Pages

Pages

Tuesday, November 13, 2012

Njaa, shida ya maji vitawatoa roho Handeni



Mbunge wa Handeni, Abdallah Kigoda
 
Na Kambi Mbwana, Aliyekuwa Handeni
MAHALI ambapo debe la mahindi linapatikana kwa zaidi ya Shilingi 10,000 hadi 12,000 ni dhahiri kuwa eneo hilo linakabiliwa na njaa kali.

Sehemu ambapo unga wa dona unapatikana kwa Shilingi 800 hadi 1,000 hapo huwezi kusema kuwa wananchi wake hawasumbuliwi na njaa.

Njaa ipo. Njaa inayosababishwa na ukame unaowaathiri watu wengi, wakiwamo hata wananchi wa mjini ambao mara kadhaa maisha yao yote hutegemea watu wa vijijini wanaojihusisha na suala la kilimo.
                                                Mkuu wa Wilaya Handeni, Muhingo Rweyemamu

Kama hivyo ndivyo, basi sishindwi kusema kuwa wakazi na wananchi wa vijiji mbalimbali vya Wilaya ya Handeni wanasumbuliwa na mdudu njaa pamoja na ukame wa hali ya juu, unaokandamiza msumari wa moto.

Msumari huo ni shida ya maji. Wilaya ya Handeni inayopatikana katika Mkoa wa Tanga, wananchi wake wamekuwa wakikabiriwa na matatizo lukuki yakiwamo maji na chakula.

Katika uwepo wangu kwa wiki moja wilayani hapa, nimetembelea katika vijiji mbalimbali kwa ajili ya kuangalia changamoto za kimaisha za watu wake.

Vijiji kama vile Kweingoma, Komsala, Kwamatuku, Misima pamoja na Handeni Mjini, watu wake wanaishi kwa ubangaizaji wa hali ya juu. Ukame umekuwa tatizo lao, hivyo kusababisha bei ya vykalula kupanda juu mno.

Ukiacha Komsala, Kweingoma na Kwamatuku ambapo huduma ya maji kwao sio tatizo, lakini kuanzia Sindeni na kuendelea, hakika hali zao ni mbaya mno. Nadhani katika hilo, kuna kila sababu ya serikali kukaa na kuliangalia suala hilo.

Kuna hatari inaweza kupatikana kwa wakazi hao, maana licha ya ugumu wa maisha waliokuwa nao, lakini pia wanatakiwa watowe kidogo walichokuwa nacho kununulia huduma muhimu za chakula na maji ili wasukume maisha yao.

Kwa mfano, eneo la Kata ya Misima, hapa kuna ukame kupita kiasi. Hakuna huduma nzuri ya maji zaidi ya wananchi kutegemea visima ambavyo wakati mwingine sio salama, huku maji yakiuzwa kwa bei ghali mno.

Ndoo ya maji kuipata katika visima hivyo lazima uwe na zaidi ya 500 hadi 700. Hali hii inaendelea hadi katika Handeni Mjini ambapo ndipo makao Makuu ya wilaya, ikiwa chini ya Mkuu wake wa Wilaya, Muhingo Rweyemamu.

Baadhi ya wakazi wa Handeni wanalalamikia sana ukame huo. Mtu anayeishi chini ya Dola moja, hawezi kumudu gharama kubwa ya maji. Kama atanunua ndoo ya maji kwa mia 500 au 700, unga 1000 maisha yake yatakuwaje?

Watoto wake atawamudu kweli? Haya ni maswali ambayo yamekuwa machungu kwa wakzi na wananchi wa Handeni kwa ujumla. Kama hivyo ndivyo, kuna haja sasa ya serikali na wananchi kwa pamoja kukaa na kuliangalia hili.

Wakazi na wananchi wa Komsala, Kweingoma, Kwamatuku na baadhi ya vijiji vya wilaya ya Handeni vinafaidi mradi wa maji unaotoka katika Wilaya ya Korogwe Mamlaka ya Maji Safi Korogwe (HTM), kuna hatari gani serikali kuupanua zaidi mradi huo?

Wakazi wa maeneo ya barabarani kama vile Sindeni, Misima, Kwenjugo na Handeni Mjini kwanini wasifaidi mradi huo? Hizi ni kero ambazo zinapoendelea kuwakabili wananchi wake wanazidi kuichukia Serikali yake kwa ujumla.

Mwananchi wa kawaida haoni kwanini afurahie serikali yake, wakati anaishi kwa tabu, chakula, maji vikimchoma kupita kiasi. Watu wanagawana majukumu. Mama anautumia muda mwingi kushinda katika visima kuvizia huduma ya maji.

Muda mwingi wa kufanya kazi watu wanautumia kutafuta huduma muhimu za maji na chukula, hivyo kudidimiza zaiid uchumi wao. Huo ndio ukweli wa mambo. Katika kuusema huo, kunahitaji moyo wa chuma na lengo la kujitolea kweli.

Nimekuwa mwepesi kutembelea katika maeneo mbalimbali ya Tanzania kwa ajili ya kujionea na kujifunza mambo ya kimaisha. Katika kuliangalia hilo, baadhi ya kero zinazowasumbua wananchi zinaepukika.

Kinachotakiwa watu ni kutimiza wajibu wao. Kufanya kazi kwa ushirikiano kutoka kwenye Serikali ya Kijiji, Wilaya, Mkoa na Taifa pamoja na wananchi wao. Kwa mfano, vipo baadhi ya vijiji vya wilaya Handeni havina mawasiliano mazuri na watu wao.

Kama hali hii ikiendelea, huwezi kumwambia mwananchi ajitolee walau kuchimba mtaro hatua chache kwa ajili ya kupeleka huduma ya maji kwake na kwa wenzao.

Lakini zamani hilo liliwezekana. Watu walifanya kazi kwa ushirikiano na kujiletea maendeleo yao. Sasa hali hiyo haipo. Ndio maana kila siku wamekuwa wakisumbuliwa na matatizo mengi kiasi cha kuyaweka rehani maisha yao.

Kama mzazi anashindwa kumudu hata hela ya kula, hawezi kugharamia masomo ya mtoto wake, hata kama anajua umuhimu wa elimu. Njaa, ukame unaoleta shida ya maji, yanazidi kuwasumbua watu wa Handeni wenye matatizo lukuki.

Kuna rafiki yangu mmoja alinipigia simu akinijulia hali, akijua kuwa nipo katika wilaya ya Handeni yenye kero za aina mbalimbali.

Baada ya salamu, akaniuliza swali, akitaka kujua siku nilizooga au nilizoshindwa kuoga kwasababu ya shida ya maji. Sikuwa na la kujibu zaidi ya kubaki kimya. Nilifavya hivyo kwakuficha aibu yangu, maana hizo sio habari ngeni.

Hii ni aibu kubwa. Serikali kwa kushirikiana na viongozi wake wanafanya nini juu ya kukabiriana na suala hili? Mbunge wa maisha wa Handeni, Abdallah Omari Kigoda, anafanya nini kupambana na maisha duni kwa wapiga kura wake?

Viongozi wa Chama na Serikali wanaoishi kwa kutegemea mgongo wa wapiga kura wao, wanafanya nini kuliondoa tatizo hili? Je, hili la ukame unaowafanya watu walale njaa wanaliangaliaje kwa ajili ya kuwakomboa wananchi wao?

Ifikie wakati watu tuwe wakweli. Hali wanazoishi wakazi na watu wa Handeni zinahitaji jicho la huruma, kutoka kwa viongozi wake. Naheshimu busara za Mkuu wa Wilaya, Rweyemamu, nikiamini kuwa ni mpambanaji.

Kama hivyo ndivyo, kuna haja ya kupita huku na kule kuangalia kero hizi kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili lililoota mizizi kwa miaka mingi. Bila hata kuweka siasa, jawabu lipatikane kwa ajili ya kuboresha maisha ya watu.

Kama njaa inasababishwa na watu kuuza chakula, basi waelimishwe juu ya kuhifadhi chakula au kulima kisasa.

Katika hilo la kuzuiwa kuuza chakula cha oleo na kesho, watafutiwe njia mbadala za kuwapatia chochote kitu kwa ajili ya kusukuma mbele gurudumu la maisha yao, badala ya kuwa kimya hadi kwenye Uchaguzi Mkuu.

Watendaji wwa serikali wasikae tu ofisini. Watoke nje kwa ajili ya kuangalia changamoto za vijiji mbalimbali vya wilaya ya Handeni, ili kujionea njaa inayowakabili wananchi wake, ukizingatia kuwa hakuna tamko lolote lilitolewa na serikali.

Katika kipindi cha miezi miwili ijayo, debe la mahindi litapatikana kwa Shilingi 15,000 hadi 20,000 maana linapanda kwa kasi ya ajabu. Huu ndio ukweli. Tuambiane kwa ajili ya kutafuta suluhisho la maisha bora kwa kila Mtanzania.

0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment