MENEJA wa zamani wa bendi ya Lufita Connection, Juma Abajalo, ameajiriwa rasmi Akudo Impact, ‘Vijana wa Masauti’, huku akiwa na matumaini kibao ya kuhakikisha kwamba wakali hao wa masauti wanafikia malengo.
Kwa siku kadhaa sasa bendi hiyo imekuwa ikifanya vibaya kiasi cha kuanza kupoteza mashabiki wake, jambo lilioufanya uongozi wa juu wa Akudo umuite mdau huyo na kumpa madaraka ya kuwa kama meneja.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana mara baada ya kukabidhiwa ofisi yake, Abajalo alisema anachofanya kwa sasa ni kuhakikisha kuwa vijana wa masauti wanarudi kwenye kiti chao cha ufalme wa muziki wa dansi.
Alisema uwezo wa wanamuziki wake wanaounda bendi hiyo akiwamo Christian Bellah na wengineo ni mfano wa kuigwa wa kuhakikisha kwamba mambo yao yanakuwa mazuri zaidi kuliko wengine.
“Nimeshukuru kuitwa na kupewa madaraka haya makubwa na mazito kwangu, ila kwa ushirikiano na wote wakiwamo wanamuziki wangu, naamini kila kitu kitakuwa sawa na kufika pale tulipokusudia.
“Naamini uwezo ni mzuri na wanamuziki wote wapo kwenye kiwango cha juu, hivyo ninachowaomba mashabiki ni moyo wao wa dhati kwetu na kuendelea kutuunga mkono ili tufike mbali zaidi,” alisema Abajalo.
Abajalo ni miongoni mwa wafanyakazi mahiri wa bendi hiyo miaka ya nyuma kidogo, kabla ya kuondoka na kunyakuliwa na bendi ya Lufita ambayo hata hivyo aliamua kuacha kazi baada ya mmiliki kushindwa kujiendesha kibiashara na mipango ya kuteka soko la muziki wa dansi hapa nchini.
No comments:
Post a Comment