Pages

Pages

Wednesday, November 21, 2012

MGODI UNAOTEMBEA




  Abdallah Kigoda, Mbunge wa Handeni

Watanzania tuchague viongozi watakaotusaidia, si wachuma fedha


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KATIKA mfululizo wa makala zangu kwenye Gazeti la Mtanzania Jumatano, ‘Mgodi Unaotembea’ pamoja na Mtanzania Jumapili, wakati mwingine nakutana na maswali ambayo, ukiyafikiria vizuri, jibu lake linaweza kukuliza.

Ndio, kama wewe unaona uozo wa jambo linalokumiza limeanzia kwa mtu mmoja aliyekuwapo madarakani kwa muda huo, ukweli ni kwamba umeanza zamani. Ingawa si kwa maeneo yote, lakini kwa kiasi kikubwa matatizo haya yanawaumiza Watanzania wengi.

Jumapili ya Novemba 11 niliandika makala iliyokwenda kwa jina la Njaa, shida ya maji vitawatoa roho Handeni. Makala hiyo ilielezea kwa kirefu matatizo yanayowakabiri watu wa Handeni na vitongoji vyake.

Maoni mengi niliyapata. Lakini, huyu alinisikitisha sana. Na huu ndio ujumbe wake ambao nikaamua kuuandikia tena makala kuweka sawa mambo niliyojadili angalau watu wafahamu na kutafutia ufumbuzi.

“Ndugu, Mbwana, Makala yako katika gazeti la Mtanzania Jumapili, Novemba 11 kuhusu tabu ya njaa na shida ya maji Handeni ni ya kusikitisha sana. Mimi nilikaa Handeni mwaka 1982 na 83 wakati wa mbunge Mussa Masomo hali ilikuwa hivyo hivyo.

“Hawa Wabunge wanafanya kazi gani? Naomba unijulishe iwapo Mussa Masomo bado yupo hai. Mimi Method Mhagachi, DSM,” ulimaliza ujumbe uliotumwa na mfuatiliaji mzuri wa gazeti la Mtanzania.

Ujumbe huu uliniumiza kichwa. Hasa baada ya kugundua kuwa kero ninayoiona mimi kubwa kwangu, haijawahi kutoka kwa wakazi na wananchi wa Handeni. Kwa bahati mbaya, si Handeni tu, bali katika maeneo mengi ya Tanzania.

Ingawa juhudi nyingine zimekuwa zikichukuliwa na serikali Kuu, chini ya Rais wake, Jakaya Mrisho Kikwete, lakini wakati mwingine anaangushwa na anaowaamini. Ndio, maana kila wilaya ina fungu lake inapata katika kila bajeti.

Pia kuna mfuko wa jimbo. Mbali na mfuko wa jimbo, bado kuna rasilimali fedha na rasilimali watu ambao kwa pamoja wanaweza kushirikiana kuleta maendeleo ya watu wao.

Katika kuliangalia hilo, jibu lake ni kwamba majimbo hayo yenye matatizo lukuki yansababishwa na wabunge wao wasiokuwa na jipya kwa wananchi wao. Tuliseme hili ingawa litakuwa chungu kwa wasiopenda ukweli.

Wale wanaosema kuwa eti tunaishi mjini habari za mikoani tunazipata wapi? Wakaongeza kuwa harakati zinazofanywa ni kuwachafua watu wachache. Sio kweli. Nimekuwa nikitembelea katika maeneo mengi kujionea hali ya mambo inavyoendelea.

Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, nimetembelea katika mikoa ya Kilimanjaro, Mwanza, Tabora, Singida, Morogoro na Tanga ambapo ndio nyumbani ninapotembelea pia vijiji na Kata zote, kama vile Misima, Kwamatuku, Komkonga, Mkata na kwingineko. Na kama tusipotumia haki ya kukosoana na kuelimishana nchi yetu haiwezi kusonga mbele.

Kati ya wabunge wengi wanaoshinda katika majimbo yao, hakika wanatumia njia za panya kuwapatia nafasi hizo nyeti. Wabunge hawa ni wale ambao wameshakaa katika majimbo yao kwa miaka mingi, huku wakikosa mwelekeo.

Majimbo yao yamekuwa na changamoto nyingi. Wananchi wanaendelea kutaabika, huku wabunge wao wakionekana kwenye luninga katika warsha, semina, ama vikao vya Bunge vinavyowalipa vizuri.

Wabunge ambao kwa miaka mingi tangu alipochaguliwa katika nafasi hiyo, hajaweza kutembelea hata mara moja kwa wananchi waliomuweka madarakani. Haya yote yanasababishwa na umasikini wa kipato na fikra sahihi.

Wananchi wengi hawana uelewa katika mambo ya uraia. Hawajui hata haki zao za msingi za kuwapata viongozi wao.

Umasikini wa fikra pevu ni wa kubaini kuwa kususia kupiga kura au kuchukua mia mbili kama rushwa ya kumuweka mtu madarakani ni hatari katika maisha yake kwa kipindi cha miaka mitano.

Kwa bahati mbaya, masikini yoyote akipewa mia 200 hakika atakubeba mgongoni hadi kufa kwako. Atakusifia kadri anavyoweza. Atakuombea kwa Mungu dhambi zako ziondolewe kwasababu tu amepewa mia 200 ya kununua dagaa.

Hizi ndio changamoto za masikini. Hizi ndio dosari za watu hasa wa mikoani ambao kwa hakika ndio kwenye maisha magumu kupita kiasi. Kwa kusema hayo, nadhani kuna haja sasa ya kila mwananchi kujitambua.

Kwanza wajuwe kura ni haki yao ya msingi. Pili wasijaribu kudanganywa kwa shilingi mia 200 wanazopewa na wenye nazo. Badala yake wahoji au watake mambo ya kimaendeleo katika maeneo ambayo kwa hakika ni kazi ya viongozi wao.

Ifahamike kwamba, kiongozi kufanikisha maisha bora kwa watu wake ni jukumu lake. Hakuwekwa madarakani ili atembelee magari ya kifahari na familia yake bali pia awatumikie mabosi wake, ambao ni wananchi wake.

Lakini kama mtu ameingia madarakani na hana analofanya huyo hafai kama ukoma. Hakuna kuangaliana usoni. Hakuna kuogopana katika kusema mambo ya maana yenye umuhimu na Taifa letu lenye kila rasilimali.

Wananchi wasikubali kupumbazwa na visenti vya kununulia sukari, badala yake wawabane zaidi viongozi wao ili waboreshe maisha yao kwa ujumla.

Waboreshe katika mambo mbalimbali, yakiwamo kilimo bora, miuundo mbinu, huduma za afya, nishati ya umeme ambayo kwa hakika ni yanaweza kupunguza makali ya maisha.

Badala ya kupokea visenti vya kula, wananchi watake kutoka kwa viongozi pembejeo za kilimo na mengineyo yenye kuinua uchumi wao.

Wakati wa uhai wa bibi yangu (Luwaya) katika kijiji chetu cha Komsala, Handeni, mkoani Tanga, nakumbuka hata kuwe na njaa vipi lakini chai kwake ni lazima. Ingawa wapo waliohangaika kutafuta chakula, lakini yeye alikuwa tofauti.

Kumbe alikuwa anaikamua miwa na na kuipika sukari kwa njia ya kienyeji. Hii iliweza kumuondolea bajeti ya sukari kutoka kwa watoto wake. Kazi yake kubwa ilikuwa ni kulima kidogo mazao aliyomudu, ikiwamo miwa, mahindi na mpunga.

Lakini vipi leo. Je, wananchi wanahamasishwa kulima? Kama wapo wanaopenda kulima. Je, changamoto za wadudu, kukosa uwezo wa kununulia pembejeo wanamudu vipi? Serikali yao ya kijiji, Kata, wilaya na Taifa inawajali?

Je, mabadiliko ya tabia nchi, kunakosababisha mvua kutonyesha kwa wakati, wananchi wanaelimishwa juu ya hilo? Nasema hivi maana katika maeneo mengi, wakulima wamekuwa wakilima kila wakati na kuambulia patupu.

Wanalima wakitegemea mvua itanyesha mwezi ujao. Lakini hainyeshi na ikinyesha si kubwa, hivyo kuozesha mbegu zao walizopata kwa shida. Mara kwa mara wanapishana na mvua. Kama hivyo ndivyo, wataalamu wetu wa kilimo ndio wakati wa kufanya kazi zao.

Kama hivyo haitoshi, wakulima waelimishwe pia kupanda mazao yanayostahimili ukame kwa baadhi ya maeneo. Waelimishwe juu ya kuhifadhi vyakula ama kutoiuza ardhi kwa matapeli wanaokwenda kuwalangua kwa njaa zao.

Haya ni mambo ya watalawa. Kama mtu muda mwingi yupo mijini na kusubiri Uchaguzi Mkuu hakika ni majuto makubwa kwa wananchi wake.

Huu ndio ukweli. Vijijini kuna changamoto nyingi sana. Ingawa tunajua kuwa kilimo ndio uti wa mgongo, lakini watu wanaoishi huko hawajaliwi wala kukumbukwa. Viongozi wengi, wakiwamo wabunge wao ni wachumia matumbo yao.

Wanachosubiri Uchaguzi Mkuu na kununua mashati ambayo ndani yake huweka mia 200 ambazo mwananchi huona nyingi na kuwapigia kura zinazowaumiza kwa miaka mitano kila mwaka, ingawa baadaye hudanganya kwamba wanakubalika.

Nani anakubalika kwa wananchi wake? Na aseme leo kuwa anakubalika kwakuwapatia maisha bora wananchi wake. Na aseme alichofanya leo kwa muda aliokaa katika jimbo lake. Kisha watu tupime ukweli na uongo wake.

Hakuna kitu. Bure kabisa. Kama wapo, sio wengi. Baadhi yao hulindwa na visenti vyao. Ndio maanza Mgodi Unaotembea unasema, masikini ukimpa mia 200 atakubeba mgongoni.

Atakuona wewe ni Mungu mtu. Hata kama uwe tapeli, mwizi. Kutokana na hilo, kuna haja ya kuangalia mustakabali wa maisha yetu.

Tukumbushane juu ya kuwachagua wenye dhamira ya kweli ya kuwaongoza Watanzania wenzao na sio wale wenye malengo ya kuvuna utajiri ili wanufaike na familia zao, wakati sisi watoto wetu wanasomea kayumba, huku wakitembea uchi kwa kukosa nguo za kuvaa.

Tukutane wiki ijayo.

0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment