Pages

Pages

Friday, November 16, 2012

Simba walikata tawi walilokalia



Haruna Moshi 'Boban'

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
ETI Simba walitangulia na baiskeli ya miti? Yani licha ya kufika mbali, lakini wenye baiskeli nzuri wamewapita kama wamesimama. Kwa bahati mbaya, baada ya kuwapita, wameacha lawama na mabishano kutoka kwa wadau na mashabiki wa timu hiyo.

Simba ipo chini ya mwenyekiti wake, Ismail Adeni Rage, ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Mjini mwenye maneno mengi. Siku zote nimekuwa nikisema, ukitaka kumuadhibu Rage, jichunge usimuangalie usoni.

Anatia huruma mtu huyu. Akiongeza na utundu wake wa kuzungumza, hata jambo la hatari, uongo kwake utakuwa wa kweli na kuona anaonewa. Kwanini nasema hivi? Simba iliweza kuchukua uamuzi wa hatari wa kujenga makundi ndani ya timu yao, licha ya kujipambanua kuwa ina ndoto za kuipaisha juu zaidi timu yao.

Wapo wachezaji wanaonekana ni zaidi kuliko wenzao. Hao hata kama wakisema nini, uongozi na benchi la ufundi litawasikiliza na kuwapigia makofi.

Kwa mfano, hivi karibuni timu ya Simba ilimuadhibu beki wake, Juma Nyosso kwa kumshusha kutoka kwenye kikosi cha kwanza hadi kutakiwa afanyie mazoezi na timu B.

Mbali na Nyosso, Simba pia ilimfungia mshambuliaji wao tegemeo, Haruna Moshi Boban kwa utovu wa nidhamu. Baada ya kuwafungia wachezaji hawa, Simba ilizidi kupoteza thamani yake kutoka kileleni hadi leo ipo nafasi ya tatu.

Mbaya zaidi, aliyekuwa nafasi za chini, Yanga, leo ipo kileleni na kuwaacha Simba wakiendelea kuparuana bila kujua kuwa walikata tawi walilokalia. Sina lengo la kuchekea makosa ya wachezaji hao waliopewa adhabu, lakini tuangalie pia na hali halisi.

Kabla ya kuwaadhibu wachezaji hao, Simba haikufungwa mechi hata moja zaidi ya kutoka sare katika michezo yao kadhaa. Yanga yenye kasi na moyo wa kujisahihisha, inaongoza ligi hiyo kwa kujikusanyia pointi 29.

Anayefuata ni Azam FC yenye pointi 24, huku Simba wao wakiwa na pointi 23, ikiwa ni tofauti ya pointi 6 kwa anayeongoza ligi hiyo. Ni hatari. Simba inahitaji marekebisho pamoja na ushirikiano kwa wachezaji wote.

Simba haihitaji roho moja ya Juma Kaseja ili itetee ubingwa wake. Wala haihitaji nguvu za Emmanuel Okwi ili ifanye vyema. Bali inahitaji nguvu za wachezaji wote bila kuangalia haiba na nguvu za mmoja mmoja.

Simba pia inahitaji utii wa uongozi mzuri wenye kila dhamira ya kuwapatia mafanikio ya kitaifa na Kimataifa. Simba haitaji kuwa na wingi za fedha kwa ajili ya kuwahonga waamuzi zaidi ya kuwaweka kitimu kuwaaminisha kuwa wana deni na timu yao.

Nilijaribu kufuatilia sakata la Nyosso na Boban na kugundua udhaifu mkubwa kutoka kwa benchi la ufundi pamoja na uongozi mzima. Simba haikuwa kitu kimoja zaidi ya jitihada za mchezaji mmoja mmoja, ambaye hata hivyo baadaye waligawanyika tena.

Pamoja na mapungufu yao, lakini wachezaji hawa ni roho ya Simba. Utasema nini kuhusu pumzi na uwezo wa Boban? Vipi kuhusu Nyosso ambaye jitihada zake uwanjani ni mbeleko ya kuibeba timu hiyo katika mechi mbalimbali.

Hivi Boban na Nyosso ndio watovu wa nidhamu peke yao Simba? Haya ni maswali ambayo majibu yake yatazidi kuipasua Simba na kuifanya ishuke zaidi ya hapa. Mwenyekiti wake, Rage na viongozi wenzake waliangalie hili.

Kukata tawi ulilokalia ni ujinga. Kila mtu afanye kazi kwa kuangalia namna ya kuleta maendeleo na sio ubabaishaji usiokuwa na faida kwa Taifa. Timu inayojaribu kuweka mwanya wa kuingiza porojo na malalamiko haiwezi kuwa na maendeleo.

Angalia, hata TP Mazembe inayotesa katika rekodi Afrika Mashariki na Kati, haiwezi kuendeleza mazuri yake kama uongozi utajiendesha kwa mizengwe. Kila mmoja lazima ajuwe mpira ni pesa na unalipa kupita kiasi.

Soka ndio mchezo unaoweza kutengeneza mabilioni ya shilingi katika dakika 90 au 120 za mchezo husika, hasa mechi zenye mguso na ushindani. Hapa kwetu, tunaangalia jinsi fedha nyingi zinavyoingia kwa kuzikutanisha timu za Simba na Yanga.

Utasema nini kuhusu mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa ya Afrika, endapo timu moja wapo ya Tanzania itaingia na kukutana na TP Mazembe, Al Ahly au nyinginezo za Afrika zenye wapenzi wengi nchini mwao?

Ni dhahiri fedha zitaingia nyingi. Lakini, watu hawaingii kwenda kuangalia mipira ya minazi isiyokuwa na metokeo mazuri kwao. Wanaingia wakijua wataburudisha nafasi zao kwa kuangalia ufundi na uchezaji soka wa kuvutia.

Lakini leo hii Simba inayojiandaa kwa michuano ya awali ya Ligi ya Mabingwa, haitakuwa na jipya maana imemaliza mzunguuko wa kwanza wa ligi na matokeo mabaya yanayoanza kuzalisha sumu ya malumbano wao kwa wao.

Matokeo hayo yamesabisha pia Makamu Mwenyekiti wake, Geofrey Kaburu kuambiwa ajiuuzulu bila sababu za kueleweka. Kwa mujibu wa vyanzo vya ndani, Kaburu amekubali kuachia ngazi, ila anasubiri kikao cha Kamati ya Utendaji, kitakachoitishwa hivi karibuni.

Haya ni maajabu. Ukiangalia kwa kina, utagundua kuwa timu hiyo haina mipango na kawaida yao ni kukata tawi inalokalia. Kwanini Kaburu na sio Rage? Kwanini wajiuzulu viongozi na sio benchi la ufundi linalojua mbinu za ushindi au kufungwa?

Kama wamekubali uongozi, basi matatizo yameanzia hatua hiyo, hasa kwa ubabaishaji wa kiongozi kuingilia mambo ya ufundi ya wachezaji wao. Ni rahisi kiongozi kutaka Fulani apangwe kwa sababu anazojua mwenyewe.

Kama hivi ndivyo, basi akiambiwa ajiuzulu hapo hakuna tatizo. Lazima ajiuzulu kwasababu ya ubabaishaji wake. Haya lazima tuyajadili leo.

Ndio ukweli wa mambo. Simba iliyoanza vyema na kushika usukani wa ligi inaweza kuachia ubingwa huo kutokana na mipango yao mibovu na kuingilia hata mambo ya kiufundi.

Hili ukilisema, uongozi utakuwa mbogo na kulazimisha msemaji wao, Ezekiel Kamwaga aitishe mkutano na wana habari kukanusha uchambuzi wa mwandishi. Hayo ni matatizo makubwa na huenda yakaitafuna Simba.

Nimewahi kusema mara kadhaa kuwa timu zetu zinajiendesha kwa ajili ya soka la nyumbani tu, maana Kimataifa, hawana mipango.

Kimataifa mtu anaweza kubashiri kuwa Simba, Yanga ikivuka hatua ya pili atafanya kitu cha kushangaza umati na kweli, mzunguko wa kwanza wakaangukia pua na kushindwa kuendelea.

Ni kwasababu ya ubabaishaji wao. Wamewekeza kwenye soka la mdomoni, kwenye kurasa za mbele au za nyuma za magazeti wakipambwa na kubebwa, hata kama wataalamu wanajua hakuna soka linalochezwa.

Waswahili wana msemo wao, siku zote mbuzi hula kwenye urefu wa kamba yake. Simba yenye migogoro isiyokwisha, kusema itaingia fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni kujipa presha ya bure tu.

Zaidi ya hapo ni kutabiri kuwa haina cha maana itakachovuna zaidi ya kuganga njaa, kuingiza mashabiki wengi katika mechi moja na kutolewa nje katika kila michuano itakayoingia, iwe ni Mabingwa au Kombe la Shirikisho Afrika.

Hali hii itaendelea kudumaza soka letu na kuwafuja wanamichezo wetu. Wachache watakaovuma nje ni kwa bidii zao wenyewe. Wachezaji kama vile Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na wengineo wapo nje kwa bidii zao wenyewe.

Ni nani atajigamba kwamba amechangia kuwapeleka hao nje nchi kucheza soka la kulipwa katika timu ya TP Mazembe ya nchini Kongo?

Na aseme leo. Jibu hakuna. Tena wapo ambao wanapoona wachezaji wao wanatakiwa nje kujaribiwa huwawekea mtimanyongo au kuwafungia kwasababu wanazojua wenyewe.

Ni ajabu na kweli. Haya lazima yasemwe na kupingwa na kila mmoja wetu. Ndio maana nasema, kinachoendelea ndani ya timu ya Simba, ni kuonyesha picha ya kushangaza, hasa pale uongozi ulipojaribu kukata tawi ililokalia.

Naomba kuwasilisha hoja.

0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment