Pages

Pages

Monday, November 26, 2012

Asha Baraka asifia vipaji Twanga Pepeta



 Asha Baraka, Mkurugenzi wa Twanga Pepeta

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MKURUGENZI wa bendi ya The African Stars, Twanga Pepeta, Asha Baraka, amesema bendi yake ina wanamuziki wengi kiasi kwamba wengine wanashindwa kupanda jukwaani zaidi ya mara tatu katika kumbi nyingi wanazofanya shoo.

Hiyo ni kauli ya kwanza kutolewa na mwanamama huyo ambaye tangu kutangaza kuondoka kwa nguli wa muziki wa dansi nchini kwenye bendi hiyo, Mwinjuma Muumini, Asha hajasikika akisema lolote juu ya kuhama kwa mkali huyo.

Akizungumza mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Asha alisema kwamba bendi yake ina waimbaji wengi na hawawezi kuwa na upungufu wa aina yoyote katika safu zao, licha ya kuhama tena kwa Muumini.

Alisema wapo waimbaji wanaopanda jukwaani mara moja kwa siku katika shoo zao, hivyo ni wazi kuwa wengine wanachukulia nafasi hiyo kutafuta mahali kwa kuonyesha makali yao zaidi katika ramani ya muziki wa dansi nchini.

“Mpaka sasa wapo waimbaji zaidi ya watano ambao ni mahiri na wana mashabiki wengi, akiwamo Kalala Junior, Dogo Rama, Salehe Kupaza, Badi Bakule, Luiza Mbutu, Janeth Isinika, Amigo Ras na wengine wenye wapenzi lukuki.

“Naamini bila hata kuangalia nani hayupo kwetu, tunapaswa kujivunia kuwa nao waliokuwapo kwasababu wanamuziki wanapokuwa wengi zaidi, lazima wachache wao waimbe wimbo mmoja shoo nzima,” alisema.

Twanga Pepeta ni miongoni mwa bendi zinazofanya vyema katika tasnia ya muziki wa dansi hapa nchini, ikiwa na nyimbo nzuri zinazopendwa na wengi, ukiwamo wa ‘Shamba la Twanga’ unaozidi kuiweka juu bendi hiyo.

No comments:

Post a Comment