Pages

Pages

Wednesday, November 14, 2012

MGODI UNAOTEMBEA


 Membe anahitaji busara za Kikwete
Bernard Membe

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NI vizuri kuwa mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Mrisho Kikwete, amekiri kuwa upepo mkali wa wimbi la wanaotaka kuteuliwa na chama chao kuwania urais 2015 linatikisa kwa kambi zote kupumuliana kooni.
Pia, akasema kuwa zipo kambi nyingi zaidi, ingawa alisema kuwa kati ya zile zinazowania nafasi hiyo, hakuna hata moja anayoishabikia. Kikwete amesema hayo akijaribu kuwaweka sawa wanachama wa CCM.
 
Kwa kutumia busara zake, aliona endapo atajaribu kukaa upande mmoja leo, ni dhahiri hata nafasi yake aliyokuwa nayo sasa, uenyekiti na urais itakuwa kwenye mtego.
Huku Kikwete akisema hayo, wadau na wachambuzi wa mambo ya kisiasa wameanza kubashiri na kutangaza kambi zinazopigana vikumbo kuiwania nafasi hiyo muhimu na inayoliliwa kwa kiasi kikubwa na wanasiasa wetu.
Kwa mfano, Kambi ya Mbunge wa Monduli na waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, imekuwa kwenye nafasi nzuri, baada ya watu wake wengi kudaiwa kutesa katika chaguzi nyingi za ndani za chama tawala mwaka huu.
Lowassa ametajwa kuwa na mpango wa kugombea urais mwaka 2015, jambo ambalo hata hivyo halijakanushwa na mwanasiasa huyo mwenye nguvu kubwa na ushawishi wa kile anachokitamka kinywani mwake.
Edward Lowassa

