Pages

Pages

Monday, November 19, 2012

KJ Traders na ziara ya Mlima Kilimanjaro





Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Generali, George Waitara, kulia akizungumzia ziara ya Mlima Kimanjaro. Anayefuata kushoto kwake ni Joseph Kitani, Mratibu Mkuu wa safari hiyo kutoka Kampuni ya KJ Traders ya jijini Dar es Salaam.

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WATANZANIA wengi wamejipa ujinga wa kuamini kuwa jukumu la kutembelea hifadhi mbalimbali lipo kwa wageni na sio wazalendo wenyewe.

Hao wanagoma kabisa kuweka taratibu za kutembelea hifadhi za Taifa kwa ajili ya kuangalia vivutio vya utalii, hivyo kueneza sumu hiyo kwa vizazi vyao.


Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki
 
Mtoto ambae hajawahi kupewa ratiba ya kufanya matembezi katika vivutio walau mara tatu kwa mwaka, kamwe hawezi kubadilisha taratibu hizo hata pale anapokuwa kwenye familia yake, anapotoka katika mikono ya wazazi.

Hilo ni tatizo kubwa. Linakuwa siku hadi siku. Hakuna mwenye mapenzi mema na moyo wa kujifunza vitu vinavyohusu historia ya maisha yao. Ni wageni kila wakati, kiasi cha kushindwa kujua mahala gani kuna vitu vya kustaajibisha.

Kwa mfano, unaweza kushangaa kusikia wapo watu wanaoishi karibu na Mlima Kilimanjaro, lakini hawajawahi hata siku moja kupanga namna ya kuupanda mlima huo mrefu Barani Afrika, badala yake wanasuburi wazungu waende kutalii.

Kwa bahati mbaya, wazawa wanagoma kuzunguukia hifadhi hizo kwa visingizio visivyokuwa na mashiko, maana katika kufanikisha suala hilo la kukuza utalii wa ndani, utaratibu mzuri umewekwa na gharama nafuu kwa kila Mtanzania.

Nadhani ni hapo unapokaa na kupongeza mawazo ya kutangaza sekta zetu za utalii, kubuni mbinu mpya za kuwafikishia ujumbe Watanzania juu ya kuweka utaratibu wa kutembelea katika hifadhi zao, ukiwamo Mlima Kilimanjaro.

Mlima ambao unasisimua kuutazama katika picha na kuleta hamu kubwa ya kuupanda, ukizingatia kwamba una historia kubwa ya maisha ya Tanzania na watu wake.

Nasema haya baada ya kuona juhudi za Kampuni ya KJ Traders kuandaa matembezi ya mlima Kilimanjaro, Desemba sita mwaka huu kwa ajili ya kutangaza sekta ya utalii wa ndani, huku wakishirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).

Matembezi hayo yamepangwa kuzinduliwa na Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Generali George Waitara, yakiwa na lengo na kutangaza mlima huo na kuamsha hisia mpya kwa Watanzania kwa ajili ya kupenda vitu vyao.

Mratibu Mkuu wa matembezi hayo ni Joseph Kitina, akileta matumaini na funzo kwa kila Mtanzania kuona kuwa ana deni la kupanga ratiba ya kutembelea sehemu mbalimbali za nchi katika hali ya kuangalia vivutio vyetu vya utalii.

Endapo tutakuwa tunaelewa thamani ya vitu vyetu, hata wale wanaokuja wataweka mkazo zaidi hivyo kuvutia makundi ya watalii watakaoingia nchini.

Kama Watanzania wenyewe watashindwa kuweka mbinu za kutangaza vivutio vyao, hakuna anayeweza kubadilisha mtazamo wao. Ndio maana kila juhudi zinazofanywa kwa ajili ya kutangaza utalii wa ndani zinakwama.

Jukumu la kutembelea vivutio vyetu visiachwe kwa wageni tu, hivyo kuna haja ya kushirikiana kwa pamoja na wadau wa sekta ya utalii, wakiwamo KJ Traders.

Huo ndio ukweli. Yoyote yule anayekwenda nje ya eneo lake na kukaa walau kwa saa 24, basi huyo ni mtalii. Haijalishi anakwenda huko kufanya kitu gani. Iwe ni kutembelea hifadhi za Taifa, kuhudhuria mikutano au kufanya biashara zake.

Tofauti ya mtalii wa ndani ni kuwa huyu analipia gharama ndogo kwa pesa za ndani, wakati mtalii kutoka nje ya nchi, hawa hulipia kwa pesa za kigeni. Mtu anapokuwa kwenye shughuli hizo za kitalii, kunakuwa na faida kubwa kwake na kwa Taifa husika.

Kazi kama vile upigaji wa picha, utafiti wa vitu mbali mbali, ukiwamo miti na wanyama, au kuangalia mbuga za wanyama, ni kati ya mambo ambayo mtu anapoyafanya eneo husika, basi amekuwa katika msingi ule wa utalii.

Wakati hayo yakiweza kufanywa na kila mdau wakiwamo hao KJ Traders kwa kushirikiana na TTB na Wizara husika ya Maliasili na Utalii, Tanzania imejaliwa kuwa na vivutio vingi vya Utalii katika kila mkoa na kuleta faida kubwa.

Ukiacha huo Mlima wa Kilimanjaro ambao baadhi yao huthubutu kusema upo katika nchi jirani ya Kenya, lakini Tanzania pia imejaliwa kuwa na maeneo mengi ambayo kila mmoja kwa nafasi yake yanaweza kuiletea tija nchi yao.

Hifadhi kama vile Ngorongoro, Mikumi, Hifadhi ya Ziwa Manyara, Ziwa Ruaha, Selous na mengineyo mengi ni kati ya sehemu ambazo zikitangazwa kwa kiasi kikubwa na Watanzania wenyewe, nchi inaweza kuingiza fedha nyingi za kigeni.

Lakini sisi wenyewe tukidharau thamani zetu zilizozaga katika mikoa mbalimbali, hakika hatuwezi kusonga mbele kwa lolote. Huo ndio ukweli. Katika kuusema, natumaini pia wale wenye mtazamo tofauti juu ya sekta ya utalii watabadilika.

Watazinduka na kuona kuwa kila mmoja lazima awe balozi wa kutangaza utalii wa ndani. Kila mmoja anapaswa kuona kuwa juhudi zake na uwepo wake unafanikisha kwa dhati kuwashawishi wageni kutembelea, endapo yeye naye ana uelewa huo.

Kampuni ya KJ inakuja na mtazamo huo wa kutembelea mlima Kilimanjaro katika kipindi ambacho, sekta ya utalii ni moja wapo ya faida kwa nchi zote duniani. Kwa kujitangaza, sekta hiyo itapiga hatua na kukuza uchumi wa Taifa.

Kila mmoja anapaswa kufunga mkanda. Awe mlinzi na balozi wa kweli. Ahoji baada ya kufahamu namna gani nchi inaweza kujitegemea kwa kupitia sekta ya utalii, sambamba na kulinda hifadhi zetu ili ziwe za kuvutia.

Maeneo ya hifadhi yenye mgogoro mkubwa na wananchi, basi kero hizo zitatuliwe kwa haraka ili kuwafanya nao wapende rasilimali hizo.

Kuna baadhi ya wananchi wamekuwa mbogo wanapoona baadhi ya vivutio vilivyopo katika maeneo yao vinachangia kuhangaika kwao ama kufanyiwa vitendo visivyokuwa vya kiungwana.

Kila mmoja ajuwe wajibu wake. Naamini kwa kuanzisha utaratibu huo wa kutembelea hifadhi ya Mlima Kilimanjaro Desemba sita na kufikia kilele chake Desemba tisa, kutachochea ari mpya kwa kila mtu na kupiga hatua ya juu zaidi.

Utalii ni fedha. Kila mtu anayekuwa karibu na eneo husika anaweza kuingiza chochote kitu kutokana na mzunguuko wa pesa, ukiacha zile fedha zinazoingia kwa serikali, hivyo kuufanya uchumi wan chi usonge mbele zaidi.

Haya yanakuja wakati ambao watu wanaamini kuwa kuna kila sababu ya kuweka mkazo katika vivutio vyetu vya utalii, sambamba na kuibua ari kwa watu kwa ajili ya kujipa tabia ya kutembelea kila wanapopata muda kwenye hifadhi za Taifa.

Tukutane wiki ijayo.

0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment