Picha juu nis: Mkuu wa kitengo cha Udhamini wa Vodacom Tanzania Tanzania, George Rwehumbiza.
Pichani; Meneja Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Salum Mwalim.
Picha ya Yanga na Simba wakiwa uwanjani.
Waandishi wa habari wakiwa kazini, hawa ni wadau wakubwa wanaostahili kuthaminiwa na kupigania maendeleo ya michezo Tanzania.
Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden RageMwenyekiti wa klabu ya Yanga, Lloyd Nchunga
.Mohamed Mharizo akiwa na Zaituni Kibwana. Hawa ni wadau wakubwa wa michezo wakiandikia magazeti ya New Habari (2006) Ltd, Mtanzania, Dimba, Rai, Bingwa na The African. Kwa ushirikiano wa wote wanaweza kuendeleza michezo Tanzania. Mungu ibariki Tanzania.
UNAFIKI WA WADAU WA MICHEZO NI HATARI KWA TAIFA
HUWA najiuliza uwapi umuhimu wa mtu kujiita mdau wa michezo, hali ya kuwa ni timu moja tu, kama sio Simba basi Yanga, ndio anayoipenda na kuiheshimu kuliko nyingine yoyote nchini?
Yupo wazi akose ibada au kufanya kazi yake kwa sababu ya kukimbilia mechi hiyo ya Simba na Yanga, timu kongwe zisizostahili kuigwa hata kidogo kwa matatizo yao lukuki, wanayofanya miaka nenda rudi.
Hali ni mbaya zaidi ya ubaya. Ila ndio hao hao wanajiita wadau wa michezo, wakati hawana nia ya kuhudhulia mchezo wa aina nyingine yoyote ukiacha huo mpira wa miguu, tena wa Simba na Yanga.
Nakuwa mnyonge na kushukuru Mungu. Nasema hivyo maana nchi hii inaharibiwa na mfumo huo mbovu. Mashabiki hao ndio wenye nguvu na ushawishi mkubwa majumbani mwao na wote kuelemea kwa timu vigogo.
Na ndio wenye nguvu pia maofisini mwao. Kwa bahati mbaya au nzuri, neon la udau wa michezo linafikiriwa vingine. Angalia, licha ya Simba na Yanga kujimudu kimaisha na kiuchumi, bado Kampuni ya Bia Tanzania TBL kupitia bia yao ya Kilimanjaro, wanaidhamini klabu hizo.
Tena ni udhamini mkubwa mno. Kwa miaka mitano hii, Simba na Yanga zitafaidi fedha nyingi mno, bila kusahau mengineyo yenye tija na mguso kwa wakongwe hao, kama vile magari, vifaa vya michezo, fedha za kuendesha mikutano yao ya mwaka na nyinginezo.
Hayo ndio matatizo ya wadau wetu wa michezo. Kwani licha ya klabu hizo kujimudu, ila wanaongezewa ulaji. Wakati huo wenzao wanaambulia fedha ndogo zinazotolewa na wadhamini wakuu wa ligi hiyo.
Vodacom ambao ndio wadhamini wa ligi hiyo, wanatoa fedha za safari kwa timu zote 14 kuanzia Yanga ambao ndio mabingwa watetezi na timu ya Oljoro FC, waliopanda daraja msimu huu.
Ni mfumo mbaya mno. Kwani aliyekuwa nao anazidi kuongezewa na wengine wakibaki kama walivyo. Hayo ndio matatizo makubwa. Kwa mtindo huo huwezi kuifananisha Villa Squad na Yanga au Simba.
Kwa mfumo huu wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) Villa Squad haiwezi kuwika wala kubaki msimu ujao. Hapo kwenyewe haina kitu, vipi ipangiwe mechi mbili kwa siku tatu? Itoke Mwanza iende Bukoba itaweza?
Kikweli haiwezi. Lakini Simba wao wanaweza kufanya hilo vizuri, maana akiba kubwa wanayo. Kwanza wanazo kupitia wadhamini wakuu Vodacom na ukiongeza hao TBL kupitia bia yao ya Kilimanjaro.
Sina nia ya kulaumu, maana hayo ndio matatizo yetu. Na hao hao baadaye hukaa kwenye vikao vyao na kujiita wadau wa michezo. Nani kasema? Wadau wa aina hiyo ni sumu kwa maendeleo ya michezo.
Hivi karibuni nilipata nafasi ya kuangalia mazoezi ya timu ya Taifa ya ngumi, yaliyokuwa yakifanyika katika Uwanja wa Ndani wa Taifa, jijini Dar es Salaam .
Nilishangaa kama sio kushikwa na uchungu. Wachezaji hao wanaojiandaa na mashindano ya ‘All African Game’, yanayotarajiwa kufanyika nchini Msumbiji, baadaye mwaka huu, hawana vifaa vya michezo.
Walikuwa wakilalamika hali hiyo ila hawakusikilizwa. Waliachwa kama watoto yatima. Inatia uchungu. Sasa hao wanaojiita wadau wa michezo wako wapi? Kwanini tusiwaite wadau wa mpira wa miguu?
Kwanini? Kuna ubaya gani sasa kuitwa wadau wa Simba na Yanga? Jamani, hakuna haja ya kufichana tunapotaka kuzungumzia mambo ya maana katika Taifa hili linalokwenda kwa kusua sua.
Tuweke maslahi ya Taifa kwanza kabla ya siasa zenu. Mnatumia vibaya vyombo vya habari na kuwapasha habari za uongo wananchi wenu. Ndio, kwani watu hao wanaojiita wadau huita wanahabari ili wapewe sapoti hiyo.
Nadhani hayo ni mambo yanayotakiwa yaangaliwe upya kwa maslahi ya michezo yetu hapa nchini. Najua timu kubwa ni suala lisiloweza kuzuilika, ikiwamo hiyo Simba na Yanga.
Hata Ulaya mambo hayo yapo. Zipo timu kubwa zinazogusa hisia za wengi, ikiwamo Manchester United, Chelsea , Liverpool , Arsenal na nyinginezo, ila pia wadau wao ni tofauti na wetu.
Kuna ubaya gani wadau hao kuzipa ‘sapoti’ na timu changa mfano wa Coastal Union , Moro United, Villa Squad, Oljoro na nyinginezo?
Si tunataka maendeleo sisi kwa mpira wa miguu? Si mnajiita wadau wa michezo nyinyi, kuna haja gani ya kuelemea Simba na Yanga? Haya ni maswali tunayotakiwa tujiulize sisi sote kwa maendeleo ya Taifa.
Kwa mtindo huo michezo haiwezi kupiga hatua kamwe. Tutaendelea kulalama tu kwakuwa hatuna mfumo mzuri. Tuambiane tu. Nadhani hata wadhamini Vodacom nao wanatakiwa walijuwe hili.
Licha ya kuiweka ligi hiyo kwenye presha kubwa ila bado mambo ni magumu. Kasoro nyingi, ikiwamo kuchelewa kwa fedha za kujikimu na kugharamia safari zao, ni sababu moja wapo ya kuharibu mfumo wao wa ligi yenye ushindani.
Hapo ndipo pabaya, kwani hilo sio tatizo kwa Simba na Yanga. Kwanza wana akiba kubwa ya wanachama na mashabiki wenye nazo huku pia wakiwa na udhamini mnono, wakiwamo TBL.
Nadhani tuliangalie hilo kwa mapana zaidi. Tujifunze kuweka mikakati yenye tija na mguso kwa maendeleo ya michezo hapa nchini. Najua inakuwa ngumu kusema ukweli ila hakuna haja ya kuogopana.
Huo ndio ukweli. Kinachotakiwa ni kuona ligi inakuwa na nguvu na ushindani, kitu kitakachowafanya wachezaji wapate nafasi kubwa zaidi, hasa kucheza soka la kulipwa duniani, ikiwamo Barani Ulaya.
Ni ligi yenye nguvu na ushindani ndiyo inayoweza kuiweka timu ya Taifa, Taifa Stars katika hali nzuri. Wachezaji wataonekana kimataifa. Huo ni mpango na mkakati wenye tija kwa wote.
Kwanini tupore haki za watu? Kwanini tujiite wadau wakati sisi ni mashabiki wa Simba na Yanga pekee? Kama wewe upo kwenye kitengo kikubwa, angalia jinsi gani unaweza kuinua mchezo wa masumbwi.
Kama wewe ni Meneja wa Kampuni, jua ipo michezo mingi na klabu nyingi zinazoweza kufanikiwa kwa kupitia wewe. Hatutaki sifa za kijinga kwa kusaini hundi kwa Simba na Yanga. Wao sio kila kitu katika nchi hii.
Zipo timu nyingi zinazohitaji msaada huo. Katika ligi iliyomalizika huku Yanga akiwa bingwa, zipo timu zilizoshuka daraja kwasababu ya ukata. Miongoni mwa timu hizo ni Majimaji ya mjini Songea na Ashanti United.
Walikuwa na wachezaji wazuri, ila tatizo ni ukata. Kama kula yao ni tabu hawawezi kuifunga Simba na Yanga wanaoweka kambi sehemu nzuri na kula vizuri.
Huu ni wakati wa kuangalia upya nyendo zetu kwa faida ya michezo. Tuwe na fikra pevu. Kila mtu awe makini. Bila hivyo tutaendelea kuwa wadau wa Simba na Yanga, licha ya kushindwa kufanya vizuri nyanja za kimataifa.
Kila siku ni Simba na Yanga tu hali ya kuwa zipo timu nyingi na zenye uwezo wa kufanya mapinduzi katika mpira wa miguu nchini. Ukiacha Azam FC, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar na nyingine za jeshi, klabu nyingine wana njaa kubwa.
Hazina uwezo kifedha wala wadhamini. Wao wenyewe ndio kila kitu. Viongozi wachache wasiokuwa na chochote wanapeana mchango kwa ajili ya timu yao .
Watu kama hao hawawezi kuzibania Simba na Yanga wenye kila kitu cha kujivunia. Huo ndio ukweli wa mambo wadau. Tuwe makini katika hilo kwa maendeleo ya michezo kwa ujumla.
Yapo makampuni mengi mno. Zipo taasisi kubwa na wafanyabiashara wenye nguvu, hivyo huu ni wakati wao wa kuingia zaidi michezoni. Nasema michezoni, maana ni mjumuiko wa michezo mingi, bila kuangalia mpira wa miguu pekee.
Hilo ndio jambo la busara kufanywa na hao wanaojiita wadau wa michezo kwa faida ya kizazi cha Tanzania , maana hakuna ubishi kuwa michezo ni ajira na inaweza kuingiza sifa kwa Taifa letu.
Naomba kutoa hoja.
0712 053949
0753 806087
3 comments:
tumekupata mdau, hoja imekulibalika hii.
by Markus Mpangala
Hodi hodi wenyeji nimepita kukusalimia lakini naona haupo basi nitarudi...
Asante Markus Mpangala, endelea kupata burudani ndani ya Handenikwetu.blogsport.com
Post a Comment