwaleta wakali hao katika mji wao huo yamekamilika, huku wakiamini kuwa mashabiki wao watapata makubwa.

Alisema kuwa Ngwasuma wamekuwa na mashabiki wengi katika mji wa Morogoro, hivyo kwakuwaleta Kilosa, mashabiki wao watapata kitu adimu na kuweka historia kamili katika tasnia ya muziki wa dansi hapa nchini.

“Tumepanga kuwaleta wakali wa muziki wa dansi hapa nchini, Wazee wa Ngwasuma kwa ajili ya kuwapatia burudani mashabiki wao watakaoingia katika uzinduzi huo wa Babylon wakiwa kama wadau na mashabiki wa muziki nchini.

“Naamini kila kitu kitakwenda sawa, hivyo wadau na mashabiki wa muziki wa dansi wa mkoani Morogoro, wajiandae kwa ajili ya burudani hiyo itakayofanyika katika ukumbi mpya wa burudani katika mji wetu wa Kilosa,” alisema Mfaume.

Wazee wa Ngwasuma ipo chini ya Rais wa Vijana, Nyosh El Sadaata, akiwa sambamba na waimbaji wengine nguli, akiwamo Patchou Mwamba, ambaye pia anatamba katika tasnia ya filamu, baada ya kucheza filamu mbalimbali zinazokubalika nchini.

Asha Baraka asifia vipaji Twanga Pepeta



 Asha Baraka, Mkurugenzi wa Twanga Pepeta

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MKURUGENZI wa bendi ya The African Stars, Twanga Pepeta, Asha Baraka, amesema bendi yake ina wanamuziki wengi kiasi kwamba wengine wanashindwa kupanda jukwaani zaidi ya mara tatu katika kumbi nyingi wanazofanya shoo.

Hiyo ni kauli ya kwanza kutolewa na mwanamama huyo ambaye tangu kutangaza kuondoka kwa nguli wa muziki wa dansi nchini kwenye bendi hiyo, Mwinjuma Muumini, Asha hajasikika akisema lolote juu ya kuhama kwa mkali huyo.

Akizungumza mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Asha alisema kwamba bendi yake ina waimbaji wengi na hawawezi kuwa na upungufu wa aina yoyote katika safu zao, licha ya kuhama tena kwa Muumini.

Alisema wapo waimbaji wanaopanda jukwaani mara moja kwa siku katika shoo zao, hivyo ni wazi kuwa wengine wanachukulia nafasi hiyo kutafuta mahali kwa kuonyesha makali yao zaidi katika ramani ya muziki wa dansi nchini.

“Mpaka sasa wapo waimbaji zaidi ya watano ambao ni mahiri na wana mashabiki wengi, akiwamo Kalala Junior, Dogo Rama, Salehe Kupaza, Badi Bakule, Luiza Mbutu, Janeth Isinika, Amigo Ras na wengine wenye wapenzi lukuki.

“Naamini bila hata kuangalia nani hayupo kwetu, tunapaswa kujivunia kuwa nao waliokuwapo kwasababu wanamuziki wanapokuwa wengi zaidi, lazima wachache wao waimbe wimbo mmoja shoo nzima,” alisema.

Twanga Pepeta ni miongoni mwa bendi zinazofanya vyema katika tasnia ya muziki wa dansi hapa nchini, ikiwa na nyimbo nzuri zinazopendwa na wengi, ukiwamo wa ‘Shamba la Twanga’ unaozidi kuiweka juu bendi hiyo.

Friday, November 23, 2012

Kinyang’anyiro cha Chalenji kuanza kesho Uganda


Mrisho Ngassa akimiliki mpira uwanjani.
                     

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MASHINDANO ya Kombe la Chalenji 2012 yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi leo nchini Uganda na kumalizika Desemba 8, katika mji wa Kampala, nchini Uganda, huku timu 12 zikionyeshana kazi katika michuano hiyo.

Timu hizo ni pamoja na Burundi, Ethiopia, Eritrea, Kenya, Malawi, Rwanda, Somalia, Sudan ya Kusini, Tanzania, Sudan, Zanzibar na Uganda, ambao ndio mabingwa watetezi wa mashindano hayo ya Kombe la Chalenji mwaka huu.

Mashindano hayo kwa mwaka huu yalikuwa yafanyike nchini Kenya, lakini wadhamini wake, Kampuni ya East African Breweries Ltd (EABL) waliomba michuano hiyo ifanyike nchini Uganda na kuridhiwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Michuano hiyo inaanza huku wawakilishi wa Tanzania, timu ya Taifa, Kilimanjaro Stars na ndugu zao Zanzibar Heroes wakiwa tayari kwa vita katika mashindano hayo yenye ushindani wa hali ya juu kwa washiriki wote.

Kwa mujibu wa CECAFA, viwanja vitakavyotumika katika mashindano ya mwaka huu ni Namboole na Nakivubo vyote vya Kampala Uganda, huku Namboole ukiweza kuchukua mashabiki zaidi ya 45,000 utakaotumika kwa ajili ya mechi za ufunguzi, mechi zote za kundi A na mechi za hatua ya robo fainali, nusu fainali na fainali.

Wakati Namboole ukichukua mashabiki 45,000, Uwanja wa Nakivubo nao una uwezo wa kuchukua mashabiki 15,000, ingawa waandaji wameupanga uwanja huo utumike katika mechi chache katika mashindano hayo.

Wawakilishi wa Tanzania, timu ya Kilimanjaro Stars, imepangwa kuanza kutimua vumbi na Sudan kesho Jumapili, ikiwa ni siku moja baada ya kuanza katika mji huo wa Kampala, nchini Uganda, ardhi ya mabingwa watetezi.

Benchi la ufundi la Tanzania linaloongozwa na kocha wake, Kim Poulsen na Sylvester Marsh, wametangaza vita katika mashindano hayo kwa ajili ya kuiwezesha kutwaa ubingwa huo na kuleta imani kwa Watanzania.

Wednesday, November 21, 2012

MGODI UNAOTEMBEA




  Abdallah Kigoda, Mbunge wa Handeni

Watanzania tuchague viongozi watakaotusaidia, si wachuma fedha


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KATIKA mfululizo wa makala zangu kwenye Gazeti la Mtanzania Jumatano, ‘Mgodi Unaotembea’ pamoja na Mtanzania Jumapili, wakati mwingine nakutana na maswali ambayo, ukiyafikiria vizuri, jibu lake linaweza kukuliza.

Ndio, kama wewe unaona uozo wa jambo linalokumiza limeanzia kwa mtu mmoja aliyekuwapo madarakani kwa muda huo, ukweli ni kwamba umeanza zamani. Ingawa si kwa maeneo yote, lakini kwa kiasi kikubwa matatizo haya yanawaumiza Watanzania wengi.

Jumapili ya Novemba 11 niliandika makala iliyokwenda kwa jina la Njaa, shida ya maji vitawatoa roho Handeni. Makala hiyo ilielezea kwa kirefu matatizo yanayowakabiri watu wa Handeni na vitongoji vyake.

Maoni mengi niliyapata. Lakini, huyu alinisikitisha sana. Na huu ndio ujumbe wake ambao nikaamua kuuandikia tena makala kuweka sawa mambo niliyojadili angalau watu wafahamu na kutafutia ufumbuzi.

“Ndugu, Mbwana, Makala yako katika gazeti la Mtanzania Jumapili, Novemba 11 kuhusu tabu ya njaa na shida ya maji Handeni ni ya kusikitisha sana. Mimi nilikaa Handeni mwaka 1982 na 83 wakati wa mbunge Mussa Masomo hali ilikuwa hivyo hivyo.

“Hawa Wabunge wanafanya kazi gani? Naomba unijulishe iwapo Mussa Masomo bado yupo hai. Mimi Method Mhagachi, DSM,” ulimaliza ujumbe uliotumwa na mfuatiliaji mzuri wa gazeti la Mtanzania.

Ujumbe huu uliniumiza kichwa. Hasa baada ya kugundua kuwa kero ninayoiona mimi kubwa kwangu, haijawahi kutoka kwa wakazi na wananchi wa Handeni. Kwa bahati mbaya, si Handeni tu, bali katika maeneo mengi ya Tanzania.

Ingawa juhudi nyingine zimekuwa zikichukuliwa na serikali Kuu, chini ya Rais wake, Jakaya Mrisho Kikwete, lakini wakati mwingine anaangushwa na anaowaamini. Ndio, maana kila wilaya ina fungu lake inapata katika kila bajeti.

Pia kuna mfuko wa jimbo. Mbali na mfuko wa jimbo, bado kuna rasilimali fedha na rasilimali watu ambao kwa pamoja wanaweza kushirikiana kuleta maendeleo ya watu wao.

Katika kuliangalia hilo, jibu lake ni kwamba majimbo hayo yenye matatizo lukuki yansababishwa na wabunge wao wasiokuwa na jipya kwa wananchi wao. Tuliseme hili ingawa litakuwa chungu kwa wasiopenda ukweli.

Wale wanaosema kuwa eti tunaishi mjini habari za mikoani tunazipata wapi? Wakaongeza kuwa harakati zinazofanywa ni kuwachafua watu wachache. Sio kweli. Nimekuwa nikitembelea katika maeneo mengi kujionea hali ya mambo inavyoendelea.

Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, nimetembelea katika mikoa ya Kilimanjaro, Mwanza, Tabora, Singida, Morogoro na Tanga ambapo ndio nyumbani ninapotembelea pia vijiji na Kata zote, kama vile Misima, Kwamatuku, Komkonga, Mkata na kwingineko. Na kama tusipotumia haki ya kukosoana na kuelimishana nchi yetu haiwezi kusonga mbele.

Kati ya wabunge wengi wanaoshinda katika majimbo yao, hakika wanatumia njia za panya kuwapatia nafasi hizo nyeti. Wabunge hawa ni wale ambao wameshakaa katika majimbo yao kwa miaka mingi, huku wakikosa mwelekeo.

Majimbo yao yamekuwa na changamoto nyingi. Wananchi wanaendelea kutaabika, huku wabunge wao wakionekana kwenye luninga katika warsha, semina, ama vikao vya Bunge vinavyowalipa vizuri.

Wabunge ambao kwa miaka mingi tangu alipochaguliwa katika nafasi hiyo, hajaweza kutembelea hata mara moja kwa wananchi waliomuweka madarakani. Haya yote yanasababishwa na umasikini wa kipato na fikra sahihi.

Wananchi wengi hawana uelewa katika mambo ya uraia. Hawajui hata haki zao za msingi za kuwapata viongozi wao.

Umasikini wa fikra pevu ni wa kubaini kuwa kususia kupiga kura au kuchukua mia mbili kama rushwa ya kumuweka mtu madarakani ni hatari katika maisha yake kwa kipindi cha miaka mitano.

Kwa bahati mbaya, masikini yoyote akipewa mia 200 hakika atakubeba mgongoni hadi kufa kwako. Atakusifia kadri anavyoweza. Atakuombea kwa Mungu dhambi zako ziondolewe kwasababu tu amepewa mia 200 ya kununua dagaa.

Hizi ndio changamoto za masikini. Hizi ndio dosari za watu hasa wa mikoani ambao kwa hakika ndio kwenye maisha magumu kupita kiasi. Kwa kusema hayo, nadhani kuna haja sasa ya kila mwananchi kujitambua.

Kwanza wajuwe kura ni haki yao ya msingi. Pili wasijaribu kudanganywa kwa shilingi mia 200 wanazopewa na wenye nazo. Badala yake wahoji au watake mambo ya kimaendeleo katika maeneo ambayo kwa hakika ni kazi ya viongozi wao.

Ifahamike kwamba, kiongozi kufanikisha maisha bora kwa watu wake ni jukumu lake. Hakuwekwa madarakani ili atembelee magari ya kifahari na familia yake bali pia awatumikie mabosi wake, ambao ni wananchi wake.

Lakini kama mtu ameingia madarakani na hana analofanya huyo hafai kama ukoma. Hakuna kuangaliana usoni. Hakuna kuogopana katika kusema mambo ya maana yenye umuhimu na Taifa letu lenye kila rasilimali.

Wananchi wasikubali kupumbazwa na visenti vya kununulia sukari, badala yake wawabane zaidi viongozi wao ili waboreshe maisha yao kwa ujumla.

Waboreshe katika mambo mbalimbali, yakiwamo kilimo bora, miuundo mbinu, huduma za afya, nishati ya umeme ambayo kwa hakika ni yanaweza kupunguza makali ya maisha.

Badala ya kupokea visenti vya kula, wananchi watake kutoka kwa viongozi pembejeo za kilimo na mengineyo yenye kuinua uchumi wao.

Wakati wa uhai wa bibi yangu (Luwaya) katika kijiji chetu cha Komsala, Handeni, mkoani Tanga, nakumbuka hata kuwe na njaa vipi lakini chai kwake ni lazima. Ingawa wapo waliohangaika kutafuta chakula, lakini yeye alikuwa tofauti.

Kumbe alikuwa anaikamua miwa na na kuipika sukari kwa njia ya kienyeji. Hii iliweza kumuondolea bajeti ya sukari kutoka kwa watoto wake. Kazi yake kubwa ilikuwa ni kulima kidogo mazao aliyomudu, ikiwamo miwa, mahindi na mpunga.

Lakini vipi leo. Je, wananchi wanahamasishwa kulima? Kama wapo wanaopenda kulima. Je, changamoto za wadudu, kukosa uwezo wa kununulia pembejeo wanamudu vipi? Serikali yao ya kijiji, Kata, wilaya na Taifa inawajali?

Je, mabadiliko ya tabia nchi, kunakosababisha mvua kutonyesha kwa wakati, wananchi wanaelimishwa juu ya hilo? Nasema hivi maana katika maeneo mengi, wakulima wamekuwa wakilima kila wakati na kuambulia patupu.

Wanalima wakitegemea mvua itanyesha mwezi ujao. Lakini hainyeshi na ikinyesha si kubwa, hivyo kuozesha mbegu zao walizopata kwa shida. Mara kwa mara wanapishana na mvua. Kama hivyo ndivyo, wataalamu wetu wa kilimo ndio wakati wa kufanya kazi zao.

Kama hivyo haitoshi, wakulima waelimishwe pia kupanda mazao yanayostahimili ukame kwa baadhi ya maeneo. Waelimishwe juu ya kuhifadhi vyakula ama kutoiuza ardhi kwa matapeli wanaokwenda kuwalangua kwa njaa zao.

Haya ni mambo ya watalawa. Kama mtu muda mwingi yupo mijini na kusubiri Uchaguzi Mkuu hakika ni majuto makubwa kwa wananchi wake.

Huu ndio ukweli. Vijijini kuna changamoto nyingi sana. Ingawa tunajua kuwa kilimo ndio uti wa mgongo, lakini watu wanaoishi huko hawajaliwi wala kukumbukwa. Viongozi wengi, wakiwamo wabunge wao ni wachumia matumbo yao.

Wanachosubiri Uchaguzi Mkuu na kununua mashati ambayo ndani yake huweka mia 200 ambazo mwananchi huona nyingi na kuwapigia kura zinazowaumiza kwa miaka mitano kila mwaka, ingawa baadaye hudanganya kwamba wanakubalika.

Nani anakubalika kwa wananchi wake? Na aseme leo kuwa anakubalika kwakuwapatia maisha bora wananchi wake. Na aseme alichofanya leo kwa muda aliokaa katika jimbo lake. Kisha watu tupime ukweli na uongo wake.

Hakuna kitu. Bure kabisa. Kama wapo, sio wengi. Baadhi yao hulindwa na visenti vyao. Ndio maanza Mgodi Unaotembea unasema, masikini ukimpa mia 200 atakubeba mgongoni.

Atakuona wewe ni Mungu mtu. Hata kama uwe tapeli, mwizi. Kutokana na hilo, kuna haja ya kuangalia mustakabali wa maisha yetu.

Tukumbushane juu ya kuwachagua wenye dhamira ya kweli ya kuwaongoza Watanzania wenzao na sio wale wenye malengo ya kuvuna utajiri ili wanufaike na familia zao, wakati sisi watoto wetu wanasomea kayumba, huku wakitembea uchi kwa kukosa nguo za kuvaa.

Tukutane wiki ijayo.

0712 053949
0753 806087

Monday, November 19, 2012

KJ Traders na ziara ya Mlima Kilimanjaro





Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Generali, George Waitara, kulia akizungumzia ziara ya Mlima Kimanjaro. Anayefuata kushoto kwake ni Joseph Kitani, Mratibu Mkuu wa safari hiyo kutoka Kampuni ya KJ Traders ya jijini Dar es Salaam.

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WATANZANIA wengi wamejipa ujinga wa kuamini kuwa jukumu la kutembelea hifadhi mbalimbali lipo kwa wageni na sio wazalendo wenyewe.

Hao wanagoma kabisa kuweka taratibu za kutembelea hifadhi za Taifa kwa ajili ya kuangalia vivutio vya utalii, hivyo kueneza sumu hiyo kwa vizazi vyao.


Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki
 
Mtoto ambae hajawahi kupewa ratiba ya kufanya matembezi katika vivutio walau mara tatu kwa mwaka, kamwe hawezi kubadilisha taratibu hizo hata pale anapokuwa kwenye familia yake, anapotoka katika mikono ya wazazi.

Hilo ni tatizo kubwa. Linakuwa siku hadi siku. Hakuna mwenye mapenzi mema na moyo wa kujifunza vitu vinavyohusu historia ya maisha yao. Ni wageni kila wakati, kiasi cha kushindwa kujua mahala gani kuna vitu vya kustaajibisha.

Kwa mfano, unaweza kushangaa kusikia wapo watu wanaoishi karibu na Mlima Kilimanjaro, lakini hawajawahi hata siku moja kupanga namna ya kuupanda mlima huo mrefu Barani Afrika, badala yake wanasuburi wazungu waende kutalii.

Kwa bahati mbaya, wazawa wanagoma kuzunguukia hifadhi hizo kwa visingizio visivyokuwa na mashiko, maana katika kufanikisha suala hilo la kukuza utalii wa ndani, utaratibu mzuri umewekwa na gharama nafuu kwa kila Mtanzania.

Nadhani ni hapo unapokaa na kupongeza mawazo ya kutangaza sekta zetu za utalii, kubuni mbinu mpya za kuwafikishia ujumbe Watanzania juu ya kuweka utaratibu wa kutembelea katika hifadhi zao, ukiwamo Mlima Kilimanjaro.

Mlima ambao unasisimua kuutazama katika picha na kuleta hamu kubwa ya kuupanda, ukizingatia kwamba una historia kubwa ya maisha ya Tanzania na watu wake.

Nasema haya baada ya kuona juhudi za Kampuni ya KJ Traders kuandaa matembezi ya mlima Kilimanjaro, Desemba sita mwaka huu kwa ajili ya kutangaza sekta ya utalii wa ndani, huku wakishirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).

Matembezi hayo yamepangwa kuzinduliwa na Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Generali George Waitara, yakiwa na lengo na kutangaza mlima huo na kuamsha hisia mpya kwa Watanzania kwa ajili ya kupenda vitu vyao.

Mratibu Mkuu wa matembezi hayo ni Joseph Kitina, akileta matumaini na funzo kwa kila Mtanzania kuona kuwa ana deni la kupanga ratiba ya kutembelea sehemu mbalimbali za nchi katika hali ya kuangalia vivutio vyetu vya utalii.

Endapo tutakuwa tunaelewa thamani ya vitu vyetu, hata wale wanaokuja wataweka mkazo zaidi hivyo kuvutia makundi ya watalii watakaoingia nchini.

Kama Watanzania wenyewe watashindwa kuweka mbinu za kutangaza vivutio vyao, hakuna anayeweza kubadilisha mtazamo wao. Ndio maana kila juhudi zinazofanywa kwa ajili ya kutangaza utalii wa ndani zinakwama.

Jukumu la kutembelea vivutio vyetu visiachwe kwa wageni tu, hivyo kuna haja ya kushirikiana kwa pamoja na wadau wa sekta ya utalii, wakiwamo KJ Traders.

Huo ndio ukweli. Yoyote yule anayekwenda nje ya eneo lake na kukaa walau kwa saa 24, basi huyo ni mtalii. Haijalishi anakwenda huko kufanya kitu gani. Iwe ni kutembelea hifadhi za Taifa, kuhudhuria mikutano au kufanya biashara zake.

Tofauti ya mtalii wa ndani ni kuwa huyu analipia gharama ndogo kwa pesa za ndani, wakati mtalii kutoka nje ya nchi, hawa hulipia kwa pesa za kigeni. Mtu anapokuwa kwenye shughuli hizo za kitalii, kunakuwa na faida kubwa kwake na kwa Taifa husika.

Kazi kama vile upigaji wa picha, utafiti wa vitu mbali mbali, ukiwamo miti na wanyama, au kuangalia mbuga za wanyama, ni kati ya mambo ambayo mtu anapoyafanya eneo husika, basi amekuwa katika msingi ule wa utalii.

Wakati hayo yakiweza kufanywa na kila mdau wakiwamo hao KJ Traders kwa kushirikiana na TTB na Wizara husika ya Maliasili na Utalii, Tanzania imejaliwa kuwa na vivutio vingi vya Utalii katika kila mkoa na kuleta faida kubwa.

Ukiacha huo Mlima wa Kilimanjaro ambao baadhi yao huthubutu kusema upo katika nchi jirani ya Kenya, lakini Tanzania pia imejaliwa kuwa na maeneo mengi ambayo kila mmoja kwa nafasi yake yanaweza kuiletea tija nchi yao.

Hifadhi kama vile Ngorongoro, Mikumi, Hifadhi ya Ziwa Manyara, Ziwa Ruaha, Selous na mengineyo mengi ni kati ya sehemu ambazo zikitangazwa kwa kiasi kikubwa na Watanzania wenyewe, nchi inaweza kuingiza fedha nyingi za kigeni.

Lakini sisi wenyewe tukidharau thamani zetu zilizozaga katika mikoa mbalimbali, hakika hatuwezi kusonga mbele kwa lolote. Huo ndio ukweli. Katika kuusema, natumaini pia wale wenye mtazamo tofauti juu ya sekta ya utalii watabadilika.

Watazinduka na kuona kuwa kila mmoja lazima awe balozi wa kutangaza utalii wa ndani. Kila mmoja anapaswa kuona kuwa juhudi zake na uwepo wake unafanikisha kwa dhati kuwashawishi wageni kutembelea, endapo yeye naye ana uelewa huo.

Kampuni ya KJ inakuja na mtazamo huo wa kutembelea mlima Kilimanjaro katika kipindi ambacho, sekta ya utalii ni moja wapo ya faida kwa nchi zote duniani. Kwa kujitangaza, sekta hiyo itapiga hatua na kukuza uchumi wa Taifa.

Kila mmoja anapaswa kufunga mkanda. Awe mlinzi na balozi wa kweli. Ahoji baada ya kufahamu namna gani nchi inaweza kujitegemea kwa kupitia sekta ya utalii, sambamba na kulinda hifadhi zetu ili ziwe za kuvutia.

Maeneo ya hifadhi yenye mgogoro mkubwa na wananchi, basi kero hizo zitatuliwe kwa haraka ili kuwafanya nao wapende rasilimali hizo.

Kuna baadhi ya wananchi wamekuwa mbogo wanapoona baadhi ya vivutio vilivyopo katika maeneo yao vinachangia kuhangaika kwao ama kufanyiwa vitendo visivyokuwa vya kiungwana.

Kila mmoja ajuwe wajibu wake. Naamini kwa kuanzisha utaratibu huo wa kutembelea hifadhi ya Mlima Kilimanjaro Desemba sita na kufikia kilele chake Desemba tisa, kutachochea ari mpya kwa kila mtu na kupiga hatua ya juu zaidi.

Utalii ni fedha. Kila mtu anayekuwa karibu na eneo husika anaweza kuingiza chochote kitu kutokana na mzunguuko wa pesa, ukiacha zile fedha zinazoingia kwa serikali, hivyo kuufanya uchumi wan chi usonge mbele zaidi.

Haya yanakuja wakati ambao watu wanaamini kuwa kuna kila sababu ya kuweka mkazo katika vivutio vyetu vya utalii, sambamba na kuibua ari kwa watu kwa ajili ya kujipa tabia ya kutembelea kila wanapopata muda kwenye hifadhi za Taifa.

Tukutane wiki ijayo.

0712 053949
0753 806087

Friday, November 16, 2012

Mtaalamu wa urembo mwenye ndoto lukuki




 Mrembo anavyoonekana baada ya kutengenezwa nywele zake na Salumu Mwombeki

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KILA kitu kinahitaji mipango kama kweli dhamira ni kukiletea maendeleo na kutambulika pia kwa jamii mbalimbali.

Wakati hao yapo kwenye sekta zote zikiwamo za sanaa, hata kwenye nyanja ya urembo huko nako ni kawaida.

Ili sekta hiyo iweze kupiga hatua na kufanya kazi kwa mafanikio makubwa, ni wazi juhudi zinahitajika pamoja na mipango kwa jamii husika.

 Salumu Abdallah Mwombeki akiwa kazini kwake.

Katika mazungumzo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, Salum Abdallah Mwombeki, ambaye ni mtaalamu wa upambaji na mitindo kwa akina mama, anamiliki saluni yake maeneo ya Tabata Chama.

Jina la kijana huyo limeenea kwa kiasi kikubwa katika mtaa huo kutokana na umati wa watu kujaa katika saluni kwa ajili ya kujilemba, ukizingatia kijana huyo kwa mikono yake, ana uwezo wa kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi.

“Nashukuru Mungu nimezidi kujipatia mafanikio makubwa kutokana na kuweza kuwamudu vyema kuwalemba akina mama, kuanzia kubuni mavazi ya kuvaa kwa wakati husika, hasa harusi na mengineyo.

“Pia wateja wangu wakija huwashauri mitindo ya kuwasuka kulingana na aina ya vichwa vyao, nikiwa na lengo la kuwapendezesha na kuwafanya waendelee kufanya kazi na mimi, ukizingatia kwamba kazi hii ni kipaji changu,” alisema.

Salum anasema katika kazi hiyo, watu wengi bila kuangalia hadhi na majina yao wamekuwa wakimtafuta kwa ajili ya kufanya kazi nae, jambo ambalo linamfanya aamini atafanikisha mipango ya kufanya kazi hiyo kwa mafanukio makubwa.

Kijana huyo anasema mipango yake ya baadaye ni kupanua biashara zake hizo za saluni ya kike, huku akipanga kumiliki saluni iliyotengenezwa maalum katika gari kubwa na kupaki mahali popote na kuwahudumia wateja wake.

Anasema gari hilo linaweza kuwekewa ratiba ya kuzunguukia maeneo mbalimbali, yakiwamo ya mikoani na kuwapa nafasi watu mbalimbali kuipata huduma yake bila kuangalia wapo mahali gani na wana kipato cha aina gani.

“Kwa mfano gari linaweza kusafiri hadi Mwanza, Arusha, Tanga, Dodoma na kupaki pembeni kwa ajili ya kuwapatia huduma hiyo watu ambao huenda walikuwa wakikosa fursa hiyo kwasababu ya makazi yake kuwa Dar es Salaam,” alisema Salum.

Kijana huyo anasema kwamba saluni yake hadi sasa inafikia mtaji wa Shilingi Milioni 15, ikiwa na vitu vya kila aina vinavyohusu mambo ya urembo wa akina mama.

Anasema mtu anapoingia hapo, hujikuta amebadilika kwa kutengenezwa vizuri nywele zake kwa mitindo ya aina mbalimbali anayoitaka mwenyewe.

Salumu aliyezaliwa miaka kadhaa iliyopita, anasema utundu wa kupamba maharusi, usukaji wa nywele za aina mbalimbali ameupata kutoka kwa Mungu, ingawa anaamini kuwa kipaji cha mama yake mzazi, Madina Nuru, pia kimechangia.

Anasema mama yake alikuwa mjuzi wa usukaji wa vitu mbalimbali, ikiwamo mikeka, jambo ambalo hata yeye limempa mwangaza huo, ambao leo unamfanya aweze kuishi vizuri kwa kutumia kichwa na viungo vyake vya mwili, hasa mikono.

Anasema katika ujuzi wake huo kwenye saluni yake, anashonea nywele za bandia, usukaji wa rasta na mitindo mbalimbali inayotamba au kubuni mingine kwa ajili ya kuwapendezesha zaidi wateja wake wanaofuata huduma yao.

Anasema awali, mwaka 2002 alikuwa akijishughulisha na biashara za kuuza nywele za akina mama, lakini duka lake lilikufa lilipovunjwa na wezi hivyo kumrudisha kutoka hatua kubwa ya kibiashara aliyokuwa nayo.

Jambo hilo lilimfanya aanze kuendeleza kipaji chake cha usukaji kwa ajili pia ya kutafuta maisha, ukizingatia kwamba tayari alishagundua uwezo wake.

Salumu anasema changamoto kubwa kwake ni kwa baadhi ya wanaume wasiomuelewa katika kazi yake hiyo, huku wengineo wakiona hana jipya zaidi ya kumendea wake za watu.

“Hapo nyuma niliwekewa mitego ya kila aina, maana wenye wake zao wanajua tuna uhusiano wowote, wakati sio kweli, ila watu wao wanafuata huduma ya urembo.

“Nashukuru maana leo wamenielewa na wengine wananipigia simu kuwawekea oda wake zao, wakiamini kuwa wamegundua mikono yangu inawapendezesha vizuri wake zao ambao naamini saluni yangu ndio chaguo lao,” alisema.

Mipango yake mingine ni kufungua kampuni ya mitindo itakayohusika na mambo mbalimbali yanayohusu medani ya urembo na mitindo hapa nchini.

Katika kutafuta mbinu za kufanya kazi kisasa na kwa mafanikio makubwa, amekuwa mwepesi kutembelea matamasha mbalimbali, pamoja na matukio ya mitindo katika kumbi za starehe na mahoteli.

Hata hivyo, huko haoni lolote, hasa anapogundua watu hao wanafanya kazi kwa kubahatisha, kiasi cha wengineo kuwaharibu hata wateja wao, wakiwamo maharusi wanaoingia katika matukio ya kukumbukwa duniani.

Kwa sasa saluni yake hajaipa jina zaidi ya wateja wake kuambiana wenyewe, huku kituo cha Tabata Chama, kikiwa maarufu kiasi cha kuleta wateja wapya kila baada ya saa chache.

“Saluni yangu sijaipa jina lakini inaleta wateja wapya, maana wanajua kuwa ramani yao ni kupanda magari yanayokwenda Tabata Kimanga na kushuka kituo cha Chama, ambapo hapo hata mtoto mdogo ananijua na kuifahamu saluni yangu.

“Nashukuru kwa dhati, maana Mungu amenipa kukubalika na kuheshimika kwa kazi yangu, ndio maana hata wasaidizi wangu nimewapa mwongozo wa kumuheshimu mteja anayetoka mbali kwa ajili ya kupata huduma zetu,” alisema Salumu.

Mtaalamu huyo anasema kikubwa anachojivunia ni uwezo wake kujua mbinu gani za kusuka nywele za wateja wake na kutoka wakiwa na furaha, huku gharama zake zikiwa ni nafuu na kuwavutia kila mtu, hivyo watu kutoka mbali na kwenda kwenye saluni yake.

Anasema makubaliano yote ya ufanyaji kazi wake, hufanywa mtu anapokwenda katika saluni yake kwa ajili ya kufanya naye kazi. Salumu anamaliza kwa kuitaka jamii kujua kuwa kazi hiyo ni nzuri na isifikiriwe vyovyote tofauti.

Anasema badala ya vijana kufanya kazi ambazo hazina maadili kwa jamii yake, kuna haja ya kuungwa mkono kwa wale wanaoamua kutafuta riziki kwa njia nzuri kama anavyofanya yeye, huku akiwa na malengo makubwa duniani.

Anamaliza kwa kuwataka watu wanaojihusisha na kazi hiyo ya saluni, kutengeneza nywele na mengineyo kuwa wepesi kujifunza na kufuata ushauri wa waliowazidi kiufundi na kipaji cha ufanyaji kazi ili iwe njia yao ya mafanikio.

Makala haya yameandikwa na Kambi Mbwana.

0712 053949
0753 806087

Simba walikata tawi walilokalia



Haruna Moshi 'Boban'

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
ETI Simba walitangulia na baiskeli ya miti? Yani licha ya kufika mbali, lakini wenye baiskeli nzuri wamewapita kama wamesimama. Kwa bahati mbaya, baada ya kuwapita, wameacha lawama na mabishano kutoka kwa wadau na mashabiki wa timu hiyo.

Simba ipo chini ya mwenyekiti wake, Ismail Adeni Rage, ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Mjini mwenye maneno mengi. Siku zote nimekuwa nikisema, ukitaka kumuadhibu Rage, jichunge usimuangalie usoni.

Anatia huruma mtu huyu. Akiongeza na utundu wake wa kuzungumza, hata jambo la hatari, uongo kwake utakuwa wa kweli na kuona anaonewa. Kwanini nasema hivi? Simba iliweza kuchukua uamuzi wa hatari wa kujenga makundi ndani ya timu yao, licha ya kujipambanua kuwa ina ndoto za kuipaisha juu zaidi timu yao.

Wapo wachezaji wanaonekana ni zaidi kuliko wenzao. Hao hata kama wakisema nini, uongozi na benchi la ufundi litawasikiliza na kuwapigia makofi.

Kwa mfano, hivi karibuni timu ya Simba ilimuadhibu beki wake, Juma Nyosso kwa kumshusha kutoka kwenye kikosi cha kwanza hadi kutakiwa afanyie mazoezi na timu B.

Mbali na Nyosso, Simba pia ilimfungia mshambuliaji wao tegemeo, Haruna Moshi Boban kwa utovu wa nidhamu. Baada ya kuwafungia wachezaji hawa, Simba ilizidi kupoteza thamani yake kutoka kileleni hadi leo ipo nafasi ya tatu.

Mbaya zaidi, aliyekuwa nafasi za chini, Yanga, leo ipo kileleni na kuwaacha Simba wakiendelea kuparuana bila kujua kuwa walikata tawi walilokalia. Sina lengo la kuchekea makosa ya wachezaji hao waliopewa adhabu, lakini tuangalie pia na hali halisi.

Kabla ya kuwaadhibu wachezaji hao, Simba haikufungwa mechi hata moja zaidi ya kutoka sare katika michezo yao kadhaa. Yanga yenye kasi na moyo wa kujisahihisha, inaongoza ligi hiyo kwa kujikusanyia pointi 29.

Anayefuata ni Azam FC yenye pointi 24, huku Simba wao wakiwa na pointi 23, ikiwa ni tofauti ya pointi 6 kwa anayeongoza ligi hiyo. Ni hatari. Simba inahitaji marekebisho pamoja na ushirikiano kwa wachezaji wote.

Simba haihitaji roho moja ya Juma Kaseja ili itetee ubingwa wake. Wala haihitaji nguvu za Emmanuel Okwi ili ifanye vyema. Bali inahitaji nguvu za wachezaji wote bila kuangalia haiba na nguvu za mmoja mmoja.

Simba pia inahitaji utii wa uongozi mzuri wenye kila dhamira ya kuwapatia mafanikio ya kitaifa na Kimataifa. Simba haitaji kuwa na wingi za fedha kwa ajili ya kuwahonga waamuzi zaidi ya kuwaweka kitimu kuwaaminisha kuwa wana deni na timu yao.

Nilijaribu kufuatilia sakata la Nyosso na Boban na kugundua udhaifu mkubwa kutoka kwa benchi la ufundi pamoja na uongozi mzima. Simba haikuwa kitu kimoja zaidi ya jitihada za mchezaji mmoja mmoja, ambaye hata hivyo baadaye waligawanyika tena.

Pamoja na mapungufu yao, lakini wachezaji hawa ni roho ya Simba. Utasema nini kuhusu pumzi na uwezo wa Boban? Vipi kuhusu Nyosso ambaye jitihada zake uwanjani ni mbeleko ya kuibeba timu hiyo katika mechi mbalimbali.

Hivi Boban na Nyosso ndio watovu wa nidhamu peke yao Simba? Haya ni maswali ambayo majibu yake yatazidi kuipasua Simba na kuifanya ishuke zaidi ya hapa. Mwenyekiti wake, Rage na viongozi wenzake waliangalie hili.

Kukata tawi ulilokalia ni ujinga. Kila mtu afanye kazi kwa kuangalia namna ya kuleta maendeleo na sio ubabaishaji usiokuwa na faida kwa Taifa. Timu inayojaribu kuweka mwanya wa kuingiza porojo na malalamiko haiwezi kuwa na maendeleo.

Angalia, hata TP Mazembe inayotesa katika rekodi Afrika Mashariki na Kati, haiwezi kuendeleza mazuri yake kama uongozi utajiendesha kwa mizengwe. Kila mmoja lazima ajuwe mpira ni pesa na unalipa kupita kiasi.

Soka ndio mchezo unaoweza kutengeneza mabilioni ya shilingi katika dakika 90 au 120 za mchezo husika, hasa mechi zenye mguso na ushindani. Hapa kwetu, tunaangalia jinsi fedha nyingi zinavyoingia kwa kuzikutanisha timu za Simba na Yanga.

Utasema nini kuhusu mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa ya Afrika, endapo timu moja wapo ya Tanzania itaingia na kukutana na TP Mazembe, Al Ahly au nyinginezo za Afrika zenye wapenzi wengi nchini mwao?

Ni dhahiri fedha zitaingia nyingi. Lakini, watu hawaingii kwenda kuangalia mipira ya minazi isiyokuwa na metokeo mazuri kwao. Wanaingia wakijua wataburudisha nafasi zao kwa kuangalia ufundi na uchezaji soka wa kuvutia.

Lakini leo hii Simba inayojiandaa kwa michuano ya awali ya Ligi ya Mabingwa, haitakuwa na jipya maana imemaliza mzunguuko wa kwanza wa ligi na matokeo mabaya yanayoanza kuzalisha sumu ya malumbano wao kwa wao.

Matokeo hayo yamesabisha pia Makamu Mwenyekiti wake, Geofrey Kaburu kuambiwa ajiuuzulu bila sababu za kueleweka. Kwa mujibu wa vyanzo vya ndani, Kaburu amekubali kuachia ngazi, ila anasubiri kikao cha Kamati ya Utendaji, kitakachoitishwa hivi karibuni.

Haya ni maajabu. Ukiangalia kwa kina, utagundua kuwa timu hiyo haina mipango na kawaida yao ni kukata tawi inalokalia. Kwanini Kaburu na sio Rage? Kwanini wajiuzulu viongozi na sio benchi la ufundi linalojua mbinu za ushindi au kufungwa?

Kama wamekubali uongozi, basi matatizo yameanzia hatua hiyo, hasa kwa ubabaishaji wa kiongozi kuingilia mambo ya ufundi ya wachezaji wao. Ni rahisi kiongozi kutaka Fulani apangwe kwa sababu anazojua mwenyewe.

Kama hivi ndivyo, basi akiambiwa ajiuzulu hapo hakuna tatizo. Lazima ajiuzulu kwasababu ya ubabaishaji wake. Haya lazima tuyajadili leo.

Ndio ukweli wa mambo. Simba iliyoanza vyema na kushika usukani wa ligi inaweza kuachia ubingwa huo kutokana na mipango yao mibovu na kuingilia hata mambo ya kiufundi.

Hili ukilisema, uongozi utakuwa mbogo na kulazimisha msemaji wao, Ezekiel Kamwaga aitishe mkutano na wana habari kukanusha uchambuzi wa mwandishi. Hayo ni matatizo makubwa na huenda yakaitafuna Simba.

Nimewahi kusema mara kadhaa kuwa timu zetu zinajiendesha kwa ajili ya soka la nyumbani tu, maana Kimataifa, hawana mipango.

Kimataifa mtu anaweza kubashiri kuwa Simba, Yanga ikivuka hatua ya pili atafanya kitu cha kushangaza umati na kweli, mzunguko wa kwanza wakaangukia pua na kushindwa kuendelea.

Ni kwasababu ya ubabaishaji wao. Wamewekeza kwenye soka la mdomoni, kwenye kurasa za mbele au za nyuma za magazeti wakipambwa na kubebwa, hata kama wataalamu wanajua hakuna soka linalochezwa.

Waswahili wana msemo wao, siku zote mbuzi hula kwenye urefu wa kamba yake. Simba yenye migogoro isiyokwisha, kusema itaingia fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni kujipa presha ya bure tu.

Zaidi ya hapo ni kutabiri kuwa haina cha maana itakachovuna zaidi ya kuganga njaa, kuingiza mashabiki wengi katika mechi moja na kutolewa nje katika kila michuano itakayoingia, iwe ni Mabingwa au Kombe la Shirikisho Afrika.

Hali hii itaendelea kudumaza soka letu na kuwafuja wanamichezo wetu. Wachache watakaovuma nje ni kwa bidii zao wenyewe. Wachezaji kama vile Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na wengineo wapo nje kwa bidii zao wenyewe.

Ni nani atajigamba kwamba amechangia kuwapeleka hao nje nchi kucheza soka la kulipwa katika timu ya TP Mazembe ya nchini Kongo?

Na aseme leo. Jibu hakuna. Tena wapo ambao wanapoona wachezaji wao wanatakiwa nje kujaribiwa huwawekea mtimanyongo au kuwafungia kwasababu wanazojua wenyewe.

Ni ajabu na kweli. Haya lazima yasemwe na kupingwa na kila mmoja wetu. Ndio maana nasema, kinachoendelea ndani ya timu ya Simba, ni kuonyesha picha ya kushangaza, hasa pale uongozi ulipojaribu kukata tawi ililokalia.

Naomba kuwasilisha hoja.

0712 053949
0753 806087

Wednesday, November 14, 2012

MGODI UNAOTEMBEA


 Membe anahitaji busara za Kikwete
Bernard Membe

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NI vizuri kuwa mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Mrisho Kikwete, amekiri kuwa upepo mkali wa wimbi la wanaotaka kuteuliwa na chama chao kuwania urais 2015 linatikisa kwa kambi zote kupumuliana kooni.
Pia, akasema kuwa zipo kambi nyingi zaidi, ingawa alisema kuwa kati ya zile zinazowania nafasi hiyo, hakuna hata moja anayoishabikia. Kikwete amesema hayo akijaribu kuwaweka sawa wanachama wa CCM.
 
Kwa kutumia busara zake, aliona endapo atajaribu kukaa upande mmoja leo, ni dhahiri hata nafasi yake aliyokuwa nayo sasa, uenyekiti na urais itakuwa kwenye mtego.
Huku Kikwete akisema hayo, wadau na wachambuzi wa mambo ya kisiasa wameanza kubashiri na kutangaza kambi zinazopigana vikumbo kuiwania nafasi hiyo muhimu na inayoliliwa kwa kiasi kikubwa na wanasiasa wetu.
Kwa mfano, Kambi ya Mbunge wa Monduli na waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, imekuwa kwenye nafasi nzuri, baada ya watu wake wengi kudaiwa kutesa katika chaguzi nyingi za ndani za chama tawala mwaka huu.
Lowassa ametajwa kuwa na mpango wa kugombea urais mwaka 2015, jambo ambalo hata hivyo halijakanushwa na mwanasiasa huyo mwenye nguvu kubwa na ushawishi wa kile anachokitamka kinywani mwake.
Edward Lowassa

Kambi nyingine inayotajwa kuwa na mpango huo ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe. Huyu naye hajakunusha kuwa hana mpango huo, jambo linalozidisha joto la wenye kiu hiyo ya urais.
Zipo kambi nyingine na huenda zikaongezeka zaidi. Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, kila mwanachama ana uweza kuchagua na kuchaguliwa. Wote wana haki sawa na hakuna mwenye haki kuliko mwenzake.
Kwa kuangalia aina ya mchakato mzima wa waliochaguliwa katika chaguzi za ndani za CCM na jinsi baadhi ya wanasiasa hao wanavyofanya mipango yao chini chini, ni dhahiri kuwa Membe anahitaji busara za Kikwete.
Ni mwanasiasa makini na mwenye uwezo wa kupanga hoja. Ana nafasi nzuri na uwezo wa kuongoza Taifa hili, lakini upepo wa chaguzi za ndani haukuwa wake. Kila aliyechaguliwa katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara hakuwa karibu yake.
Vyombo vingi vya habari vilieleza hili kwa marefu kwa ajili ya kuonyesha nani amefanya lile na yupi anajibu kwa ajili ya kujiweka sawa katika mbio hizo za urais zinazoshika kasi na kuibua hisia tofauti kwa wenye mlengo nao.
Membe anategemea ngome moja tu kwa sasa. Ngome hiyo ni mkoa wa Lindi, ambao upo chini ya Profesa wa siasa, mkongwe Ally Mohamed Mtopa, mwenye umri wa miaka 86. Huyu naye alimanusura aanguke.
Watu wengi walikuwa wakimpinga kutokana na ukongwe wake pamoja na kupata hati chafu kwa miaka kadhaa, wakati ni Mwenyekiti wa Halmashauri kwa miaka mingi tu. Waliofuatilia uchaguzi wa CCM Lindi wanajua jinsi mkongwe huyo alivyotumia nguvu ya ziada, akiwa ni silaha kuu ya Membe, ambaye naye alikuwapo kwenye uchaguzi huo.
Kwa kusema hayo, Membe leo hawezi kushindana na watu waliojieneza na kujipenyeza katika kila mkoa. Kama kweli mteule atatokana na kura za wajumbe na uchaguzi huo ukifanywa leo, hakika ushindi kwa mwanasiasa huyo ni ndoto.
Lakini, anaweza kujiweka pazuri kama ataungwa mkono na mwenyekiti wa sasa, ambaye naye ni Rais wa Tanzania, anayemaliza muda wake. Sina lengo la kusema nani ni zaidi ya mwenzake, lakini mchakato na upepo unavyovuma, hakika ni busara za JK ndio zitakazompa ahueni mwanasiasa huyo anayesubiri kuoteshwa ili agombee urais.
Wote ni wana CCM na wana haki ya kugombea nafasi yoyote wanaoyohitaji wao. Na mabosi wakuu ni wanachama, wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho, kabla ya kibao kugeuzwa kwa Watanzania wote wenye jukumu la kupiga kura.
Kwanini nasema busara za Kikwete? Yeye ndio mwenyekiti. Walau anaheshima na mvuto mkubwa kwa wanachama wake. Kama akisema lake, sidhani kama idadi kubwa haitamsikiliza, hivyo kutimiza ndoto za wengine.
Na kama akisema hilo, inaweza kuwa mtego mbaya wa kisiasa wa Kikwete. Kwa wale ambao hawatasikiliza maneno au ushauri huo katika mchakato wa mrithi wake, basi siri hiyo itavuja na kunaswa pia na wabaya wake.
Endapo ndoto za anayetaka kusafiria nyota yake hazitatimia, basi ataingia upya katika kitanzi cha rais ambaye hakuwa na kundi naye, au alikuwa naye kabla ya kuachana dakika za mwisho alimsafishia njia mtu mwingine.
Haya ni mambo ambayo yanaweza kukigawa zaidi chama cha Mapinduzi au kukiweka katika hatua nzuri ya uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2015. Kwa muda mrefu, wanasiasa hao wanaotaka urais wamekuwa wakipita chini chini na kupitisha hoja ambazo kwa kiasi kikubwa ni pigo kwa wapinzani wao.
Katika chaguzi za ndani za chama hicho, karibia wote walikuwa wakirushiana makombora, yakiwamo yale ya kudaiwa baadhi yao kutoa rushwa ili wachaguliwe. Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye, alitumia muda mwingi kulalama kuwa chama chake kimepoteza dira na rushwa ya mtandao imeshika kasi.
Katibu Mkuu, Willson Mukama akamjia juu na kukataa kilio cha mwanachama huyo, ambaye naye ametajwa kuwa na mpango wa kuwania urais, hivyo kuonyesha safari ngumu ya chama hicho hadi pale atakapopatikana mrithi wa Kikwete.
Pamoja na hayo, huo sio mtindo mgeni machoni mwa watu. Kwa chama kama CCM chenye watu wengi na kuungwa mkono na Watanzania, vitendo vya makundi, uhasama, chuki au kusemana vibaya sio vigeni, ingawa hutakiwa viachwe.
Kwa mfano, mara baada ya mrithi wa Kikwete atakapopatikana hapo baadaye, basi wanachama wote wangekuwa kitu kimoja kumfanyia kampeni aliyeteuliwa kwa faida ya CCM inayoingia katika uchaguzi wakati ambao vyama vya upinzani vinazidi kuimarika na kupata hamu kubwa ya kuingia Ikulu na kuwaongoza Watanzania.
Mteule wa Kikwete atapatikana wakati ambao kila kijana ambaye yupo tofauti na vyama vya upinzani, huonekana mbumbumbu, asiyejua baya na zuri kama wanavyodhani baadhi ya watu, wakiwamo viongozi wa vyama hivyo vya siasa.
Lakini haya huwezi kukwepa. Kwa Tanzania hii ambayo inazalisha wanasiasa wenye uchu wa madaraka kuliko wataalamu ni jambo la kushangaza, kama waliokuwa kwenye dhamira ya kuwakosoa watu hao hawatasemwa au kutukanwa.
Hata Membe au kundi lake linaweza kuingia kwenye malumbano na Mgodi Unaotembea, kisa umejaribu kuonyesha picha inavyoendelea ndani ya CCM. Kundi hilo litasema limewakandamiza na kubebwa wapinzani wao.
Pamoja na yote hayo, ukweli utaonekana. Yule mwanachama makini na chaguo halisi la CCM na Tanzania kwa ujumla litapatikana. Tatizo vipi wale ambao hawatateuliwa katika mbio hizo za urais licha ya kufanya kila wawezalo?
Watakubali kushindwa na kuwa kitu kimoja au ndio watahamia upinzani? Watawaunga mkono au ndio watakuwa wanaCCM machoni na rohoni wapinzani wa kutupwa? Vipi Kikwete, mwenyekiti wa CCM, ataunasua mtego huu wa wanaolilia nafasi ya urais 2015?
Hawa wanaotaka nafasi ya urais 2015 watabebwa kweli na makundi yao waliyoyaingiza maeneo yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au vipi?
Tusubiri.
0712 053949
0753 806087

Tuesday, November 13, 2012

Njaa, shida ya maji vitawatoa roho Handeni



Mbunge wa Handeni, Abdallah Kigoda
 
Na Kambi Mbwana, Aliyekuwa Handeni
MAHALI ambapo debe la mahindi linapatikana kwa zaidi ya Shilingi 10,000 hadi 12,000 ni dhahiri kuwa eneo hilo linakabiliwa na njaa kali.

Sehemu ambapo unga wa dona unapatikana kwa Shilingi 800 hadi 1,000 hapo huwezi kusema kuwa wananchi wake hawasumbuliwi na njaa.

Njaa ipo. Njaa inayosababishwa na ukame unaowaathiri watu wengi, wakiwamo hata wananchi wa mjini ambao mara kadhaa maisha yao yote hutegemea watu wa vijijini wanaojihusisha na suala la kilimo.
                                                Mkuu wa Wilaya Handeni, Muhingo Rweyemamu

Kama hivyo ndivyo, basi sishindwi kusema kuwa wakazi na wananchi wa vijiji mbalimbali vya Wilaya ya Handeni wanasumbuliwa na mdudu njaa pamoja na ukame wa hali ya juu, unaokandamiza msumari wa moto.

Msumari huo ni shida ya maji. Wilaya ya Handeni inayopatikana katika Mkoa wa Tanga, wananchi wake wamekuwa wakikabiriwa na matatizo lukuki yakiwamo maji na chakula.

Katika uwepo wangu kwa wiki moja wilayani hapa, nimetembelea katika vijiji mbalimbali kwa ajili ya kuangalia changamoto za kimaisha za watu wake.

Vijiji kama vile Kweingoma, Komsala, Kwamatuku, Misima pamoja na Handeni Mjini, watu wake wanaishi kwa ubangaizaji wa hali ya juu. Ukame umekuwa tatizo lao, hivyo kusababisha bei ya vykalula kupanda juu mno.

Ukiacha Komsala, Kweingoma na Kwamatuku ambapo huduma ya maji kwao sio tatizo, lakini kuanzia Sindeni na kuendelea, hakika hali zao ni mbaya mno. Nadhani katika hilo, kuna kila sababu ya serikali kukaa na kuliangalia suala hilo.

Kuna hatari inaweza kupatikana kwa wakazi hao, maana licha ya ugumu wa maisha waliokuwa nao, lakini pia wanatakiwa watowe kidogo walichokuwa nacho kununulia huduma muhimu za chakula na maji ili wasukume maisha yao.

Kwa mfano, eneo la Kata ya Misima, hapa kuna ukame kupita kiasi. Hakuna huduma nzuri ya maji zaidi ya wananchi kutegemea visima ambavyo wakati mwingine sio salama, huku maji yakiuzwa kwa bei ghali mno.

Ndoo ya maji kuipata katika visima hivyo lazima uwe na zaidi ya 500 hadi 700. Hali hii inaendelea hadi katika Handeni Mjini ambapo ndipo makao Makuu ya wilaya, ikiwa chini ya Mkuu wake wa Wilaya, Muhingo Rweyemamu.

Baadhi ya wakazi wa Handeni wanalalamikia sana ukame huo. Mtu anayeishi chini ya Dola moja, hawezi kumudu gharama kubwa ya maji. Kama atanunua ndoo ya maji kwa mia 500 au 700, unga 1000 maisha yake yatakuwaje?

Watoto wake atawamudu kweli? Haya ni maswali ambayo yamekuwa machungu kwa wakzi na wananchi wa Handeni kwa ujumla. Kama hivyo ndivyo, kuna haja sasa ya serikali na wananchi kwa pamoja kukaa na kuliangalia hili.

Wakazi na wananchi wa Komsala, Kweingoma, Kwamatuku na baadhi ya vijiji vya wilaya ya Handeni vinafaidi mradi wa maji unaotoka katika Wilaya ya Korogwe Mamlaka ya Maji Safi Korogwe (HTM), kuna hatari gani serikali kuupanua zaidi mradi huo?

Wakazi wa maeneo ya barabarani kama vile Sindeni, Misima, Kwenjugo na Handeni Mjini kwanini wasifaidi mradi huo? Hizi ni kero ambazo zinapoendelea kuwakabili wananchi wake wanazidi kuichukia Serikali yake kwa ujumla.

Mwananchi wa kawaida haoni kwanini afurahie serikali yake, wakati anaishi kwa tabu, chakula, maji vikimchoma kupita kiasi. Watu wanagawana majukumu. Mama anautumia muda mwingi kushinda katika visima kuvizia huduma ya maji.

Muda mwingi wa kufanya kazi watu wanautumia kutafuta huduma muhimu za maji na chukula, hivyo kudidimiza zaiid uchumi wao. Huo ndio ukweli wa mambo. Katika kuusema huo, kunahitaji moyo wa chuma na lengo la kujitolea kweli.

Nimekuwa mwepesi kutembelea katika maeneo mbalimbali ya Tanzania kwa ajili ya kujionea na kujifunza mambo ya kimaisha. Katika kuliangalia hilo, baadhi ya kero zinazowasumbua wananchi zinaepukika.

Kinachotakiwa watu ni kutimiza wajibu wao. Kufanya kazi kwa ushirikiano kutoka kwenye Serikali ya Kijiji, Wilaya, Mkoa na Taifa pamoja na wananchi wao. Kwa mfano, vipo baadhi ya vijiji vya wilaya Handeni havina mawasiliano mazuri na watu wao.

Kama hali hii ikiendelea, huwezi kumwambia mwananchi ajitolee walau kuchimba mtaro hatua chache kwa ajili ya kupeleka huduma ya maji kwake na kwa wenzao.

Lakini zamani hilo liliwezekana. Watu walifanya kazi kwa ushirikiano na kujiletea maendeleo yao. Sasa hali hiyo haipo. Ndio maana kila siku wamekuwa wakisumbuliwa na matatizo mengi kiasi cha kuyaweka rehani maisha yao.

Kama mzazi anashindwa kumudu hata hela ya kula, hawezi kugharamia masomo ya mtoto wake, hata kama anajua umuhimu wa elimu. Njaa, ukame unaoleta shida ya maji, yanazidi kuwasumbua watu wa Handeni wenye matatizo lukuki.

Kuna rafiki yangu mmoja alinipigia simu akinijulia hali, akijua kuwa nipo katika wilaya ya Handeni yenye kero za aina mbalimbali.

Baada ya salamu, akaniuliza swali, akitaka kujua siku nilizooga au nilizoshindwa kuoga kwasababu ya shida ya maji. Sikuwa na la kujibu zaidi ya kubaki kimya. Nilifavya hivyo kwakuficha aibu yangu, maana hizo sio habari ngeni.

Hii ni aibu kubwa. Serikali kwa kushirikiana na viongozi wake wanafanya nini juu ya kukabiriana na suala hili? Mbunge wa maisha wa Handeni, Abdallah Omari Kigoda, anafanya nini kupambana na maisha duni kwa wapiga kura wake?

Viongozi wa Chama na Serikali wanaoishi kwa kutegemea mgongo wa wapiga kura wao, wanafanya nini kuliondoa tatizo hili? Je, hili la ukame unaowafanya watu walale njaa wanaliangaliaje kwa ajili ya kuwakomboa wananchi wao?

Ifikie wakati watu tuwe wakweli. Hali wanazoishi wakazi na watu wa Handeni zinahitaji jicho la huruma, kutoka kwa viongozi wake. Naheshimu busara za Mkuu wa Wilaya, Rweyemamu, nikiamini kuwa ni mpambanaji.

Kama hivyo ndivyo, kuna haja ya kupita huku na kule kuangalia kero hizi kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili lililoota mizizi kwa miaka mingi. Bila hata kuweka siasa, jawabu lipatikane kwa ajili ya kuboresha maisha ya watu.

Kama njaa inasababishwa na watu kuuza chakula, basi waelimishwe juu ya kuhifadhi chakula au kulima kisasa.

Katika hilo la kuzuiwa kuuza chakula cha oleo na kesho, watafutiwe njia mbadala za kuwapatia chochote kitu kwa ajili ya kusukuma mbele gurudumu la maisha yao, badala ya kuwa kimya hadi kwenye Uchaguzi Mkuu.

Watendaji wwa serikali wasikae tu ofisini. Watoke nje kwa ajili ya kuangalia changamoto za vijiji mbalimbali vya wilaya ya Handeni, ili kujionea njaa inayowakabili wananchi wake, ukizingatia kuwa hakuna tamko lolote lilitolewa na serikali.

Katika kipindi cha miezi miwili ijayo, debe la mahindi litapatikana kwa Shilingi 15,000 hadi 20,000 maana linapanda kwa kasi ya ajabu. Huu ndio ukweli. Tuambiane kwa ajili ya kutafuta suluhisho la maisha bora kwa kila Mtanzania.

0712 053949
0753 806087