Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SERIKALI kwa kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, imeombwa
kuwasaidia wajasiriamali kwa kuwawezesha kwa mikopo ili waweze
kufanya kazi za kwa ufanisi na kuongeza pato la Taifa.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Grace Products, Elizabeth Kilili,
alipozungumza na Habari na Matukio jana jijini Dar es Salaam.
Akizungumza zaidi, Elizabeth alisema kwamba wapo wajasiriamali
wadogo na wakubwa ambao kwa kiasi fulani wanaweza kusonga mbele kama
serikali yao itawasaidia hata kwa kuwafanikishia suala zima la
mikopo.
Alisema watu wengi wamekuwa wakishindwa kufanya biashara zao kwa
kiwango cha Kimataifa, huku changamoto kubwa ikiwa ni upatikanaji wa
vifaa vya kuwafanyia kazi kutokana na kukosa uwezo mkubwa kifedha.
“Tunaiomba serikali kuwa makini katika hili la kusaidia
wafanyabiashara wa Tanzania, wakiwamo wale ambao uwezo wao ni mdogo
na hawana uwezo au sifa za kukopesheka kama wanavyofanya baadhi yao
hapa nchini.
“Kwa mfano mimi nafanya biashara ya kutengeneza bidhaa zangu
mbalimbali ikiwamo ya sabuni ya kuogea ya Grace Manjano, Shampoo na
nginginezo zenye nembo ya Grace Products Ltd, lakini ukosefu wa fedha
ni tatizo kwangu,” alisema.
Elizabeth ni miongoni mwa wajasiriamali wenye uchu wa mafanikio,
huku bidhaa zake zikianza kufanya vizuri na kuvuka mipaka, jambo
ambalo linaweza kuipatia nchi mafanikio makubwa zaidi kama
atawezeshwa na serikali yake.
No comments:
Post a Comment