Kambi nyingine inayotajwa kuwa na mpango huo ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe. Huyu naye hajakunusha kuwa hana mpango huo, jambo linalozidisha joto la wenye kiu hiyo ya urais.
Zipo kambi nyingine na huenda zikaongezeka zaidi. Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, kila mwanachama ana uweza kuchagua na kuchaguliwa. Wote wana haki sawa na hakuna mwenye haki kuliko mwenzake.
Kwa kuangalia aina ya mchakato mzima wa waliochaguliwa katika chaguzi za ndani za CCM na jinsi baadhi ya wanasiasa hao wanavyofanya mipango yao chini chini, ni dhahiri kuwa Membe anahitaji busara za Kikwete.
Ni mwanasiasa makini na mwenye uwezo wa kupanga hoja. Ana nafasi nzuri na uwezo wa kuongoza Taifa hili, lakini upepo wa chaguzi za ndani haukuwa wake. Kila aliyechaguliwa katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara hakuwa karibu yake.
Vyombo vingi vya habari vilieleza hili kwa marefu kwa ajili ya kuonyesha nani amefanya lile na yupi anajibu kwa ajili ya kujiweka sawa katika mbio hizo za urais zinazoshika kasi na kuibua hisia tofauti kwa wenye mlengo nao.
Membe anategemea ngome moja tu kwa sasa. Ngome hiyo ni mkoa wa Lindi, ambao upo chini ya Profesa wa siasa, mkongwe Ally Mohamed Mtopa, mwenye umri wa miaka 86. Huyu naye alimanusura aanguke.
Watu wengi walikuwa wakimpinga kutokana na ukongwe wake pamoja na kupata hati chafu kwa miaka kadhaa, wakati ni Mwenyekiti wa Halmashauri kwa miaka mingi tu. Waliofuatilia uchaguzi wa CCM Lindi wanajua jinsi mkongwe huyo alivyotumia nguvu ya ziada, akiwa ni silaha kuu ya Membe, ambaye naye alikuwapo kwenye uchaguzi huo.
Kwa kusema hayo, Membe leo hawezi kushindana na watu waliojieneza na kujipenyeza katika kila mkoa. Kama kweli mteule atatokana na kura za wajumbe na uchaguzi huo ukifanywa leo, hakika ushindi kwa mwanasiasa huyo ni ndoto.
Lakini, anaweza kujiweka pazuri kama ataungwa mkono na mwenyekiti wa sasa, ambaye naye ni Rais wa Tanzania, anayemaliza muda wake. Sina lengo la kusema nani ni zaidi ya mwenzake, lakini mchakato na upepo unavyovuma, hakika ni busara za JK ndio zitakazompa ahueni mwanasiasa huyo anayesubiri kuoteshwa ili agombee urais.
Wote ni wana CCM na wana haki ya kugombea nafasi yoyote wanaoyohitaji wao. Na mabosi wakuu ni wanachama, wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho, kabla ya kibao kugeuzwa kwa Watanzania wote wenye jukumu la kupiga kura.
Kwanini nasema busara za Kikwete? Yeye ndio mwenyekiti. Walau anaheshima na mvuto mkubwa kwa wanachama wake. Kama akisema lake, sidhani kama idadi kubwa haitamsikiliza, hivyo kutimiza ndoto za wengine.
Na kama akisema hilo, inaweza kuwa mtego mbaya wa kisiasa wa Kikwete. Kwa wale ambao hawatasikiliza maneno au ushauri huo katika mchakato wa mrithi wake, basi siri hiyo itavuja na kunaswa pia na wabaya wake.
Endapo ndoto za anayetaka kusafiria nyota yake hazitatimia, basi ataingia upya katika kitanzi cha rais ambaye hakuwa na kundi naye, au alikuwa naye kabla ya kuachana dakika za mwisho alimsafishia njia mtu mwingine.
Haya ni mambo ambayo yanaweza kukigawa zaidi chama cha Mapinduzi au kukiweka katika hatua nzuri ya uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2015. Kwa muda mrefu, wanasiasa hao wanaotaka urais wamekuwa wakipita chini chini na kupitisha hoja ambazo kwa kiasi kikubwa ni pigo kwa wapinzani wao.
Katika chaguzi za ndani za chama hicho, karibia wote walikuwa wakirushiana makombora, yakiwamo yale ya kudaiwa baadhi yao kutoa rushwa ili wachaguliwe. Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye, alitumia muda mwingi kulalama kuwa chama chake kimepoteza dira na rushwa ya mtandao imeshika kasi.
Katibu Mkuu, Willson Mukama akamjia juu na kukataa kilio cha mwanachama huyo, ambaye naye ametajwa kuwa na mpango wa kuwania urais, hivyo kuonyesha safari ngumu ya chama hicho hadi pale atakapopatikana mrithi wa Kikwete.
Pamoja na hayo, huo sio mtindo mgeni machoni mwa watu. Kwa chama kama CCM chenye watu wengi na kuungwa mkono na Watanzania, vitendo vya makundi, uhasama, chuki au kusemana vibaya sio vigeni, ingawa hutakiwa viachwe.
Kwa mfano, mara baada ya mrithi wa Kikwete atakapopatikana hapo baadaye, basi wanachama wote wangekuwa kitu kimoja kumfanyia kampeni aliyeteuliwa kwa faida ya CCM inayoingia katika uchaguzi wakati ambao vyama vya upinzani vinazidi kuimarika na kupata hamu kubwa ya kuingia Ikulu na kuwaongoza Watanzania.
Mteule wa Kikwete atapatikana wakati ambao kila kijana ambaye yupo tofauti na vyama vya upinzani, huonekana mbumbumbu, asiyejua baya na zuri kama wanavyodhani baadhi ya watu, wakiwamo viongozi wa vyama hivyo vya siasa.
Lakini haya huwezi kukwepa. Kwa Tanzania hii ambayo inazalisha wanasiasa wenye uchu wa madaraka kuliko wataalamu ni jambo la kushangaza, kama waliokuwa kwenye dhamira ya kuwakosoa watu hao hawatasemwa au kutukanwa.
Hata Membe au kundi lake linaweza kuingia kwenye malumbano na Mgodi Unaotembea, kisa umejaribu kuonyesha picha inavyoendelea ndani ya CCM. Kundi hilo litasema limewakandamiza na kubebwa wapinzani wao.
Pamoja na yote hayo, ukweli utaonekana. Yule mwanachama makini na chaguo halisi la CCM na Tanzania kwa ujumla litapatikana. Tatizo vipi wale ambao hawatateuliwa katika mbio hizo za urais licha ya kufanya kila wawezalo?
Watakubali kushindwa na kuwa kitu kimoja au ndio watahamia upinzani? Watawaunga mkono au ndio watakuwa wanaCCM machoni na rohoni wapinzani wa kutupwa? Vipi Kikwete, mwenyekiti wa CCM, ataunasua mtego huu wa wanaolilia nafasi ya urais 2015?
Hawa wanaotaka nafasi ya urais 2015 watabebwa kweli na makundi yao waliyoyaingiza maeneo yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au vipi?
Tusubiri.
0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment