Tatizo ni gesi, siasa au choyo na ubaguzi?
Waandamanaji wanaopinga gesi kuja Dar es Salaam.
Na Kambi Mbwana,
Dar es Salaam
TANZANIA yetu inazidi kuingia katika shimo baya
la uvunjifu wa amani, kutokana na baadhi yao
kufanya mambo kwa faida yao.
Kwa bahati mbaya, habari nyingi mbaya zinazotokea katika Taifa letu, zinapokewa
vibaya na wadau wengi.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
Sio jambo geni.
Inajulikana kuwa habari mbaya ndiyo inayovuma sana kuliko ile nzuri. Vitu kama migomo na
maandamano ni kawaida sasa. Leo hii kusikia kiongozi Fulani amepigwa risasi au
kanisa limechomwa moto pia ni kawaida.
Kuna msomaji
wangu alinitumia meseji fupi tu. Ilisomeka hivi; ‘hii ndio Tanzania
uitakayo ya migomo, vurugu na maandamano’. Ujumbe wa msomaji huyo uliingia
akielezea zaidi maandamano ya Watanzania wa Lindi na Mtwara kupinga gesi
kusafirishwa kutoka Mtwara hadi Dar es
Salaam.
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika
Ujumbe huu
sijaushangaa. Sijaushangaa maana aliyeutuma aliubadilisha kutoka kwa wanaodai
haki ya kuitosafirisha gesi hiyo hadi lawama kwa Serikali, hasa Chama cha
Mapinduzi (CCM).
Wenyewe wanadai
kuwa tatizo ni CCM. Sawa, hayo ndio maono ya baadhi yao, lakini najiuliza kiini cha maandamano ya
watu wa Mtwara. Kwanini nasema hivyo. Ni dhahiri kadhia hiyo imebadilishwa
mbinu na kushambuliwa zaidi CCM na serikali yake.
Kama hivyo ndivyo, sioni kwanini wananchi wa
Mtwara waliweza kubeba mabango yaliyosema Mtwara kwanza vyama baadaye.
Wakati
watu wanasema hivyo, wanasahau kuwa maandamano yameratibiwa kwa kiasi kikubwa
na vyama vya siasa vya Chadema, NCCR-Mageuzi, Sau, Tanzania Labour Party TLP,
APPT Maendeleo, ADC, UDP na DP, wakishirikiana na wananchi wa mikoa hiyo.
Maandamano hayo
yalianzia katika kijiji cha Mtawanya hadi Mtwara mjini kupitia barabara ya
kwenda Msimbati eneo ambako gesi asilia inapatikana.
Pamoja na kuwa
na hoja nzuri ya kudai haki ya gesi asilia, lakini kwa undani zaidi sakata hilo lilipaliwa kisiasa.
Watu walikuwa kwenye kazi ya kunufaisha vyama vyao vya siasa. Hili ukisema,
baadhi yao
hawatakubali.
Katika kulijua hilo, lazima kila
Mtanzania awe tayari kutetea rasilimali za Taifa bila kuangalia zilizokuwapo
katika Mkoa wake. Wananchi wa Mtwara na Lindi kazi yao ni kudai maendeleo na si kuandamana
wakitaka gesi hiyo ibaki kwao.
Ndio maana
nasema, huenda wazo lilikuwa zuri, lakini limeharibiwa kwa kuratibiwa kisiasa
zaidi, ndio maana tumeshuhudia baadhi ya wanasiasa wakiinua midomo yao, wakiwa na nia ya
kukidhoofisha zaidi Chama cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake, ikiwa chini ya
Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
Kwa mujibu wa
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, rasilimali zote
zinazopatikana katika Taifa hili, zinatumika kwa ajili ya Watanzania wote na
sio wa eneo moja linapopatikana katika mkoa husika.
Ni kauli njema
inayotoa shaka kuwa sisi sote tunaishi katika Taifa moja, hivyo sioni ubaguzi
unakujaje katika jambo kama hilo.
Mtwara wangekuwa na hoja kama licha ya bidhaa
hiyo, gesi asilia kutoka kwao, lakini serikali haitatui kero zao.
Mtwara wangelia
zaidi, kama wamegundua gesi asilia inayotoka
kwao, inatumika vibaya, au ikinufaisha mataifa mengine. Kuisema hoja hii lazima
ujifanye chizi usiyeumizwa na hoja dhaifu za baadhi ya Watanzania.
Kila
anayepambana na suala hilo
la gesi asilia, hakika kwa asilimia kadhaa anatatua kero hiyo kwa faida ya
chama chake cha siasa. Watu wa aina hiyo hawastahili kuchekewa. Hatuwezi kujiendesha
kwa kuangalia mikoa, majimbo au vijiji vyenye rasilimali husika.
Kama hivyo ndivyo, Taifa hili haliwezi kuwa
moja. Litameguka kadri siku zinavyokwenda mbele, huku shari hiyo ikijengwa
zaidi na wanasiasa. Siasa za vyama vingi hazijaletwa ili zivunje amani ya
Watanzania.
Siasa hizo
zimekuja ili kuwa wakosoaji wakubwa wa serikali, lakini si kwa kila
linalofanywa hata kama liwe na tija
linastahili kukemewa. Huo ndio ukweli. Lazima tufanye mambo yetu kwa kuangalia
matokeo sahihi.
Tunajiendesha
vibaya kwa kuingiza chembe chembe za siasa za vyama vyetu vya siasa, bila
kuangalia hasara inayoweza kupatikana. Tangu kuibuka kwa sakata hilo la maandamano ya
Mtwara, nilibaki najiuliza faida na hasara.
Mkoa wa Mtwara
hauna mbunge kutoka upinzani. Wabunge wote ni CCM. Lakini Lindi kuna majimbo
mawili yanayoshikiliwa na Chama cha Wananchi (CUF).
Kwa maana hiyo,
nashawishika kusema kuna dalili kuwa sakata hili la gesi asilia limebebwa
katika mgongo wa siasa, wakiwa na lengo la kuonyesha ukarimu wao kwa wananchi
wa Mtwara.
Kama ni uongo, basi upo karibu na ukweli.
Wakati mwingine nasema, kinachotakiwa ni kuweka mbele maslahi ya Taifa. Hilo suala la nani
anapaswa au hapaswi kunufaika linahitaji kuwekwa kando.
Hivi kabla ya
gesi hiyo haijagunduliwa, serikali haipaswi kuwahudumia watu wa Lindi na
Mtwara? Je, maeneo ambayo hayana rasilimali kama hizo za gesi, madini nazo
hazipaswi kuhudumiwa na serikali yao?
Mimi nilidhani
viongozi wa mkoa, kuanzia madiwani, wabunge na wengineo wangekaa na kujadili
namna gani Taifa linaweza kunufaika na rasilimali hizo. Lakini kuanza kuweka
chokochoko kutoka katika vichwa vya walalahoi ni kuwasumbua.
Muda huo wa
maandamano ungetumiwa kubuni namna gani ya kujiletea maendeleo kwa kupitia
fursa za kiuchumi na sio kupambana naa nguvu za dola. Huu ndio ukweli. Mkuu wa
Mkoa wa Mtwara, Kanali Mstaafu, Joseph Simbakalia, aliwajia juu watu hao kwa
madai kuwa ajenda yao
hiyo haina mashiko.
Simbakalia
alishangazwa pia na baadhi ya watu kwenye maandamano hayo waliotaka atimuliwe
katika Mkoa huo. Mambo kama haya hutokea
katika migogoro na maandamano mengi kutoka katika kila mahali.
Nilipenda kauli
ya John Mnyika, Mbunge wa Ubungo, ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Nishati na
Madini juu ya kutumia nafasi yake bungeni kuomba nakala ya mkataba wa mkopo wa
Dola za Kimarekani Bilioni 1.225, sawa na Shilingi Trilioni 1.86 kutoka nchini China kwa ajili
ya kujenga miundo mbinu ya kusafirisha gesi hiyo asilia kutoka Mtwara kwenda
Dar es Salaam.
Kauli ya Mnyika
imekuja wakati tayari chama chake kilishiriki kwa karibu kuratibu maandamano
hayo. Kumbe alikuwa na malengo haya, kwanini wasingeshauri wananchi wao, kama uwezo huo wanao kusubiri hadi aone nakala hiyo?
Kikubwa ni
maendeleo ya Tanzania
na sio mkoa gani unastahili kubakiwa na rasilimali husika. Hatuwezi kujiendesha
kimkoa, kimajimbo au wilaya kama wanavyotaka
baadhi ya watu, maana ajenda hii ni mbaya na haina mashiko.
Ifikie wakati
watu waache porojo, nyimbo za kisiasa kwa kuangalia zaidi maendeleo ya Tanzania, iwe
kwenye gesi, madini na mengineyo. Tusipofanya hivyo, hatari itakuwa kubwa,
maana tunazalisha sumu ya kuleta mapigano wakati ingeweza kujadiliwa kwa amani
kwa kutumia vikao na nia ya dhati ya tunu ya Taifa letu.
Tusimtafute
mchawi, lakini pia watu wa Mtwara na Lindi wajuwe hawapaswi kufanya vurugu kwa
kulala barabarani, kuandamana au kurushiana maneno na viongozi wa serikali,
huku ajenda yao ni kutaka rasilimali walizonazo zisiende kwingine kwa sababu za
choyo, roho mbaya na fitina zinazojengwa zaidi na wanasiasa wetu wenye sera ya
kujiendesha kwa majimbo.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment