Diouf wa Twanga afanya makubwa
Romario wa Msondo naye apenya
MIMI ni miongoni mwa wadau wa muziki wa dansi nchini wanaokoshwa kwa kiasi kikubwa na muziki huo, licha ya bendi chache kuonekana kuwa juu wakati wenzao wanaendelea kuwa chini kila siku ya Mungu.
Hata hivyo, sikati tamaa wala kuhudhunika. Hilo ni jambo la kawaida kwakuwa bendi zote haziwezi kuwa juu. Kubadilishana namba hilo ni jambo la kawaida katika kazi. Hata wanahabari hawawezi kufanana uwezo.
Kutesa kwa bendi hizo nchini, kunatoa hoja ya kujadili wanamuziki wanaozifanya bendi hizo ziwe juu, hasa wale wanaoghani mashairi yao , yani marepa. Wanamuziki hawa husubiri wimbo uchanganye ndipo waingie.
Wana umuhimu mkubwa katika maisha ya muziki wa dansi hapa nchini, maana wengineo pia ni waimbaji na watunzi wazuri. Kwa kila shabiki, atakuwa na namba anazopenda, japo sidhani kama anaweza kuwa tofauti na mtiririko huu.
Kutokana na hilo, Gazeti lako ulipendalo la Mtanzania, linakuletea 10 bora wanaotamba katika muziki wa dansi upande wa marepa. Ni vijana wanaotingisha kupita kiasi. Wana mashabiki wengi kupita kiasi.
Wanatamba. Wanazifanya bendi zao ziingize mashabiki wengi kwa kupitia wao, ndio maana wanatunzwa na kuthaminiwa kwa kiasi kikubwa. Na hawa ndio marepa waliopewa namba moja hadi 10 kutokana na uwezo wao.
Wewe ni shabiki wa kweli wa muziki wa dansi? Unaingia kwenye maonyesho ya bendi hizo? Basi kama ni hivyo, utajua nani ni bora kuliko mwenzake, maana huu ni utafiti wangu na wewe unaweza kujua unavyojua mwenyewe.
Hata hivyo nashukuru kwa kipindi kifupi cha maisha ya kona hii, mashabiki wamekuwa wakinielewa japo kuwa wachache wao hutofautiana na mimi hasa kwenye namna nne hadi sita, kutokana na watu hao kuangalia zaidi umri na sio kipaji.
1. Msafiri Diouf Twanga Pepeta
Wahenga wamesema mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Huu ni msemo ambao kwa kiasi kikubwa utakuwa ukimhusisha mkali wa The African Stars Twanga Pepeta, Msafiri Diouf. Kijana huyu amejaliwa uwezo wa kutisha mno.
Anajua kucheza na sauti yake anapokuwa jukwaani. Naweza kusema kuwa ni repa asiyekuwa na mpinzani kwa kwakweli. Hata hivyo nje ya maisha yake ya muziki, amekuwa akihusishwa na kashfa za aina mbalimbali. Sitaki kutaja kashfa hizo, maana wadau kweli wanazijua aidha kwa kuziona au kuzisikia kwa watu.
Pamoja na mambo mengine, ila bado uwezo wake upo juu katika kona ya muziki wa dansi, kitu kilichonifanya nimuweke namba moja katika mtiririko wangu wa wiki hii. Hata kama iwe vipi, huwezi kumuweka pembeni Diouf maana hana mpinzani.
Yupo Twanga Pepeta na anastahili kuwaongoza marepa wengine waliozagaa katika bendi mbalimbali hapa nchini.
2. Totoo ze Bingwa Akudo Impact
Kama wewe unaingia katika shoo ya bendi moja tu, huwezi kujiita ni mdau wa muziki wa dansi hapa nchini. Ila jina zuri litakalokufaa wewe ni shabiki tu, ukiweka mbele jina la bendi unayopenda kuangalia maonyesho yao .
Ni katika hilo , huwezi kuliacha jina la Totoo ze Bingwa kutoka Akudo Impact. Sauti yake imejaa mvuto wa hali ya juu. Anajua anachokifanya anapokuwa jukwaani. Kwa mimi mdau wa muziki, najua uwezo wa kijana.
Wakati fulani alipokuwa peke yake kwenye bendi hiyo, bado aliweza kurapu bila kuchoka kwa siku zote za wiki anapokuwa kwenye maonyesho na vijana hao wa Masauti. Kikweli kabisa, bila kuangalia wapi walitoka wanamuziki hao, Ze Bingwa anaipamba safu yetu wiki hii akishika nafasi ya pili, nyuma ya Diof wa Twanga Pepeta.
Ameshiriki katika nyimbo mbalimbali za bendi hiyo inayoongozwa na Christian Bellah. Hakika kama hujawahi kuona manjonjo ya Ze Bingwa, wakati ni wako wa kuingia kwenye shoo zao katika kumbi mbalimbali kujionea makali yake.
3. Saulo Jonh ‘ Ferguson ’ Extra Bongo
Mwanamuziki huyu kwa sasa ndio mhimili mkubwa kwa bendi ya Extra Bongo, upande wa marepa. Kabla ya kujiunga na bendi hiyo inayomilikiwa na Ally Choky, alikuwa kwenye bendi ya Twanga Pepeta.
Saulo Jonh ama Ferguson kama anavyotambuliwa na wengi kwa jina hilo ni mkali katika ulingo wa muziki wa dansi nchini. Anaonyesha makeke mengi anapokuwa jukwaani. Hadi leo bado rapu zake zinatingisha Twanga Pepeta.
Nadhani hata ukiwauliza wadau na mashabiki wa muziki huo watakwambia Ferguson nani, kwani Diouf mwenyewe alikuwa akipumulia mashine, akipata upinzani mkali kutoka kwa kijana huyo mwenye kipaji cha hali ya juu.
Wakati Fulani nilikuwa nashangaa. Ni vipi anaweza kulinda jina lake lisichuje ? Ila nikaelewa kuwa habahatishi, hivyo ataendelea kuwa juu. Nani asiyejua rapu zake zinatingisha Twanga Pepeta? Unaijua ile Iko ‘busy’ na nyinginezo?
Katika hilo tu linaonyesha manjonjo na kipaji cha hali ya juu cha kijana huyo anayewapa raha mashabiki wa bendi ya Extra Bongo. Kama wewe hujawahi kuona vitu vya Ferguson , tafadhari jaribu kujiunga nao, Wazee hao wa next Level.
4. Kitokololo FM Academia
Anaitwa Kitokololo maana yake kuku. Huyu ni repa wa FM Academia. Yupo sambamba na wakali wengine kwenye bendi hiyo..
Anajua anachokifanya. Ana kipaji kikubwa. Mashabiki wake wanakubali vitu vyake, ndio maana ameiweka juu bendi hiyo. Nikiwa kama shabiki na mdau wa muziki wa dansi nchini, Kitokololo anaingia kwenye kona hii, akishika nafasi ya nne.
Hakika hutajutia maamuzi yako. Yeye ni repa mwenye kipaji cha hali ya juu, hivyo ameipamba kona yetu wiki hii kwa kushika nafasi ya nne nyuma ya Ferguson . Sitaki kuzitaja rapu zake, maana mashabiki wanazijua.
5. Khalid Chokoraa Mapacha Watatu
Khalid Chuma Chokoraa ni mwanamuziki wa ajabu sana . Kila kitu anajua. Ukimuweka kwenye utunzi hapo ndipo kwake. Ukimwambia acheze jukwaani hapo ndio usiseme. Hata hivyo haitoshi, Chokoraa ni repa mwenye kipaji cha kutisha.
Hii ndio sababu inayomuweka juu katika ulimwengu wa muziki wa dansi maana ni kiraka, huku akijua kazi yake vema. Amewahi kunyakua tuzo kadhaa kwa kipengele hichoo.
Sidhani kama wadau wanaompigia kura wanabahatisha. Wanajua wanachokifanya, huku wakiangalia uwezo wake kimuziki. Kwa sasa Chokoraa yupo na Mapacha Watatu, akiwa sambamba na Kalala Junior na Jose Mara.
Kabla ya kuasisi bendi hiyo, mwanamuziki huyo alikuwa kwenye bendi ya Twanga Pepeta, kabla ya kuamua kutafuta maisha yake katika bendi hiyo ya Mapacha Watatu. Kitu hicho kinamfanya Chokoraa aendelee kuwa juu.
Hapa leo pia ameingia na kushika nafasi ya tano nyuma ya Kitokololo, akionyesha uwezo wa kutisha katika harakati zake kimuziki. Kama hujawahi kushuhudia manjonjo yake, basi wakati ni wako kuungana nao.
6. Canal Top Akudo Impact
Wote ni wanamuziki na wanafanya vema. Nasema hivyo maana najua watu wengine wasioelewa watachangia tofauti. Wapo wanaopinga utafiti huu, ila najua huwezi kupendwa na wote.
Katika jambo lolote usitarajie kupendwa na wote au kupingwa na wote. Nashukuru, maana wanaoniunga mkono ni wengi..
Ni kutokana na hilo , Canal Top kutoka Akudo Impact, maarufu kama Vijana wa Masauti, naye anaingia kwenye 10 bora wiki hii akishika nafasi ya sita nyuma ya Chokoraa.
Kijana huyo mwenye umbo nene kidogo, anashirikiana kwa karibu na Ze Bingwa katika bendi hiyo, inayopoteza thamani yake japo sio sana katika ramani ya muziki wa dansi nchini.
7. Sauti ya Radi Mashujaa
Sauti ya Radi ni miongoni mwa marepa wazuri wanaofanya vema katika sanaa ya muziki wa dansi hapa nchini, akipatikana kwenye bendi ya Mashujaa. Huyu ni miongoni mwa wakali kadhaa wanaohakikisha bendi zao zinakuwa juu.
Kikweli kabisa, Sauti ya Radi amejaliwa kipaji na ndio maana jina lake na sauti yake ipo kwa kiasi kikubwa kwenye tasnia ya muziki huo wa dansi hapa nchini. Nimepata nafasi ya kumuona mara kadhaa akiwa jukwaani.
Sibahatishi na uamuzi wangu huu ni sahihi kabisa. Kwa wale wadau na mashabiki wa muziki huu watakubaliana na mimi. Kwakuwa nia ni kuweka mwanya wa wanamuziki hao kuongeza bidii katika kazi zao, hii ni dhahiri kuwa Sauti ya Radi anastahili kuwa hapa alipo.
Ameshika nafasi ya saba nyuma ya Canal Top wa Akudo Impact. Ana kipaji na anafaa kuwa hapa alipo, hivyo kama wewe ni shabiki wa muziki tafuta nafasi ya kuona manjonjo ya kijana huyo aliyejiunga na bendi hiyo hivi karibuni.
8. G-Seven FM Academia
Bado naendelea na mtiririko huu katika kuangalia nani ni nani katika harakati hizi za muziki wa dansi, zinazoendelezwa pia na wanamuziki mahiri wakiwamo marepa. Hawa ni wazuri na wana nafasi kubwa kwao.
Ndio maana wapo wengi na wanafanya mambo makubwa kuhakikisha kwamba wao na bendi zao wanakuwa juu. Hakika katika hilo , G-Seven kutoka FM Academia naye ni mkali na anastahili kuwa juu zaidi.
Kwa mashabiki wa kweli wa muziki wa dansi wanakubali vitu vyake, kwani ameweza kufanya makubwa katika tasnia hiyo ya muziki wa dansi, hasa hao FM Academia, maarufu kama Wazee wa Ngwasuma.
G-Seven ana mashabiki wengi. Anapendwa. Anaheshimika pia katika muziki huo wa dansi, ndio maana naye ameingia katika mtiririko huu wa 10 bora ya marepa wanaotamba katika kona ya muziki wa dansi nchini.
9. Greyson Semsekwa Twanga Pepeta
Greyson Semsekwa ni miongoni mwa marepa wenye uwezo wa juu kimuziki. Yupo kwenye bendi ya Twanga Pepeta, licha ya kuingia kwenye mgogoro na mabosi wake hao. Hata hivyo, sio kitu cha busara kumuweka kando, maana sauti yake ni imara.
Semsekwa amewahi kufanya kazi na bendi mbalimbali nchini, ikiwamo Extra Bongo. Kikweli, uwezo wake ni mkubwa ndio maana mashabiki wa bendi yake hiyo wanakubali uwezo wake, hasa baada ya Gerguson kuondoka Twanga Pepeta.
Naamini Semsekwa anastahili kuwa hapa alipo ndio maana ameshika nafasi ya tisa nyuma ya G-Seven wa FM Academia, maarufu kama Wazee wa Ngwasuma.
10. Romario Msondo Ngoma
Wengi wanaweza kushangaa ila huo ndio ukweli wa mambo. Romani Mng’ande maarufu kwa jina la ‘Romario’, anaipamba safu hii kwa kujipatia nafasi ya 10 nyuma ya Semsekwa. Ni mkali kutoka Msondo Ngoma.
Ni repa pekee katika bendi hiyo ya wakongwe wa muziki wa dansi nchini. Anastahili kuwapo hapa, japo kuwa bendi yao inapiga muziki wa kikongwe kidogo. Kuna kitu naomba kieleweke hapa. Msondo ipo, Romario yupo na anawapa raha mashabiki wake.
Hivyo basi, naamini anastahili kuwa hapa alipo na mashabiki ni wakati wenu wa kwenda kuona uwezo wake, anapokuwa jukwaani.
UHAKIKI: Msomaji wangu naamini tutakuwa pamoja. Hivyo ni wakati wako wa kutoa maoni yako ya kujenga, maana itaboresha kasi ya muziki wa dansi nchini.
Makala haya yameandikwa na Kambi Mbwana
Toa maoni yako
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment