https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Tuesday, September 27, 2011

Akudo Impact yapata bosi mpya


MENEJA wa zamani wa bendi ya Lufita Connection, Juma Abajalo, ameajiriwa rasmi Akudo Impact, ‘Vijana wa Masauti’, huku akiwa na matumaini kibao ya kuhakikisha kwamba wakali hao wa masauti wanafikia malengo.

Kwa siku kadhaa sasa bendi hiyo imekuwa ikifanya vibaya kiasi cha kuanza kupoteza mashabiki wake, jambo lilioufanya uongozi wa juu wa Akudo umuite mdau huyo na kumpa madaraka ya kuwa kama meneja.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana mara baada ya kukabidhiwa ofisi yake, Abajalo alisema anachofanya kwa sasa ni kuhakikisha kuwa vijana wa masauti wanarudi kwenye kiti chao cha ufalme wa muziki wa dansi.

Alisema uwezo wa wanamuziki wake wanaounda bendi hiyo akiwamo Christian Bellah na wengineo ni mfano wa kuigwa wa kuhakikisha kwamba mambo yao yanakuwa mazuri zaidi kuliko wengine.

“Nimeshukuru kuitwa na kupewa madaraka haya makubwa na mazito kwangu, ila kwa ushirikiano na wote wakiwamo wanamuziki wangu, naamini kila kitu kitakuwa sawa na kufika pale tulipokusudia.

“Naamini uwezo ni mzuri na wanamuziki wote wapo kwenye kiwango cha juu, hivyo ninachowaomba mashabiki ni moyo wao wa dhati kwetu na kuendelea kutuunga mkono ili tufike mbali zaidi,” alisema Abajalo.

Abajalo ni miongoni mwa wafanyakazi mahiri wa bendi hiyo miaka ya nyuma kidogo, kabla ya kuondoka na kunyakuliwa na bendi ya Lufita ambayo hata hivyo aliamua kuacha kazi baada ya mmiliki kushindwa kujiendesha kibiashara na mipango ya kuteka soko la muziki wa dansi hapa nchini.

Mbunge wa Kilwa amlipua kocha wa Stars

MBUNGE wa Kilwa Kaskazini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Murtaza Mangungu, amemjia juu kocha wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Jan Poulsen, akisema kuwa uwezo wake hauridhishi na ipo haja ya kuwekwa pembeni kwa manufaa ya maendeleo ya michezo, hasa mpira wa miguu.

Mangungu ambaye pia ni miongoni mwa wabunge mashuhuri na wanaopenda michezo, alisema hadi sasa tayari kocha huyo ameshashindwa kuiletea maendeleo Tanzania kwa kupitia mpira wa miguu, licha ya kuendelea kukumbatiwa na wadau wachache likiwamo Shirikisho la Soka nchini (TFF).

Akizungumza jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mangungu alisema ingekuwa nchi nyingine za wenye kuhitaji maendeleo, kocha huyo angeshatimuliwa maana haan jipya na uwezo wake hauridhi.

Alisema kitu kama hicho kinatakiwa kiangaliwe upya na wadau wa michezo, maana hata aina ya upangaji wake wa timu wakati mwingine haina jipya na malengo kwenye medani ya mpira wa miguu.

“Lazima Watanzania tuwe na uthubutu na malengo ya kweli, maana si kila Mzungu anaweza kufundisha soka Tanzania, ndio maana ujio wa Paulsen hauna mpya na ipo haja ya kuwa wakali katika hilo.

“Kama kocha aliyeipa mafanikio Tanzania, Mbrazil, Marcio Maximo amemaliza mkataba wake, kulikuwa na sababu kubwa ya kupatikana mwingine mwenye uelewa na juhudi za dhati kuliko kupeana ajira zinazopoteza fedha nyingi za Watanzania na hakuna cha maana kinachopatikana,” alisema Mangungu.

Stars inajiandaa na mechi yake dhidi ya Morocco, inayotarajiwa kupigwa Oktoba 9, nchini humo, huku malengo ya mashabiki wa Tanzania yakizidi kupotea kutokana na uchezaji mbovu wa wachezaji wake.

Monday, September 26, 2011

Wimbo wa Kizunguzungu wa Rachel wa THT

Nifunguwe macho, ningoze popote uendapo
Wewe thamani yangu, chozi langu
Pendo langu utalosema, niyasema ndiyo
Kama baya nitasema sio,
Mara chache mpenzi, kukataa lisemalo nifurahie
Baby kwa kila zuri nitendalo
 
Kiitikio
Ama kweli kizunguzungu
Kinanichanganya mpaka kinanipa wazimu
Siishi kuwaza kunywa sumu
Sababu ya huyu brother Man x 2
 
Ubeti 2
 
Ufunguwe moyo naukabidhi kwako
Uwe wako, wewe ndiyo nyota yangu
Chozi langu mwanga wangu
Utalosema nitasema ndiyo
Na kama baya nitasema siyo
Mara chache mpenzi
Kukataa usemalo
Nifurahie baby kwa kila zuri nitendalo
 
 
Kiitikio
 
Ama kweli kizunguzungu
Kinanichanganya mpaka kinanipa wazimu
Siishi kuwaza kunywa sumu
Sababu ya huyu brother Man x 2
 
Kibwagizo
Ni wewe niliyekuona
Mbele ya macho yangu
Niliwazee, nikuliwazee iyee
Nisiwaze, umezaliwa wewe uwe wangu x 2
 

Zifanyie kazi kasoro zako muungwana

KARIBU kwenye ulingo huu wa mambo ya malavidavi huku tukiwekana sawa katika vitu hivyo vitamu kunoga. Katika mfululizo wa kona hii, msomaji utapata habari nzuri zinazohusu uhusiano na maisha.
 
Nia ni kuwekana sawa, ukizingatia kuwa hakuna aliyekamilika hapa chini ya jua. Nikiwa kama muungwana nashukuru kwa kila anayeguswa na kazi zangu, ikiwamo hii inayoelezea mambo ya kimapenzi.
 
Naamini hali hiyo inanipa changamoto na ushawishi wa kuendelea kuwa pamoja kila wiki, katika dhana ya kuiendeleza kona hii.
 
Ndugu msomaji wangu, lazima ujuwe wewe ni nani na upo vipi katika jamii. Nasema hivyo, huku nikiwa muwazi kabisa kwako, kwamba fanyia kazi kasoro zako.
 
Jiangalie mara mbili mbili kwa nia ya kubaini matatizo yako, ili unapokuwa na mtu wako umfanyie yale unayohisi kuwa atavutiwa nayo.
 
Wapo watu wanaojifanya wao ndio kila kitu. Licha ya kukera sana wenzao kwa sababu moja ama nyingine, ila wanabaki kimya, kama wao ni wafalme.
 
Hiyo ni mbaya mno. Kwani wale wanaokosewa kwa makusudi na watu wao, huwa nafasi yao kutafuta sehemu nyingine zenye utulivu.
 
Si ameshakujua ulivyo? Ameshajua wewe ni wa moja tu, huwezi kuvaa kumi moja, hivyo lazima afanye ya kuweza kumpa amani moyoni mwake.
 
Kwa siku kadhaa sasa nimekuwa nikipata maoni ya aina mbalimbali, jambo linalonifanya nizame kutoa mada zinazotoa majibu kwa wale wapenzi haswa wa kona hii inayokujia kila Jumamosi.
 
Wapo watu ambao licha ya kuwa na kasumba zinazowakera watu wapenzi wao, ila wamekuwa kimya kabisa. Wanachofanya wao ni kujiweka karibu na vitu vya kileo, kama luninga, manukato ya aina aina bila kujua kuwa hali zao kihusiano ni mbaya.
 
Lazima uwe makini ndugu yangu. Unaweza kuishi vizuri bila tatizo lolote, endapo uhusiano wako utakuwa umetulia. Na kwa bahati mbaya, hakuna mwingine wa kuuweka sawa zaidi yako mwenyewe.
 
Kwa mikono yako unaweza kujenga nyumba yako na pia kuimoboa kwa mikono yako mwenyewe. Kuwa na uchungu wa kweli msomaji wangu.
 
Kwanini? Jivuwe gamba leo na uape kuishi vema na mwenziwako ili mfurahie ndoa yenu au uhusiano wenu. Nasema hivyo nikiamini kuwa wengi wanavunja uhusiano wao kwa tabia zao za ajabu.
 
Wanashindwa kujiweka sawa na kuona huruma nafasi za wenzao, kitu kinachotakiwa hekima kubwa. Kutojitambua ni kupoteza muda wa mwenzako.
 
Unajua fika unachofanya hakiwezi kumfurahisha mwenzako zaidi ya kumchukiza. Faida ya chuki ni kusambaratisha maana hakuna anayeweza kuishi na mtu ambaye amejaa kasumba za kila aina.
 
Huu ni wakati wako wa kujifanyia marekebisho, maana unachofanya ni kujiharibia wewe mwenyewe. Angalia yote utendayo kwa faida ya uhusiano wako.
 
Kama hufahamu kasoro zako jaribu kumshirikisha mwenzako kwa faida yenu. Sidhani kama anaweza kuwa kimya bila kukwambia ukweli wakati hana amani na kasumba zako za kila siku ya Mungu.
 
Mapenzi hapo ndipo huzaa utamu wake. Kwanza kujitambua na kujifanyia marekebisho kwa faida yenu wote, maana bila hivyo ni hatari kubwa.
 
Angalia kwa makini na kuufanyia kazi urembo wako, maana haitakuwa picha nzuri kuharibu ulipokuwapo sasa, ukizingatia kuwa huko utakapokwenda kunaweza kuwa kubaya kupita kiasi, hivyo kujisumbua.
 
Hapo unapopendwa ndio pakushika kwa nguvu zote, ila tu, ukiwa makini na kuficha nyufa zinazoweza kujitokeza wakati wowote unapobaini mapungufu yako.

Marepa 10 bora wanaotingisha Tanzania

 
Diouf wa Twanga afanya makubwa
Romario wa Msondo naye apenya

MIMI ni miongoni mwa wadau wa muziki wa dansi nchini wanaokoshwa kwa kiasi kikubwa na muziki huo, licha ya bendi chache kuonekana kuwa juu wakati wenzao wanaendelea kuwa chini kila siku ya Mungu.
 
Hata hivyo, sikati tamaa wala kuhudhunika. Hilo ni jambo la kawaida kwakuwa bendi zote haziwezi kuwa juu. Kubadilishana namba hilo ni jambo la kawaida katika kazi. Hata wanahabari hawawezi kufanana uwezo.
 
Kutesa kwa bendi hizo nchini, kunatoa hoja ya kujadili wanamuziki wanaozifanya bendi hizo ziwe juu, hasa wale wanaoghani mashairi yao , yani marepa. Wanamuziki hawa husubiri wimbo uchanganye ndipo waingie.
 
Wana umuhimu mkubwa katika maisha ya muziki wa dansi hapa nchini, maana wengineo pia ni waimbaji na watunzi wazuri. Kwa kila shabiki, atakuwa na namba anazopenda, japo sidhani kama anaweza kuwa tofauti na mtiririko huu.
 
Kutokana na hilo, Gazeti lako ulipendalo la Mtanzania, linakuletea 10 bora wanaotamba katika muziki wa dansi upande wa marepa. Ni vijana wanaotingisha kupita kiasi. Wana mashabiki wengi kupita kiasi.
 
Wanatamba. Wanazifanya bendi zao ziingize mashabiki wengi kwa kupitia wao, ndio maana wanatunzwa na kuthaminiwa kwa kiasi kikubwa. Na hawa ndio marepa waliopewa namba moja hadi 10 kutokana na uwezo wao.
 
Wewe ni shabiki wa kweli wa muziki wa dansi? Unaingia kwenye maonyesho ya bendi hizo? Basi kama ni hivyo, utajua nani ni bora kuliko mwenzake, maana huu ni utafiti wangu na wewe unaweza kujua unavyojua mwenyewe.
 
Hata hivyo nashukuru kwa kipindi kifupi cha maisha ya kona hii, mashabiki wamekuwa wakinielewa japo kuwa wachache wao hutofautiana na mimi hasa kwenye namna nne hadi sita, kutokana na watu hao kuangalia zaidi umri na sio kipaji.
 
1. Msafiri Diouf  Twanga Pepeta
 
Wahenga wamesema mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Huu ni msemo ambao kwa kiasi kikubwa utakuwa ukimhusisha mkali wa The African Stars Twanga Pepeta, Msafiri Diouf. Kijana huyu amejaliwa uwezo wa kutisha mno.
 
Anajua kucheza na sauti yake anapokuwa jukwaani. Naweza kusema kuwa ni repa asiyekuwa na mpinzani kwa kwakweli. Hata hivyo nje ya maisha yake ya muziki, amekuwa akihusishwa na kashfa za aina mbalimbali. Sitaki kutaja kashfa hizo, maana wadau kweli wanazijua aidha kwa kuziona au kuzisikia kwa watu.
 
Pamoja na mambo mengine, ila bado uwezo wake upo juu katika kona ya muziki wa dansi, kitu kilichonifanya nimuweke namba moja katika mtiririko wangu wa wiki hii. Hata kama iwe vipi, huwezi kumuweka pembeni Diouf maana hana mpinzani.
 
Yupo Twanga Pepeta na anastahili kuwaongoza marepa wengine waliozagaa katika bendi mbalimbali hapa nchini.
 
2. Totoo ze Bingwa Akudo Impact
 
Kama wewe unaingia katika shoo ya bendi moja tu, huwezi kujiita ni mdau wa muziki wa dansi hapa nchini. Ila jina zuri litakalokufaa wewe ni shabiki tu, ukiweka mbele jina la bendi unayopenda kuangalia maonyesho yao .
 
Ni katika hilo , huwezi kuliacha jina la Totoo ze Bingwa kutoka Akudo Impact. Sauti yake imejaa mvuto wa hali ya juu. Anajua anachokifanya anapokuwa jukwaani. Kwa mimi mdau wa muziki, najua uwezo wa kijana.
 
Wakati fulani alipokuwa peke yake kwenye bendi hiyo, bado aliweza kurapu bila kuchoka kwa siku zote za wiki anapokuwa kwenye maonyesho na vijana hao wa Masauti. Kikweli kabisa, bila kuangalia wapi walitoka wanamuziki hao, Ze Bingwa anaipamba safu yetu wiki hii akishika nafasi ya pili, nyuma ya Diof wa Twanga Pepeta.
 
Ameshiriki katika nyimbo mbalimbali za bendi hiyo inayoongozwa na Christian Bellah. Hakika kama hujawahi kuona manjonjo ya Ze Bingwa, wakati ni wako wa kuingia kwenye shoo zao katika kumbi mbalimbali kujionea makali yake.
 
3. Saulo Jonh ‘ Ferguson ’ Extra Bongo
 
Mwanamuziki huyu kwa sasa ndio mhimili mkubwa kwa bendi ya Extra Bongo, upande wa marepa. Kabla ya kujiunga na bendi hiyo inayomilikiwa na Ally Choky, alikuwa kwenye bendi ya Twanga Pepeta.
 
Saulo Jonh ama Ferguson kama anavyotambuliwa na wengi kwa jina hilo ni mkali katika ulingo wa muziki wa dansi nchini. Anaonyesha makeke mengi anapokuwa jukwaani. Hadi leo bado rapu zake zinatingisha Twanga Pepeta.
 
Nadhani hata ukiwauliza wadau na mashabiki wa muziki huo watakwambia Ferguson nani, kwani Diouf mwenyewe alikuwa akipumulia mashine, akipata upinzani mkali kutoka kwa kijana huyo mwenye kipaji cha hali ya juu.
 
Wakati Fulani nilikuwa nashangaa. Ni vipi anaweza kulinda jina lake lisichuje ? Ila nikaelewa kuwa habahatishi, hivyo ataendelea kuwa juu. Nani asiyejua rapu zake zinatingisha Twanga Pepeta? Unaijua ile Iko ‘busy’ na nyinginezo?
 
Katika hilo tu linaonyesha manjonjo na kipaji cha hali ya juu cha kijana huyo anayewapa raha mashabiki wa bendi ya Extra Bongo. Kama wewe hujawahi kuona vitu vya Ferguson , tafadhari jaribu kujiunga nao, Wazee hao wa next Level.
 
4. Kitokololo FM Academia
 
Anaitwa Kitokololo maana yake kuku. Huyu ni repa wa FM Academia. Yupo sambamba na wakali wengine kwenye bendi hiyo..
 
Anajua anachokifanya. Ana kipaji kikubwa. Mashabiki wake wanakubali vitu vyake, ndio maana ameiweka juu bendi hiyo. Nikiwa kama shabiki na mdau wa muziki wa dansi nchini, Kitokololo anaingia kwenye kona hii, akishika nafasi ya nne.
 
Hakika hutajutia maamuzi yako. Yeye ni repa mwenye kipaji cha hali ya juu, hivyo ameipamba kona yetu wiki hii kwa kushika nafasi ya nne nyuma ya Ferguson . Sitaki kuzitaja rapu zake, maana mashabiki wanazijua.
 
5. Khalid Chokoraa Mapacha Watatu
 
Khalid Chuma Chokoraa ni mwanamuziki wa ajabu sana . Kila kitu anajua. Ukimuweka kwenye utunzi hapo ndipo kwake. Ukimwambia acheze jukwaani hapo ndio usiseme. Hata hivyo haitoshi, Chokoraa ni repa mwenye kipaji cha kutisha.
 
Hii ndio sababu inayomuweka juu katika ulimwengu wa muziki wa dansi maana ni kiraka, huku akijua kazi yake vema. Amewahi kunyakua tuzo kadhaa kwa kipengele hichoo.
 
Sidhani kama wadau wanaompigia kura wanabahatisha. Wanajua wanachokifanya, huku wakiangalia uwezo wake kimuziki. Kwa sasa Chokoraa yupo na Mapacha Watatu, akiwa sambamba na Kalala Junior na Jose Mara.
 
Kabla ya kuasisi bendi hiyo, mwanamuziki huyo alikuwa kwenye bendi ya Twanga Pepeta, kabla ya kuamua kutafuta maisha yake katika bendi hiyo ya Mapacha Watatu. Kitu hicho kinamfanya Chokoraa aendelee kuwa juu.
 
Hapa leo pia ameingia na kushika nafasi ya tano nyuma ya Kitokololo, akionyesha uwezo wa kutisha katika harakati zake kimuziki. Kama hujawahi kushuhudia manjonjo yake, basi wakati ni wako kuungana nao.
 
6. Canal Top Akudo Impact
 
Wote ni wanamuziki na wanafanya vema. Nasema hivyo maana najua watu wengine wasioelewa watachangia tofauti. Wapo wanaopinga utafiti huu, ila najua huwezi kupendwa na wote.
 
Katika jambo lolote usitarajie kupendwa na wote au kupingwa na wote. Nashukuru, maana wanaoniunga mkono ni wengi..
 
Ni kutokana na hilo , Canal Top kutoka Akudo Impact, maarufu kama Vijana wa Masauti, naye anaingia kwenye 10 bora wiki hii akishika nafasi ya sita nyuma ya Chokoraa.
 
Kijana huyo mwenye umbo nene kidogo, anashirikiana kwa karibu na Ze Bingwa katika bendi hiyo, inayopoteza thamani yake japo sio sana katika ramani ya muziki wa dansi nchini.
 
7. Sauti ya Radi Mashujaa
 
Sauti ya Radi ni miongoni mwa marepa wazuri wanaofanya vema katika sanaa ya muziki wa dansi hapa nchini, akipatikana kwenye bendi ya Mashujaa. Huyu ni miongoni mwa wakali kadhaa wanaohakikisha bendi zao zinakuwa juu.
 
Kikweli kabisa, Sauti ya Radi amejaliwa kipaji na ndio maana jina lake na sauti yake ipo kwa kiasi kikubwa kwenye tasnia ya muziki huo wa dansi hapa nchini. Nimepata nafasi ya kumuona mara kadhaa akiwa jukwaani.
 
Sibahatishi na uamuzi wangu huu ni sahihi kabisa. Kwa wale wadau na mashabiki wa muziki huu watakubaliana na mimi. Kwakuwa nia ni kuweka mwanya wa wanamuziki hao kuongeza bidii katika kazi zao, hii ni dhahiri kuwa Sauti ya Radi anastahili kuwa hapa alipo.
 
Ameshika nafasi ya saba nyuma ya Canal Top wa Akudo Impact. Ana kipaji na anafaa kuwa hapa alipo, hivyo kama wewe ni shabiki wa muziki tafuta nafasi ya kuona manjonjo ya kijana huyo aliyejiunga na bendi hiyo hivi karibuni.
 
8. G-Seven FM Academia
 
Bado naendelea na mtiririko huu katika kuangalia nani ni nani katika harakati hizi za muziki wa dansi, zinazoendelezwa pia na wanamuziki mahiri wakiwamo marepa. Hawa ni wazuri na wana nafasi kubwa kwao.
 
Ndio maana wapo wengi na wanafanya mambo makubwa kuhakikisha kwamba wao na bendi zao wanakuwa juu. Hakika katika hilo , G-Seven kutoka FM Academia naye ni mkali na anastahili kuwa juu zaidi.
 
Kwa mashabiki wa kweli wa muziki wa dansi wanakubali vitu vyake, kwani ameweza kufanya makubwa katika tasnia hiyo ya muziki wa dansi, hasa hao FM Academia, maarufu kama Wazee wa Ngwasuma.
 
G-Seven ana mashabiki wengi. Anapendwa. Anaheshimika pia katika muziki huo wa dansi, ndio maana naye ameingia katika mtiririko huu wa 10 bora ya marepa wanaotamba katika kona ya muziki wa dansi nchini.
 
9. Greyson Semsekwa Twanga Pepeta
 
Greyson Semsekwa ni miongoni mwa marepa wenye uwezo wa juu kimuziki. Yupo kwenye bendi ya Twanga Pepeta, licha ya kuingia kwenye mgogoro na mabosi wake hao. Hata hivyo, sio kitu cha busara kumuweka kando, maana sauti yake ni imara.
 
Semsekwa amewahi kufanya kazi na bendi mbalimbali nchini, ikiwamo Extra Bongo. Kikweli, uwezo wake ni mkubwa ndio maana mashabiki wa bendi yake hiyo wanakubali uwezo wake, hasa baada ya Gerguson kuondoka Twanga Pepeta.
 
Naamini Semsekwa anastahili kuwa hapa alipo ndio maana ameshika nafasi ya tisa nyuma ya G-Seven wa FM Academia, maarufu kama Wazee wa Ngwasuma.
 
10. Romario Msondo Ngoma
 
Wengi wanaweza kushangaa ila huo ndio ukweli wa mambo. Romani Mng’ande maarufu kwa jina la ‘Romario’, anaipamba safu hii kwa kujipatia nafasi ya 10 nyuma ya Semsekwa. Ni mkali kutoka Msondo Ngoma.
 
Ni repa pekee katika bendi hiyo ya wakongwe wa muziki wa dansi nchini. Anastahili kuwapo hapa, japo kuwa bendi yao inapiga muziki wa kikongwe kidogo. Kuna kitu naomba kieleweke hapa. Msondo ipo, Romario yupo na anawapa raha mashabiki wake.
 
Hivyo basi, naamini anastahili kuwa hapa alipo na mashabiki ni wakati wenu wa kwenda kuona uwezo wake, anapokuwa jukwaani.
 
UHAKIKI: Msomaji wangu naamini tutakuwa pamoja. Hivyo ni wakati wako wa kutoa maoni yako ya kujenga, maana itaboresha kasi ya muziki wa dansi nchini.
 

Makala haya yameandikwa na Kambi Mbwana
Toa maoni yako
0712 053949
0753 806087

Sanaa ni kazi, wauza sura zindukeni

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
SANAA ni moja ya vitu vyenye mguso mkubwa kitu kinachotakiwa kipewe kipaumbele na wadau wote wakiwamo wasanii wenyewe.
 
Sio kukaa tu na kujipodoa kwa nia ya kupata nafasi zaidi ya kuuza sura, kitu kinachoweza kuharibu mfumo mzima na kiu ya mafanikio kwa wasanii wetu.
 
Kupenda kwangu kuchunguza aina ya maisha ya wasanii wetu, kumenifanya nijuwe mambo mengi kupita kiasi. Wapo wasanii waliovuma miaka ya 2002 lakini sasa hawapo au wapo lakini hawana jipya.
 
Kwa bahati mbaya, hata maisha yao yamekuwa machungu mno kwao. Kuomba sawa wanaweza, ila watamuomba nani wakati walifunga vioo wakati huo wanatoa albamu moja na kupewa gari la Milioni mbili?
 
Hayo ni maswali ninayojiuliza kutwa kucha, ila mwisho wa siku lazima wasanii wenyewe wawe makini. Sanaa ni kazi. Wengi wanaweza kufanikiwa, ila sio kwa kupenda kuuza sura ovyo huku kazi zikiwa mbovu.
 
Sio kuuza sura tu, wakati wanashindwa kufanya mambo yenye tija kwa ajili ya sanaa zao. Kwa bahati mbaya kiloa siku wasanii wanazidi kuongezeka, ila sidhani kama wanazijua athari zinazoweza kuwakumba.
 
Bongo Fleva, ni miongoni mwa sanaa rahisi kufanywa, kitu kinachowafanya vijana wengi waone wana haki na wajibu wa kuitwa wasanii, hata hivyo kasumba yake ni hatari kwa wale wanaojihusisha na sanaa hiyo.
 
Hawafanikiwi kamwe. Maisha yao ni ya kubahatisha, licha ya kuwa kwenye kitu kinachowapa utajiri mkubwa watu wengi duniani.
 
Angalia Barani Ulaya. Wasanii wa kule, waandaaji wa muziki na wengineo wanafanya jeuri ya pesa. Wanashindania fedha, kila mmoja akijiona ni zaidi ya mwenzake.
 
Hapo utashangaa watoto wadogo wanavyoweza kuvuna fedha nyingi kwasababu ya sanaa. Wanaimba kama wanavyoimba wengine.
 
Ila, maisha yao ni ya gharama na yenye mvuto kutokana na kuzaliwa katika nchi zinazopigania maendeleo, maana wanajuwa kuvuma kwa msanii ni dalili njema ya kuvuna utajiri kutoka kwake.
 
Wapo wangapi wanaovuma Marekani? Je, nchi yap imenufaika vipi kwa kukatwa kodi wao, licha ya kuimba wenyewe?
 
Hayo ni maswali tunayotakiwa tujiulize mimi na wewe, maana hakuna haja ya kukesha kwenye kioo kujiremba, wakati hadi jana umeimba bure katika shoo iliyowaingizia watu pesa nyingi na kunufaika na familia zao.
 
Unaona raha kutangazwa? Unaona furaha, maana ndio njia yako ya kujulikana kwa watu kwakuwa huna lengo lingine zaidi ya kuuza sura.
 
Huo ni udhaifu mkubwa na utaendelea kuwakumba wasanii wengi wa Tanzania , maana akili zao hazikuwi. Kila siku ni wale wale.
 
Jamani kwanini mnakuwa hivyo? Hivi hamuoni kufuru za kina Jennifer Lopez, Rihanna, Beyonce na wengineo wana huko wanavyoishi maisha ya gharama.
 
Wao wapo wapo tu. Kama mijisanamu vile. Jamani, sijui Mungu amewaroga Watanzania? Upo uwezekano mkubwa kuwa kasumba hizi kwa wasanii zitaendelea miaka nenda rudi maana hawajitambui.
 
Wasanii wa Tanzania hawana uthubutu. Wameridhika kuwa chanzo cha utajiri wa wenzao, huku wenyewe wakiambulia nafasi ya kuuza sura.
 
Uzeni tu kwa raha zenu, ila hakuna haja yakuingia kwenye sanaa isiyolipa. Ukiacha huko kuuza sura faida gani nyingine wanayopata wasanii wetu, hasa hawa wa Bongo Fleva.
 
Au nao wanataka kuwa wanasiasa kama Mh Joseph Mbilinyi, maarufu kama Mr Two? Sugu huyu ni sawa na ubongo wa Diamond, Mr Blue, Madee, Godzilla na wengineo?
 
Sawa, ila ipo haja ya wasanii wenyewe kujitambua maana huko kuuza sura, bila kuwa na mipango ni sawa na kupoteza muda wao.
 
Watunge nyimbo nzuri zinazovutia bila kusahau kupambana na yote yanayoharibu maisha yao , maana sanaa ni kazi na wale wanaoingia kwa kuuza sura watafute njia nyingine.
 
0712 053949
0753 806087

Tatizo la maji Kilwa lapatiwa ufumbuzi

MFANYABIASHARA maarufu Mustafa Sabodo na Mtanzania anayeishi nchini Marekani, Faraja Ukondwa, wameahidi kuchimba visima vya maji safi na salama 133, wilayani Kilwa, hivyo kupunguza tatizo la uhaba wa maji linaloyakumbuka maeneeo mengi mjini humo.

Hayo yamesemwa na mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), jijini Dar es Salaam jana, alipokuwa akizungumza na Mtanzania kuhusiana na kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wake.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mangungu mmoja wa wabunge machachari waliopita katika uchaguzi wa mwaka jana, alisema kwa kupitia msaada huo, wananchi wa Kilwa watanufaika na maji hayo, mara baada ya visima 30 kutoka kwa Sabodo na visima 100 msaada wa Ukondwa, kukamilika.

Alisema kero ya ukosefu wa maji ni kubwa katika maeneo hayo, hivyo kujitokeza kwa watu hao ni dalili njema za kuanza kufanyia kazi matatizo yanayowakabili wananchi wote na wakazi wa Kilwa.

“Nimekuwa katika presha kubwa kutafuta namna ninavyoweza kusaidia maendeleo katika jimbo langu na maeneo yote ya Kilwa, hivyo kujitokeza kwa wafanyabiashara hao kutapunguza matatizo hayo.

“Naamini wananchi wote watafaidika na maji hayo, hivyo ni jukumu la kila mwenye uwezo wake kushirikiana kwa karibu kutafuta namna tunavyoweza kuwakomboa watu wa Kilwa wenye utajiri mkubwa, japo kuwa wanaishi katika umaskini wa kutupwa,” alisema Mangungu.

Kwa mujibu wa Mangungu, yupo kwenye hatua za mwisho za kufanya ziara katika maeneo yote ya jimbo lake, akiwa na nia ya kuangalia jinsi ya kuweza kukabili changamoto kwenye eneo lake.

Waandishi wa habari za michezo wamegeuzwa kandambili










Waandishi wa habari juu na Ofisa Habari wa TFF Boniface Wambura picha ya chini.



NIMEKUWA karibu kufuatilia sakata la waandishi wa habari za michezo, Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo TASWA na Shirikisho la Soka nchini (TFF), ambao wote kwa pamoja wanatakiwa wafanye kazi zao kwa ushirikiano mkubwa.

Mengi nayaona na kuyaacha yapite. Mengine yananichekesha mara baada ya kusumbua akili yangu kwa dakika kadhaa kuyachambua kadri ninavyoona inafaa. Hata hivyo, katika hili la waandishi wa habari za michezo kugeuzwa kandambili, siwezi kuvumilia.

Nasema hivyo kwasababu mchango wa waandishi wa habari unajulikana na wanatakiwa waheshimiwe kwa namna moja ama nyingine. Takribani mwaka mmoja sasa, watu hawa wameendelea kunyanyasika.

Mara kadha wanajituma kupita kiasi kuwahabarisha wadau wa michezo, hata hivyo mwisho wa siku wanachoambulia ni matusi ya reja reja. Utawakuta wakishinda kutwa nzima katika ofisi za Shirikisho la Soka nchini (TFF), wakisubiri vitambulisho vya kuingia uwanjani.

Hiyo huja katika mechi za Kimataifa, ambazo kabla ya mechi hizo, vyombo vya habari na waandishi wao hufanya juhudi kubwa kutoa habari kwa wadau na mashabiki na kuingia kwa wingi uwanjani, kitu kinachowafanya waingize fedha nyingi.

Hapa lazima tufanye jambo. Maana hali hii ikiendelea, waandishi wa habari za michezo wataendelea kuwa kandambili, kuogewa na baadaye kuachwa nje.

Mbaya zaidi, juhudi zinazofanywa haziwezi kuokoa thamani yao. Mchango wao ni mkubwa mno. Hawa hawastahili kunyanyasika. Waandishi hawa wanaosifiwa kila siku kwa kazi zao, waliwahi kuachwa katika kivuko kwa sababu nilizoshindwa kuzielewa.

Mengi yalizungumzwa. TFF yenyewe ilisema waandishi wa habari baadhi yao, walitoa maneno ya kashfa zilizowachukiza wahusika. Sawa, huwenda ni kweli. Ila, nani alistahili kulipa gharama za kivuko, ni waandishi wenyewe au TFF waliowaita?

Kwanini utaratibu wa kuingilia uwanjani ubadilishwe? Je, zile zilizokuwa zikitumika kabla yao, wakati Fredrick Mwakalebela ndio Katibu Mkuu, ni mbaya? Kwa mujibu wa takwimu zilizofika TFF na TASWA, waandishi jumla ya 170 waliombewa vitambulisho vya kuingilia uwanjani.

Kwanini mpaka sasa havijatoka? Ukiangalia kwa jinsi vyombo vya habari vilivyokuwa vingi ni idadi ndogo mno. Nasema hivyo kwasababu wanachoandika ni thamani na matangazo ya bure kwa TFF.

Kama wangepaswa walipe kama matangazo kwa kila kinachoandikwa na magazeti, redio au televisheni, ni dhahiri fedha hizo hawana uwezo wa kulipa? Kama waandishi wamechangia kuingia mamilioni ya shilingi, kuna ubaya gani waandishi 170 kuingia bure uwanjani, tena sio wote wanaoweza kuhudhulia mechi.

Ngoja niseme ukweli maana najua ndio unaoweza kuokoa ushirikiano unaoelekea mwishoni kwa waandishi wa habari na TFF, japo kuwa najua naweza kujiweka tabuni kwa wale wasiopenda kuambiwa ukweli. Uwanjani kila mtu huwenda kwa kazi yake. Wengine huwenda uwanjani kwa ajili ya kuandika makala na mengineyo.

Wengine huingia kwa ajili ya kuripoti mechi. Hugawana majukumu. Hakika hali ni mbaya mno. TFF wanasema wahariri wasiingie bure uwanjani.

Na kama wakitaka kuingia, vyombo vyao vya habari viwalipie. Jamani, mhariri ni nani na mwandishi ni nani? Ndio  maana nasema suala hili lazima lichukuliwe kipaumbele maana hali inazidi kuwa mbaya? Leo, mambo yanavyozidi kuwa magumu, ushirikiano ni jambo la lazima,

Tamaa ya pesa nyingi zinazotokana na waandishi wa habari zisipoteze thamani yao na kusababisha kususa. Unaweza kushangaa, ila kikweli siwezi kuvumilia. Nawaonea huruma TFF kupitia kwa Rais wao Leodgar Tenga na Katibu Mkuu wake Angetile Osiah.

Muda wao mwingi wanautumia kurushiana maneno na waandishi wa habari 170 waliombewa vitambulisho na kukosa ujuzi na maarifa ya kuendeleza michezo. Timu ya Taifa, Taifa Stars ilishindwa kwenda Sudan huku wao wapo ofisini.

Yanga, Simba wamekuwa watawala wa soka nchini. Wasemalo wao ndio linalofanywa. Wamekaa tu. Wakija kuzungumza ni aina ya kadi chache za waandishi wakitaka wasiingie uwanjani, maana nafasi zitajaa.

Kwanini? Nani amewatuma? Huu ni wizi mtupu na ubabaishaji mkubwa? Osiah ni mwandishi anajua mchango wa ndugu zake hao wasiokuwa na thamani kwa TFF ya leo. Ujinga huu utakwisha lini? Inakuwaje mvutano huo umalize mwaka?

Kwa kila mechi, vyombo vya habari viwalipie waandishi wao 170 kwa tiketi ya elfu 10,000 kila moja ni sawa na shilingi 1,700,000. Vipo vyombo vingi vya habari, lakini magazeti 13 kwa siku yalipiwe Shilingi 1,000,000 ni ndogo ya pesa zilizolipiwa kwa waandishi.

TFF wameangalia suala hili? Mnajua thamani ya matangazo? Kwanini Watanzania mnapenda kupayuka yuka ovyo? Iwapi thamani ya elimu zenu? Mmesomea wapi hadi mkose walau robo ya kuangalia faida na hasara?

Sina nia ya kuwarushia makombora wadau hao na viongozi wa TFF, kwakuwa lengo langu ni zuri. Napenda tujenge nyumba yenye maendeleo.

Tanzania inazidi kufanya vibaya kwenye medani ya Kimataifa. Huu ni muda wa kukaa pamoja kuangalia tatizo lipo wapi na sio kukimbizana na waandishi au kuwagandisha kusuburia kadi zinazobadilishwa kila siku ya Mungu.

Leo hii ligi inaendelea, lakini hutashangaa kuambiwa mwandishi yupo TFF anasubiria kadi na tiketi ya kuingilia uwanjani. Huu ni ujinga. Hii ni aibu yenu na ninasema japo kuwa najua ni vibaya kumsema mtu mkubwa.

Kwanini? Nadhani hapa ipo haja ya waandishi wa habari kuikataa dhambi hii ya kufanywa kandambili, kuwatangazia mechi zao na mwisho wa siku husahau na kukimbilia fedha zinazopatikana kwa mchango wa waandishi.

Ona wakati mwingine uwanja haujai kabisa. Utawaona wamekaa na wadhamini wao, wamewapa viti maalum, lakini wanahabari wamechanganyika na mashabiki. Huyu anarusha chupa, yule amesimama akitoa matusi?

Hawajatengewa sehemu yao ya kukaa na kufanya kazi zao kwa ufanisi. Nadhani hili liangaliwe kwa mapana zaidi.

Chonde chonde TASWA, BMT, TFF na Serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo chini ya Waziri wake, Emmanuel Nchimbi, kuirudisha thamani ya waandishi wa habari za michezo.

Inakera ndio maana siwezi kuvumilia
0712 053949
0753 806087


LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...