Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WAHENGA wana msemo wao, fisi
akiwa hakimu, mbuzi sheria hana. Chochote atakachofanya, uamuzi lazima uwe
mgumu kwake, ukizingatia kuwa anayemhukumu ni adui yake.
DiamondDayna na Kalajelemia
Ally Choki, mwanamuziki wa dansi
Nimeamua kuutumia msemo huu ili
kutetea hoja yangu ninayopanga kuielezea katika makala haya, hasa kuangalia
wimbo wa wizi wa kazi za wasanii unavyoendelea kuimbwa kila siku ya Mungu.
Wimbo huu umeimbwa na unachosha
kwa kiasi kikubwa kuendelea kuusikiliza kwa namna moja ama nyingine, hasa
unapogundua kuwa hakuna kinachofanikiwa.
Amgalia, wakati serikali
inaanza kujipambanua kuwa inapambana na wizi wa kazi za wasanii, inasahau kuwa
yenyewe ndio mwiba mkali kwa wasanii wa Tanzania.
Serikali imekuwa ikitumia sanaa
mara nyingi katika shughuli zake zenye mkusanyiko wa watu wengi. Pamoja na yote
hayo, serikali inamiliki vituo vya redio na televisheni vinavyotumia kazi za
wasanii tena bila kuwalipa kitu chochote.
Katika kuliangalia suala hilo,
ndipo unapogundua kuwa serikali hii mara zote imekuwa ikifanya siasa na porojo
kwa mahali ambako hakuhitaji masihala hata kidogo.
Wizi huo wa kazi za wasanii
umegawanyika katika makundi mengi mno na yote yanahitaji kuangaliwa upya. Ni
wakati wa serikali kutangaza sera zenye mashiko, hasa kwa kuona yenyewe inakuwa
mfano wa kuigwa kwa faida ya sanaa na wasanii kwa ujumla.
Kinachoendelea sasa juu ya
malumbano ya baadhi ya wasanii ni ugumu tu wa maisha. Kama wasanii watawekewa
mfumo mzuri hakika maisha yao yatakuwa mazuri.
Ni wakati sasa wa serikali
kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara na ile ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo kuona mbinu zinazotumiwa kupambana na wezi hao.
Serikali inaweza kufika mbali
zaidi kwa kuisimamia vizuri sera wanazotangaza, hasa kuona hata Shirika la Utangazaji
nchini TBC inatenga fedha kwa ajili ya kuwalipa wasanii.
Endapo serikali itafanya hivyo,
vituo vingine vya watu binafsi navyo vitafuata nyuma kwa ajili ya maisha ya
sanaa na wasanii wetu Tanzania, ukizingatia kuwa ndio ajira yao.
Huu si wakati wa kupiga porojo.
Wizi wa kazi za wasanii umegawanyika katika makundi mengi kama nilivyosema hapo
juu. Tusingalie wale wanaodurufu CD kwenye vibanda mtaani.
Tunaweza kufika mbali zaidi
kuhakikisha kuwa kila kinachowanyonya wasanii kinafanyiwa kazi. Hii ndio inayowafanya
wasanii waishi maisha magumu hapa Tanzania.
Fikiria mchango wa muziki wa
Tanzania, tangu nchi inapata Uhuru wake hadi leo hii. Ni wanamuziki wangapi
wamenufaishwa na sauti zao, nyimbo zao kutumiwa ovyo ovyo mitaani.
Leo kama Chama Cha Mapinduzi CCM
kinafanya mkutano wake lakini muda mwingi inapiga nyimbo za wasanii, ni vipi
watu hao watanufaika kwa kupitia vipaji vyao?
Kama Chama Cha Demokrasia na
Maendeleo Chadema, Chama Cha Wananchi CUF na vingine vinaona haviwezi kufanya
mikutano yao bilaa muziki, nao inawaangalia vipi wasanii?
Kutokana na kulipigania suala
hilo, TBC ilipaswa kuanza kulipa mirahaba kwa wasanii tangu mwaka 2003. Je,
mpango huo umeisha wapi? Au ndio mpango huo umeminywa?
Katika kuliangalia hilo, ndipo
unapozidi kushangazwa na mfumo za uongozi wa Tanzania. Kila siku inajadili
jambo lile lile. Inakera kama hakuna linalofanikiwa.
Kuna uwezekano mkubwa
kinachojadiliwa leo kwenye Bunge la Bajeti mjini Dodoma kuzungumzwa tena bajeti
ijayo. Inashangaza sana. Je, huu ndio mfumo wa uongozi wetu?
Waziri anaposema kuwa lazima
wezi wa sanaa wakamatwe, inashangaza maana wizi huo umekubaliwa na serikali
yenyewe, ndio maana hakuna jipya linalofanikiwa.
Huu sio muda wa porojo. Ni
kupambana kikweli pamoja na kutoa uamuzi wenye mashiko kwa sanaa ya Tanzania.
Kuona kuwa kila anayetumia sanaa, muziki lazima awalipe wasanii.
Bila hivyo kuna siku serikali
haitaheshimika kwa namna moja ama nyingine, maana kila inachosema hakina
mashiko zaidi ya kupiga porojo katika vikao muhimu kama Bunge.
Hili haliwezi kuchekewa na
kufumbiwa macho, zaidi ya kuufahamu wizi unaolalamikiwa na kutokomezwa kwa
namna moja ama nyingine ili sanaa iwe na faida kwa wasanii wetu.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment